Iran yawanyonga watu watatu waliokamatwa wakati wa maandamano
Mamlaka ya mahakama nchini Iran imetekeleza hukumu ya kifo dhidi ya watu watatu waliokamatwa kufuatia maandamano yaliyotikisa mji wa Karaj mwezi Januari, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mizan, linalohusishwa na idara ya mahakama nchini humo.
Walionyongwa ni Hassan Deoband, Hamid Kazemi na Reza Zanganeh.
Kwa mujibu wa Mizan, watatu hao walipatikana na hatia ya kushirikiana na Israel na Marekani katika shughuli za kiusalama, pamoja na kushiriki kwa silaha kwenye maandamano ya Januari 8 na 9. Pia walituhumiwa kuhusika katika uharibifu na uchomaji wa maeneo ya umma pamoja na miundombinu ya umeme.
Shirika hilo limesema hukumu za kifo dhidi yao zilitekelezwa Jumapili baada ya kuidhinishwa na Mahakama ya Juu ya Iran. Mali zao pia zimeamriwa kutaifishwa.
Mizan imeongeza kuwa watu wengine 10 walikamatwa kuhusiana na kesi hiyo, huku washtakiwa wengine wakihukumiwa vifungo vya kati ya miaka mitano na 10 jela.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikosoa mara kwa mara matumizi ya hukumu ya kifo nchini Iran, hasa katika kesi zinazohusiana na maandamano na masuala ya usalama wa taifa.
Soma pia:





















