Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Saudi yadai kudungua makombora matatu na droni nne za Houthi

Mamlaka ya Ulinzi wa Raia ya Saudi Arabia ilitoa tahadhari za mapema kuhusu tishio la shambulizi katika Mkoa wa Mashariki na wilaya ya Al-Kharj, kabla ya kutangaza baadaye kuwa hatari ilikuwa imeondoka.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Israel yapiga kura huku Iran ikitikisa siasa za uchaguzi

    Raia wa Israel wanapiga kura leo, ikiwa ni uchaguzi mkuu wa kwanza tangu wapiganaji wa Hamas walipofanya mashambulizi Oktoba 7, mwaka 2023.

    Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi, mgawanyiko mkubwa ulijitokeza kati ya Waziri mkuu anayetetea kiti chake Benjamin Netanyahu na mkuu wake wa majeshi juu ya mpango wa kuishambulia Iran kabla ya uchaguzi.

    Waziri wa Ulinzi Israel Katz amelazimika kukanusha taarifa kadhaa kwamba Waziri mkuu Netanyahu ana nia ya kumfukuza kazi Jeneral Eyal Zamir iwapo atashinda awamu nyingine madarakani.

    Mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi huo Gadi Eisenkot, amemtupia lawama Netanyahu kutumia kitisho cha Iran, kujinufaisha kisiasa.

    Wizara ya Sheria ya Marekani imefungua mashtaka mapya dhidi ya Mkurugenzi wa zamani wa FBI, James Comey, ikimtuhumu kuvujisha taarifa za usalama wa taifa kwa mwandishi wa habari, muongo mmoja uliopita.

    Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja kwa utawala wa Rais Donald Trump kujaribu kumshtaki James Comey, ambaye alifukuzwa kazi na Rais Trump mwaka 2017.

    Akijibu tuhuma dhidi yake James Comey amesema bado hana hatia na kwamba bado haogopi. Amekuwa mkosoaji wa Rais.

    Wanasheria wake awali walidai kuwa utawala umekuwa ukiendesha mashtaka yenye misingi ya siasa dhidi yake.

    Soma Zaidi:

  2. Trump atilia shaka uadilifu wa uchaguzi wa Lula nchini Brazil

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amedokeza kuwa uchaguzi wa urais uliofanyika Brazil Jumapili iliyopita haukuwa huru na wa haki, akidai kuwa ulionekana kama uchaguzi mwingine uliochezewa matokeo.

    “Sikuegemea upande wowote, lakini ulionekana kama uchaguzi mwingine ambao matokeo yake yalipangwa,” alisema Trump Jumatatu, akizungumzia uchaguzi ambao Rais wa sasa wa mrengo wa kushoto, Luiz Inácio Lula da Silva, alimshinda mgombea wa mrengo wa kulia, Flávio Bolsonaro.

    “Uchaguzi unapaswa kuwa huru na usioacha nafasi ya mashaka, lakini kwa mtazamo wangu, hali ilionekana kuwa mbaya sana,” aliongeza Trump, bila kutoa ushahidi wowote mahususi kuunga mkono madai yake.

    Hata hivyo, alipoulizwa kama alikusudia kuchukua hatua yoyote kuhusu uchaguzi huo, Trump alisema: “Mimi siiongozi Brazil. Ninaiongoza Marekani.”

    Trump pia alisema kuwa ana uhusiano mzuri sana na Lula, lakini akaeleza kuwa muda wa uchaguzi kuendelea zaidi ya ilivyotarajiwa ulikuwa wa kushangaza sana.

    Lula alipata ushindi wa kihistoria kwa kuwa mgombea wa kwanza tangu Brazil irejeshe utawala wa kidemokrasia kushindwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi, kisha kurejea na kushinda katika duru ya pili.

    Kwa mujibu wa Tume ya Juu ya Uchaguzi ya Brazil (TSE), baada ya kura zote kuhesabiwa, Lula alipata asilimia 51.7 ya kura, huku Bolsonaro akipata asilimia 48.2.

    Tofauti ya kura kati ya wagombea hao wawili ilikuwa takribani kura milioni 4.3.

  3. Wanawake na wasichana wabeba mzigo mkubwa wa vita duniani, ripoti ya UN yaonya

    Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama imebaini kuwa wanawake na wasichana wanaendelea kubeba mzigo mkubwa wa vita na migogoro ya silaha duniani, huku idadi ya vifo vyao ikiongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni.

    Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo mjini New York, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Nyaradzayi Gumbonzvanda, amesema dunia imekuwa ikiruhusu hali hiyo kuendelea licha ya kuwa vita na migogoro vinaweza kuzuiwa.

    Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya raia 37,000 waliuawa katika migogoro ya silaha duniani mwaka 2025, ambapo mmoja kati ya kila watu wanne waliouawa alikuwa mwanamke au msichana. Umoja wa Mataifa unasema kiwango hicho kimeongezeka maradufu ikilinganishwa na mwaka 2021.

    Ripoti hiyo inaeleza kuwa angalau wanawake na wasichana 25 huuawa kila siku kutokana na migogoro ya silaha, huku zaidi ya wanawake na wasichana milioni 750 duniani wakiishi ndani ya umbali wa kilomita 50 kutoka maeneo yenye mapigano.

    Gumbonzvanda amesema kwa wanawake wengi wanaoishi katika maeneo hayo, vita si jambo la kutazama kwenye runinga au simu, bali ni sehemu ya maisha yao ya kila siku.

    "Vita vinafuata wanawake hadi katika wodi za wazazi, mashuleni, majumbani na sehemu ambazo familia zinapaswa kuwa salama," alisema.

    Ripoti hiyo pia imeonyesha athari kubwa kwa afya ya uzazi katika maeneo ya migogoro. Umoja wa Mataifa unasema mwanamke anayejifungua katika nchi iliyoathiriwa na vita ana uwezekano mara tano zaidi wa kufariki kutokana na matatizo ya uzazi kuliko mwanamke anayejifungua katika nchi iliyo imara.

    Katika Ukanda wa Gaza, ripoti hiyo inasema uharibifu wa hospitali na vituo vya afya ya uzazi umechangia kupungua kwa asilimia 41 kwa watoto wanaozaliwa hai na kuongezeka kwa asilimia 300 kwa visa vya mimba kuharibika.

    Kwa upande wa elimu, wasichana katika nchi zinazokumbwa na migogoro wana uwezekano mara mbili na nusu zaidi wa kukosa masomo kuliko wenzao katika mazingira ya kawaida. Umoja wa Mataifa umeitaja Afghanistan kuwa miongoni mwa maeneo yenye mgogoro mkubwa zaidi wa haki za wanawake duniani, ambapo mamilioni ya wasichana bado hawaruhusiwi kupata elimu.

    Ripoti hiyo imeeleza pia ongezeko kubwa la ukatili wa kingono unaohusishwa na migogoro ya silaha. Mwaka 2025, Umoja wa Mataifa ulithibitisha visa 9,788 vya ukatili wa kingono unaohusiana na vita, idadi ambayo ni zaidi ya mara mbili ya ile ya mwaka uliotangulia.

    Nchini Haiti pekee, visa vilivyoripotiwa vya ukatili wa kingono viliongezeka kwa asilimia 163, huku wanawake na wasichana wakitajwa kuwa miongoni mwa walengwa wakuu wa aina hiyo ya ukatili.

    Licha ya changamoto hizo, Umoja wa Mataifa umesema wanawake wanaendelea kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kujenga amani kwa kusuluhisha migogoro ya kijamii, kusaidia manusura wa ukatili na kuunganisha jamii wakati taasisi za serikali zinaposhindwa kufanya kazi.

    Hata hivyo, ripoti hiyo imebaini kuwa wanawake bado hawapewi nafasi ya kutosha katika maamuzi ya amani. Mwaka 2025, wanawake walikuwa asilimia tano tu ya wajadiliano katika michakato 57 ya amani duniani.

    UN Women imezitaka serikali na jumuiya ya kimataifa kuongeza ushiriki wa wanawake katika mazungumzo ya amani, kuheshimu sheria za kimataifa na kuchukua hatua za haraka kulinda raia dhidi ya madhara ya vita.

    "Vita ni uchaguzi wa binadamu, na amani pia ni uchaguzi wa binadamu," alisema Gumbonzvanda. "Dunia haihitaji taarifa zaidi kuhusu mateso ya raia. Inahitaji hatua za kuyamaliza."

    Soma Pia:

  4. Saudi yadai kudungua makombora matatu na droni nne za Houthi

    Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen umesema Jumanne ulidungua na kuharibu makombora ya masafa marefu na ndege zisizo na rubani zilizorushwa na waasi wa Houthi kuelekea maeneo mawili ya Saudi Arabia.

    Kwa mujibu wa muungano huo, Wahouthi walirusha makombora matatu ya balestiki kuelekea Mkoa wa Mashariki wa Saudi Arabia na ndege nne zisizo na rubani kuelekea kusini mwa nchi hiyo.

    Mamlaka ya Ulinzi wa Raia ya Saudi Arabia ilitoa tahadhari za mapema kuhusu tishio la shambulizi katika Mkoa wa Mashariki na wilaya ya Al-Kharj, kabla ya kutangaza baadaye kuwa hatari ilikuwa imeondoka.

    Saudi Arabia imeongeza mashambulizi yake dhidi ya Wahouthi tangu mwezi uliopita, baada ya kundi hilo kudhibiti maeneo ya kimkakati kando ya pwani ya Bahari ya Shamu nchini Yemen na kusonga kuelekea Mlango wa Bab el-Mandeb, njia muhimu ya usafirishaji wa kimataifa kwa wazalishaji mafuta wa Ghuba.

    Mapigano mapya kati ya pande hizo mbili yamevuruga makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyodhaminiwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2022, ambayo kwa kiasi kikubwa yalikuwa yamesitisha mashambulizi kati ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia unaounga mkono serikali inayotambuliwa kimataifa ya Yemen, na Wahouthi, ambao wanadhibiti mji mkuu wa Sanaa.

    Soma Zaidi Hapa:

  5. Hujambo na karibu katika matamgazo yetu mubashara.