Moja kwa moja , Bunge la Marekani lapinga jaribio la kumuondoa Waziri wa Ulinzi madarakani

Jaribio la kumpata Waziri wa Ulinzi na hatia kwa utovu wa nidhamu na hatimaye kumwondoa madarakani lilifeli bungeni.

Muhtasari

  • Bangladesh: Polisi wawatawanya wafuasi wa Hasina wanaotaka arejee nchini humo
  • Thomas Markle, babake Meghan Markle, akamatwa tena Marekani
  • Mwanajeshi wa Marekani akamatwa Uingereza kwa kuwa jasusi wa Urusi
  • Tetesi za Soka Ulaya: Arsenal yamtaka Endrick Januari
  • Bunge la Marekani lapinga hoja ya kumuondoa Hegseth Madarakani

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Bodi ya Amani ya Trump yaitaka Israel kuruhusu misaada kuingia Gaza

    .

    Bodi ya Amani inayoongozwa na Rais wa Marekani Donald Trump imetoa wito kwa Israel kuruhusu mara moja kuingizwa kwa misaada yote muhimu ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza, baada ya mvua kusababisha mafuriko eneo hilo, na kuharibu mahema yanayoishi watu.

    Shirika la kijeshi la Israel linalosimamia uratibu wa misaada inayoingia Gaza limesema limeruhusu kuingizwa kwa makumi ya maelfu ya mahema pamoja na malori yaliyobeba vifaa vya kukabiliana na majira ya baridi.

    Hata hivyo jeshi hilo limeongeza kuwa, shughuli za kuijenga upya Gaza, "zinaweza kuanza tu baada ya Hamas kusalimisha silaha zake".

    Soma pia:

  2. Bangladesh: Polisi wawatawanya wafuasi wa Hasina wanaotaka arejee nchini humo

    .

    Polisi nchini Bangladesh wametumia vitoa machozi na risasi za mpira kuwatawanya wafuasi wa aliyekuwa Waziri Mkuu Sheikh Hasina, wanaotaka arejee nchini humo.

    Gari moja la polisi lilichomwa moto katika wilaya ya Gopalganj, ambako wafuasi wa tawi la wanafunzi la chama cha Hasina cha Awami League, ambacho kimepigwa marufuku, walikabiliana na vikosi vya usalama.

    Maandamano ya kitaifa yaliyoandaliwa na wafuasi wa Hasina yalianza siku moja baada ya kiongozi huyo wa zamani kusema alikuwa ameomba pasipoti ili aweze kurejea Bangladesh kutoka uhamishoni nchini India.

    Maandamano hayo yaliyoandaliwa na tawi la wanafunzi linalojulikana kama Bangladesh Chhatra League (BCL), limeonekana kuwa jaribio la kwanza lla wafuasi wa Hasina kuonyesha nguvu zao, tangu alipoondolewa madarakani mwezi Agosti 2024 kufuatia maandamano makubwa ya kumpinga.

    Usafiri ulitatizika katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo huku waandamanaji wakijaribu kufunga barabara kwa kutumia magurudumu yaliyoashwa moto.

    Hasina alikimbilia nchini India miaka miwili iliyopita, kufuatia uasi mkubwa uliomaliza utawala wake wa miaka 15.

    Soma pia:

  3. Thomas Markle, babake Meghan Markle, akamatwa tena Marekani

    .

    Thomas Markle, baba yake Meghan Markle, ambaye ni mke wa mwanafalme wa Uingereza,anazuiliwa na polisi nchini Marekani, baada ya kuondoa kifaa cha kielektroniki cha kufuatilia mienendo yake alichokuwa amefungwa mguuni.

    Markle alifikishwa mahakamani katika jiji la Tampa, Florida hapo jana na alinyimwa dhamana.

    Waendesha mashtaka wanasema aliondoa kifaa hicho mapema asubuhi ya siku hiyo.

    Jaji wa Marekani Lindsay S Griffin, alitoa uamuzi kuwa Markle alikuwa amekiuka masharti ya kuachiliwa kwa dhamana akisubiri kusikilizwa kwa kesi yake.

    Markle, ambaye amekanusha tuhuma za kumiliki picha zinazoashiria unyanyasaji wa kingono dhidi ya watoto, alikamatwa eneo la Florida wiki iliyopita na kuwekwa chini ya ulinzi wa nyumbani. Pia aliamriwa kuvaa kifaa cha kielektroniki cha kufuatilia mienendo yake.

    Soma pia:

  4. Mwanajeshi wa Marekani akamatwa Uingereza kwa kuwa jasusi wa Urusi

    .

    Mwanajeshi mmoja anayehudumu katika Jeshi la Marekani amekamatwa nchini Uingereza kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa niaba ya Urusi, hii ni kulingana na idara ya polisi ya Uingereza inayoshughulikia masuala ya kukabiliana na ugaidi.

    Mwanajeshi huyo mwenye umri wa miaka 41, alikamatwa karibu na mji wa Gloucester hapo jana.

    Polisi wa London wanaoshughulikia masuala ya kukabiliana na ugaidi wamesema mwanajeshi huyo alikamatwa chini ya vifungu vya kwanza na vya tatu vya Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 2023.

    Kifungu cha kwanza cha sheria hiyo kinahusu kupata au kutoa taarifa muhimu, huku kifungu cha tatu kikihusu kusaidia huduma za kijasusi za nchi za kigeni.

    BBC imebaini kuwa mwanajeshi huyo alikuwa akihudumu katika kambi ya kijeshi ya Imjin Barracks, iliyoko Innsworth, Gloucestershire. Kambi hiyo ni makao makuu ya Kikosi cha Majibu ya Haraka cha Muungano wa NATO, ambacho ni kituo muhimu cha kimkakati kwa shughuli za kijeshi za muungano huo.

    Soma pia:

  5. Raia watatu wa Iran wanazuiliwa na Marekani kwa tuhuma za kutaka kuishambulia Ulaya

    .

    Idara ya Sheria ya Marekani (DOJ) imetangaza mashtaka dhidi ya watu watatu wanaodaiwa kufanya kazi kwa niaba ya Iran na ambao inawashutumu kuhusika katika mipango kadhaa ya kutekeleza mashambulizi nchini Marekani na Ulaya.

    DOJ imesema majasusi wa Iran "walipanga kutekeleza shambulio la kigaidi katika kambi ya jeshi la anga nchini Uingereza", katika tukio lililotokea mwezi Septemba karibu na kambi ya kijeshi ya RAF Fairford nchini Uingereza.

    Mmoja wa washukiwa hao, raia mwenye uraia wa nchi mbili za Iran na Iraq, anatuhumiwa kuwasiliana na washirika wake nchini Uingereza akiwa katika gereza moja mjini New York, ambako anasubiri kufikishwa mahakamani kuhusiana na mashtaka aliyokuwa nayo awali.

    Washukiwa wengine wawili wanadaiwa kufanya mawasiliano kama hayo wakiwa nchini Iran.

    Iran imekanusha vikali kuhusika katika tukio la RAF Fairford, ambalo liligunduliwa baada ya magari yaliyotiliwa shaka kuripotiwa kuonekana karibu na kambi hiyo.

    Wanaume saba wamekamatwa nchini Uingereza kuhusiana na tukio hilo.

    Raia wa Iran Mohsen Mohajeri, raia wa Iraq Mohammad Ali al-Hassani na raia mwenye uraia wa Iran na Iraq Mohammad Baqer Saad Dawood al-Saadi wameshtakiwa kupitia hati ya mashtaka iliyowekwa wazi hapo jana na DOJ.

    Soma pia:

  6. Tetesi za Soka Ulaya: Arsenal yamtaka Endrick Januari

    .

    Arsenal wanataka kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Endrick, kwa mkopo katika dirisha dogo la usajili la Januari. Klabu hiyo inatarajia kutumia uhusiano uliopo kati ya mkurugenzi wake wa michezo, Andrea Berta, na wakala anayemsimamia mshambuliaji huyo raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 20. (Talksport)

    Arsenal inakabiliwa na ushindani kutoka kwa Roma na Sporting Lisbon, ambazo pia zinamtaka Endrick kwa mkopo hadi mwisho wa msimu. Hata hivyo, mshambuliaji huyo bado hajakata tamaa ya kuendelea na maisha yake ya soka pale Real Madrid. (AS)

    Manchester United imeongeza majina mawili katika orodha ya wachezaji wanaoweza kuwasajili Januari. Wachezaji hao ni beki wa kati wa Brentford na timu ya taifa ya Jamhuri ya Ireland, Nathan Collins, 25, pamoja na beki wa Fulham na timu ya taifa ya Nigeria, Calvin Bassey, 26. (Daily Mail)

    Arsenal pia inafuatilia uwezekano wa kuwasajili kiungo wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya Hispania, Alex Baena, 25, winga wa RB Leipzig na Norway, Antonio Nusa, 21, pamoja na mshambuliaji wa Bournemouth, Eli Junior Kroupi, 20, kama sehemu ya mipango ya kuimarisha safu yake ya ushambuliaji. (The Independent)

    Beki wa kulia wa Liverpool, Jeremie Frimpong, ataendelea kusalia Anfield hadi mwisho wa msimu huu. Taarifa zinazomhusisha mchezaji huyo raia wa Uholanzi, mwenye umri wa miaka 25, na uwezekano wa kuhamia Ligi ya Saudia hazina ukweli. (Teamtalk)

    Zipo habari kwamba Al-Hilal ya Saudi Arabia inamfuatilia Frimpong, lakini Liverpool haiko tayari kumuuza katika dirisha la Januari. Klabu hiyo itafikiria kutoa ofa kubwa ya kumsajili mchezaji huyo katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani. (Football Insider)

    Aston Villa inakaribia kukamilisha mikataba mipya ya wachezaji wake wanne. Wachezaji hao ni beki wa kushoto Ian Maatsen, 24, winga Emiliano Buendia wa Argentina, 29, kiungo Amadou Onana wa Ubelgiji, 25, na kiungo Ross Barkley wa England, 32. (The Telegraph)

    .

    Newcastle United haitafanya jitihada za kumsajili mshambuliaji Ivan Toney wa Al-Ahli katika dirisha la Januari. Mshambuliaji huyo raia wa England, mwenye umri wa miaka 30, aliwahi kuichezea Newcastle kati ya mwaka 2015 na 2018, na pia kufanya kazi chini ya kocha wa sasa wa klabu hiyo, Matthias Jaissle, alipokuwa Al-Ahli. (The i)

    Newcastle United, Sunderland na Leeds United zimejiunga na Manchester United, Brighton, Tottenham na Everton katika kumfuatilia mshambuliaji wa Dinamo Zagreb na timu ya taifa ya Croatia, Dion Beljo, 24. (Teamtalk)

    Chelsea inaweza kumruhusu winga Jamie Gittens kuondoka kwa mkopo katika dirisha la Januari, huku klabu kadhaa za Ligi Kuu England zikionyesha nia ya kumsajili mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22. (Football Insider)

    Everton inaweza kufanya jaribio la kushtukiza kumsajili kiungo wa Napoli na timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin De Bruyne, 35, katika dirisha la Januari. Mchezaji huyo aliwahi kuichezea Manchester City kabla ya kujiunga na Napoli. (Calciomercato)

    Newcastle United na Leeds United zimekuwa zikimfuatilia kwa karibu kiungo wa Coventry City, Jack Rudoni, 25, ambaye ni raia wa England. (Teamtalk)

    Fulham na Coventry City zinachuana kuwania saini ya winga wa Real Betis, Rodrigo Riquelme, 26, raia wa Hispania. (4-4-2.ch)

    Kipa wa zamani wa Manchester United, David de Gea, 36, anatarajiwa kuachwa na Fiorentina mkataba wake utakapomalizika mwakani. (Corriere dello Sport)

  7. Jaribio la kumuondoa Waziri wa Ulinzi wa Marekani madarakani, lakosa uungwaji mkono

    .

    Jaribio la kumuondoa Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, madarakani limefeli.

    Hegseth alikuwa anatuhumiwa kuanzisha vita dhidi ya Iran bila kupata idhini ya Bunge la Congress.

    Wabunge wengi wa Bunge la Wawakilishi walikubaliana kuwasilisha hoja za kumng'oa madarakani.

    Mswada huo uliwasilishwa na mbunge wa chama cha Republican, Thomas Massie, kutoka jimbo la Kentucky.

    Katika mkutano wake wa kwanza na wanahabari kutoka makao makuu ya Wizara ya Ulinzi au Pentagon, Hegseth alilitaja jaribio hilo la kutaka kumuondoa madarakani kuwa "mzaha".

    Jaribio la kumpata waziri huyo na hatia kwa utovu wa nidhamu na hatimaye kumwondoa madarakani lilikuwa na uwezekano mdogo wa kufanikiwa, kwani lingehitaji baadhi ya wabunge wa Republican kwenda kinyume na Rais Donald Trump.

    Jaribio hilo lilishindwa kwa kura 211 dhidi ya 204, huku zaidi ya wabunge 12, wakiwemo 11 wa chama cha Democratic, wakikosa kushiriki katika upigaji kura.

    Rais Trump aliadhimisha matokeo hayo kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social, akisema jaribio hilo "limeshindwa vibaya".

  8. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumatano ya leo