Waridi wa BBC: 'Nimeshawahi kunyimwa kazi kisa mimi ni mwanamke'

Chanzo cha picha, Monica Maduhu Makindi
Monica Maduhu Makindi, dereva wa malori makubwa mwenye umri wa miaka 27 kutoka Bariadi, mkoani Simiyu, anasema amewahi kunyimwa nafasi za kazi kwasababu tu ni mwanamke. Licha ya changamoto hizo, ameendelea na kazi ya udereva wa masafa marefu, inayomwezesha kujitegemea, kulea watoto wake wawili na kumsomesha mdogo wake.
"Unajisikia vibaya ukiangalia umepambana, umesoma, umepata leseni kwa shida, halafu unaambiwa hatuajiri wanawake," anasema Monica.
Kwa miaka kadhaa sasa, Monica amekuwa akiendesha malori makubwa yanayosafirisha mizigo katika safari za masafa marefu, ikiwemo safari za kuvuka mipaka ya nchi. Anasema mapenzi yake kwa kazi hiyo yalianza baada ya kuona wanaume wakiendesha malori na kujiuliza kwa nini yeye asingeweza.
"Mbona wanaume wanaendesha? Kwanini mimi nisiweze?" anakumbuka akijiuliza.
Monica alianza kuendesha malori mwaka 2021, lakini safari yake kuelekea katika kazi hiyo ilianza akiwa bado kijana, baada ya kukabiliwa na changamoto za maisha.
Alizaliwa na kukulia Bariadi, ambako anasema alilelewa na bibi yake baada ya kufiwa na mama yake. Kutokana na ugumu wa maisha, alitoroka nyumbani akiwa na umri wa takribani miaka 14, akitafuta namna ya kujikimu.
Baadaye alielekea Dar es Salaam, ambako alifanya kazi za ndani kabla ya kuanza kuvutiwa zaidi na udereva wa malori.
Anasema alipopanda malori akiwa kama abiria, aliona wanaume wakifanya kazi hiyo na akaanza kutamani kuwa dereva mwenyewe. Mkutano wake na mwanamke aliyekuwa akiendesha gari ulimwongezea motisha ya kuamini kuwa wanawake pia wanaweza.
"Yeye ndiye alinitia uchungu, kwanini ukaweza mimi nisiweze, nina nini?" anasema.
Baadaye alipata madereva waliomsaidia kujifunza kuendesha malori. Miongoni mwao ni John, ambaye anamtaja kama mtu aliyemsaidia kupata ujuzi wa udereva.
Kukabiliana na ubaguzi

Chanzo cha picha, Monica Maduhu Makindi
Licha ya kupata uzoefu wa kuendesha malori, Monica anasema bado kuna kampuni ambazo haziko tayari kuajiri wanawake katika kazi hiyo.
Anakumbuka kufika kwenye baadhi ya kampuni akitafuta kazi na kuambiwa wazi kuwa haziwaajiri wanawake.
"Nimeshawahi kunyimwa kabisa kazi, wananiambia sisi hapana, hatuajiri wanawake," anasema.
Pia anasema wakati mwingine watu hutilia shaka uwezo wake kwa sababu ya umbo lake au mwonekano wake wa ujana, bila hata kutathmini uzoefu wake.
Baadhi ya watu wanaomwona kwenye mitandao ya kijamii humuuliza kama kweli yeye ndiye anayeendesha malori anayojipiga nayo picha.
"Hivi kweli wewe unaendesha hiyo gari au huwaga unapigia tu picha?" anasema, akieleza swali ambalo amekuwa akikutana nalo.
Hata hivyo, anaamini mitazamo kuhusu wanawake wanaofanya kazi ambazo zimezoeleka kufanywa na wanaume inaanza kubadilika.
"Sasa hivi inabadilika, kwasababu zamani walikuwa wanaona sisi wanawake hatuwezi," anasema.
Hata wanawake walitilia shaka uwezo wake
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Monica anasema wakati mwingine mashaka kuhusu uwezo wake wa kuendesha lori yamejitokeza hata kutoka kwa wanawake wenzake.
Anakumbuka tukio moja alipokuwa akisafiri usiku katika eneo la Igunga, mkoani Tabora. Alikutana na wanawake watatu waliokuwa wamesimama kando ya barabara wakiwa na mtoto, akaamua kuwapa lifti.
Anasema kwa kawaida huwa hapendi kubeba abiria akiwa peke yake, kwasababu ya kuzingatia usalama wake. Hata hivyo, siku hiyo alikuwa na msaidizi wake, jambo lililomfanya ajisikie salama zaidi kuwasaidia wanawake hao.
Lakini mmoja wa wanawake hao aliposikia kuwa dereva wa lori hilo ni mwanamke, alikataa kupanda.
"Yule mmoja alipoona, 'Eh, eh, mimi sipandi…mwanamke, sipandi,' waligoma kupanda kwenye ile gari," anasimulia Monica.
Tukio hilo lilimuumiza, hasa kwa kuwa nia yake ilikuwa kuwasaidia wanawake wenzake waliokuwa wamekwama barabarani usiku.
"Unasimama kutoa msaada, mtu anakataa, haumuombi hata hela, eti kisa wewe ni mwanamke," anasema.
Monica anasema tukio hilo lilimfanya ajisikie vibaya, akijiuliza kwa nini baadhi ya watu bado wanaamini kuwa mwanamke hawezi kuendesha lori kubwa kwa usalama.
Licha ya kukutana na mitazamo hiyo, anaendelea kufanya kazi yake na anaamini wanawake wana uwezo wa kufanya kazi za udereva wa malori kama wanaume.

Chanzo cha picha, Monica Maduhu Makindi
Safari ya kwanza iliyompa ujasiri
Monica anakumbuka safari yake ya kwanza ya kupeleka mzigo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo ilikuwa na hofu na changamoto nyingi.
Anasema alikabidhiwa lori lililobeba makontena ya mitumba, lakini hakuwa bado ameuzoea vizuri mfumo wa clutch wa gari hilo.
"Nilikuwa natembea natetemeka njia nzima," anakumbuka.
Kwa kuwa hakuwa akiifahamu vizuri njia, aliomba madereva wenzake waliokuwa wakielekea upande huo wa safari wasafiri pamoja naye. Walimsaidia kufika alikokuwa akielekea, na kadiri alivyoendelea na safari, ndivyo alivyozidi kupata uzoefu na kujiamini.
Leo hii, anasema kazi yake ni muhimu kwake kwasababu imemwezesha kusimamia maisha yake na kutimiza majukumu yake ya kifamilia.
"Kazi yangu naipenda sana, inanipa nguvu ya kusimama, na Mungu ndiyo kila kitu," anasema.
Kati ya safari na malezi ya watoto

Chanzo cha picha, Monica Maduhu Makindi
Mbali na changamoto za kazi, Monica pia anapaswa kusawazisha majukumu ya udereva na malezi ya watoto wake wawili.
Anasema safari zake zinaweza kumweka mbali na familia kwa siku nne hadi tano, na wakati mwingine hadi wiki moja.
Anaporejea nyumbani, hujitahidi kutumia muda wake kuwa karibu na watoto wake, kucheza nao na kufurahia muda ambao amekuwa mbali nao.
"Nikiwa nyumbani, unajua watoto… unacheza cheza nao. Watoto wanakuwa wanajisikia furaha sana," anasema.
Monica anasema kazi hiyo pia imemwezesha kumsomesha mdogo wake, ambaye kwa sasa anasoma ngazi ya diploma mkoani Shinyanga, pamoja na kumudu gharama za malezi na elimu ya watoto wake.
"Ninajivunia sana kwa sababu nina mdogo wangu namsomesha mpaka sasa hivi yupo diploma Shinyanga. Mdogo wangu mimi namsomesha mwenyewe. Sina mgongo wa mtu," anasema.
Wito kuhusu usalama na mazingira ya kazi
Monica anasema moja ya changamoto zinazowakabili madereva wanawake ni kukaa kwa muda mrefu kwenye foleni za malori, hasa katika mipaka ya nchi.
Anasema foleni hizo zinaweza kudumu kwa siku kadhaa, huku kukiwa na changamoto ya kupata maeneo ya kuoga na huduma nyingine muhimu.
"Naomba serikali yetu ya Tanzania watusaidie, wanawake tusikae foleni… kwa sababu unakaa foleni hadi siku mbili. Ukiwa mwanamke ni changamoto," anasema.
Pia anakumbuka tukio la gari lake kuharibika usiku katika eneo la Vwawa, mkoani Mbeya. Anasema baadhi ya vijana walimfuata na kumtisha, hali iliyomfanya amwite rafiki yake ili aje kuwa naye hadi gari lilipotengenezwa.
Tukio hilo lilimfanya kutambua umuhimu wa tahadhari za kiusalama kwa madereva, hasa wanapokwama barabarani wakiwa peke yao.
Kwa upande mwingine, anasema jamii inapaswa kutambua mchango wa madereva katika usafirishaji wa bidhaa na mahitaji mbalimbali, huku waajiri wakihakikisha mishahara na posho za safari zinazingatia majukumu yao.
"Kazi ya udereva ni kazi nzuri sana, na ina hela sana, ukiwa na akili," anasema.
Kwa vijana wanaotamani kuingia katika sekta hiyo, Monica anatoa ujumbe wa kutokata tamaa kwa sababu ya changamoto au maneno ya watu.
"Tumeweza, ndiyo. Kila mtu anaweza ukiamua," anasema.
Kwa Monica, udereva wa malori si kazi tu, bali ni njia ya kujitegemea, kutunza familia yake na kuonyesha kuwa uwezo wa kufanya kazi haupaswi kuamuliwa na jinsia ya mtu.



































