AFCON kuandaliwa kila baada ya miaka miwili - CAF

Chanzo cha picha, Getty Images
Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) litarejea kufanyika kila baada ya miaka miwili, baada ya Kamati Tendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kubatilisha kwa kauli moja uamuzi wake wa awali wa kuandaa mashindano hayo kila baada ya miaka minne.
Rais wa CAF, Dkt Patrice Motsepe, alikuwa ametangaza wakati wa mkutano wa mkakati wa shirikisho hilo uliofanyika Cabo Verde kuanzia tarehe 7 hadi 9 Oktoba 2026, kuwa kamati hiyo itapitia upya uamuzi uliofikiwa mwaka jana.
Motsepe amesema kurejea kwa mfumo wa miaka miwili ni kwa manufaa ya soka la Afrika, vyama 54 wanachama wa CAF pamoja na wachezaji wa Afrika wanaocheza katika klabu nje ya bara hilo.
Ameeleza kuwa mpango wa kuanzisha Ligi ya Mataifa ya Afrika, ambayo ilipendekezwa kuchukua nafasi ya AFCON kama mashindano ya kila baada ya miaka miwili, ungehitaji miaka kadhaa kuzalisha mapato makubwa yanayohitajika kuendeleza soka la Afrika na kuongeza ushindani wake kimataifa.
Toleo lijalo la AFCON litafanyika mwaka 2027, likiwa limeandaliwa kwa pamoja na Kenya, Tanzania na Uganda.
Mashindano yatakayofuata yamepangwa kufanyika mwaka 2028, 2031 na 2033, huku toleo la mwaka 2030 likiachwa ili kutoa nafasi kwa Kombe la Dunia la FIFA.
Motsepe amesema AFCON si mashindano ya soka pekee, bali pia ni jukwaa muhimu la kuadhimisha utajiri wa tamaduni, mila na watu wa Afrika.
Soma Pia:























