Mazungumzo ya amani Ukraine yaanza upya, pande zote zikilegeza misimamo yao

Chanzo cha picha, Getty Images
Wapatanishi wa Marekani wamesema kuwa Moscow na Kyiv zimeonyesha kulegeza makali yao, katika mazungumzo kuhusu suala la nani atadhibiti maeneo ya mashariki mwa Ukraine baada ya vita.
Kauli hizo zimetolewa siku moja kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya kwanza, yanayolenga kumaliza vita vya Ukraine.
Maafisa waandamizi kutoka Moscow, Kyiv na Washington wanakutana mjini Abu Dhabi, vita vya Ukraine vikikaribia kuingia mwaka wa tano sasa.
Jared Kushner, mkwe wa Rais Donald Trump, pamoja na mjumbe maalumu Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, wamesema mazungumzo hayo yanalenga kushughulikia "masuala ya usalama baada ya vita" kwa Urusi na Ukraine.
"Sehemu muhimu ya mchakato huu ni kuhimiza pande zote kuanza kufikiria kwa uzito kuhusu kitakachotokea baada ya vita," Kushner aliandika kwenye mtandao wa X.
Hata hivyo, misimamo ya Moscow na Kyiv kuhusu namna ya kumaliza vita hivyo bado unatofautiana pakubwa.
Mojawapo ya maeneo muhimu yanayozua mzozo ni eneo la Donetsk, mashariki mwa Ukraine, ambalo kwa sasa sehemu kubwa linadhibitiwa na Urusi.


