Lula ashinda muhula wa nne wa urais Brazil

Chanzo cha picha, Reuters
Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva, amechaguliwa kuhudumu kwa muhula wa nne baada ya kumshinda seneta Flávio Bolsonaro katika duru ya pili ya uchaguzi wa urais nchini humo.
Baada ya asilimia 98.87 ya masanduku ya kura kuhesabiwa, Mahakama ya Uchaguzi ya Brazil (TSE) ilimtangaza Lula kuwa mshindi kwa mujibu wa hesabu za kura zilizokuwa zimepatikana. Lula alipata asilimia 51.79 ya kura, dhidi ya asilimia 48.21 alizopata Bolsonaro.
Tofauti hiyo ya kura ilikuwa kubwa kuliko ushindi wa Lula dhidi ya baba yake Flávio, rais wa zamani Jair Bolsonaro, katika uchaguzi wa mwaka 2022.
Matokeo hayo yalikuwa ya kushangaza, yakiwa mara ya kwanza tangu Brazil irejee katika mfumo wa demokrasia kwa mgombea aliyeshindwa katika duru ya kwanza kugeuza matokeo na hatimaye kushinda urais.
Katika hotuba yake ya kwanza baadaya kutangazwa mshindi Lula amesema “Demokrasia iishi milele,”.
Aidha, ameongezea kuwa, “Muhula huu wangu wa nne utakuwa bora kuliko muhula wowote wa rais katika historia ya nchi hii.”
“Utakuwa muhula ambao nitawasikiliza zaidi wananchi wa Brazil.”
Ushindi huo ulifuatia kampeni kubwa iliyofanywa na wafuasi wa Lula kwenye mitandao ya kijamii, pamoja na maandamano yaliyovutia mamia ya maelfu ya watu katika miji mikuu ya nchi hiyo, ikiwemo Rio de Janeiro na São Paulo.
Siku ya uchaguzi pia ilishuhudia idadi kubwa ya wapiga kura wakijitokeza. Kiwango cha kutoshiriki uchaguzi kilipungua kwa kiasi kikubwa zaidi kati ya duru ya kwanza na ya pili kuliko katika uchaguzi wowote wa urais nchini humo tangu mwaka 1989.
Hata hivyo, uchaguzi huo haukukosa utata. Kampeni ya Lula ilidai kuwa baadhi ya wapiga kura walizuiwa kushiriki baada ya uhaba wa mabasi kufanya iwe vigumu kwao kufika katika vituo vya kupigia kura katika miji kadhaa, ikiwemo São Paulo na Salvador, kaskazini-mashariki mwa Brazil.
Kampeni ya Flávio Bolsonaro nayo iliomba muda wa kupiga kura uongezwe kutokana na hali mbaya ya hewa kusini mwa Brazil. Hatimaye, Mahakama ya Juu iliongeza muda wa upigaji kura kwa saa mbili.
Jair Bolsonaro kwa sasa yuko kizuizini baada ya kutiwa hatiani mwezi Septemba 2025 kwa kujaribu kufanya mapinduzi ya serikali kufuatia kushindwa na Lula katika uchaguzi wa mwaka 2022.
Kwa ushindi huo, Lula anakuwa rais wa kwanza katika historia ya Brazil kuchaguliwa kuhudumu kwa muhula wa nne. Ataendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2030.
Flávio Bolsonaro alikuwa mgombea ambaye Rais wa Marekani Donald Trump alimpigia upatu kuwa rais wa Brazil.
Soma pia:







