Moja kwa moja , Hisa za makampuni makubwa ya teknolojia zaporomoka baada ya uchaguzi Marekani

Hisa za makampuni makubwa ya teknolojia zaporomoka Marekani na Asia, huku ushindi wa Democrats ukizidisha hofu kuhusu mustakabali wa uwekezaji katika AI.

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Papa Leo XIV aanza ziara Amerika Kusini wiki tatu baada ya kufanyiwa upasuaji wa saratani ya mapafu

    n

    Papa Leo XIV anaanza ziara ndefu katika mataifa ya Amerika Kusini, wiki tatu tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa saratani ya mapafu.

    Ziara hiyo inajumuisha kile kinachotarajiwa kuwa kurejea kwake kwa furaha nchini Peru, ambako aliwahi kuhudumu kama kasisi kwa miaka mingi.

    Vatican imesema hakuna hatua zozote za ziada zinazochukuliwa kuhusiana na afya ya Papa huyo. Imemtaja kuwa ni mtu mwenye umri wa miaka 71 aliyefanyiwa upasuaji, na si mtu mwenye tatizo la kiafya la kudumu.

    Ni Papa Leo mwenyewe aliyefichua mwezi uliopita kuwa madaktari waligundua uvimbe kwenye mapafu yake wakati wa uchunguzi wa kawaida wa afya. Uvimbe huo uliondolewa pamoja na sehemu ya chini ya pafu lake la kulia. Baadaye, timu yake ya madaktari ilithibitisha kuwa saratani hiyo haikuwa imesambaa katika sehemu nyingine za mwili.

    Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Roma kabla ya safari hiyo, ambayo itamfikisha Uruguay, Argentina na Peru, msemaji wa Vatican alisema Papa Leo ana nguvu nyingi za kimwili na ana shauku kubwa kuhusu ratiba ya ziara hiyo.

    Alisema ratiba hiyo ilithibitishwa binafsi na Papa bila kufanyiwa mabadiliko yoyote.

    Ujumbe wa Vatican kupitia ziara hiyo ni kwamba tatizo la kiafya alilopata Papa lilikuwa la muda mfupi na sasa amerejea katika shughuli zake za kawaida, anasema Profesa Massimo Faggioli wa Chuo Kikuu cha Villanova, akizungumza na BBC.

    Anasema Papa amekuwa na ratiba yenye shughuli nyingi tangu kurejea kazini baada ya upasuaji huo.

    "Tumemwona katika siku hizi akitoa hotuba, akipokea wageni na kushiriki shughuli mbalimbali. Anaonekana kuwa katika hali nzuri sana. Hilo lilikuwa muhimu," amesema.

    Ziara hiyo itaanzia Uruguay, ambako idadi ya Wakatoliki imepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni. Nchi hiyo inatarajia kupokea ziara ya kwanza ya Papa baada ya takribani miongo minne.

    Baadaye, Leo ataelekea Argentina, nchi alikozaliwa Papa Francis, mtangulizi wake.

    Vatican imesema kuwa katika mataifa yote matatu, Papa atakutana na manusura wa unyanyasaji wa kingono uliofanywa na viongozi wa Kanisa Katoliki. Suala hilo lilitawala mjadala wakati wa ziara ya Papa Francis nchini Chile na Peru mwaka 2018.

    Profesa Faggioli anaona ziara hiyo kama njia ya Papa Leo kuimarisha tena uhusiano wa upapa na Amerika Kusini baada ya kipindi cha Papa Francis, ambaye baadhi ya ziara zake katika eneo hilo zilikumbwa na changamoto.

    Anaamini Papa Leo ana mtazamo mpana kuhusu umoja wa nchi za Amerika kama bara moja.

    "Demokrasia zinakabiliwa na changamoto huko, kwa hiyo kuna mambo mengi anayoweza kuyazungumzia," anasema.

    Hata hivyo, anasema swali kubwa ni lini Papa Leo atatembelea Marekani. Anasema hakuna shaka kuwa Papa anataka kufanya ziara hiyo, lakini bado haijulikani kama atakwenda wakati Donald Trump akiwa bado rais wa Marekani.

    Soma pia:

  2. Trump asaini agizo la kuzuia marais wajao kubadilisha Ofisi ya Oval

    n

    Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini agizo la kiutendaji analosema litalizuia marais watakaomrithi kufanya mabadiliko fulani katika Ofisi ya Oval ndani ya Ikulu ya White House.

    Trump, ambaye awali alikuwa mfanyabiashara mkubwa wa majengo, amebadilisha kwa kiasi kikubwa muonekano wa ofisi hiyo rasmi ya rais katika muhula wake wa pili, ikiwemo kuongeza mapambo mengi ya rangi ya dhahabu.

    "Tunaitangaza kuwa eneo la urithi wa kitaifa, na hakuna mtu atakayeruhusiwa kuligusa, kulibomoa au kuliharibu kwa ajili ya kujenga kitu chenye umbo tofauti kidogo, kwa sababu tu ya mawazo ya watu wasio na busara," Trump aliwaambia waandishi wa habari Alhamisi.

    Agizo hilo linakuja miezi kadhaa baada ya Trump kubomoa jengo lote la East Wing la Ikulu ya White House katika mradi ambao umekabiliwa na changamoto za kisheria.

    Mradi huo pia haukupata idhini ya Bunge la Marekani. Hata hivyo, ujenzi umeendelea, huku mipango ikiwa ni kubadilisha eneo hilo kuwa ukumbi mpya mkubwa wa hafla.

    Kwa sasa, marais wa Marekani wana mamlaka ya kufanya baadhi ya mabadiliko katika Ikulu ya White House, lakini miradi mikubwa huhitaji idhini ya Bunge.

    Agizo hilo la kiutendaji, alilolitia saini Trump Alhamisi, linaitangaza Ofisi ya Oval pamoja na baadhi ya vyumba vinavyoizunguka kuwa eneo la urithi wa kitaifa.

    Hata hivyo, waraka huo unasema agizo hilo "halizuii mamlaka ya Rais kubadilisha mapambo ya eneo hilo, kuchagua samani au kufanya marekebisho ya kawaida ya kiutendaji na kiusalama, mradi yasiharibu kwa kiasi kikubwa muundo wake wa kihistoria au sifa zake za usanifu."

  3. Rais wa Paraguay Santiago Peña ajiuzulu baada ya benki kubwa nchini kufilisika

    ,

    Rais wa Paraguay, Santiago Peña, amejiuzulu baada ya kuanguka kwa moja ya benki kubwa zaidi nchini humo.

    Peña alitangaza uamuzi huo wakati bunge likiendelea na mchakato wa kumuondoa madarakani kutokana na uhusiano wake na Benki ya Ueno, ambayo kufilisika kwake kulisababisha karibu nusu ya wananchi wa Paraguay kushindwa kupata akiba zao.

    Katika ujumbe wa video kwa taifa, Peña aliomba radhi kwa wananchi wa Paraguay akisema haikuwa nia yake kamwe kuvunja imani waliyoonyesha kwake.

    Wabunge wanamtuhumu kwa matumizi mabaya ya fedha za malipo ya uzeeni na kuficha matatizo yaliyokuwa yakiikumba benki hiyo kabla ya kuporomoka kwake.

    Shinikizo dhidi yake liliongezeka baada ya chama chake mwenyewe kuungana na upinzani kupiga kura dhidi yake bungeni.

    Kuanguka kwa Benki ya Ueno kumesababisha hasira kubwa miongoni mwa wananchi, huku mamilioni wakikosa uwezo wa kupata fedha zao walizoweka kama akiba.

    Wapinzani wa kisiasa wanasema serikali ilipuuzia dalili za hatari kwa muda mrefu na kushindwa kulinda maslahi ya wateja wa benki hiyo.

    Kujiuzulu kwa Peña kunafungua kipindi kipya cha sintofahamu ya kisiasa nchini Paraguay huku viongozi wakitarajiwa kujadili hatua za mpito na namna ya kurejesha imani ya wananchi katika mfumo wa fedha wa nchi hiyo.

  4. Kenya: Mahakama kutoa hukumu kwa Paul Mackenzie katika kesi ya vifo vya Shakahola

    n

    Mahakama nchini Kenya inatarajiwa kutoa hukumu dhidi ya mhubiri Paul Nthenge Mackenzie na washitakiwa wenzake katika kesi inayohusiana na vifo vya wafuasi wa dhehebu lake katika msitu wa Shakahola, iliyolishtua wengi nchini Kenya.

    Mackenzie alipatikana na hatia ya mauaji ya watu 191, wakiwemo watoto 190, huku waendesha mashtaka wakitaka ahukumiwe kifo.

    Mhubiri huyo na viongozi wengine 29 wa dhehebu lake walipatikana na hatia katika hukumu iliyosomwa na Jaji Diana Mochache katika Mahakama ya Mombasa Jumatatu, Oktoba 19.

    Mahakama ilieleza kuwa Mackenzie aliwashawishi wafuasi wake kuamini kuwa wangekutana na Yesu mbinguni iwapo wangefunga hadi kufa.

    Mafundisho yake pia yalipinga elimu rasmi na huduma za kisasa za afya, akizihusisha na maovu.

    Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takriban saa nane, Jaji Mochache alieleza jinsi mafundisho ya Mackenzie yalivyowafanya wafuasi wake kujitenga na jamii na kuamini kuwa kufa kwa njaa kungewawezesha kupata wokovu wa kiroho.

    Uchunguzi ulioanza mwaka 2023 katika msitu wa Shakahola ulisababisha kupatikana kwa miili ya zaidi ya watu 400, wengi wao wakiwa wamefariki kutokana na njaa.

    Pia unaweza kusoma:

  5. California yabadilisha hukumu za kifo kwa wafungwa wote kuwa kifungo cha maisha

    n

    Gavana wa California, Gavin Newsom, ameanzisha mchakato wa kubadilisha hukumu zote za kifo katika jimbo hilo kuwa kifungo cha maisha gerezani bila uwezekano wa kuachiliwa kwa msamaha.

    "Kwa sasa tunaweza kuwaacha wahalifu hawa wafe bila kujulikana, huku tukiendelea kuwakumbuka na kuwaenzi waathiriwa milele," alisema Newsom katika barua yake.

    Uamuzi wa kubadilisha hukumu za wafungwa waliohukumiwa kifo una uzito zaidi wa kiishara katika jimbo ambalo halijatekeleza hukumu ya kifo tangu mwaka 2006. Hata hivyo, wataalamu wanasema hatua hiyo inaweza kuokoa mamilioni ya dola zinazotumika kila mwaka katika gharama za kesi mahakamani.

    Ni wafungwa 13 pekee ambao wameuawa tangu wapiga kura waliporejesha adhabu ya kifo mwaka 1978.

    Uamuzi huo unakuja wakati Newsom, kiongozi wa chama cha Democratic katika jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini Marekani, akitajwa miongoni mwa wanaoweza kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2028.

    Newsom, ambaye muda wake wa uongozi unamzuia kuwania muhula mwingine, anamalizia miezi yake ya mwisho madarakani. Mwanachama mwenzake wa Democratic, Xavier Becerra, anatarajiwa kumrithi baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Jumanne.

    Katika barua yake, Newsom alisema anatumia mamlaka aliyopewa na Katiba ya Marekani kutoa msamaha kwa kubadilisha hukumu za wafungwa hao kuwa kifungo cha maisha bila uwezekano wa kuachiliwa huru.

    "Baada ya takribani miaka 30 katika utumishi wa umma, nimeelewa mipaka ya kile ambacho serikali inaweza kutekeleza kwa haki," alisema Newsom.

    "Nimechukua hatua hii kwa sababu ninaamini kwa dhati kuwa mauaji yanayoidhinishwa na serikali hayaendani na misingi ya California, yanadhoofisha misingi ya mfumo wetu wa sheria na yanapunguza utu wa kila mmoja wetu."

    Kwa muda mrefu, California imekuwa na idadi kubwa zaidi ya wafungwa waliohukumiwa kifo nchini Marekani.

    Mwaka 2019, Newsom aliamuru kusitishwa kwa utekelezaji wa hukumu ya kifo katika jimbo hilo.

    Newsom amesema adhabu ya kifo ni kinyume na misingi yake ya maadili na ameiomba Mahakama Kuu ya jimbo hilo kuyahifadhi maisha ya wafungwa wote 548 wanaosubiri kunyongwa.

    Ana mamlaka ya kubadilisha takriban asilimia 40 ya hukumu hizo, huku zilizobaki zikihitaji idhini ya mahakama.

  6. Ikulu ya Marekani yakanusha taarifa za Hegseth na Rubio kujiuzulu

    m

    Rais Donald Trump amesema hana mpango wa kumwondoa Pete Hegseth kama Waziri wa Ulinzi, licha ya madai kwamba vita vya Iran vilichangia pakubwa kushindwa kwa chama cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika siku ya Jumanne.

    Akizungumza na shirika moja la Marekani Trump alisema bado ana imani waziri huyo.

    Kauli hiyo imejiri wakati mbunge wa Republican, Thomas Massie, akisema atawasilisha tena hoja ya kumng'oa Hegseth madarakani wakati Baraza la Wawakilishi litakapokutana tena.

    Massie amesema anaamini kuna wabunge wa Republican wa kutosha kuunga mkono hoja hiyo.

    Hata hivyo, Trump amekiri kwamba huenda ikawa rahisi kumtafuta mtu mwingine wa kuongoza Pentagon kabla ya chama cha Democratic kuchukua udhibiti wa Bunge mwezi Januari.

  7. Hisa za makampuni makubwa ya teknolojia zaporomoka baada ya uchaguzi Marekani

    m

    Mabilioni ya dola katika thamani ya soko yamefutika kutoka kwa makampuni makubwa ya teknolojia nchini Marekani na Asia, baada ya soko la hisa kuyumba kufuatia uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, ulioibua hofu ya kupungua kwa kasi ya maendeleo ya teknolojia ya Akili Unde (AI).

    Hisa za makampuni mbalimbali katika sekta ya teknolojia na AI zilishuka kwa kasi baada ya wagombea wa chama cha Democratic kupata ushindi katika uchaguzi ambao kampeni zake zilijikita katika kupunguza kasi ya maendeleo ya AI.

    Faharasa ya Nasdaq Composite, inayojumuisha kwa kiasi kikubwa makampuni ya teknolojia, ilifungwa ikiwa imeshuka kwa zaidi ya asilimia 5.5. Kwa mujibu wa takwimu za Dow Jones, hasara hiyo ilifuta takriban dola trilioni 2.5 za Marekani katika thamani ya soko.

    Faharasa nyingine kuu za hisa nchini Marekani pia zilipata hasara kubwa, katika siku yake mbaya zaidi tangu mwaka 2025.

    Kushuka huko kwa hisa kumeongeza wasiwasi uliokuwepo kuhusu iwapo uwekezaji mkubwa unaofanywa katika teknolojia ya AI utaleta faida iliyotarajiwa.

    Barani Asia, faharasa zinazojumuisha kwa kiasi kikubwa makampuni ya teknolojia zilishuka kwa kasi Ijumaa asubuhi, huku hisa za kampuni zinazotengeneza chip za kompyuta na vifaa vingine vinavyowezesha teknolojia ya AI zikiporomoka.

    Nchini Japan, faharasa ya Nikkei 225 ilikuwa imeshuka kwa asilimia sita katika saa za mwanzo za biashara. Hisa za kampuni ya Kioxia inayotengeneza chip za kuhifadhi kumbukumbu zilipoteza zaidi ya asilimia 12.6, huku mpinzani wake Tokyo Electron akishuka kwa asilimia 9.5.

    Nchini Korea Kusini, hisa za kampuni ya SK Hynix zilishuka kwa zaidi ya asilimia 11.5, huku Samsung ikipoteza karibu asilimia 10 ya thamani yake.

    Mporomoko huo katika soko la Seoul uliifanya faharasa ya Kospi kushuka kwa zaidi ya asilimia 8.5, hali iliyosababisha kusimamishwa kwa muda kwa biashara ya hisa kupitia utaratibu maalumu unaolenga kuzuia wawekezaji kuuza hisa kwa hofu.

    Katika kampeni zao kote Marekani, wagombea wa Democratic waliahidi kupunguza kasi ya ujenzi wa vituo vikubwa vya kuhifadhi na kuchakata data pamoja na maendeleo ya AI. Kulikuwa na mapendekezo kadhaa yaliyowasilishwa kwa wapiga kura katika maeneo mbalimbali nchini humo, yakilenga kuzuia au kudhibiti ujenzi wa vituo hivyo muhimu katika kuendesha teknolojia hiyo.

    Chama cha Democratic kilishinda viti katika Seneti na Baraza la Wawakilishi katika uchaguzi wa Jumanne, na hivyo kupata udhibiti wa Bunge la Marekani kwa kipindi kilichosalia cha urais wa Donald Trump.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump aliwalaumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kushuka kwa soko la hisa.

    “Soko la hisa limepitia mojawapo ya siku mbaya zaidi katika historia, kutokana na matokeo ya uchaguzi,” alisema.

    “Kumbukeni, hawakuwa Republicans, bali Dumocrats. Hata hivyo, msiwe na hofu. Hivi karibuni, kwa njia moja au nyingine, tutakuwa wakubwa na wenye nguvu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. TUIFANYE MAREKANI IWE KUU TENA!”

    Baadhi ya wanasiasa wa Democratic wamesema sekta ya AI imekua kwa kasi kubwa bila kuwepo kwa mifumo ya kutosha ya udhibiti na usimamizi. Wameahidi kutumia nguvu yao mpya bungeni kushughulikia suala hilo.

    “Wamarekani hawataki matajiri wachache wanaotawala sekta kubwa ya teknolojia waharibu mazingira, waangamize ajira na kuhatarisha mustakabali wa binadamu. TUNATAKA KUSITISHWA KWA MUDA UJENZI WA VITUO VYA DATA NCHINI KOTE, SASA,” alisema Seneta wa Democratic Bernie Sanders katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X siku ya Alhamisi.

    Hisa za makampuni yanayohusika kwa kiasi kikubwa na ujenzi na uendeshaji wa vituo vya data vya AI, yakiwemo yanayotengeneza chip na vifaa vya kisemikondakta, zilishuka kwa kasi Alhamisi. Hali hiyo imeonyesha wasiwasi wa wawekezaji ambao ulikuwa tayari umeanza kuongezeka.

    Hisa za kampuni ya Nvidia zilishuka kwa zaidi ya asilimia tisa, na kufuta zaidi ya dola bilioni 400 katika thamani yake ya soko.

    Watengenezaji wengine wa chip pia waliathirika. Hisa za AMD na Micron zilishuka kwa zaidi ya asilimia 17 kila moja. Hisa za Intel zilipoteza asilimia 10.3, huku kampuni ya SanDisk inayotengeneza vifaa vya kuhifadhi data ikishuhudia hisa zake zikishuka kwa zaidi ya asilimia 22.

    Faharasa ya Philadelphia Semikondakta, inayofuatilia mwenendo wa makampuni 30 makubwa yanayohusika na uzalishaji wa vifaa vya kisemikondakta, ilishuka kwa zaidi ya asilimia 12.

    Hisa za makampuni ya Elon Musk, SpaceX na Tesla, pia ziliporomoka kwa asilimia nane na karibu asilimia 11 mtawalia. Kushuka huko kulifuta zaidi ya dola bilioni 300 katika thamani ya soko ya makampuni hayo siku ya Alhamisi.

    Musk alikuwa ametumia karibu dola milioni 450 kuunga mkono kampeni za wagombea wa Republican, zikiwemo angalau dola milioni 45 kumsaidia Ken Paxton katika kinyang'anyiro cha kiti cha Seneti nchini Texas. Hata hivyo, Texas ilikuwa miongoni mwa majimbo yaliyogeuka na kuunga mkono Democratic katika wimbi kubwa la ushindi wa chama hicho usiku wa Jumanne.

    Kwa ujumla, makampuni saba makubwa ya teknolojia yanayojulikana kama Magnificent Seven, yakiwemo Apple, Nvidia na Tesla, yalipoteza jumla ya dola trilioni moja katika thamani ya soko ndani ya siku moja ya biashara.

    Kushuka kwa hisa hizo pia kuliathiri faharasa nyingine kuu za soko la Marekani. Faharasa ya S&P 500 ilifungwa ikiwa imeshuka kwa asilimia 4.4, huku Dow Jones Industrial Average ikifuta faida iliyopata Jumatano na kufungwa ikiwa imeshuka kwa zaidi ya asilimia 3.4.

    Kushuka kwa Nasdaq Composite kulikuwa kukubwa kiasi cha kuiingiza katika kile wachambuzi wa masoko wanachokiita kiwango cha marekebisho ya soko. Hali hii hutokea pale thamani ya faharasa au kampuni inaposhuka kwa angalau asilimia 10 kutoka kiwango chake cha juu cha hivi karibuni.

  8. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 06/11/2026.