Utulivu kati ya Marekani na China ni wa kupotosha - The Guardian

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Katika uchanganuzi wa magazeti ya leo, tunaangazia masuala mawili yanayounganisha siasa na uchumi.

Kuanzia uwezekano wa kuibuka upya kwa mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na China, maandalizi ya Ikulu ya White House kukabiliana na hali ambayo huenda Rais Donald Trump akapoteza udhibiti wa Bunge la Congress.

Tunaanza na gazeti la The Guardian, ambalo limechapisha uchambuzi wa Edward Porter wenye mada "Vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vinaweza kuongezeka tena", unaoangazia ushindani wa kibiashara kati ya mataifa hayo mawili.

Mwandishi huyo anaamini kuwa hisia zilizokuwepo awali kwamba Beijing na Washington zinaelekea kuafikia makubaliano ya wazi ya kiuchumi zimepungua, huku masuala mengine yakichukua nafasi kubwa katika mijadala ya kimataifa.

Hata hivyo, anasema hali hiyo ya utulivu ni ya kupotosha. Kulingana naye licha ya kutokuwa na mvutano mkubwa unaoonekana hadharani, dunia inazidi kuelekea kwenye vita vya kiuchumi, ambavyo kwa kuzingatia historia vinaweza kwa urahisi kugeuka kuwa makabiliano halisi.

Porter anasema kuwa licha ya pande hizo mbili kufikia makubaliano ya kusitisha kwa muda mzozo huo wa kibiashara, hatua iliyopunguza mvutano kati ya China na Marekani, hakuna upande uliofanya juhudi za kutosha kuweka dhamana za pamoja ambazo zingesaidia kuzuia kuzuka kwa awamu nyingine ya mzozo huo.

Badala yake, mwandishi huyo anaamini kuwa Washington na Beijing zimejikita katika mikakati ya kuhakikisha zinapata ushindani wa kimkakati dhidi ya upande mwingine katika kile kinachoonekana kuwa awamu nyingine isiyoepukika ya mzozo huo.

Haya yote yanajiri katika mazingira ambayo mataifa hayo mawili yanachukulia ushindani huo kuwa suala muhimu la usalama wa taifa, pamoja na kuwa na umuhimu mkubwa katika kuhakikisha yanapata nguvu na ushawishi zaidi katika nyanja za uchumi, teknolojia na kijeshi.

.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Tofauti katika mzozo huu wa sasa, kwa mujibu wa mwandishi, ni kwamba hakuna mashindano ya kutengeneza silaha ambazo zinaweza kuiwezesha nchi moja kuiangamiza nyingine.

Badala yake, Porter anaeleza kuwa pande zote mbili zimejikita katika kuhakikisha zinaendelea kupata bidhaa na malighafi kupitia mifumo ya kimataifa ya usambazaji, ambayo kila moja inaitegemea. Wakati huohuo, kila upande unajaribu kuzuia mpinzani wake kupata malighafi na bidhaa muhimu zinazohitajika ili kufikia ubora wa kiuchumi na kiteknolojia.

Hilo lina maana gani?

Mwandishi anasema utawala wa Rais Donald Trump unawekeza mamia ya mamilioni ya dola katika miradi ya uchimbaji na uchakataji wa madini adimu pamoja na madini mengine muhimu, kwa matumaini ya kupunguza pengo kati ya Marekani na China katika sekta hiyo.

Wakati huohuo, Washington inaongeza juhudi za kuzuia Beijing kupata semikondakta za kisasa, pamoja na kuizuia kununua vifaa vinavyohitajika kutengeneza teknolojia hizo.

Kwa upande wake, China imetangaza mfululizo wa vikwazo dhidi ya usafirishaji wa teknolojia za kisasa, ikiwemo teknolojia zinazohusiana na chipu za akili unde (AI) na nishati ya jua.

Aidha, Beijing imetishia kuchukua hatua za kuadhibu nchi zitakazoshirikiana kupunguza utegemezi wake kwa uagizaji wa madini kutoka China.

Mwandishi anasema hali hii inaweza kuwaumiza viongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels na wale wa Washington, lakini si sababu ya kuanzisha vita.

Hata hivyo, anaonya kuwa China nayo italazimika kukubali kwamba mkakati wake wa kiuchumi unaotegemea sera za biashara za kujilinda dhidi ya ushindani wa nje hauwezi kuendelea kuwa endelevu kwa mataifa mengine duniani.

Eduardo Porter anahitimisha kwa kusema:

"Kuongeza kwa kiwango kikubwa mauzo ya bidhaa nje ya nchi huku uagizaji wa bidhaa kutoka nje ukibaki bila kuongezeka si hali inayoweza kudumu."

"Kushindwa kwa Trump kunaweza kuifanya Washington ikumbwe na mkwamo wa kisiasa"

.

Gazeti hilo pia limechapisha makala iliyoandikwa na mwandishi wake mkuu wa habari za Washington, Conor Stringer, yenye kichwa "Trump atapita pembeni ya Bunge la Congress litakalodhibitiwa na Wademokrasia".

Makala hiyo inaeleza kuwa wanasheria wa Ikulu ya White House wanaandaa mikakati ya kujaribu mipaka ya mamlaka ya Rais Donald Trump iwapo chama cha Republican kitashindwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

Stringer anasema maafisa wakuu wa Ikulu ya White House wametumia miezi kadhaa kuandaa mpango utakaomwezesha Trump kuendelea kutekeleza sera na kupitisha maamuzi ya kiutawala bila kuhitaji idhini ya Bunge la Congress.

Mwandishi anaamini kuwa kushindwa kwa Trump katika uchaguzi huo kunaweza kuisukuma Washington katika hali ya mkwamo wa kisiasa, kwa kuwa rais huyo atajikuta akikabiliana na Bunge lenye wingi wa wajumbe kutoka chama cha Democratic, jambo litakalofanya iwe vigumu kwake kupitisha miswada ya sheria.

Stringer anadokeza kuwa iwapo Wademokrasia wataibuka washindi katika uchaguzi huo na kupata udhibiti wa Bunge, Trump anakusudia kutegemea zaidi mamlaka yake ya urais kutekeleza ajenda yake ya kisiasa.

Gazeti hilo limemnukuu mtu mwenye ufahamu wa mipango hiyo akisema kuwa mashirika ya serikali ya shirikisho tayari yamewasilisha mapendekezo pamoja na tathmini za kisheria kuhusu hatua ambazo utawala wa Trump unaweza kuchukua bila kuhitaji idhini ya Bunge.

Stringer anabainisha kuwa Ikulu ya White House imekataa kujadili uwezekano wa chama cha Republican kushindwa, huku ikiishutumu vyombo vya habari kwa kueneza simulizi zisizo za kweli.

Wakati huohuo, Trump amerejea katika mikutano ya kampeni katika maeneo mbalimbali nchini Marekani, akijaribu kuhakikisha chama chake kinabaki na udhibiti wa Bunge la Congress. Hata hivyo, kwa mujibu wa mwandishi, wasaidizi wake wanajiandaa kwa siri kukabiliana na hali tofauti kabisa ya kisiasa mwaka 2027.

Anaongeza kuwa Wademokrasia nao wanaweza kukataa kupitisha miswada ya sheria inayoungwa mkono na Trump. Hata hivyo, rais huyo anaweza kutumia mamlaka yake ya kura ya turufu (veto) kuzuia miswada inayopendekezwa na Wademokrasia ambayo haikubaliani nayo.

Kwa mujibu wa Stringer, kuna uwezekano mdogo wa Wademokrasia kupata idadi ya kutosha ya kura katika Baraza la Wawakilishi ili kubatilisha kura hiyo ya turufu ya rais.