Tundu Lissu: Safari ya Siku 577 kutoka kukamatwa hadi siku ya uamuzi

Aprili 9, 2025 – Novemba 06, 2026
Kesi ya Uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, ni moja ya kesi kubwa za kisiasa nchini Tanzania ikirindima kwa zaidi ya mwaka mmoja. Lissu alikamatwa Mbinga, mkoani Ruvuma tarehe 9 Aprili 2025.
Mpaka sasa zimetimia siku 577 (mpaka siku ya hukumu Novemba 6, 2026) , na kati ya siku hizo, kumekuwa na matukio mengi yaliyovuta hisia za umma ndani na nje ya Tanzania.
Tunaendelea kukumbusha kutoka kukamatwa kwake katikati ya mkutano wa kisiasa, mgomo wake wa kula, hadi uamuzi wake wa kujitetea mwenyewe bila mawakili wengine, akiwahoji ana kwa ana mashahidi wa siri wa Jamhuri.
Haya ndiyo yaliyotokea kwenye safari hiyo ya takribani miezi 19
Aprili 9, 2025: Kukamatwa Mbinga
Jioni ya Aprili 9, 2025, baada ya Lissu kuhutubia mkutano wa CHADEMA mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, katika kampeni ya chama iliyokuwa ikiongozwa na kauli ya "No Reforms, No Election" yaani Bila Mageuzi, Hakuna Uchaguzi.
Polisi waliingilia mkutano huo na kuwatawanya wafuasi kwa mabomu ya machozi. Lissu alikamatwa na kupelekwa kituo cha polisi Mbinga. Mashirika ya haki za binadamu yalidai kuwa hakuelekezwa mara moja sababu za kukamatwa kwake na kwamba alizuiliwa bila mawasiliano kwa muda. Baadaye alisafirishwa hadi Dar es Salaam.
CHADEMA na mashirika ya kisheria yalipinga namna ya kukamatwa kwake, yakisema kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kisheria na haki zake za msingi. Serikali, kwa upande wake, imeendelea kulinda uhalali wa mchakato wa kisheria dhidi yake.
Aprili 10: Mashtaka ya uhaini
Siku iliyofuata, yaani Aprili 10, Lissu alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Alikabiliwa na shtaka moja la uhaini chini ya kifungu cha 39(2)(d) cha Penal Code pamoja na mashtaka matatu ya uchapishaji wa taarifa za uongo chini ya sheria ya makosa ya mtandao.
Shtaka la uhaini ndilo lililokuwa zito zaidi kwa sababu ni kosa lisilokuwa na dhamana na linaweza kupelekea adhabu ya kifo iwapo mtu atapatikana na hatia.
Katika hatua hiyo, Lissu hakupata nafasi ya kujibu shtaka la uhaini kwa sababu Mahakama ya Kisutu haikuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa kiwango hicho; ilibaki na jukumu la taratibu za awali kabla ya kesi kupelekwa Mahakama Kuu.
Aprili: Mabishano kuhusu mahakama ya mtandao
Katika hatua zilizofuata, mahakama ilielekeza baadhi ya taratibu za awali zifanyike kwa njia ya mtandao. Hapo ndipo mzozo mkubwa ulipoanza.
Lissu alikataa kushiriki katika baadhi ya vikao vya mtandao akisisitiza kwamba, kwa kesi yenye uzito wa uhaini, alipaswa kufikishwa mahakamani yeye mwenyewe.
Mnamo Aprili 24 na Aprili 28, hakushiriki katika vikao vya mtandao, huku upande wa utetezi ukisisitiza umuhimu wa Lissu kusikilizwa akiwa mahakamani.
Wakati huo pia kulikuwa na msuguano mkubwa nje ya mahakama kati ya polisi na wafuasi wa CHADEMA waliokwenda kufuatilia kesi hiyo.

Mei: Mgomo wa kula
Mvutano kuhusu usikilizwaji kwa njia ya mtandao ulifikia hatua nyingine pale Lissu alipoanza mgomo wa kula akiwa kizuizini, akipinga kuendelea kufanyiwa vikao kwa njia ya video badala ya kufikishwa mahakamani.
Hatua hiyo iliongeza shinikizo kwa mahakama. Mei 6, Mahakama ya Kisutu ikaamuru Lissu afikishwe mwenyewe mahakamani Mei 19 badala ya kushiriki kwa njia ya mtandao.
Mei 19: Lissu anaonekana mahakamani
Mei 19, 2025, Lissu alifikishwa katika Mahakama ya Kisutu kwa mara ya kwanza tangu kukamatwa kwake.
Aliingia akiwa amevalia fulana yenye ujumbe "No Reforms, No Election", akionyesha ishara ya ushindi na kuwataka wafuasi wake wasiogope.
Jamhuri iliomba muda zaidi kukamilisha uchunguzi, na Lissu akaendelea kusalia mahabusu.
Siku hiyo pia ikawa ya kimataifa baada ya wanasiasa na wanaharakati kutoka nchi jirani kujaribu kufika Tanzania kufuatilia kesi hiyo.
Mei: Wanaharakati wa Kenya na Uganda wakamatwa
Katika harakazti za kufuatilia kesi hiyo, mwanaharakati wa Kenya Boniface Mwangi na mwanasheria wa Uganda Agather Atuhaire walikamatwa nchini Tanzania walipokuwa wamekuja kufuatilia kesi ya Lissu.
Tukio hilo liliongeza shinikizo la kimataifa kuhusu namna Tanzania inavyoshughulikia kesi hiyo na nafasi ya waangalizi wa kimataifa.
Mei 30: Kesi yafikishwa Umoja wa Mataifa
Mawakili wa Lissu waliwasilisha malalamiko kwa UN Working Group on Arbitrary Detention, wakiomba chombo hicho kitathmini uhalali wa kukamatwa na kuwekwa kwake kizuizini.
Hii ilikuwa hatua muhimu kwa sababu kesi hiyo haikubaki tena kuwa suala la ndani la Tanzania pekee; ilianza kufuatiliwa katika ngazi za kimataifa za haki za binadamu.
Agosti 2025: Kesi ya Lissu yaingia hatua ya Ushahidi
Mchakato wa kesi ulipoendelea, suala la ulinzi wa mashahidi likawa moja ya mambo makubwa yaliyokuwa yakibishaniwa.
Agosti 4, 2025, Mahakama Kuu iliidhinisha hatua za kuwalinda baadhi ya mashahidi wa Jamhuri. Chini ya utaratibu huo, mashahidi waliolindwa wangeweza kutumia majina ya bandia na utambulisho wao kufichwa. Pia kulikuwa na masharti kuhusu kutotangazwa kwa taarifa zinazoweza kuwabainisha.
Kwa upande wa Lissu, suala hili lilikuwa nyeti sana kwa sababu alikuwa akikabiliwa na shtaka ambalo adhabu yake inaweza kuwa kifo. Hoja ya msingi ya utetezi ilikuwa: mtuhumiwa anawezaje kukabiliana kikamilifu na shahidi ambaye hawezi kumuona au kumtambua?
Agosti 18: Kuripoti moja kwa moja kesi kwapigwa marufuku
Mahakama pia iliweka zuio la kuripoti moja kwa moja mwenendo wa kesi hiyo.
Agosti 18, 2025, Mahakama ya Kisutu ilipiga marufuku live streaming, live broadcasting na usambazaji wa moja kwa moja wa maudhui ya kesi kwenye mitandao ya kijamii, hatua ambayo ilielezwa kuwa inalenga kulinda utambulisho wa mashahidi.
Lissu alipinga hatua hiyo akisema ingeathiri uwazi wa mchakato wa haki.

Septemba: Kesi yafika Mahakama Kuu
Baada ya taratibu za awali, kesi ilifikishwa Mahakama Kuu.
Septemba 22, 2025, Lissu alisomewa rasmi shtaka la uhaini na akalikana. Alikubali baadhi ya taarifa za msingi kuhusu yeye mwenyewe, lakini akapinga kwamba matamshi yaliyotajwa na Jamhuri yalifikia kiwango cha kosa la uhaini.
Katika hatua hii Lissu pia aliomba baadhi ya viongozi wakuu wa serikali waitwe kama mashahidi wa upande wake, wakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Jamhuri ilieleza kuwa ilikuwa na mpango wa kuita takribani mashahidi 30, huku Lissu akitarajia kuwa na takribani mashahidi 15.
Oktoba 6, 2025: Ushahidi waanza kusikilizwa
Oktoba 6, 2025, baada ya takribani miezi sita tangu kukamatwa kwake, kesi ilianza kusikilizwa kwa ushahidi katika Mahakama Kuu.
Hii ilikuwa hatua ya muhimu zaidi katika kesi hiyo.
Shahidi wa kwanza wa Jamhuri alikuwa ASP George Wilbard Bagyemu, ambaye alitoa ushahidi kuhusu uchunguzi wa matamshi ya Lissu na video iliyotumika kama sehemu ya msingi wa kesi.
Lissu, ambaye alikuwa akijiwakilisha mwenyewe, alianza kupinga sehemu ya ushahidi huo akisema baadhi ya maelezo hayakuhusiana moja kwa moja na shtaka la uhaini.
2025–2026: Mashahidi wanaolindwa
Kadiri kesi ilivyoendelea, baadhi ya mashahidi wa Jamhuri walipewa ulinzi maalumu.
Mashahidi hao walipewa majina ya bandia na, katika baadhi ya mazingira, walitoa ushahidi wakiwa wamefichwa wasionekane na umma. Mmoja wao alijulikana kama P6.
Februari 2026, shahidi huyo alipokuwa akichunguzwa na Lissu, alikanusha kuwa aliwahi kutishiwa au kutishwa kwa sababu ya kutoa ushahidi.
Lakini suala la mashahidi wa siri halikuishia hapo.
Februari 2026: Mzozo wa "shahidi wa kizimba"
Kesi iliporudi mahakamani Februari 9, 2026 baada ya kusimama kwa muda, kulizuka mzozo mwingine kuhusu shahidi aliyelindwa kwa utambulisho wa P11.
Upande wa mashtaka ulitaka shahidi huyo kutoa ushahidi akiwa ndani ya eneo maalumu lililofichwa, "kizimba" ili asiweze kutambuliwa.
Lissu alipinga vikali utaratibu huo, akisema ni vigumu kwake kukabiliana na shahidi ambaye hawezi kumuona vizuri, hasa katika kesi ya uhaini ambayo inaweza kupelekea adhabu ya kifo.
Hili likawa moja ya mapambano makubwa zaidi ya kisheria kuhusu haki ya mtuhumiwa kukabiliana na mashahidi wanaomshutumu.
Februari 24, 2026: Ushahidi mpya wakataliwa
Mzozo mwingine mkubwa ulitokea pale Jamhuri ilipojaribu kuingiza ushahidi mpya katika kesi hiyo.
Mahakama Kuu ilikataa ombi hilo, hasa jaribio la kuingiza ushahidi wa ziada kutoka kwa shahidi ambaye tayari alikuwa ameshatoa ushahidi.
Jamhuri haikukubaliana na uamuzi huo na ikaenda Mahakama ya Rufani kutafuta mapitio ya uamuzi huo. Hatua hiyo ilisimamisha mwenendo wa kesi kwa miezi kadhaa.
Februari 2026: Umoja wa Mataifa watoa uamuzi kuhusu kuzuiwa Lissu
Karibu na wakati huo, UN Working Group on Arbitrary Detention ilitoa Opinion No. 74/2025 ikisema kizuizi cha Lissu kilikuwa cha kiholela na kuitaka Tanzania imuachilie mara moja na kumpa fidia na marekebisho mengine.
UN ilieleza kuwa kizuizi hicho kilihusishwa na matumizi ya haki zake za msingi, ikiwemo uhuru wa kujieleza na kushiriki katika shughuli za kisiasa, pamoja na hoja kuhusu haki yake ya kupata mchakato wa haki.
Hata hivyo, uamuzi huo haukumaanisha kwamba kesi ya jinai nchini Tanzania ilikuwa imefutwa moja kwa moja.
Juni–Julai 2026: Rufaa ya Jamhuri
Kwa miezi kadhaa kesi ilisimama huku Mahakama ya Rufani ikishughulikia ombi la Jamhuri la kupitia uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu ushahidi mpya.
Kulikuwa na tarehe kadhaa za kusikiliza suala hilo, lakini mchakato huo ulichelewa.
Hatimaye, Julai 30, 2026, Mahakama ya Rufani iliikataa hoja ya Jamhuri.
Jopo la majaji watatu liliamua kuwa ombi hilo halikuwa na msingi na hivyo likaruhusu uamuzi wa Mahakama Kuu uliokuwa umezuia kuongezwa kwa ushahidi huo mpya.
Hii ilikuwa hatua muhimu kwa Lissu kwa sababu iliondoa kikwazo kilichokuwa kimesimamisha kesi kwa miezi kadhaa.
Agosti 10, 2026: Kesi yarudi Mahakama Kuu
Baada ya Mahakama ya Rufani kutoa uamuzi wake, kesi ilirejea Mahakama Kuu Agosti 10, 2026.
Safari hii Jamhuri iliendelea na mashahidi wake, huku Lissu akiendelea kujiwakilisha na kuwahoji mashahidi.
Miongoni mwa mashahidi waliotoa ushahidi alikuwa Mkuu wa Upelelezi wa kesi hiyo, ACP Amin Mahamba.
Agosti 11–13: Lissu amhoji Mkuu wa Upelelezi
Katika siku zilizofuata, Lissu alimhoji kwa muda mrefu shahidi huyo mkuu wa Jamhuri.
Alitumia zaidi ya saa 11 katika siku tatu kumuuliza maswali kuhusu uchunguzi wa kesi, namna ushahidi ulivyokusanywa na mazingira yaliyozunguka mashtaka dhidi yake.
Hii ilikuwa moja ya sura muhimu zaidi za kesi hiyo kwa sababu ilimpa Lissu nafasi ya moja kwa moja kuhoji msingi wa uchunguzi wa Jamhuri.
Agosti 17: Jamhuri yafunga kesi yake
Baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa kesi, Jamhuri ilitangaza kuwa imefunga upande wake wa mashtaka Agosti 17, 2026.
Ingawa awali ilisema ilikuwa na takribani mashahidi 30, hatimaye iliwaita mashahidi 17 katika hatua ya ushahidi.
Hii ilifungua ukurasa mpya: sasa Mahakama ilipaswa kuamua kama ushahidi uliowasilishwa na Jamhuri unatosha kumlazimisha Lissu kuanza kujitetea.
21 Agosti 2026 Mahakama: Lissu ana kesi ya kujibu
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jopo la majaji watatu katika Mahakama Kuu liliamua kuwa upande wa mashtaka umewasilisha ushahidi wa kutosha kuhitaji kujitetea.
Mahakama iilifafanua kwamba uamuzi huo haukumaanishi amepatikana na hatia.
Utetezi huo uliendelea mpaka Septemba 18, 2026 Lissu alipofunga utetezi wake baada ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, kusema hatatoa ushahidi kwa upande wa utetezi katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kwa mujibu wa Lissu.
Lissu aliiambia Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, , kwamba amekutana na DCI Kingai na kuzungumza naye kuhusu maeneo aliyotarajia ayatolee ushahidi.
Kwa mujibu wa Lissu, Kingai amemweleza kuwa hayuko tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi.
Lissu pia amesema Kingai amemweleza kuwa mashahidi wengine wawili ambao mahakama imeagiza wapewe wito, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Nkunda, na Inspekta Jenerali wa Polisi, Camillius Wambura, nao hawatakuwa tayari kutoa ushahidi kwa upande wa utetezi watakaporejea nchini na kupokea wito wa mahakama.
Novemba 6, 2026: Je, Lissu ataachiwa au kuhukumiwa kunyongwa?

Hili ndilo swali linalosubiriwa kwa hamu zaidi: Je, Tundu Lissu atapatikana na hatia ya uhaini au ataachiwa huru?
Mahakama Kuu ya Dar es Salaam inatarajiwa kutoa hukumu Ijumaa, Novemba 6, 2026, katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu. Hukumu hiyo itaamua hatima yake katika kesi hiyo, ikiwemo uwezekano wa kukabiliwa na adhabu ya kifo iwapo atapatikana na hatia.
Kuna uwezekano wa maamuzi mawili.
Kwanza, Mahakama inaweza kumkuta Lissu hana hatia na kumuachia huru ikiwa itaridhika kuwa upande wa mashtaka haujathibitisha tuhuma dhidi yake kwa kiwango kinachotakiwa kisheria.
Pili, Mahakama inaweza kumkuta na hatia ikiwa itaridhika kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka umethibitisha kosa la uhaini dhidi yake. Katika hali hiyo, Mahakama itatoa hukumu kwa mujibu wa sheria.
Kwa hiyo, Novemba 6 ndiyo siku ambayo Mahakama itatoa uamuzi wa mwisho kuhusu hatima ya kesi ya uhaini inayomkabili Tundu Lissu.


































