Shakahola: Mwana wa Mackenzie afichua ndugu zake bado wanalazimishwa kufunga

Dan Mackenzie, 27, amesema aliripoti suala hilo kwa polisi, ambao waliwaokoa watoto wanane, wakiwemo ndugu zake watano wadogo.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Lizzy Masinga & Mariam Mjahid

  1. Shakahola: Mwana wa Mackenzie afichua ndugu zake bado wanalazimishwa kufunga

    .

    Mwana mkubwa wa kiongozi wa dhehebu tata nchini Kenya, Paul Mackenzie, anasema ndugu zake wadogo waliendelea kulazimishwa kufunga kula hadi wiki mbili zilizopita, licha ya baba yao kupatikana na hatia ya mauaji ya watu 191.

    Dan Mackenzie, mwenye umri wa miaka 27, amesema aliripoti suala hilo kwa polisi, ambao waliwaokoa watoto wanane, wakiwemo ndugu zake watano wadogo, kutoka nyumbani kwa bibi yao na kuwapeleka katika kituo cha uokoaji.

    “Kwa hakika walilazimishwa kufunga kwa sababu walinyimwa chakula kwa karibu siku tatu,” aliiambia BBC katika kipindi cha Newsday.

    Siku ya Jumatatu, baba yake alipatikana na hatia ya kuwaua watoto 190 na mtu mzima mmoja waliokufa kwa njaa katika msitu wa Shakahola, karibu na pwani ya Kenya.

    Mackenzie alikuwa amewaamuru wafuasi wa dhehebu lake kujinyima chakula wao pamoja na watoto wao hadi kufa, akidai kuwa wangekutana na Yesu.

    Viongozi wengine 28 wa dhehebu hilo pia walipatikana na hatia ya mauaji.

    Mackenzie amwita mwanawe msaliti baada ya hukumu

    Dan amesema hukumu hiyo imewapa waathiriwa wa mkasa wa Shakahola afueni, huku akieleza kuwa alikutana kwa muda mfupi na baba yake baada ya mahakama kutoa uamuzi.

    “Tumepata afueni kidogo sisi kama waathiriwa wa kilichotokea Shakahola, kwa sababu sasa kesi hii inafikia mwisho na amepatikana na hatia,” amesema.

    Alipoulizwa kuhusu mazungumzo yake na baba yake baada ya hukumu kutolewa, Dan alisema alipata nafasi ya kumsalimia wakati Mackenzie alipokuwa akipelekwa kwenye gari.

    “Nilipata nafasi kidogo wakati akipelekwa kwa gari. Nikamsalimia na akaniambia kuwa ninamsaliti. Nikacheka tu kwa sababu sikuwa na la kumwambia,” amesema.

    Dan amesema haelewi ni kwa nini baba yake alimwita msaliti, lakini anaamini huenda kauli hiyo inahusiana na hatua yake ya kuzungumza kuhusu yaliyotokea katika dhehebu hilo.

    “Sijui anamaanisha nini. Pengine kuna kiapo kati ya mzazi na mtoto kwamba hapaswi kuzungumza ukweli, au sijui ni kiapo gani kinachofanya aone kwamba nimemsaliti,” amesema.

    Dan, ambaye awali alikuwa akimtetea baba yake, amesema alikuja kuelewa ukubwa wa mkasa huo wakati wa kusikilizwa kwa kesi mahakamani.

    Anasema pia alipitia maisha magumu akiwa mtoto ndani ya dhehebu hilo.

    “Nilipokuwa na umri wa miaka 12, nililazimishwa kufunga kwa karibu wiki moja,” amesema.

    Pia anakumbuka jinsi waumini wa kanisa hilo walivyokuwa wakimpiga kwa saa nyingi ili kumlazimisha kuhudhuria ibada alipokuwa mtoto.

    Dan anasema aliondoka shuleni akiwa na umri wa miaka saba, kutokana na mafundisho ya dhehebu hilo yaliyopiga marufuku elimu na kueleza kuwa dawa za kisasa zilikuwa “uovu”.

    Amesema aliamua kujitenga na maisha hayo mwaka 2018 au 2019, baada ya kuchoshwa na hali aliyokuwa akipitia. Kwa mujibu wake, baba yake alimnunulia pikipiki ili aweze kujitegemea.

    Dan pia ameeleza kuhusu kifo cha ndugu yake mdogo zaidi, aliyekuwa na umri wa takriban mwaka mmoja na nusu, katika mkasa wa Shakahola.

    Maisha ya Dan baada ya kujitenga na dhehebu

    Kwa sasa Dan anaishi Malindi, katika pwani ya Kenya, ambako anajipatia kipato kwa kufanya kazi ya udereva wa bodaboda. Pia anawasaidia ndugu zake wadogo.

    Amesema hajawahi kupata huduma za kisaikolojia licha ya kupitia matukio magumu akiwa mtoto na kupoteza ndugu yake katika mkasa huo.

    Akizungumzia jinsi jamii inavyompokea licha ya uhalifu unaohusishwa na baba yake, Dan amesema baadhi ya watu walikuwa na hasira, lakini hawakumlaumu yeye moja kwa moja.

    “Wananiona kila wakati na kusema, ‘Huyo ni baba yako, si wewe.’ Walikuwa na hasira na wakati mmoja walibomoa ukuta, lakini mimi hawakunigusa. Tumeendelea kuishi vizuri,” amesema.

    Dan anasema alihisi pia kuwa na wajibu wa kuwaripoti wanafamilia ambao bado wanaamini mafundisho ya Mackenzie ili kuwaokoa ndugu zake wadogo.

    “Nililazimika kumripoti bibi yangu,” amesema.

    Amesema anatumaini hukumu hiyo itawapa faraja wale waliopoteza marafiki na jamaa zao.

    Familia zilizopoteza watoto zafurahishwa na hukumu

    Siku ya Jumatatu, Stephen Mwiti, mwenye umri wa miaka 48, ambaye alisema alipoteza watoto wake wote sita kutokana na dhehebu hilo, alikaribisha hukumu hiyo.

    “Nina furaha kwamba watu wote wamepatikana na hatia,” aliiambia BBC nje ya mahakama.

    Aliyekuwa mke wake ni miongoni mwa watu waliopatikana na hatia ya mauaji pamoja na Mackenzie.

    Katika hukumu yake iliyochukua saa nane mjini Mombasa, Jaji Diana Mochache alisema wafuasi wa Mackenzie waliamini kuwa alikuwa “msemaji wa Yesu”.

    Mmoja wa washtakiwa wenzake aliiambia mahakama kuwa Mackenzie alikuwa amesema mtu yeyote aliyekataa kufunga alipaswa kulazimishwa kwenda mbinguni “kwa mateke na makofi”.

    Jaji huyo alisema mazishi yaliyofanyika katika msitu ambako dhehebu hilo lilikuwa na makao yake yalielezwa kuwa “harusi”, huku waliokufa wakisherehekewa kwa madai kuwa walikuwa “wamefunga ndoa na Yesu”.

    Mackenzie anakabiliwa na kesi nyingine

    Mackenzie na viongozi wengine wa dhehebu hilo pia wanakabiliwa na kesi tofauti zinazohusu ugaidi, itikadi kali na kunyima watoto haki ya kupata elimu.

    Hukumu ya mauaji ndiyo uamuzi wa kwanza kuhusu mashtaka mazito zaidi dhidi ya mchungaji huyo, aliyekamatwa mwaka 2023 baada ya miili ya zaidi ya watu 400 kugunduliwa katika makaburi ya kina kifupi katika msitu wa Shakahola, karibu na pwani ya Kenya.

    Mahakama inatarajiwa kutangaza adhabu yake tarehe 6 Novemba.

    Pia unaweza kusoma:

  2. Somalia: Mahakama yaamua nani ni baba mzazi wa mvulana katika mzozo uliohusishwa na vifo vya watu saba

    d

    Mahakama nchini Somalia imeamua kuwa Liban Tahliil Haji Aden ndiye baba wa mvulana mwenye umri wa miaka 16, baada ya wanaume wawili kudai kuwa baba wa mtoto huyo katika mzozo wa muda mrefu uliohusishwa na vifo vya watu saba.

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya ndani, watu saba wameuawa na wengine 21 kujeruhiwa katika vurugu zinazohusishwa na mzozo huo kati ya familia hizo mbili.

    Uamuzi huo ulitolewa Jumanne mjini Galkayo na jopo la wanazuoni watatu wa Kiislamu walioteuliwa na mamlaka za eneo la Puntland, linalojitawala kwa kiasi fulani.

    Majaji walikubali madai ya Liban na kuyakataa ya Farah Awil Ali, ambaye anasema alimlea mvulana huyo kwa miaka 13. Wanaume hao wawili wamesema wanaukubali uamuzi wa mahakama.

    Kesi hiyo imevuta hisia kubwa nchini Somalia, huku ushahidi wa mama wa mvulana huyo, Halimo Yusuf Mohamed, ukiwa sehemu muhimu ya maamuzi ya mahakama.

    Wakati wa usikilizaji wa kesi uliochukua siku tatu, Halimo alisema aliolewa na Liban Julai 2006, kabla ya kutalikiana naye miaka minne baadaye.

    Alisema baadaye aliolewa na Farah Oktoba 2010, lakini ndoa hiyo ilivunjika mwaka 2013.

    Halimo alisisitiza kuwa Liban ndiye baba wa mwanawe na kwamba hakupata mtoto na Farah. Mashahidi wawili pia waliiambia mahakama kuwa walihudhuria harusi ya Halimo na Liban mwaka 2006.

    Liban aliapa na kuiambia mahakama kuwa Halimo alimweleza alikuwa mjamzito walipotalikiana Julai 2010.

    Mvulana huyo naye alihojiwa kupitia video na kusema kuwa Liban ndiye baba yake.

    Katika kutoa uamuzi, majaji walizingatia ushahidi wa mashahidi, maelezo ya mama na kauli ya mvulana huyo, pamoja na sheria za Kiislamu kuhusu kuthibitisha nasaba. Hata hivyo, uamuzi huo haukutaja vipimo vya vinasaba vya DNA.

    Baada ya uamuzi huo, Farah alisema anauheshimu, lakini akauliza kuhusu fedha alizotumia kumlea mvulana huyo kwa miaka 13.

    Aliwaomba wanazuoni wa Kiislamu na maafisa wa serikali kuzingatia gharama alizobeba katika kipindi hicho.

    Mahakama haikueleza iwapo Farah atarejeshewa fedha hizo wala namna malezi ya mvulana huyo yatakavyopangwa kuanzia sasa.

    Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa watu saba wameuawa na wengine 21 kujeruhiwa katika vurugu zinazohusishwa na mzozo huo. BBC haijathibitisha kwa kujitegemea idadi hiyo ya vifo na majeruhi.

    Akizungumza baada ya uamuzi wa Jumanne, Liban aliomba msaada kwa walioathiriwa na vurugu hizo.

    “Watu wamefariki. Watu wamejeruhiwa. Kuna watoto yatima,” alisema, akiahidi kuwasaidia familia zilizopoteza wapendwa wao na waliojeruhiwa.

    Majaji wamezitaka familia zote mbili kuheshimu uamuzi huo na kuepuka vurugu zaidi.

    Hata hivyo, mahakama haikutoa uamuzi kuhusu nani anawajibika kwa mauaji hayo wala madai ya Farah ya kurejeshewa fedha alizotumia kumlea mvulana huyo.

  3. Kylie Jenner azua mjadala baada ya kuvaa sidiria yenye thamani ya dola milioni 50

    d

    Nyota wa vipindi vya uhalisia, Kylie Jenner, amezua hisia mseto baada ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika maonyesho ya mitindo ya Victoria’s Secret, akiwa amevalia sidiria yenye thamani ya dola milioni 50, sawa na takriban pauni milioni 37.

    Mjasiriamali huyo wa vipodozi aliwashangaza watazamaji katika maonyesho ya kila mwaka ya kampuni hiyo ya nguo za ndani siku ya Jumapili, alipovaa sidiria maarufu ya Fantasy Bra, iliyotengenezwa kwa dhahabu ya karati 18 na almasi 4,410, kwa mujibu wa mbunifu wake.

    Kwa miaka mingi, Fantasy Bra imekuwa sehemu muhimu ya maonyesho hayo, huku kuchaguliwa kuivaa kukichukuliwa kama heshima kubwa na hatua muhimu katika taaluma ya mwanamitindo.

    Baadhi ya mashabiki walifurahia kuchaguliwa kwa Jenner, mwenye umri wa miaka 29 na nyota wa kipindi cha The Kardashians. Hata hivyo, wengine waliikosoa kampuni hiyo kwa kutompa fursa mwanamitindo mkongwe.

    Mtaalamu wa mitandao ya kijamii na masoko, Joel Marlinarson, amesema hatua hiyo ilipangwa kwa makini na kuzua mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wa uanamitindo na mitandao ya kijamii.

    Ameiambia BBC Newsbeat kuwa Jenner anawakilisha kizazi kipya cha umaarufu, ambapo kampuni zinatanguliza watu wanaoweza kuvutia watazamaji wengi badala ya kuzingatia vigezo vya kawaida vya mwanamitindo.

    Marlinarson amesema watazamaji vijana wanajihisi kuwa karibu na Jenner kwa sababu wamekua wakimfuatilia kwenye mitandao ya kijamii na kupitia kipindi chake cha uhalisia pamoja na dada zake wa familia ya Kardashian.

    Hata hivyo, amesema baadhi ya watazamaji wanaokumbuka enzi ya mwanamitindo maarufu Naomi Campbell wanaweza kuona kupewa kwa Jenner fursa hiyo kuwa ni usaliti wa kile walichokizoea katika ulimwengu wa mitindo.

  4. Christiane Amanpour kuondoka CNN mwakani baada ya miaka 43

    d

    Mwandishi wa habari wa kimataifa wa kituo cha televisheni cha CNN, Christiane Amanpour, ametangaza kuwa ataondoka katika kituo hicho mwakani baada ya kukitumikia kwa zaidi ya miaka 40.

    “Baada ya miezi kadhaa ya kutafakari na kukosa usingizi kwa usiku mwingi, nimeamua kuondoka CNN, ambako nimefanya kazi kwa miaka 43 iliyojaa kumbukumbu nzuri,” amesema Amanpour katika taarifa yake.

    Mwandishi huyo mwenye umri wa miaka 68, mwenye asili ya Uingereza na Iran, amesema anatarajia kushiriki katika miradi mipya na yenye kuvutia siku zijazo, huku akisisitiza kuwa ataendelea kukiunga mkono CNN.

    Rais wa CNN, Mark Thompson, amemtaja Amanpour kuwa “miongoni mwa waandishi wa habari wanaoheshimika na kupendwa zaidi duniani.”

    Thompson amesema kituo hicho kitatumia muda uliosalia kabla ya kuondoka kwake mwakani kutambua na kuenzi mchango wake katika tasnia ya uandishi wa habari.

    Amanpour alianza kazi yake CNN mwaka 1983 akiwa msaidizi katika idara ya habari za kimataifa. Hatua kwa hatua, alijijengea jina na kuwa mmoja wa waandishi wa habari wanaotambulika zaidi kwenye televisheni.

    Katika kipindi chake cha uandishi wa habari, amekuwa akiripoti mara kwa mara kutoka maeneo ya vita na maeneo yaliyoathiriwa na migogoro. Pia amewahoji viongozi kadhaa wa dunia na watu mashuhuri.

    Tangu mwaka 2009, amekuwa akiendesha kipindi chake cha kila usiku cha mahojiano na mijadala katika CNN International.

  5. Vance: Simuungi Netanyahu kuchaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Israel

    s

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amekataa kuweka wazi iwapo anamuunga mkono Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, katika uchaguzi ujao nchini humo, licha ya Rais Donald Trump kueleza kumuunga mkono kiongozi huyo.

    Katika mahojiano na chombo cha habari cha mtandaoni, Vance amesema hataki kuingilia uchaguzi wa Israel, akieleza kuwa anajikita zaidi katika siasa za Marekani na uchaguzi wa katikati ya muhula unaotarajiwa kufanyika nchini humo.

    Vance, ambaye awali alitembelea Budapest wakati wa uchaguzi nchini Hungary na kueleza kumuunga mkono Viktor Orbán, amesema anaunga mkono wagombea wa Marekani, wala si wa nchi nyingine.

    Amesema: “Sipingi Netanyahu kuchaguliwa tena, lakini pia simuungi mkono kuchaguliwa kwake tena. Sitaki kuingilia uchaguzi wa Israel.”

    Israel inatarajiwa kufanya uchaguzi wiki ijayo. Huo utakuwa uchaguzi wa kwanza nchini humo tangu shambulio la Hamas la Oktoba 7.

  6. Kura za maoni zaonyesha Waalberta wengi wanataka kubaki ndani ya Canada

    d

    Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa wakazi wa Alberta wamepiga kura kwa wingi kuunga mkono kubaki sehemu ya Canada, badala ya kuitisha kura ya maoni kuhusu kujitenga na nchi hiyo baadaye.

    Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Alberta, zaidi ya theluthi mbili ya wapiga kura wamechagua kubaki ndani ya Canada, huku kura nyingi zikiwa tayari zimehesabiwa.

    Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, amesema matokeo hayo yanaonyesha uamuzi ulio wazi wa wananchi wa Alberta.

    Katika mkutano wa wafuasi wa kujitenga na Canada mjini Edmonton, shangwe zilipungua haraka baada ya matokeo kutangazwa. Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa vuguvugu hilo la kujitenga amesisitiza kuwa kampeni yao bado haijafikia mwisho.

    Kura hiyo iliitishwa mapema mwaka huu na kiongozi wa Alberta, Danielle Smith, kufuatia ombi lililowasilishwa na wananchi. Ilionekana kuwa kipimo muhimu cha mshikamano wa kitaifa wa Canada.

  7. Marekani yatoa tahadhari kwa raia wake kuhusu safari za Kenya

    d

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Jumatatu imepandisha kiwango cha tahadhari ya usafiri kwa raia wake wanaopanga kutembelea Kenya, ikiwashauri kufikiria upya mipango yao kutokana na hatari za kiafya na kiusalama.

    Tahadhari hiyo imepandishwa kutoka kiwango cha pili, kinachowataka wasafiri kuchukua tahadhari zaidi, hadi kiwango cha tatu.

    Wizara hiyo imetaja vitisho vilivyopo nchini Kenya kuwa ni pamoja na magonjwa, uhalifu, utekaji nyara, ugaidi, ghasia na hatari zinazohusiana na usalama barabarani.

    Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Kenya kuthibitisha kisa kipya cha Ebola, na kufikisha watu wanane waliothibitishwa kuambukizwa ugonjwa huo nchini.

  8. Selena Gomez asema matumizi ya sigara za kielektroniki yamebadilisha sauti yake

    d

    Mwimbaji na mwigizaji Selena Gomez amesema matumizi ya sigara za kielektroniki zenye nikotini yamebadilisha sauti yake.

    “Ninahisi sitawahi tena kurejesha sauti yangu ya awali,” alisema mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 34 katika ujumbe alioweka kwenye Instagram Jumapili. “Nilikuwa nikitumia sigara za kielektroniki mara nyingi.”

    Gomez alisema kuacha kutumia nikotini ni jambo gumu sana, akiwahimiza watu wanaojaribu kuacha au wanaofikiria kuanza kutumia sigara hizo kutafakari uamuzi wao.

    “Kuacha nikotini ni vigumu sana. Nilitaka tu kusema kwamba ikiwa unahangaika kuacha, au hata unafikiria kuanza kutumia sigara za kielektroniki, haifai kabisa,” alisema.

    Aliendelea kusema kuwa matumizi hayo yalikuwa uamuzi usiofaa na kwamba yalibadilisha sauti yake. Kisha alicheka na kuongeza kuwa wale wasiopenda kusikiliza sauti yake wanaweza kuchagua kutomsikiliza.

    Hata hivyo, mwimbaji na mwigizaji huyo, ambaye anaishi na ugonjwa wa lupus, unaosababisha mfumo wa kinga ya mwili kushambulia tishu na viungo vyake wenyewe, amewahi kueleza kuwa ugonjwa huo pia huathiri nyuzi zake za sauti.

    Alipoulizwa kuhusu mabadiliko ya sauti yake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye Instagram mwezi Desemba mwaka jana, alisema wakati mwingine koo lake huvimba na kusababisha sauti yake kubadilika.

    Mlipuko wa dalili za lupus unaweza kusababisha uvimbe katika eneo linalozunguka nyuzi za sauti, hali inayoweza kufanya sauti kuwa nzito au kukwaruza na kusababisha ugumu wa kuzungumza. Dalili hizo zinaweza kufanana na zile za mafua.

    Aidha, sauti ya Gomez imekuwa nzito zaidi kadiri anavyozeeka, jambo ambalo si la kawaida nje ya mabadiliko ya sauti yanayotokea kadiri umri unavyoongezeka.

    Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wake wamekuwa wakifuatilia mabadiliko hayo kwa karibu, huku wakichapisha video kwenye YouTube zinazoonyesha jinsi sauti na namna yake ya kuzungumza vilivyobadilika kwa miaka mingi.

  9. DR Congo: MSF kufunga kituo cha matibabu ya Ebola mjini Bunia

    d

    Shirika la kimataifa la kutoa huduma za matibabu bila faida, Médecins Sans Frontières (MSF), limetangaza mipango ya kufunga kituo chake cha matibabu ya Ebola kilichopo Elikiya, mjini Bunia, mwishoni mwa mwezi Oktoba, huku likibadilisha mkakati wake wa kukabiliana na mlipuko unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo).

    Kituo hicho ni miongoni mwa vituo vya kwanza vilivyoanzishwa kwa dharura mjini Bunia baada ya mlipuko wa Ebola kuongezeka mwezi Juni mwaka huu. MSF inasema katika kipindi cha miezi minne iliyopita, wagonjwa 572 wa Ebola wametibiwa katika kituo hicho.

    MSF imeeleza kuwa tangu wakati huo, vituo vingine vya matibabu vimeanzishwa katika maeneo mbalimbali ya mji huo, hivyo kuongeza uwezo wa kupokea na kutibu wagonjwa.

    Kwa mujibu wa shirika hilo, timu za kukabiliana na dharura zitatumwa katika maeneo mengine yaliyoathiriwa na mlipuko huo, ambako mahitaji ya msaada ni makubwa zaidi.

    Shughuli za kufikia jamii na kutoa elimu kuhusu Ebola katika maeneo ya Bigo, Ndibe na Nzere, mjini Bunia, pia zinatarajiwa kukamilika kufikia katikati ya mwezi Novemba.

    Hata hivyo, MSF imesema itaendelea kuunga mkono juhudi za jumla za kukabiliana na Ebola. Shirika hilo limewataka wakazi kuendelea kuwa waangalifu na kuwajulisha mamlaka mara moja wanaposhuku kuwa mtu ameambukizwa ugonjwa huo.

    Takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na chombo kinachosimamia juhudi za kukabiliana na Ebola nchini humo zinaonyesha kuwa mlipuko huo bado unaendelea kuenea.

    Takwimu za hadi Oktoba 18 zinaonyesha kuwa visa vipya 97 vya Ebola vimethibitishwa katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Ituri na Haut-Uélé.

    Katika kipindi hicho hicho, mamlaka zimeripoti vifo 41. Kati ya waliofariki, watu 30 walikufa wakiwa katika jamii, huku 11 wakifariki katika vituo vya matibabu ya Ebola. Aidha, wagonjwa 20 walitangazwa kupona baada ya kupimwa na kuthibitishwa kutokuwa na virusi vya Ebola mara mbili.

    Tangu mlipuko huo uanze, jumla ya watu 9,552 wamethibitishwa kuambukizwa Ebola nchini DR Congo. Kati yao, watu 4,602 wamefariki, sawa na zaidi ya asilimia 48 ya waliothibitishwa kuambukizwa.

    Jimbo la Ituri linaendelea kuwa kitovu cha mlipuko huo, likiwa na karibu robo tatu ya visa vyote vilivyothibitishwa nchini humo.

    Maelezo zaidi:

  10. Trump asema yuko tayari kukutana na Putin na Xi kujadili kupunguza silaha za nyuklia

    C

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari kushiriki mkutano wa pande tatu na Rais wa Urusi Vladimir Putin na Rais wa China Xi Jinping, kufuatia taarifa kwamba Putin amependekeza mkutano maalumu kujadili mustakabali wa Ukraine.

    Hata hivyo, Trump amesema mkutano huo hautajikita katika suala la Ukraine, bali katika kutafuta njia za kuondoa au kupunguza idadi ya silaha za nyuklia duniani.

    Trump amesema, kwa maoni yake, Urusi imeshughulikia suala la Ukraine kwa njia inayofaa.

    Taarifa kuhusu pendekezo la Putin, iliyoripotiwa na gazeti la Wall Street Journal, imezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Ulaya na kulaaniwa vikali nchini Ukraine.

    Trump pia amerejea kumkosoa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, akisema huenda wakati umefika wa mtu mwingine kuongoza mazungumzo ya kutafuta amani.

    Wakati huohuo, vita kati ya Ukraine na Urusi vinaendelea. Mamlaka za Ukraine zimeripoti kuwa watu wanne waliuawa katika mashambulizi ya Urusi usiku uliopita.

    Watu watatu waliuawa katika eneo la Kyiv, huku mwingine akipoteza maisha katika mji wa Zaporizhzhia. Watu wengine 11 walijeruhiwa.

    Mashambulizi hayo yalitokea baada ya Rais Zelensky kutangaza kuwa Ukraine itaendelea kushambulia miundombinu ya mafuta ya Urusi, kama hatua ya kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi yanayoendelea kulenga mitambo ya umeme nchini Ukraine.

    Soma Pia:

  11. Ronaldo asimamishwa kuichezea timu ya taifa ya Ureno kwa siku 30 na kutozwa faini

    d

    Cristiano Ronaldo amesimamishwa kuichezea timu ya taifa ya Ureno kwa siku 30 na kutozwa faini ya euro 255 na Shirikisho la Soka la Ureno (FPF), baada ya kuondoka kambini mwa timu hiyo kufuatia kutokubaliana na kocha Jorge Jesus.

    Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41 na nahodha wa timu ya taifa ya Ureno, aliondoka kambini Julai 9 akiwa amekasirishwa na kutochezeshwa katika mechi ya Ureno dhidi ya Norway. Aidha, alikuwa amearifiwa kuwa hangeanza katika kikosi cha kwanza cha Ureno kwenye mechi iliyofuata dhidi ya Denmark.

    Ronaldo alisema aliamua kuondoka kwa sababu Jorge Jesus hakuheshimu makubaliano waliyokuwa wamefikia. Alimtuhumu kocha huyo kwa kusaliti imani aliyokuwa amemwekea.

    Kwa upande wake, kocha huyo wa Ureno amekanusha kuwapo kwa makubaliano yoyote na Ronaldo, lakini amesema mlango wa kurejea kikosini ulikuwa wazi wakati wowote mchezaji huyo alipotaka kujiunga tena na timu hiyo.

    Ronaldo, ambaye ameshinda tuzo ya Ballon d'Or mara tano, ndiye mchezaji mwenye idadi kubwa zaidi ya mechi za kimataifa katika soka la wanaume, akiwa ameichezea Ureno mara 146.

    Soma pia:

  12. Mshauri wa Zelensky: Waukraine wanakufa kutokana na kupungua kwa ushirikiano wa kijasusi wa Marekani

    F

    Raia wa Ukraine wameuawa kutokana na kile kinachoelezwa kuwa tahadhari zisizo sahihi kutoka Marekani kuhusu mashambulizi ya Urusi, kwa mujibu wa mmoja wa washauri wakuu wa Rais Volodymyr Zelensky.

    Serhii “Flash” Beskrestnov aliiambia BBC kuwa baadhi ya watu wameuawa katika mashambulizi hayo kwa sababu hakukuwa na muda wa kutosha wa kuwaonya wananchi kuhusu mashambulizi ya makombora ya balistiki.

    “Ni hatari... Nafikiri hili ni jambo baya sana... Watu wameuawa,” alisema.

    Mshauri huyo pia alisema kuwa vikwazo vinavyoweka mipaka kwa Ukraine kutumia huduma ya intaneti ya satelaiti ya Starlink bado vinaendelea kutekelezwa.

    Hata hivyo, Ikulu ya Marekani imesema kuwa hakuna mabadiliko yaliyofanyika katika ushirikiano wa kijasusi kati ya Washington na Kyiv.

    Wiki iliyopita, Ukraine ilitangaza kusitishwa kwa ushirikiano wa kijasusi na Marekani. Hatua hiyo ilijiri huku mvutano kati ya Kyiv na utawala wa Rais Donald Trump ukiongezeka kutokana na mkataba wenye utata wa kuingiza mafuta ya Urusi nchini Marekani, hali iliyozorotesha uhusiano kati ya nchi hizo mbili.

    Licha ya Washington kukanusha kuwa kumekuwa na mabadiliko yoyote, baadhi ya watu nchini Ukraine wanahisi kuwa changamoto hizo zinahusiana na mvutano huo.

    Jumatatu asubuhi, Zelensky aliandika kwenye mtandao wa X kuwa mji mkuu wa Kyiv ulikabiliwa na mashambulizi mawili ya makombora ya balistiki usiku uliotangulia.

    “Usiku uliopita, makombora mawili ya balistiki yalishambulia mji mkuu. Shambulizi moja halikutanguliwa na tahadhari yoyote, huku jingine likiwa na tahadhari ya muda mfupi sana kiasi cha kutowawezesha watu kupata hifadhi kwa wakati,” aliandika.

    Soma pia:

  13. Ethiopia yaionya Eritrea dhidi ya kuunga mkono makundi ya upinzani

    g

    Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ameionya Eritrea na kuwatishia kuwakabili na majibu makali iwapo itaendelea kuunga mkono makundi ya upinzani nchini Ethiopia, akiitaja serikali ya Eritrea kuwa “mjumbe wa uharibifu”.

    Katika mahojiano ya hivi karibuni kwa lugha ya Kitigrinya yaliyorushwa na televisheni ya taifa, Abiy amesema Eritrea imegeuka kuwa chombo kinachotumiwa na maadui wa Ethiopia.

    Uhusiano kati ya nchi hizo mbili umedorora kwa kiasi kikubwa, huku uhusiano wa kidiplomasia ukikatika na mvutano ukiendelea kuongezeka. Ethiopia imeishutumu Eritrea kwa kuyaunga mkono makundi yenye silaha yanayopinga serikali yake na kuhusika katika mzozo unaoendelea kaskazini mwa Ethiopia. Eritrea imekanusha madai hayo.

    Mzozo wa kidiplomasia ulizidi kuongezeka baada ya Ethiopia kutangaza kufungwa kwa ubalozi wake mjini Asmara, mji mkuu wa Eritrea, tarehe mosi Oktoba 2026, na kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Eritrea. Eritrea ilijibu kwa kuchukua hatua kama hizo, na hatimaye kukata uhusiano wa kidiplomasia na Ethiopia.

    Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Abiy amesema nchi zinazoiunga mkono Eritrea hazitaweza kuikinga na matokeo ya vitendo vyake.

    “Ninaamini kwa dhati kuwa wale wanaoiunga mkono Eritrea hawawezi kufanya zaidi ya kuipatia risasi, wala hawawezi kutatua matatizo ya Eritrea,” amesema, bila kutaja nchi au wahusika aliokuwa akiwazungumzia.

    Abiy pia ameishutumu Eritrea kwa kuchagua kuwa “uwanja wa michezo wa maadui” badala ya kuwa mshirika katika maendeleo ya kikanda.

    “Hata hivyo, ikiwa itaendelea kupuuza wito wetu, hatari itakuwa kubwa sana,” ameonya.

    Waziri mkuu huyo pia amekosoa hali ya ndani ya Eritrea, akidai kuwa serikali ya nchi hiyo imeshindwa kuweka maendeleo kuwa kipaumbele.

    “Kabla ya uhuru, miji ya Eritrea ilikuwa hai na yenye maendeleo. Leo hii, hata hivyo, imegeuzwa kuwa vijiji,” amesema.

    Abiy ameongeza kuwa Waeritrea wengi wamepoteza fursa za kiuchumi tangu nchi hiyo ipate uhuru, akisema changamoto zinazowakabili zimetokana na kushindwa kwa serikali katika utawala.

    “Watu wa Eritrea, ambao ni wachapakazi na wakarimu, wamekuwa ishara ya uhamiaji na maisha ya dhiki. Mtu akiuliza kwa nini hali hii imetokea, ni kwa sababu serikali iliacha kuwekeza katika maendeleo na ujenzi wa taasisi, na badala yake ikawa chombo cha maadui wa Ethiopia,” amesema.

    Soma Pia:

  14. Jeshi la Iran ladai kudungua droni ya Marekani

    .

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) ladai kuilenga droni ya kijeshi ya Marekani

    Katika taarifa iliyotolewa Jumanne asubuhi, Oktoba 19, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) lilisema kuwa droni ya kijeshi ya Marekani aina ya MQ-9 Centcom "ilizuiwa na kuharibiwa" katika anga juu ya Mlango-Bahari wa Hormuz.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, droni hiyo ilidunguliwa kwa kutumia mfumo mpya wa kisasa wa ulinzi wa anga wa kikosi hicho, ukiwa chini ya usimamizi wa mtandao wa pamoja wa ulinzi wa anga wa Iran.

  15. Miji ya Ufaransa yawa tulivu usiku kucha baada ya amri za kutotoka nje

    Vikosi

    Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sébastien Lecornu, amesema kuwa utekelezaji wa amri maalum za kutotoka nje katika maeneo mbalimbali umechangia kuwepo kwa utulivu usiku uliopita, kufuatia wikendi iliyoshuhudia ghasia na uporaji katika sehemu kadhaa za nchi.

    Amri hizo zilianzishwa katika maeneo ya katikati ya jiji la Paris, ikiwemo Place de la République, ambako waandamanaji walikuwa wamekusanyika mwishoni mwa wiki, pamoja na eneo la biashara la Les Halles.

    Hatua nyingine za kuzuia mikusanyiko na kudhibiti harakati za vijana pia ziliwekwa katika miji ya Marseille, Bordeaux, Nice na Lyon kusini mwa Ufaransa, pamoja na Lille na miji mingine ya kaskazini.

    Lecornu aliwashukuru maafisa wa polisi na askari wa Gendarmerie kwa kusimamia na kutekeleza hatua hizo za usalama, akisema zimechangia kurejesha utulivu katika maeneo yaliyoathirika.

    Aidha, amesema uamuzi kuhusu kuendelea au kutekelezwa kwa amri nyingine za kutotoka nje usiku wa Jumanne utafanywa kulingana na hali ya usalama katika kila eneo.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Lecornu alisema maamuzi hayo yatafanywa "moja kwa moja katika maeneo husika" na mamlaka za mikoa pamoja na mameya wa serikali za mitaa kulingana na mahitaji ya kila eneo.

  16. Lissu ateuliwa hatua ya mwisho na Bunge la Ulaya katika tuzo ya Sakharov

    Lissu

    Bunge la Ulaya limetangaza orodha ya wagombea watatu wa mwisho wa Tuzo ya Sakharov ya Haki za bindamu 2026, kwa kutambua mchango wao katika kutetea haki za binadamu, uhuru na demokrasia.

    Walioteuliwa kufika hatua ya mwisho ni:

    • Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na maafisa wake
    • Tundu Lissu wa Tanzania
    • Taraneh Rahimi na Romina Rahimi wa Iran

    Tuzo ya Sakharov hutolewa kila mwaka kwa watu binafsi au mashirika yanayojitokeza kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi duniani kote.

    Kila mwaka, Bunge la Ulaya hutunuku Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo kwa watu binafsi au mashirika yanayoonyesha ujasiri wa kipekee katika kutetea haki za binadamu, demokrasia na uhuru wa msingi duniani.

    Mwaka 2025, tuzo hiyo ilitolewa kwa Andrzej Poczobut, mwandishi wa habari na mwanaharakati wa jamii ya Wapolandi nchini Belarus, pamoja na Mzia Amaglobeli, mwandishi wa habari kutoka Georgia na mwanamke wa kwanza kutambuliwa kama mfungwa wa kisiasa nchini humo tangu taifa hilo lipate uhuru wake.

    Kwa upande wa tuzo ya mwaka 2026, kamati za Mambo ya Nje na Maendeleo za Bunge la Ulaya zinatarajiwa kupigia kura orodha ya wagombea watatu wa mwisho tarehe 19 Oktoba mjini Strasbourg. Baadaye, Mkutano wa Marais wa Bunge la Ulaya utaamua mshindi wa tuzo hiyo tarehe 22 Oktoba 2026.

    Unaweza kusoma;

  17. Maafisa 13 wa uhifadhi na usalama wakamatwa baada ya vifo vya watu wanne Tanzania

    Mikono ikitiwa pingu

    Polisi nchini Tanzania wamewakamata maafisa 13 wa uhifadhi na usalama kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha watu wanne waliokuwa wakisafirisha mkaa kwa pikipiki katika wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, kaskazini-magharibi mwa nchi.

    Tukio hilo lilitokea majira ya saa 1:00 asubuhi GMT Jumamosi katika kijiji cha Kanyamika, kando ya barabara ya Muleba-Biharamulo, takribani kilomita 140 kutoka mpaka wa Tanzania na Uganda.

    Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera, Blasius Chatanda, watuhumiwa hao ni pamoja na askari watatu wa Hifadhi ya Taifa, (TANAPA), askari sita maalumu wa misitu kutoka Tanzania Forest Services (TFS) na maafisa wanne wasaidizi wa usalama.

    Polisi wamesema uchunguzi unaendelea ili kubaini mazingira halisi yaliyosababisha tukio hilo la vifo.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, doria za maafisa hao zilikutana na watu waliokuwa wakisafirisha mkaa kwa pikipiki 10 ndani ya hifadhi ya misitu. Inadaiwa kuwa watu hao walikataa kukamatwa na kujaribu kuwanyang'anya silaha maafisa hao.

    “Watu hao walikataa kujisalimisha na walijaribu kuwanyang'anya maafisa silaha, hali iliyosababisha mashambulizi yaliyosababisha vifo vya watu wanne,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

    Polisi walieleza kuwa walikamata pikipiki 10, magunia 22 ya mkaa na mapanga matano, miongoni mwa vielelezo vingine. Pia walipata bunduki tatu aina ya AK-47 na gari la serikali lililokuwa limeharibiwa, huku vioo vya mbele na vya pembeni vikiwa vimevunjwa.

    Kamanda Chatanda aliwataka wananchi kuzingatia sheria na kuepuka kujichukulia sheria mkononi wanapokutana na polisi au mamlaka nyingine za utekelezaji wa sheria.

    Taarifa hiyo imezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya wananchi wamehoji iwapo wahusika watawajibishwa na kama matokeo ya uchunguzi yatawekwa wazi kwa umma.

    Mwezi Agosti mwaka huu, polisi waliwakamata askari watatu wa hifadhi kaskazini mwa Tanzania baada ya mtu mmoja kufariki na mwingine kujeruhiwa katika eneo la uhifadhi ambako walidaiwa kuingia kinyume cha sheria.

    Kwa muda mrefu, mashirika ya haki za binadamu nchini Tanzania yamekuwa yakieleza wasiwasi kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaohusishwa na operesheni za utekelezaji wa sheria katika maeneo ya uhifadhi wa mazingira.

  18. Tetesi za soka Jumanne: Liverpool, Manchester United wamuweka Nmecha kwenye rada zao

    Felix Nmecha

    Liverpool na Manchester United ni miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England zinazomfuatilia kiungo wa Borussia Dortmund na timu ya taifa ya Ujerumani, Felix Nmecha.

    Liverpool inatajwa kumuona mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ambaye thamani yake inakadiriwa kuwa pauni milioni 84, kama mbadala wa Alex Scott wa Bournemouth na England.

    Kiungo wa Argentina Emiliano Buendía yuko karibu kukubaliana mkataba mpya na Aston Villa baada ya mazungumzo kuonesha maendeleo mazuri.

    Mlinzi wa kulia wa England Trent Alexander-Arnold anadaiwa kutafakari mustakabali wake Real Madrid kutokana na kutoridhishwa na muda mdogo wa kucheza. Klabu yake ya zamani ya Liverpool ni miongoni mwa timu zinazomfuatilia.

    Kuondoka kwa mshambuliaji chipukizi wa England mwenye umri wa miaka 16, JJ Gabriel, kutoka Manchester United kunatajwa kuwa karibu kutokea. Real Madrid imewasilisha ofa kubwa kwa mchezaji huyo, huku Barcelona na Bayern Munich nazo zikivutiwa naye.

    Manchester United pia inamfuatilia mlinzi wa pembeni wa Brazil mwenye umri wa miaka 23, Wesley, anayeichezea Roma, kabla ya uwezekano wa kumsajili katika dirisha la usajili la Januari.

    Winga wa England mwenye umri wa miaka 18, Rio Ngumoha, ameondoa uvumi wa kuhamia Arsenal na kusema mazungumzo ya kuongeza mkataba wake na Liverpool yanaendelea vizuri.

    Mlinzi wa zamani wa Real Madrid na Hispania, Sergio Ramos, anaangalia uwezekano wa kurejea Ulaya na La Liga, huku Getafe ikionesha nia ya kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 40.

    Manchester United inaweza kulazimika kushindana na Juventus endapo itataka kumteua kocha wa Italia Antonio Conte kuchukua nafasi ya Michael Carrick, iwapo kocha huyo wa United ataachishwa kazi.

    Unaweza kusoma;

  19. Mkosoaji wa Rais wa Rwanda aliyekuwa uhamishoni apatikana akiwa amekatwa kichwa

    Robert Kabera

    Aliyekuwa Sajenti Meja wa Jeshi la Rwanda, ambaye baadaye alijulikana kwa kuwa mkosoaji wa wazi wa Rais Paul Kagame, amepatikana akiwa amekatwa kichwa nchi jirani ya Uganda.

    Robert Kabera, mwenye umri wa miaka 50, alikimbia Rwanda baada ya kushtakiwa kwa madai ya unyanyasaji wa kingono, ambayo aliyakanusha. Aliomba hifadhi nchini Uganda akidai kuwa alikuwa akifuatiliwa kwa misingi ya kisiasa.

    Msemaji wa Polisi wa Uganda, Kituuma Rusoke, alisema Jumatatu kwamba kichwa cha Kabera bado hakijapatikana. Mwili wake ulipatikana na wakazi wa eneo moja lililo pembezoni mwa mji wa Kampala mwishoni mwa wiki.

    Serikali ya Rwanda haijatoa tamko rasmi kuhusu mauaji hayo. Wakosoaji kadhaa wa Kagame wameuawa, ndani ya Rwanda na pia nje ya nchi.

    Mjane wake, Jeanne d'Arc Rwigema Uwizeye, aliiambia BBC idhaa ya Maziwa Makuu kwa ujumbe wa maandishi kwamba sasa ana hofu kuhusu usalama wa familia yake.

    “Inatisha. Nahisi kama nimechanganyikiwa. Mimi na watoto wangu hatuna usalama,” alisema.

    Kwa mujibu wa familia yake, Kabera alikuwa amesafiri kwenda kukagua eneo la ujenzi lililoko takribani kilomita 45 kutoka Kampala kabla ya kuuawa.

    Kabera alikuwa amejijengea umaarufu kama mwanamuziki na mtayarishaji wa maudhui kwenye YouTube. Kituo chake cha YouTube kilikuwa na zaidi ya wafuasi 144,000 na zaidi ya video 800, nyingi zikiwa zikimkosoa Kagame na utawala wake.

    Likizungumzia taarifa za kuuawa kwake, kundi la upinzani lililo uhamishoni la Rwanda National Congress (RNC) lilitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa kina na wa uwazi ili wale wote waliohusika na mauaji hayo wafikishwe mbele ya sheria.

    Katika taarifa iliyochapishwa kwenye mtandao wa X, RNC ilisema:

    "Leo, familia yake inaomboleza, sauti yake imezimwa, na Wanyarwanda wanaoishi uhamishoni wanakabiliwa na swali la kutisha: tunaweza kuwa salama wapi?"

    Kifo chake kimeongeza wasiwasi kuhusu usalama wa wapinzani na wakosoaji wa serikali ya Rwanda wanaoishi uhamishoni katika mataifa mbalimbali.

    Mwaka 2014, Patrick Karegeya, aliyekuwa mkuu wa zamani wa idara ya ujasusi ya Rwanda na mmoja wa waanzilishi wa RNC, alipatikana amefariki katika chumba chake cha hoteli mjini Johannesburg, Afrika Kusini.

    Tukio la kuuawa kwa Kabera limeibua tena mijadala kuhusu usalama wa wakosoaji wa serikali ya Rwanda waliopo nje ya nchi, huku mashirika ya haki za binadamu na makundi ya upinzani yakitaka uchunguzi huru ufanyike ili kubaini waliohusika na tukio hilo.

  20. Vikosi vya Yemen vyashambuliana vikali na wanamgambo wa Houthi mpakani mwa Saudi Arabia

    Houthi

    Vikosi vya serikali ya Yemen na kundi la Wahouthi vimeendelea kushambuliana vikali katika maeneo mbalimbali ya Yemen na mpakani mwa Saudi Arabia, huku taarifa zikieleza kuwepo kwa makumi ya waliouawa na kujeruhiwa.

    Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na pande hizo mbili, vikosi vya serikali vilitekeleza mashambulizi dhidi ya ngome na maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi, huku vikidai kufanikisha operesheni kadhaa za kijeshi na kusababisha hasara kubwa kwa wapiganaji wa kundi hilo.

    Kwa upande mwingine, Wahouthi walitangaza kuwa walifanya mashambulizi kadhaa ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo ya kijeshi na miundombinu ndani ya Saudi Arabia.

    Kundi hilo lilidai kuwa mashambulizi hayo yalikuwa sahihi na yalifanikiwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.

    Taarifa kutoka pande zote zinaonesha kuwa mapigano hayo yamesababisha vifo na majeraha ya watu kadhaa, wakiwemo wapiganaji na wanajeshi, ingawa idadi kamili ya waliopoteza maisha haijathibitishwa kwa uhuru.

    Mapigano haya yanaonesha kuendelea kwa mzozo wa muda mrefu nchini Yemen, ambao umesababisha maelfu ya vifo, mamilioni ya watu kuhitaji msaada wa kibinadamu, na kuathiri utulivu wa eneo la Mashariki ya Kati.

    Unaweza kusoma;