Ardhi zisizo na raia wala serikali: Kwa nini maeneo haya hayana mmiliki?

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati mwingine, matukio yenye athari kubwa katika maisha ya kila siku hutuchochea kutafakari maswali ambayo huenda hayana umuhimu wa haraka, lakini yanavutia sana.
Hilo ndilo lililomtokea Nigel, mmoja wa wasikilizaji waaminifu wa BBC. Akiwa anafuatilia mvutano wa Iran na mzozo wa baharini unaohusu udhibiti wa Mlango wa Hormuz, mawazo yake yaligeukia swali pana zaidi na, kwa hakika, lisilo la dharura: Je, ni sehemu gani ya dunia ambayo haimilikiwi na nchi yoyote?
Wazo hilo lina mvuto wa kipekee. Fikira ya kuwepo kwa eneo lisilo chini ya mamlaka ya taifa lolote huamsha taswira ya sehemu tulivu, iliyo mbali na misukosuko ya siasa za kimataifa, vichwa vya habari vya kusikitisha na changamoto za maisha ya kila siku.
Ili kupata jibu la swali hilo, tulizungumza na Mark Cooper-Jones, mtaalamu wa jiografia na mmoja wa wanachama wa kundi maarufu la YouTube la Uingereza, Map Men.
"Ni sehemu gani ya Dunia haimilikiwi na mtu yeyote? Hili ni swali la kuvutia sana, lakini jibu lake linategemea namna unavyolifasiri," alieleza.
Kwa kuwa sehemu kubwa ya uso wa Dunia imefunikwa na bahari kuliko nchi kavu, bahari ndiyo sehemu ya kwanza inayostahili kuangaliwa.
"Mara tu unapokuwa umbali wa maili 200 za baharini (takriban kilomita 370) kutoka pwani ya nchi yoyote, unaingia kwenye eneo linalojulikana kama bahari kuu (high seas). Kulingana na sheria za kimataifa za bahari, maeneo haya hayamilikiwi na taifa lolote na yanakusudiwa kunufaisha wanadamu wote. Hivyo, watu wa mataifa mbalimbali wanaweza kuvua samaki au kufanya utafiti wa kisayansi huko," anaeleza Mark Cooper-Jones.
Wazo kwamba bahari kuu hazipaswi kuwa hmali ya nchi yoyote si jipya. Asili yake inaweza kufuatiliwa hadi karne ya 17, wakati mwanasheria na mwanafalsafa Mholanzi, Hugo Grotius, alipoweka msingi wa hoja hiyo katika risala yake maarufu ya Mare Liberum (kwa Kilatini, "Bahari Huru").
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika maandiko hayo, Grotius alitetea dhana kwamba bahari zinapaswa kubaki wazi kwa matumizi ya watu wote na zisidhibitiwe na taifa moja pekee. Dhana hiyo imeendelea kuwa msingi muhimu wa sheria za kimataifa zinazotawala matumizi ya bahari hadi leo.
Mantiki yake ilikuwa rahisi: mtu anaweza kumiliki kitu ambacho matumizi yake yanaweza kukimaliza au kukizuia wengine kukitumia. Kwa kuwa bahari ni kubwa mno na rasilimali zake haziwezi kumilikiwa kikamilifu na mtu au taifa moja, haiwezi kuwa mali ya yeyote.
Hivyo ndivyo dhana ya maji ya kimataifa ilivyozaliwa. Na tunazungumzia sehemu kubwa sana ya sayari yetu. Kwa mujibu wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF), takriban asilimia 43 ya uso wa Dunia ni maji ya kimataifa ambayo hayako chini ya mamlaka ya nchi yoyote.
Lakini je, hali hiyo ipo pia katika nchi kavu? Bado kuna maeneo ambayo hayamilikiwi na taifa lolote?
Ili kupata jibu la swali hilo, ni wakati wa kufahamu dhana nyingine inayotokana na Kilatini.
Ardhi isiyomilikiwa na yeyote

Chanzo cha picha, Getty Images
Terra nullius: Ardhi isiyomilikiwa na yeyote
Dhana ya terra nullius, inayomaanisha "ardhi isiyomilikiwa na yeyote", ni zaidi ya istilahi ya kijiografia, anaeleza Cooper-Jones. Ni kanuni iliyotumiwa kuruhusu mataifa kudai maeneo ambayo hayakuwa chini ya mamlaka ya nchi nyingine.
"Hii ni dhana iliyotumiwa kwa njia yenye utata mkubwa, hasa wakati wa upanuzi wa ukoloni. Ingawa maeneo mengi yaliyotwaliwa na wakoloni yalikuwa na wakazi, yalitangazwa kuwa terra nullius kwa sababu wakazi wake hawakuwa wamejipanga katika mifumo ya dola iliyotambuliwa na mataifa ya Ulaya," anasema.
Anaongeza kuwa hata leo kuna ramani zinazoonyesha sehemu kubwa za Afrika kama terra nullius katika kipindi hicho cha kihistoria, licha ya ukweli kwamba bara hilo lilikuwa na jamii nyingi zilizoishi humo.
"Ilikuwa njia ya kusema: 'Hapa si kama Uingereza, Hispania au Austria, hivyo tunaweza kulichukua eneo hili.'"
Leo, terra nullius hurejelea eneo ambalo halijadaiwa na taifa lolote na haliko chini ya mamlaka ya serikali yoyote inayotambuliwa kimataifa.
Hata hivyo, katika dunia ya sasa karibu kila sehemu ya ardhi ina mwenyewe. Yamebaki maeneo machache sana yasiyodaiwa, likiwemo eneo moja kubwa linalojitokeza zaidi kuliko mengine yote.
Marie Byrd Land
Eneo kubwa zaidi duniani lisilodaiwa na taifa lolote liko Antaktika. Lina ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba milioni 1.6 na linajulikana kama Marie Byrd Land, jina lenye historia ya kipekee.
"Ilikuwa Richard Byrd, nahodha wa Jeshi la Wanamaji la Marekani na mpelelezi wa Antaktika, aliyelipa eneo hili jina hilo takriban miaka 100 iliyopita. Mke wake, Marie, alikuwa akimtumia barua alipokuwa akivuka jangwa hilo kubwa la barafu, na Byrd akaamua kulitaja eneo gumu zaidi kulichunguza kwa jina lake. Kwa hiyo, kama kuna mtu ambaye angeweza kudai umiliki wa eneo hili, basi ni Marie Byrd. Lakini alifariki dunia takriban miaka 60 iliyopita," anaeleza Cooper-Jones.
Mwaka 1959, Mkataba wa Antaktika ulitiwa saini, ukisitisha madai ya umiliki wa maeneo mbalimbali katika bara hilo la barafu na kuliweka chini ya mfumo wa kimataifa unaolenga amani na utafiti wa kisayansi pekee.
Hata hivyo, wala mataifa saba yaliyowasilisha madai rasmi ya maeneo ya Antaktika, yaani Argentina, Australia, Chile, Ufaransa, New Zealand, Norway na Uingereza, wala Marekani na Urusi, ambazo zimehifadhi haki ya kuwasilisha madai yao siku za usoni, hazijawahi kudai Marie Byrd Land.
Kwa nini bado halina mwenyewe?
Kwa kiasi kikubwa, jibu linapatikana katika kutengwa kwake kijiografia, anaeleza Cooper-Jones.
"Hata kwa viwango vya Antaktika, eneo hili liko mbali mno. Pwani yake haiko karibu na ncha ya Amerika Kusini, Australia wala eneo jingine lolote linalofikika kwa urahisi. Ni mahali pagumu sana kufika. Karibu hakuna ndege zinazopitia juu yake, isipokuwa zile zinazofanya shughuli za utafiti na uchoraji wa ramani."
Anaongeza kuwa hali hiyo inaweza kubadilika siku zijazo.
"Kwa sasa mambo yanaendelea kama yalivyo. Lakini mtu akigundua rasilimali yenye thamani kubwa sana, au ikiwa barafu za Antaktika zitaanza kuyeyuka kwa kiwango kikubwa, unaweza kuwa na uhakika kwamba eneo hili litageuka haraka kuwa chanzo cha mvutano na madai ya umiliki."
Nje ya Antaktika, karibu kila kipande cha ardhi duniani kinamilikiwa na taifa fulani. Hata hivyo, yapo maeneo mawili ya kipekee yanayounda kitendawili cha kuvutia katika siasa za kimataifa. Kinachovutia zaidi ni kwamba yanaendelea kuwepo si kwa sababu hakuna anayeyataka, bali kwa sababu mataifa yanayohusika yanaona ni bora kuyaacha bila mmiliki ili kulinda maslahi makubwa zaidi yanayopatikana kwingine.
Provide your feedback on BizChat
Bir Tawil: Ardhi ambayo hakuna taifa linalotaka
Bir Tawil liko katika mpaka kati ya Misri na Sudan, na limejikuta katika hali ya kipekee kutokana na uamuzi uliofanywa na Waingereza zaidi ya karne moja iliyopita walipochora mistari miwili tofauti ya mpaka kati ya nchi hizo mbili walizokuwa wameziweka chini ya usimamizi wao.
Mpaka wa kwanza, uliowekwa mwaka 1899, ulikuwa mstari ulionyooka kabisa. "Tulikuwa mabingwa wa kuchora mistari iliyonyooka," anatania Cooper-Jones. Hata hivyo, mwaka 1902, Waingereza waliamua kuweka mpaka mwingine kwa madhumuni ya kiutawala.
"Wakati huu walionyesha ubunifu zaidi na kuuchora katika umbo la herufi S, ukiteremka chini na kisha kupanda tena juu ya mstari wa kwanza," anaeleza Cooper-Jones.
Matokeo yake ni kwamba kila nchi inatambua mpaka tofauti. Katikati ya mistari hiyo miwili kuna Pembetatu ya Hala'ib, eneo lenye ardhi yenye rutuba ambalo, kwa mujibu wa mpaka wa mwaka 1899, ni sehemu ya Misri, lakini kwa mujibu wa mpaka wa mwaka 1902, ni sehemu ya Sudan.
Hata hivyo, mpaka wa pili pia uliacha eneo jingine dogo na lisilo na thamani kubwa kama Hala'ib, linaloitwa Bir Tawil. Hapo ndipo kuna kitendawili chake. Kutokana na namna mpaka huo ulivyochorwa, nchi yoyote itakayodai umiliki wa Bir Tawil italazimika kuachana na madai yake juu ya Pembetatu ya Hala'ib.
Kwa sababu hiyo, Misri na Sudan zote zinadai Hala'ib, lakini hakuna inayotaka Bir Tawil. Matokeo yake, Bir Tawil imebaki kuwa terra nullius kwa vitendo, yaani eneo ambalo halijadaiwa na taifa lolote.
Lakini ingekuwaje kama mtu angeamua kulidai?
Mwaka 2014, mwanamume Mmarekani aitwaye Jeremiah Heaton aliamua kujaribu bahati yake.
"Alikwenda huko, akapandisha bendera katikati ya jangwa na kisha akatokea katika kipindi cha habari kutangaza kwamba sasa yeye ndiye mmiliki wa nchi mpya. Alisema alikuwa amelichukua eneo hilo ili binti yake awe binti mfalme wa kweli. Nafikiri binti huyo lazima aliona aibu sana," anasema Cooper-Jones.
"Sidhani kama Jeremiah alipata utambuzi wowote wa kimataifa kwa taifa lake jipya. Lakini wapo watu wengine ambao wamekwenda mbali zaidi kuliko yeye."
Gornja Siga
Kisa kingine cha terra nullius kinapatikana kati ya Croatia na Serbia. Mpaka rasmi wa kiutawala kati ya nchi hizo mbili uliwekwa mwaka 1945, mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, katika kipindi cha kuundwa kwa Shirikisho la Kisoshalisti la Yugoslavia.
Mpaka huo ulifuata mpaka wa asili, ambao ni Mto Danube. Hata hivyo, uliwekwa kwa kuzingatia mkondo wa mto ulivyoonyeshwa katika ramani za ardhi za Dola ya zamani ya Austria-Hungary za karne ya 19, ambazo hazikuwa zimeboreshwa ili kuendana na mabadiliko ya baadaye.
Lakini, kama mwanafalsafa wa kale Heraclitus alivyoonyesha, mito hubadilisha mikondo yake. Katika kisa hiki, mabadiliko hayo yalikuwa makubwa zaidi kwa sababu mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20 kulifanyika miradi mikubwa ya uhandisi iliyolenga kunyoosha mkondo wa Danube na kurahisisha usafiri wa majini.
"Hali hiyo ingesababisha Croatia kupoteza sehemu kubwa ya ardhi kwenda Serbia. Croatia inasisitiza kuwa mpaka unapaswa kufuata mkondo wa zamani wa mto uliokuwa na mikunjo mingi, ambao sasa kwa kiasi kikubwa umekauka. Serbia, kwa upande wake, inasisitiza kuwa mpaka unapaswa kufuata mkondo wa sasa wa mto," anaeleza Cooper-Jones.
Marekebisho ya mkondo wa Danube yaliacha kipande kidogo cha ardhi kinachoitwa Gornja Siga. Hata hivyo, kama ilivyo kwa Bir Tawil, kukubali umiliki wa eneo hilo kungekuwa na gharama yake. Kwa Croatia, kufanya hivyo kungemaanisha kukubali kwamba mpaka unafuata mkondo mpya wa mto, jambo ambalo lingelazimu kuachana na madai yake katika maeneo mengine yaliyoishia upande wa Serbia.
Matokeo yake ni ya kipekee: kila nchi inadai kuwa kipande hicho kidogo cha ardhi kinapaswa kumilikiwa na nchi nyingine. Hivyo, Gornja Siga nayo imebaki kuwa terra nullius nyingine.
Je, kuna mtu aliyewahi kujaribu kuidai?
Ndiyo.
Mwaka 2015, mwanasiasa wa Czech, Vít Jedlička, alitangaza kuanzishwa kwa taifa analoliita Liberland katika eneo hilo. Liberland ni taifa dogo lisilotambuliwa kimataifa, linalojengwa juu ya falsafa ya uhuru mkubwa wa mtu binafsi na kuingiliwa kidogo kwa serikali katika maisha ya wananchi.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa majaribio mengine ya kuanzisha mataifa katika maeneo yasiyodaiwa, Liberland haijatambuliwa rasmi na jumuiya ya kimataifa na haichukuliwi kuwa nchi huru ndani ya mfumo wa mataifa duniani.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Amejitangaza kuwa rais wa eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 700 na anadai kuwa na zaidi ya raia 1,000," anasema Cooper-Jones.
Hata hivyo, anapoingia katika eneo analoliita nchi yake, mara kwa mara hukamatwa na polisi wa Croatia kwa kuwa mamlaka za nchi hiyo hazitambui madai yake.
Liberland imekuwa ikijaribu kuthibitisha kuwa inakidhi vigezo vya kutambuliwa kama taifa kwa mujibu wa sheria za kimataifa, ikiwemo kuwa na idadi ya watu wa kudumu.
Lakini licha ya madai ya viongozi wake kwamba makazi yanaendelea kuanzishwa katika eneo hilo, hali halisi ni tofauti. Kwa kuwa Gornja Siga iko kwenye mpaka wa nje wa Umoja wa Ulaya, mamlaka za Croatia hudhibiti kwa ukali eneo hilo na kuzuia ujenzi wa makazi ya kudumu.
Matokeo yake, Liberland imeendelea kuwepo zaidi kama taifa la mtandaoni kuliko nchi halisi. Kivitendo, Gornja Siga bado ni terra nullius - ardhi ambayo haijadaiwa rasmi na taifa lolote.
Kwa ujumla, takriban asilimia 43 ya uso wa Dunia haiko chini ya umiliki wa nchi yoyote, lakini karibu eneo lote hilo ni maji ya kimataifa. Maeneo ya nchi kavu yasiyomilikiwa ni machache sana na yanachukua chini ya theluthi moja ya asilimia moja ya uso wote wa Dunia.
Makala hii imechochewa na kipindi cha BBC kiitwacho More or Less.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi
































