Ziwa la ajabu linalowageuza wanyama kuwa mawe

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Hebu fikiria unatembea kando ya ziwa la ajabu kaskazini mwa Tanzania. Mbele yako unaona maji yenye rangi nyekundu, waridi na chungwa yaking'aa chini ya mwanga wa jua. Ukiwa unaendelea kutazama mandhari hiyo ya kuvutia, macho yako yananaswa na umbo linalofanana na ndege aliyesimama kimya karibu na ufukwe.

Unaposogea karibu zaidi, unagundua jambo la kushangaza. Ndege huyo si hai. Wala hajaoza. Badala yake, anaonekana kana kwamba amegeuzwa kuwa sanamu ya jiwe.

Ni tukio linaloweza kuonekana kama sehemu ya hadithi za kubuni au filamu ya kusisimua. Lakini mahali hapa ni halisi. Hapa ni Ziwa Natron, lililopo karibu na mpaka wa Tanzania na Kenya, eneo ambalo kwa miaka mingi limewavutia wanasayansi, wapiga picha na watalii kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Kutoka juu, Ziwa Natron linaonekana kama mchoro wa kuvutia. Maji yake yenye rangi angavu huunda mandhari ya kipekee katikati ya Bonde la Ufa la Afrika Mashariki. Uzuri wake unaweza kukufanya udhani ni mojawapo ya sehemu tulivu zaidi duniani.

Lakini nyuma ya mwonekano huo wa kupendeza kuna mazingira magumu sana kwa viumbe wengi. Maji ya ziwa hili yana kiwango kikubwa cha alkali, kiasi kwamba uwezo wake wa kikemia unafanana na baadhi ya kemikali zinazotumika kusafishia majumbani. Wakati wa kiangazi, joto la maji katika maeneo yenye kina kifupi linaweza kufikia takriban nyuzi joto 60 za Selsiasi, hali inayoweza kuhatarisha maisha ya viumbe wengi.

Asili ya mazingira haya ya kipekee inatokana na madini yanayotoka katika Mlima Ol Doinyo Lengai, volkano hai iliyopo karibu na Ziwa Natron. Mlima huu, unaojulikana kwa Wamasai kama "Mlima wa Mungu", huachilia madini yanayoingia ndani ya ziwa na kuyapa maji yake sifa za kipekee za kikemia zinazolitofautisha na maziwa mengine duniani.

Tofauti na muonekano wake wa kuvutia kwa mbali, Ziwa Natron linafichua nguvu za kipekee za maumbile unapolisogelea. Uzuri wake wa kuvutia macho umeambatana na mazingira makali yanayolifanya kuwa mojawapo ya maeneo ya ajabu na ya pekee zaidi barani Afrika.

Kwa nini wanyama wanaofia humo huonekana kama mawe?

.

Sifa ya Ziwa Natron ya kuonekana kana kwamba linageuza wanyama kuwa mawe inatokana na mazingira yake ya kipekee. Ndege na popo wengine hugonga kwa bahati mbaya uso wa maji ya ziwa hilo unaong'aa kama kioo, huku wengine wakishindwa kustahimili mazingira yake makali.

Wanyama hao wanapokufa, miili yao hufunikwa polepole na madini yaliyomo ndani ya maji ya ziwa. Chini ya jua kali la Afrika Mashariki, mabaki hayo hukauka na kuhifadhiwa kwa muda mrefu.

Matokeo yake ni ya kushangaza. Miili yao hubaki katika umbo lake la awali, lakini ikiwa imefunikwa na tabaka la madini linaloifanya ionekane kama sanamu iliyochongwa kwa mawe.

Picha za wanyama hao zimesambaa duniani kote, na kuwafanya watu wengi kuamini kwamba Ziwa Natron lina uwezo wa kuwageuza viumbe kuwa mawe.

Hata hivyo, si kweli kwamba wanyama hao hubadilika na kuwa mawe. Kinachotokea ni mchakato wa asili wa uhifadhi unaosababishwa na madini ya ziwa, ambao huipa miili yao mwonekano unaofanana na sanamu za mawe.

Ziwa Natron ni chemchemi ya uhai

Flamingo

Licha ya sifa zake za kuwa na mazingira magumu kwa viumbe wengi, ziwa hili ni moja ya maeneo muhimu zaidi ya kuzaliana kwa ndege barani Afrika.

Kila mwaka, mamilioni ya flamingo wadogo hukimbilia Ziwa Natron kutaga mayai na kulea vifaranga vyao. Maji yake yenye alkali nyingi na maeneo yake ya mbali husaidia kuwalinda dhidi ya wawindaji wengi, na kulifanya kuwa mahali salama kwa uzazi wao.

Kwa sababu hiyo, Ziwa Natron lina nafasi ya kipekee katika maisha ya flamingo hawa. Inakadiriwa kuwa idadi kubwa ya flamingo wadogo duniani huzaliwa katika eneo hili, jambo linalolifanya kuwa moja ya maeneo muhimu zaidi kwa uhai wa ndege hao duniani.

Kwa nini flamingo hustawi hapa

Kwa viumbe wengi, mazingira ya Ziwa Natron ni magumu kuhimili. Lakini hali hiyo hiyo ndiyo inayolifanya kuwa kimbilio bora kwa flamingo.

Miguu yao imara huwasaidia kutembea kwenye maji yenye alkali nyingi, huku tezi maalumu zikiondoa chumvi iliyozidi mwilini. Aidha, matope ya moto yanayozunguka maeneo ya kutagia mayai huwazuia maadui kama fisi, mbweha na mbwa mwitu wa porini kuwafikia.

Hali hiyo huwapa flamingo mazingira salama ya kutaga mayai, kulea vifaranga na kustawi. Kwao, Ziwa Natron ambalo linaonekana kuwa hatari kwa viumbe wengine wengi ni kimbilio salama la uhai.

Kinaya kikubwa cha maumbile

Wanaotembelea Ziwa Natron mara nyingi huondoka wakiwa na hisia mseto.

Kwa upande mmoja, kuna mabaki ya ndege yaliyohifadhiwa na madini kwa njia ya ajabu, yakionekana kama sanamu za mawe zilizogandishwa.

Kwa upande mwingine, kuna taswira ya kushangaza ya mamilioni ya flamingo wanaostawi katika mazingira ambayo yanaonekana kuwa magumu kwa uhai.

Ziwa Natron linafunza somo muhimu kuhusu maumbile: si kila kinachoonekana kuwa hatari humaanisha mwisho wa uhai. Wakati mwingine mazingira magumu zaidi ndiyo yanayotoa ulinzi na nafasi ya maisha kustawi, kama ilivyo kwa mamilioni ya flamingo wanaolifanya ziwa hili kuwa makazi yao.

Zaidi ya ziwa la mawe

Huenda hiyo ndiyo inayolifanya Ziwa Natron kuwa la kuvutia sana.

Si mahali pa kuhifadhi mabaki ya wanyama pekee.

Ni ziwa lenye sura mbili zinazokinzana. Mahali ambapo kifo na uhai huishi pamoja. Mandhari yanayoonekana kuwa magumu na yasiyofaa kwa maisha, lakini yanayosaidia kudumisha mojawapo ya maajabu makubwa ya wanyamapori barani Afrika.

Uzuri wakipekee wa Ziwa Natron ni kwamba kile kinachoonekana kuwa tishio kwa baadhi ya viumbe ndicho kimbilio salama kwa wengine.