Wanasayansi wafafanua kwanini tunauwezo wa kuona mapepo na kuhisi uwepo wa viumbe visivyoonekana

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kuanzia simulizi za kale za Mesopotamia kuhusu mizimu iliyokuwa ikitunzwa na ndugu zao walio hai, hadi kitabu cha Charles Dickens "A Christmas Carol", binadamu wamekuwa wakisimulia hadithi kuhusu mambo ya kimiujiza kwa karne nyingi.

Je, inawezekanaje kwamba licha ya maendeleo ya sayansi, mvuto wa binadamu kwa masuala ya mizimu haujapungua?

Christine Simmonds-Moore, profesa wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha West Georgia nchini Marekani, anasisitiza kuwa watu wengi hupitia matukio wanayoyaamini kuwa yanahusiana na nguvu zisizo za kawaida.

Neno hilo kwa kawaida hutumiwa kurejelea matukio au uzoefu ambao sayansi bado haijaweza kuueleza kikamilifu.

"Kwa watu wanaopitia matukio hayo, ni mambo halisi kabisa na yanaweza kuwa na athari kubwa katika maisha yao," anasema.

Hata hivyo, hilo halimaanishi kuwa kuna nguvu za kimiujiza zinazosababisha matukio hayo.

'Kati ya usingizi na kuamka'

Kulingana na Profesa Simmonds-Moore, matukio yanayochukuliwa kuwa ya kimiujiza huenda yakahusiana na hali inayojulikana kama hypnagogic state kipindi cha mpito kati ya usingizi na kuamka, ambapo inakuwa vigumu zaidi kutofautisha mawazo na uhalisia.

Huu pia ni wakati ambapo mtu anaweza kupatwa na hali ya kupooza kwa muda akiwa usingizini (sleep paralysis).

Mapitio ya tafiti zilizochapishwa mwaka 2011 katika jarida la Sleep Medicine Reviews yalibaini kuwa asilimia 7.6 ya watu duniani wamewahi kukumbwa na hali hiyo.

Profesa Chris French wa Chuo Kikuu cha Goldsmiths, London, anaeleza kuwa hali ya sleep paralysis hutokea pale mtu anaporejesha fahamu kabla mwili wake haujaamka kikamilifu kutoka usingizini.

Hali hiyo mara nyingi huambatana na hisia kali kwamba kuna mtu au kitu ndani ya chumba, hata kama hakuna kinachoonekana wala kusikika.

.

Wakati wa hali ya kupooza kwa muda ukiwa usingizini au sleep paralysis, watu wanaweza pia kupata ndoto za kuona au kuhisi vitu kwa uhalisia mkubwa sana, zikiwemo hisia za kimwili.

"Uzoefu huo unaweza kutisha sana," anasema Profesa French, akisisitiza kuwa hayo ni maono yanayosababishwa na ubongo na si matukio halisi.

Wataalamu pia wanaelekeza kwenye hali inayojulikana kama pareidolia, yaani tabia ya ubongo wa binadamu kuona maumbo au kutambua maana katika vitu visivyo na mpangilio maalumu.

Kwa mujibu wa Profesa Rodney Schmaltz wa Chuo Kikuu cha MacEwan nchini Canada, watu wanaweza kukosea na kudhani kuwa vivuli au maumbo yanayojitokeza kwa muda mfupi ni nyuso za binadamu, hasa wanapoyaona kwa pembe ya macho.

Profesa Simmonds-Moore anaongeza kuwa msongo wa mawazo unaweza kuongeza uwezekano wa mtu kuona au kutambua maumbo na mifumo hiyo katika mazingira yanayomzunguka.

.

Baadhi ya wanasaikolojia wanaamini kuwa hisia za kuwepo kwa mtu mwingine karibu zinaweza kuhusishwa na hali inayojulikana kama dissociation, ambapo ubongo hutenganisha kwa muda vipengele mbalimbali vya uzoefu wa mtu na namna anavyojitambua.

Kwa mujibu wa Profesa Simmonds-Moore, hali hii inaweza kujitokeza wakati wa msongo mkubwa wa mawazo, kwa mfano baada ya mtu kupata ajali, lakini pia katika shughuli za kawaida za kila siku, kama vile kuendesha gari kwenye njia anayoifahamu vizuri huku akili ikiwa haijazingatia kikamilifu anachofanya.

Mtafiti huyo anaeleza kuwa hisia za kuwepo kwa mtu mwingine zinaweza kutokea pale sehemu ya mawazo au ufahamu wa mtu inapohisiwa kana kwamba inatoka kwa mtu mwingine.

Uzoefu wa aina hii unaweza kujitokeza zaidi wakati mtu anapokuwa na msongo wa mawazo au anapokosa usingizi wa kutosha.

.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baadhi ya tafiti zimehusisha uzoefu wa matukio yanayoaminika kuwa ya kimiujiza na sifa inayojulikana kama transliminality. Kwa mujibu wa Profesa Simmonds-Moore, watu wanaopata alama za juu katika kipimo cha sifa hii kwa kawaida huwa wabunifu zaidi na wenye uwezo mkubwa wa kuwaza.

Mara nyingi watu hao hupitia hisia kali wanapotazama sanaa au kusikiliza muziki. Pia huwa na uwezekano mkubwa wa kukumbuka ndoto zao na kutafuta maana iliyojificha ndani yake.

Mtafiti huyo anasisitiza kuwa watu wenye sifa hizi pia wana uwezekano mkubwa wa kuripoti hisia za kuwepo kwa mtu au kitu kisichoonekana karibu nao.

Baadhi yao pia hupitia hali inayojulikana kama synesthesia, ambapo kichocheo cha hisi moja husababisha hisia inayohusishwa na hisi nyingine. Kwa mfano, mtu anaweza kuhusisha rangi fulani na harufu maalumu moja kwa moja bila kukusudia.

Kwa mujibu wa Profesa Simmonds-Moore, uzoefu huu wa kuhusisha hisi mbalimbali unaweza kusaidia kueleza kwa sehemu baadhi ya taarifa za matukio yanayochukuliwa kuwa ya kimiujiza.

Hata hivyo, maelezo ya kisaikolojia si nadharia pekee zinazojaribu kufafanua matukio hayo.

Mazingira

Kwa mujibu wa Profesa French, baadhi ya maeneo yana mazingira yanayoweza kumfanya mtu ahisi woga au kutokuwa na utulivu zaidi kuliko maeneo mengine.

"Kwa mfano, tunapotoka eneo lenye mwanga wa kutosha na kuingia katika chumba chenye mwanga hafifu, hali hiyo inaweza kuathiri namna tunavyotambua mazingira yanayotuzunguka. Hali hiyo pia hutokea katika vyumba vyenye dari refu, ambako mara nyingi watu huhisi kutokuwa na utulivu," anasema.

Hata hivyo, baadhi ya vichocheo vya kimazingira vina maelezo changamano zaidi. Miongoni mwa hivyo ni infrasound, yaani mawimbi ya sauti yenye masafa ya chini ya hertz 20.

Mawimbi hayo yanaweza kuzalishwa na aina mbalimbali za vifaa, magari yanayopita barabarani, na hata mifumo ya mabomba ya maji na vifaa vya kupasha joto, hasa katika majengo ya zamani.

.

Ukweli dhidi ya kujiokoa

Baadhi ya watafiti wanaamini kuwa tabia ya binadamu kuhisi uwepo wa mtu mwingine au kutambua tishio inaweza kuwa na mizizi katika mchakato wa mageuzi ya binadamu.

Mtaalamu wa ngano na simulizi za jadi, Deborah Hyde, anasema kuwa ubongo wa binadamu uliendelezwa kwa namna inayotanguliza usalama na uhai kuliko kutathmini mambo kwa usahihi.

Kwa mtazamo huo, ilikuwa salama zaidi kudhani kuwa kivuli kisichoeleweka au sauti ya ajabu inaweza kuwa ishara ya hatari, badala ya kuipuuza na kuhatarisha maisha.

Binadamu pia wana tabia ambayo watafiti huiita intentionality detection, yaani mwelekeo wa kudhani kuwa kuna kiumbe au mtu mwenye nia au uwezo wa kutenda nyuma ya jambo fulani.

Kwa mujibu wa Profesa French, jambo lisilo la kawaida linapotokea, kwa kawaida akili zetu hutafuta mtu au kiumbe anayehusika na tukio hilo.

Mtafiti huyo anaeleza kuwa mwelekeo huu unaweza kusaidia kuelewa kwa nini baadhi ya watu hutafsiri matukio wasiyoweza kuyaeleza kama ushahidi wa kuwepo kwa nguvu zisizoonekana au za kimiujiza.

.

Hali inayojulikana kama confirmation bias, yaani upendeleo wa kuthibitisha kile ambacho mtu tayari anakiamini, inaweza pia kuathiri namna watu wanavyotafsiri matukio yasiyo ya kawaida.

Hyde anabainisha kuwa imani katika nguvu zisizo za kawaida imeenea katika tamaduni nyingi duniani. Naye Profesa French anasema kuwa watu wanaoamini uwepo wa mizimu wana uwezekano mkubwa wa kukubali kuwa mizimu ndiyo chanzo cha matukio ambayo hawawezi kuyafafanua.

Profesa French anaongeza kuwa binadamu huwa na tabia ya kuzingatia zaidi taarifa zinazothibitisha imani walizonazo tayari.

Baadhi ya watu huvutiwa zaidi na simulizi kuhusu mizimu kwa sababu zinaonekana kutoa ushahidi wa uwezekano wa maisha baada ya kifo. Jambo hilo huwafanya kuwa wepesi zaidi kukubali uwezekano wa kuwepo kwa mizimu.