Gadi Eisenkot: Mfahamu jenerali mstaafu anayemkosesha usingizi Netanyahu

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, huenda akakabiliwa na changamoto kubwa ya kusalia madarakani baada ya uchaguzi wa Jumanne, Oktoba 27.

Kura za maoni zinaonyesha kuwa muungano wa chama chake cha Likud pamoja na vyama vya mrengo mkali wa kulia na vya Kiyahudi wenye msimamo mkali wa kidini unaweza kushindwa kupata wingi wa viti bungeni.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa ni kuibuka kwa Gadi Eisenkot, mwenye umri wa miaka 66 na mkuu wa zamani wa majeshi ya Israel, ambaye amejitokeza kama mpinzani mkubwa wa kisiasa dhidi ya Netanyahu, kiongozi ambaye ametawala siasa za Israel kwa sehemu kubwa ya miongo mitatu iliyopita.

Ingawa ni mgeni kiasi katika siasa, Eisenkot alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2022 kupitia chama cha National Unity, kabla ya kukihama kutokana na kile alichosema kuwa tofauti za kiitikadi.

Mwaka jana, alijitenga na viongozi wengine wa upinzani na kuanzisha chama chake cha mrengo wa kati kiitwacho Yashar (linalomaanisha "mnyoofu" au "mwaminifu"). Tangu wakati huo, amefanikiwa kujijengea nafasi kama mshindani mkuu wa Netanyahu katika uchaguzi huu.

Netanyahu amekuwa akikabiliwa na tuhuma za ufisadi ambazo amekuwa akizikanusha, pamoja na ukosoaji kuhusu namna serikali yake ilivyoshughulikia mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023. Pia amekosolewa kutokana na mpango wake wa mageuzi ya mahakama uliosababisha maandamano makubwa nchini Israel.

Uamuzi wa Gadi Eisenkot kuwania uongozi dhidi ya Benjamin Netanyahu ulichochewa pia na mkasa mkubwa wa kifamilia alioupitia wakati wa vita vya Gaza.

Gal Eisenkot, mwana wa mwisho wa Gadi Eisenkot, aliuawa akiwa vitani mwaka 2023 alipokuwa akihudumu katika jeshi la Israel huko Gaza.
Maelezo ya picha, Gal Eisenkot, mwana wa mwisho wa Gadi Eisenkot, aliuawa akiwa vitani mwaka 2023 alipokuwa akihudumu katika jeshi la Israel huko Gaza.

Mwanawe wa mwisho kati ya watoto watano, Gal Eisenkot, aliyekuwa sajini meja katika jeshi la Israel, aliuawa mwezi Desemba 2023 kufuatia mlipuko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza. Wakati huo alikuwa akishiriki operesheni ya kutafuta miili ya mateka wawili wa Israel waliotekwa na Hamas katika mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kifo cha mwanawe kilimgusa Eisenkot binafsi na kumfanya kuwa sauti inayosikika zaidi katika mjadala kuhusu mwelekeo wa vita na uongozi wa nchi. Kwa wafuasi wake, uzoefu huo ulimpa uelewa wa moja kwa moja wa gharama ya vita kwa familia za Waisraeli.

Leo, Eisenkot anatambulika si tu kama jenerali mstaafu wa jeshi la Israel, bali pia kama baba aliyempoteza mwanawe vitani na mwanasiasa anayejaribu kujijenga kama mbadala wa Netanyahu katika uchaguzi wa kwanza wa kitaifa tangu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023.

Eisenkot amesema bado hajapata nguvu ya kupekua vitu vya mwanawe, ambavyo vilivyorudishwa kwake vikiwa vikiwa katika masanduku kadhaa anayoyatunza nyumbani kwake mjini Herzliya, mji wa pwani ulioko kaskazini mwa Tel Aviv.

Amesema masanduku hayo hayafunguliwa tangu yalipowasili, yakibeba kumbukumbu nzito za msiba wa kumpoteza mwanawe katika vita vya Gaza. Hadi wa leo, bado hajapata ujasiri wa kuyapitia.

"Bado sijayafungua. Nimekuwa nikiendelea kuahirisha kufanya hivyo," alisema.

Kifo cha mwanawe Gal, pamoja na vifo vya wapwa wake wawili wakati wa vita vya Gaza, kilichangia kuimarisha azma ya Eisenkot kuingia kwenye siasa za ushindani.

"Siwezi kurudisha nyuma muda. Nitafanya kila niwezalo kuenzi sadaka aliyotoa Gal," alisema.

Eisenkot amekuwa akisisitiza kuwa Netanyahu na serikali yake wanapaswa kuwajibika kwa jinsi walivyoshughulikia mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7.

Baada ya mashambulizi hayo, alijiunga na serikali ya vita iliyoundwa kwa lengo la kuonyesha umoja wa kitaifa. Hata hivyo, alijiuzulu mwaka 2024, akimtuhumu Netanyahu kwa kushindwa kuchukua hatua za haraka kuwezesha kuachiliwa kwa mateka waliotekwa na Hamas.

Netanyahu ameendelea kuyakanusha madai hayo.


Eisenkot (kulia) aliwahi kuwa Mkuu wa Wafanyakazi wa Jeshi kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 katika serikali ya Netanyahu.
Maelezo ya picha, Eisenkot (kulia) aliwahi kuwa Mkuu wa Jeshi kuanzia mwaka 2015 hadi 2019 katika serikali ya Netanyahu.

Netanyahu anadai kuwa Eisenkot alipinga baadhi ya operesheni muhimu za kijeshi huko Gaza alipokuwa mjumbe wa baraza la mawaziri la vita.

"Nakumbuka Gadi Eisenkot na wengine walivyokuwa wakisema akiwa bado tuko Gaza. Walitaka tufikie makubaliano, tuwaokoe mateka na tuondoke Gaza," alisema Netanyahu.

Kwa mujibu wa Netanyahu, msimamo huo ungezuia Hamas kushindwa kabisa na kuwawezesha viongozi wake kuendelea kubaki madarakani.

Eisenkot amepinga madai hayo na kumtaka Netanyahu kuweka wazi kumbukumbu za mikutano ya baraza la mawaziri la vita pamoja na matokeo ya kura zilizopigwa.

Vipaumbele vya Eisenkot

Wachambuzi wa siasa za Israel wanasema kwamba msiba wa kumpoteza mwanawe ulimpa Eisenkot dhamira mpya ya kisiasa na kuongeza azma yake ya kuingia katika uongozi wa taifa.

Lengo lake si tu kuimarisha chama chake cha Yashar, bali pia kujijenga kama mbadala mkuu wa Netanyahu na kuongoza muungano mpya wa serikali.

Kama Netanyahu, Eisenkot anaamini kuwa Hamas lazima iondolewe madarakani Gaza. Amesema analenga kuhakikisha kundi hilo linapoteza uwezo wake wa kijeshi na kisiasa ndani ya miezi 18.

Hata hivyo, jenerali huyo mstaafu amekuwa na mtazamo tofauti kuhusu mustakabali wa Wapalestina. Hamuungi mkono kwa sasa mpango wa mataifa mawili, akisema mazingira ya sasa hayatoi msingi wa utekelezaji wake.

Badala yake, ametaka kuwepo kwa mfumo mpya wa mahusiano kati ya Israel na Mamlaka ya Palestina, akisisitiza kuwa Wapalestina wanapaswa kujiongoza wenyewe.

"Mamlaka ya Palestina inapaswa kuwaongoza Wapalestina. Sitaki kufanya hivyo mimi," alisema.

.

Eisenkot ameahidi kukabiliana na vitendo vya vurugu vinavyofanywa na baadhi ya walowezi wa Kiyahudi dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.

Ingawa anaunga mkono upanuzi wa baadhi ya makazi makubwa ya walowezi, amepinga mipango yenye utata ya kuongeza makazi katika maeneo mengine, hususan mradi wa kupanua makazi katika eneo la E1 karibu na Jerusalem Mashariki.

Hivi karibuni, Eisenkot pia ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya walowezi wenye misimamo mikali wanaohusika na mashambulizi dhidi ya Wapalestina. Kauli hiyo imeonekana kama juhudi za kupunguza mvutano unaozidi kuongezeka katika Ukingo wa Magharibi na kujibu ukosoaji wa kimataifa kuhusu makazi ya walowezi.

Ahadi ya uchunguzi kuhusu Oktoba 7

Miongoni mwa ahadi zake kuu za kampeni ni kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu mashambulizi ya Hamas ya Oktoba 7, 2023, ili kubaini kama kulikuwa na mapungufu ya kiusalama au ya kiuongozi ndani ya serikali ya Israel.

Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti madai kwamba Netanyahu alipokea maonyo kuhusu uwezekano wa shambulio kutoka Gaza kabla ya mashambulizi hayo kutokea.

Netanyahu amekanusha madai hayo, amefungua kesi dhidi ya gazeti lililoyachapisha kwa mara ya kwanza, na amepinga wito wa kufanyika kwa uchunguzi unaolenga wajibu wa serikali yake.

Kwa Eisenkot, suala la uwajibikaji kuhusu matukio ya Oktoba 7 limekuwa mojawapo ya nguzo kuu za kampeni yake na tofauti muhimu kati yake na Netanyahu katika uchaguzi huu.

Eisenkot pia aliahidi kuanzisha mpango wa dharura wa kushughulikia tatizo la Waisraeli wenye ujuzi wa hali ya juu kuondoka nchini, na kuhimiza kuwasili kwa wahamiaji wapya.

Pia anataka kuondoa kanuni zinazotoa msamaha kwa jamii za Wayahudi wa mrengo wa kihafidhina (ultra-Orthodox) na Waarabu wa Israel dhidi ya utumishi wa kijeshi—suala ambalo ni nyeti sana nchini humo.

Juhudi za awali za kupanua wigo wa utumishi wa kijeshi, ikiwemo lile lililofanywa na serikali ya Netanyahu, yalisababisha maandamano kutoka kwa jamii za Wayahudi wa mrengo wa kihafidhina.

Asili yake na taaluma ya kijeshi

Kura za maoni zinaonyesha ushindani mkali sana kati ya Gadi Eisenkot na Benjamin Netanyahu, ingawa hakuna hata mmoja anayetarajiwa kupata wingi kamili wa kura.

Gadi Eisenkot alizaliwa mjini Tiberias na kukulia Eilat, mbali na ngome kuu za siasa za Israel za Jerusalem na Tel Aviv. Ni mtoto wa wahamiaji wa asili ya Morocco waliowasili Israel katika miaka ya 1950 na kuishi maisha ya kawaida.

Ametokea katika jamii ya Wayahudi wa Mizrahi, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihisi kutengwa kisiasa. Baadhi ya wachambuzi wanaamini historia yake inaweza kumsaidia kuvutia wapiga kura ambao hapo awali walimuunga mkono Netanyahu.

Tofauti na Netanyahu, aliyekulia katika mazingira ya tabaka la juu jijini Jerusalem, Eisenkot amejijengea jina kupitia taaluma yake ya kijeshi.

Alijiunga na jeshi la Israel akiwa na umri wa miaka 18 na kulitumikia kwa takriban miaka 40, hadi kufikia cheo cha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel kati ya 2015 na 2019.

Katika taaluma yake ya kijeshi, aliongoza operesheni za Israel katika Ukingo wa Magharibi wakati wa Intifada ya Pili. Pia alihusishwa na mkakati wa kijeshi unaojulikana kama Dahieh Doctrine, unaosisitiza matumizi makubwa ya nguvu za kijeshi dhidi ya maeneo yanayotumiwa kushambulia Israel.

Licha ya tofauti zake za kisiasa na Netanyahu, Eisenkot hajawahi kupinga hadharani operesheni ya kijeshi ya Israel dhidi ya Hamas baada ya mashambulizi ya Oktoba 7, 2023.

Ingawa si mwanasiasa wa mrengo wa amani, ameonekana kwa wengi kama kiongozi makini na mwenye uzoefu mkubwa wa usalama wa taifa.

Changamoto ya kuunda serikali

Benjamin Netanyahu

Pamoja na kuongezeka kwa umaarufu wake, Eisenkot anatarajiwa kuhitaji washirika wa kisiasa ili kuunda serikali, kwani chama chake hakitabashiriwi kupata wabunge wa kutosha kuongoza peke yake.

Hapo ndipo Netanyahu anaonekana kuwa na faida ya uzoefu. Katika chaguzi kadhaa zilizopita, amefaulu mara nyingi kuunda serikali za muungano na kubaki madarakani.

Wafuasi wa Netanyahu wanadai Eisenkot angehitaji uungwaji mkono wa vyama vya Waarabu ili kuunda serikali. Eisenkot amesema hatarajii kuvijumuisha serikalini, ingawa hajaondoa uwezekano wa kushirikiana navyo bungeni katika juhudi za kuiondoa serikali ya Netanyahu.

Kwa mujibu wa wachambuzi, nguvu kubwa ya Eisenkot katika uchaguzi huu ni historia yake ya kijeshi. Nchini Israel, jeshi linaaminiwa na kuheshimiwa kwa kiwango kikubwa, jambo linalomfanya aonekane kama mpinzani mwenye uzito dhidi ya Netanyahu.