Anthony Zurcher: Uchaguzi wa katikati ya muhula zimemdhoofisha Trump ila bado ana nguvu

Donald Trump
Maelezo ya picha, Donald Trump
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Wakati sherehe za ushindi wa chama cha Democratic ziikuwa zikiendelea baada ya matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, akaunti rasmi ya Ikulu ya White House ilichapisha picha kwenye mtandao wa X ikimuonyesha Rais Donald Trump akiwa na sura ya ukali, amesimama nyuma ya meza yake katika ofisi ya Rais ya The Oval.

"Trump bado ndiye rais wenu," Ilisema ujumbe ulioambatana na picha hiyo kwenye X.

Huu ni ujumbe ambao Trump anataka kuuwasilisha kwa Wamarekani kwamba bado ni rais mwenye mamlaka kamili na ambaye hajayumbishwa na pigo kubwa la kisiasa alilopata katika uchaguzi huo.

Aidha, hata bila kudhibiti Bunge la Congress, marais wa Marekani bado wana mamlaka makubwa wanayoweza kuyatumia. Na Trump tayari ameonyesha kuwa yuko tayari kuvuka mipaka ya mamlaka aliyopewa na Katiba kama rais.

Ujumbe huo haukuzingatia ukweli kwamba muda wa Trump kuongoza Marekani unaendelea kuyoyoma, na kadri siku zinavyosonga, itazidi kuwa vigumu kwake kutumia mamlaka aliyonayo.

Hatua nyingi muhimu alizochukua zimekuwa kupitia maagizo ya rais badala ya sheria zinazopitishwa na Bunge la Congress, ambalo sasa linadhibitiwa na Democrats.

Hatua hizo zinajumuisha ushuru wa bidhaa alioweka dhidi ya washirika na wapinzani wa Marekani, pamoja na operesheni za kijeshi zilizofanyika Venezuela na Iran.

Nchini Marekani, Trump pia alipunguza kwa upande mmoja matumizi ya fedha za serikali katika taasisi mbalimbali, licha ya matumizi hayo kuwa tayari yameidhinishwa na Congress.

Hata baada ya chama cha Democratic kupata wingi wa viti katika Baraza la Wawakilishi na Seneti, Trump bado anaweza kuendelea kutekeleza hatua kama hizo, na nyingine zaidi, katika miaka miwili iliyosalia ya muhula wake.

Na iwapo Democrats watajaribu kuzuia hatua hizo kupitia sheria, Katiba ya Marekani inampa Trump njia yenye nguvu ya kukabiliana nao ambayo ni mamlaka ya kupiga kura ya turufu au veto, dhidi ya sheria zinazopitishwa na Congress.

Uamuzi huo unaweza kubatilishwa tu iwapo wabunge watapata wingi wa kura ulio juu zaidi ya ule ambao Democrats watakuwa nao.

.

Ingawa Trump bado ana mamlaka hayo haimaanishi kuwa atakuwa na utashi wa kisiasa wa kuyaendeleza. Kutakuwa na wabunge wengi wapya wa Democrats ambao wataingia Washington wakiwa wameahidi kupinga kila hatua atakayoichukua.

Ila huenda vikwazo vikubwa zaidi kwake visitokane na upinzani wa Democrats, bali kutoka ndani ya chama chake mwenyewe cha Republican.

Makamu wa rais, JD Vance
Maelezo ya picha, Makamu wa rais, JD Vance
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa kipindi cha miaka miwili, Rais Trump amekuwa na ushawishi mkubwa katika chama cha Republican, akihakikisha kuwa wabunge wa chama chake katika Congress na maeneo mbalimbali nchini Marekani wanafuata msimamo wake. Amefanya hivyo kwa kutumia mchanganyiko wa zawadi za kisiasa na vitisho vikali.

Hata hivyo, sasa kuna dalili kwamba ushawishi wake huo umeaanza kupungua.

Baadhi ya wabunge wa Republican wameanza kuonyesha utayari wa kuikosoa serikali yake kwa namna ambayo miezi michache iliyopita wengi wao wasingethubutu kufanya.

Makamu wake wa Rais, JD Vance, aliandika ujumbe mrefu kwenye mitandao ya kijamii akilaumu vita dhidi ya Iran, ambavyo Trump alianzisha kwa kushirikiana na Israel, kuwa sababu ya kushindwa vibaya kwa Republican katika uchaguzi wa Jumanne.

"Ikiwa unataka kusema kuwa vita hivyo vilikuwa na manufaa na kwamba kupoteza udhibiti wa Seneti kwa kipindi cha miaka sita ijayo kulikuwa na thamani yake, basi sema hivyo," Vance aliandika.

"Lakini kila mtu anajua sababu iliyotufanya tushindwe. Na mazungumzo yoyote ya kweli kuhusu tunakokwenda kuanzia hapa lazima yaanze na suala hilo."

Tayari uvumi umeanza kusambaa kwamba baadhi ya maafisa katika timu ya utawala wa Trump wanaweza kuondolewa madarakani.

Kulingana na shirika la habari la CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, rais amewauliza washauri wake wa karibu iwapo anapaswa kumwondoa Waziri wa Ulinzi, Pete Hegseth, mmoja wa watu waliohusika kwa kiasi kikubwa katika kuandaa vita hivyo. Trump amekanusha taarifa hizo.

Hatua hiyo inafanana na ile ya Rais wa zamani George W. Bush wa kumwondoa Donald Rumsfeld, aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuanzishwa kwa vita vya Iraq, kufuatia kushindwa vibaya kwa chama chake katika uchaguzi wa katikati ya muhula mwaka wa 2006. Huo ndio ulikuwa uchaguzi wa mwisho ambao Democrats walipata wingi wa viti katika Congress kwa kiwango kinacholingana na ushindi wao wa Jumanne.

Bunge la Congress
Maelezo ya picha, Bunge la Congress

Jumanne usiku, Trump alichapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii na kuzungumza na vyombo mbalimbali vya habari, akieleza moja kwa moja jinsi atakavyoshughulikia chama cha Democratic. Wakati mmoja aliahidi kushirikiana nao, lakini muda mfupi baadaye akatishia kutumia mamlaka yake ya turufu au veto kuzuia miswada ya sheria inayoungwa mkono na Democrats.

"Nitashirikiana na Democrats, isipokuwa kama wataamua kufanya mambo yenye kuleta madhara. Lakini nina mamlaka ya kupiga kura ya turufu," alisema Trump.

Mwaka wa 1995, miezi michache baada ya Republican kuchukua udhibiti wa Congress kupitia ushindi mkubwa wa uchaguzi uliowaacha Democrats katika hali kama hiyo, Rais wa wakati huo Bill Clinton, akiwa amejikuta katika mazingira ya kisiasa ya upweke na kujitetea, alisisitiza kuwa bado alikuwa na umuhimu na mamlaka ya kutumia.

"Bado rais ana nafasi na umuhimu wake hapa," alisema kwa msisitizo.

Clinton, ambaye wakati huo alikuwa katika muhula wake wa kwanza, alikuwa bado na muda wa kurejesha ushawishi wake wa kisiasa, na alifanikiwa kuchaguliwa tena mwaka uliofuata.

Hata hivyo, kwa Trump, muda hauko upande wake.

Lakini kadri siku zinavyosonga, rais huyo anayependa kuwa kitovu cha mijadala ya kisiasa nchini Marekani anaweza kujikuta akipoteza mamlaka yake na, ushawishi wa kisiasa.