Moja kwa moja , Maandamano Ujerumani: Gharama ya maisha yachochea ghasia na uporaji

Ghasia pia ziliripotiwa katika miji ya Berlin, Cologne na Hamburg, huku polisi wakitumia maji kuwatawanya waandamanaji.

Muhtasari

  • Trump aidhinisha viza kwa mama wa kijana Mghana aliyeuawa Marekani
  • Mawaziri wa Ethiopia wapewa mafunzo ya kijeshi
  • Gharama ya maisha yachochea ghasia na uporaji Ujerumani

Moja kwa moja

Ambia Hirsi

  1. Trump aidhinisha viza kwa mama wa kijana Mghana aliyeuawa Marekani

    .

    Rais wa Marekani Donald Trump amekubali kutoa viza kwa mama wa kijana Mghana, Javits Frimpong, aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Bronx, New York, ili aweze kusafiri kwenda Marekani kumuaga mwanawe.

    Hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo ya simu kati ya Meya wa New York, Zohran Mamdani, na Trump.

    Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Mamdani alisema mama huyo anastahili kupata fursa ya kumuomboleza mwanawe ana kwa ana.

    Doris Adu Gyamfi, mama wa kijana huyo, anayeishi Kumasi nchini Ghana, anatarajiwa kuwasili Accra kwa ajili ya kuanza mchakato wa kupata viza.

    Frimpong, mwenye umri wa miaka 15, alipigwa risasi na kuuawa Alhamisi asubuhi alipokuwa njiani kuelekea shuleni.

    Polisi wanasema bado wanawatafuta washukiwa watatu waliotoroka baada ya tukio hilo, huku picha za kamera za usalama zikionyesha kijana huyo akijaribu kukimbia kuokoa maisha yake.

    Serikali ya Ghana imelaani mauaji hayo na kuitaka Marekani kufanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wahusika wanawajibishwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema serikali itaendelea kulinda na kutetea maslahi ya raia wake popote walipo.

    Mauaji hayo yamezua maombolezo makubwa katika jamii ya Waghana wanaoishi Bronx. Hadi sasa, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

  2. Mawaziri wa Ethiopia wapewa mafunzo ya kijeshi

    Abiy Ahmed na viongozi wa serikali yake

    Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, amewaweka mawaziri wake na maafisa wengine waandamizi wa serikali kwenye mafunzo ya kijeshi, akisema kuwa nidhamu ya kijeshi inaweza kusaidia kujenga viongozi imara zaidi na kuharakisha maendeleo ya taifa.

    Picha alizochapisha kwenye mitandao ya kijamii zinamwonyesha akishiriki mazoezi hayo pamoja na mawaziri, manaibu mawaziri na wakuu wa taasisi za serikali katika Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Hurso.

    Hatua hiyo ni ya kipekee nchini Ethiopia, ambako maafisa waandamizi wa serikali kutoka sekta ya kiraia mara chache huonekana wakipitia mafunzo ya kijeshi.

    Miongoni mwa washiriki wa mafunzo hayo ni Spika wa Baraza la Shirikisho, Muferiat Kamil, Waziri wa Fedha Fitsum Assefa na Waziri wa Afya Mekdes Daba.

    Bado haijafahamika mafunzo hayo yalianza lini au yatadumu kwa muda gani.

    Katika chapisho lake, Abiy alisema kuwa azma ya Ethiopia ya kufikia ustawi wa wote inahitaji viongozi wenye afya njema, maadili thabiti na uwezo mkubwa wa kiakili.

    Alieleza kuwa taasisi za kijeshi hutoa mafunzo muhimu katika nyanja za nidhamu, uzalendo, ushirikiano, uwajibikaji na uongozi.

    "Wanajeshi wana shabaha, huku raia wakiwa na malengo. Dhamira ya pande zote mbili ni ushindi," alisema, akiongeza kuwa kuunganisha taaluma za kijeshi na za kiraia kunaweza kusaidia kujenga kizazi chenye uwezo wa kufanikisha yote mawili.

  3. Gharama ya maisha yachochea ghasia na uporaji Ujerumani

    ..

    Maandamano dhidi ya gharama ya maisha nchini Ujerumani yaligeuka kuwa ya vurugu Jumamosi jioni, baada ya waandamanaji kupora maduka katikati ya jiji la Frankfurt.

    Ghasia pia ziliripotiwa katika miji ya Berlin, Cologne na Hamburg, huku polisi wakitumia maji kuwatawanya waandamanaji waliowarushia fataki, mawe na chupa maafisa wa usalama na wahudumu wa dharura.

    Awali, maelfu ya watu walikuwa wamejitokeza kushiriki maandamano yaliyoandaliwa na kundi la kampeni la Gen Z regelt ("Gen Z wanachukua jukumu"), kupinga ongezeko la gharama ya maisha, ufadhili mdogo wa shule, kupunguzwa kwa matumizi ya umma na sera za huduma ya kijeshi.

    Machafuko hayo yanajiri wakati maandamano makubwa yanayoongozwa na vijana pia yakishuhudiwa nchini Ufaransa, ambako zaidi ya watu 320,000 waliripotiwa kuandamana Jumamosi.

    Shirika la habari la AFP liliripoti kuwa polisi walifunga sehemu kubwa ya barabara kuu ya kibiashara ya Frankfurt, huku watu kadhaa wakikamatwa.

    Mamlaka katika Frankfurt, Munich na Berlin zilikadiria idadi ya waandamanaji kuwa karibu 18,000, ingawa waandaaji walikuwa wamekadiria idadi kubwa zaidi.

    Vyombo vya habari vya Ujerumani viliripoti kuwa maelfu ya watu walishiriki maandamano katika miji mbalimbali nchini humo.

    Msemaji wa Gen Z regelt, Lina Friedrich, alisema maandamano hayo yalikuwa ya kutetea amani na uhuru..

    "Tunachotilia mkazo zaidi ni kuboreshwa kwa mifumo ya afya na elimu. Tunapinga utumishi wa kijeshi wa lazima na tunaunga mkono mgawanyo wa majukumu kwa usawa," alisema.

  4. Natumai hujambo.