Kwanini uchaguzi wa katikati ya muhula Marekani ni muhimu kwa Trump?

Zikiwa zimesalia siku chache kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, wapiga kura wanajiandaa kupiga kura katika uchaguzi ambao unaweza kuwa na athari kubwa katika kipindi kilichosalia cha urais wa Donald Trump.
Uchaguzi wa katikati ya muhula ni nini?
Tarehe 3 mwezi Novemba, raia wa Marekani watawachagua wajumbe wa Bunge la Congress, ambalo linaundwa na Baraza la Wawakilishi na Seneti.
Uchaguzi huo hufanyika kila baada ya miaka miwili. Unapofanyika katikati ya muhula wa miaka minne wa rais, hujulikana kama uchaguzi wa katikati ya muhula (Midterm Elections).
Mojawapo ya majukumu muhimu ya Congress ni kutunga sheria za shirikisho zinazotumika kote nchini Marekani.
Matokeo ya uchaguzi huo yataamua chama cha kisiasa kitakachodhibiti Congress, kati ya chama cha Republican cha Trump na chama cha upinzani cha Democratic, na hivyo kuathiri kiwango cha urahisi ambacho rais ataweza kutekeleza mipango yake.
Matokeo hayo pia yatachukuliwa kama kipimo cha jinsi Wamarekani wanavyoridhishwa na utendaji wa rais hadi sasa.

Chanzo cha picha, Getty
Nani anachaguliwa?
Wajumbe wote 435 wa Baraza la Wawakilishi, ambalo ni bunge la chini la Congress, watachaguliwa. Wajumbe hao huhudumu kwa muhula maalumu wa miaka miwili.
Baraza la Wawakilishi hushughulikia zaidi uwasilishaji na mijadala ya miswada ya sheria.
Aidha, uchaguzi utafanyika kwa ajili ya kujaza nafasi 35 kati ya viti 100 vya Seneti, ambayo ni sehemu ya juu ya Bunge la Congress. Maseneta huhudumu kwa mihula ya miaka sita.
Miongoni mwa majukumu mengine, Seneti ina mamlaka ya kuidhinisha au kuzuia miswada ya sheria inayopitishwa na Baraza la Wawakilishi.
Siku hiyo hiyo, wapiga kura katika maeneo mengi nchini Marekani pia watawachagua magavana wa majimbo yao.
Uchaguzi wa ugavana katika majimbo ya California, Florida, Georgia na Michigan ni miongoni mwa uchaguzi unaotarajiwa kufuatiliwa kwa karibu zaidi.
Ni changamoto zipi kuu?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Uchumi wa Marekani ni mojawapo ya masuala yanayowatia wasiwasi wapiga kura wengi wanaokabiliwa na kupanda kwa bei za mafuta, chakula, nyumba na huduma za afya.
Mfumuko wa bei bado uko juu ya kiwango kinacholengwa na Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve - Fed), hali ambayo kwa kiasi fulani inachangiwa na vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran mwezi Februari.
Chama cha Democratic kinasema mpango wa Rais Trump wa kutoza ushuru wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nchi nyingine pia umechangia kupandisha bei kwa Wamarekani.
Uhamiaji ni suala jingine muhimu. Warepublican wanasema Trump anatekeleza moja ya ahadi zake kuu alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi wa 2024 kwa kuimarisha usalama wa mipaka na kuanzisha operesheni pana ya kupambana na uhamiaji haramu, hatua ambayo mara nyingi imezua utata.
Katika wiki za hivi karibuni, wasiwasi kuhusu teknolojia ya akili bandia (AI) umeongezeka. Wanasiasa waandamizi kutoka vyama vyote viwili wanakubaliana kuwa teknolojia hiyo inahitaji kudhibitiwa kupitia sheria, msimamo unaotofautiana na wa Trump, ambaye amepinga wazo la kutungwa kwa sheria za kudhibiti maendeleo ya teknolojia hiyo.
Hatari gani zinazohusika?
Congress, pamoja na urais na mahakama, ni mojawapo ya mihimili mitatu ya serikali ya Marekani. Mamlaka ya Congress katika kuunda na kupitisha sheria ni muhimu sana.
Kwa sasa, vyama vya Republican vinadhibiti Baraza la Wawakilishi na Seneti. Hata hivyo, wingi wao wa viti ni mdogo.
Warepublican wana viti 218 katika Baraza la Wawakilishi, idadi ya chini kabisa inayohitajika kudhibiti chombo hicho. Pia wana mbunge mmoja asiyeegemea chama chochote anayepiga kura pamoja nao.
Katika Seneti, Warepublican wana viti 53.
Udhibiti wa Seneti unaweza kubadilika iwapo chama cha Democratic kitashinda viti 51. Iwapo vyama vyote viwili vitapata viti 50 kila kimoja, makamu wa rais, ambaye kwa sasa ni Republican, anaweza kupiga kura ya uamuzi kuvunja mkwamo huo.
Iwapo chama cha upinzani cha Democratic kitafanikiwa kurejesha udhibiti wa angalau moja ya mabunge hayo mawili, kitapata uwezo wa kuweka miswada yake katika ajenda ya kujadiliwa na kupitishwa kuwa sheria.
Nani anaweza kushinda?
Kwa kawaida, wapiga kura nchini Marekani wamekuwa na tabia ya kukiadhibu chama cha rais kwa kukipigia kura chama pinzani katika uchaguzi wa katikati ya muhula.
Tafiti za hivi karibuni za maoni zinaonesha kuwa rais ana kiwango cha chini cha kuungwa mkono na wananchi. Kwa mujibu wa tovuti ya utafiti wa maoni ya Silver Bulletin, Trump, ambaye alianza muhula wake wa pili akiwa na kiwango cha kuungwa mkono kilichokuwa juu kidogo ya asilimia 50, alishuhudia kiwango hicho kikishuka hadi takribani asilimia 37 mwanzoni mwa Oktoba.
Asilimia 61 ya wananchi hawaridhishwi na utendaji wake.
Hata hivyo, si viti vyote katika mabunge hayo mawili vinavyotarajiwa kuwa na ushindani mkali, kwani baadhi ya majimbo yanaelekea kuendelea kuunga mkono chama cha Republican au Democratic.
Shirika la habari la CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, limetaja uchaguzi wa viti 10 vya Seneti unaopaswa kufuatiliwa kwa karibu katika majimbo kama Iowa na New Hampshire, pamoja na uchaguzi wa viti 42 vya Baraza la Wawakilishi katika majimbo kama Arizona na Ohio.
Uchaguzi wa mwaka huu pia unatarajiwa kuwa na ushindani usiotabirika kutokana na mvutano kati ya vyama hivyo viwili kuhusu namna mipaka ya majimbo ya uchaguzi ya Baraza la Wawakilishi inavyopaswa kuchorwa.
Warepublican walijaribu kujinufaisha kwa kuweka mipaka ya majimbo ya uchaguzi inayowapa nafasi nzuri ya kushinda katika baadhi ya majimbo, huku chama cha Democratic nacho kikichukua hatua kama hizo kujipatia faida ya kisiasa.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hii inamaanisha nini kwa Trump?

Chanzo cha picha, Getty
Iwapo chama cha Democratic kitashinda udhibiti wa Baraza la Wawakilishi au Seneti, itakuwa vigumu zaidi kwa Trump kupitisha miswada yoyote ya sheria kupitia Congress. Hali hiyo inaweza kuvuruga mipango yake ya kisiasa ndani ya nchi.
Hata hivyo, Trump amekuwa akitafuta njia za kutumia mamlaka yake bila kutegemea uungwaji mkono wa sehemu kubwa ya chama chake.
Iwapo chama cha Democratic kitafanikiwa kudhibiti mabunge yote mawili ya Congress, kitapata fursa ya kutumia kamati zake kufanya uchunguzi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu utawala wa Trump.
Madai ya ufisadi, ujenzi wa ukumbi mpya wa mikutano katika Ikulu ya White House, pamoja na mbinu zinazotumiwa na Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE) kuwakamata na kuwafukuza wahamiaji nchini humo, ni miongoni mwa masuala yanayoweza kuchunguzwa.
Pia kuna mjadala ndani ya chama cha Democratic kuhusu uwezekano wa kumuondoa Trump madarakani. Hatua hiyo itahusisha kuwasilishwa kwa mashtaka bungeni yatakayokuwa msingi wa mchakato wa kisiasa wa kumwondoa rais madarakani, ambao si kesi ya jinai.
Iwapo chama cha Republican kitaendelea kudhibiti Congress, Trump ataweza kuendelea kutekeleza mipango yake katika kipindi kilichosalia cha muhula wake wa urais.
Hii inamaanisha nini kwa uchaguzi wa 2028?
Jina la rais halitakuwa kwenye karatasi za kupigia kura katika uchaguzi wa katikati ya muhula. Hata hivyo, Trump amewahimiza Warepublican kufanya uchaguzi huo kana kwamba jina lake pia lipo kwenye karatasi za kura, kwa kuwapigia kura wagombea wa chama chake kama njia ya kuunga mkono hatua alizochukua hadi sasa.
Bila kujali matokeo ya uchaguzi huo, wachambuzi huenda wakayatumia kutathmini maoni ya wapiga kura kuhusu mwelekeo ambao Marekani inaelekea chini ya uongozi wa Trump.
Trump hawezi kugombea urais kwa mara ya tatu. Baada ya uchaguzi wa katikati ya muhula, huenda kukaanza mijadala na makisio kuhusu nani atamrithi kama mgombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa urais wa 2028, na nani atakayewania urais kwa tiketi ya chama cha Democratic.



































