Ujasusi wa mapenzi unavyotumika kuwaangusha watu mashuhuri duniani

Chanzo cha picha, Reuters
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wakati Wakurugenzi watendaji wakuu wa kampuni za teknolojia, wanasiasa mashuhuri na viongozi wa mataifa wanapokumbwa ghafla na kashfa zinazohusiana na mahusiano ya siri, mara nyingi umma huona suala hilo kama kushindwa kwao kimaadili katika maisha binafsi.
Hata hivyo, uchunguzi wa kijasusi kuhusu watu mashuhuri katika sekta ya teknolojia, kama vile Mkurugenzi Mtendaji wa Nvidia, Jensen Huang, unaonyesha kuwa kashfa za kimapenzi wakati mwingine huficha mikakati iliyopangwa kwa lengo la kupata taarifa nyeti.
Katika ulimwengu wa ujasusi, mbinu hiyo inajulikana kama honey trap au sexpionage. Kwa lugha rahisi, ni pale mtu anapotumia mahusiano ya kimapenzi au ukaribu wa kimwili kumshawishi mwingine afichue taarifa za siri, kupata nyaraka nyeti au kumuweka katika mazingira ya kutishiwa na kudhibitiwa.
Mbinu hii ilitumika wakati wa Vita Baridi na baadhi ya visa vyake vimehusisha watu waliokuwa na nyadhifa kubwa serikalini na katika taasisi za kimataifa.
Baadhi ya watu mashuhuri katika historia wamejikuta wakiporomoka kutokana na mitego ya kimapenzi.
Hebu tuangalie baadhi ya visa hivyo vilivyotikisa historia.
1. John Profumo: Waziri wa Uingereza aliyejikuta katikati ya kashfa

Chanzo cha picha, Getty Images/PA
Mwaka 1961, John Profumo alikuwa Waziri wa Masuala ya Vita wa Uingereza. Alikuwa mwanasiasa mwenye ushawishi na aliyekuwa akipanda kwa kasi katika Chama cha Conservative.
Lakini maisha yake ya kisiasa yalibadilika baada ya kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na Christine Keeler, mwanamitindo mwenye umri wa miaka 19.
Kilichofanya suala hilo kuwa nyeti zaidi ni kwamba Keeler pia alikuwa na uhusiano na Yevgeny Ivanov, afisa wa jeshi la wanamaji la Sovieti aliyekuwa akifanya kazi katika ubalozi wa nchi hiyo mjini London na aliyeshukiwa kuwa jasusi.
Habari za mahusiano hayo zilipoibuka, zilizua wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wa taifa la Uingereza.
Mwanzoni, Profumo alilidanganya Bunge kuhusu uhusiano huo. Lakini baadaye alikiri kuwa hakuwa amesema ukweli na kulazimika kujiuzulu.
Kashfa hiyo ilidhoofisha serikali ya Waziri Mkuu Harold Macmillan, ambaye naye alijiuzulu baadaye mwaka 1963.
2. Bernard Boursicot: Udanganyifu wa miaka 20

Chanzo cha picha, AP
Hiki ni kisa ambacho kinaweza kukushangaza zaidi.
Bernard Boursicot alikuwa mwanadiplomasia wa Ufaransa aliyekuwa akifanya kazi katika ubalozi wa nchi hiyo mjini Beijing katika miaka ya 1960.
Akiwa huko, alikutana na Shi Pei Pu, msanii wa opera ya jadi ya China, ambaye alimvutia na hatimaye wakaanzisha uhusiano wa kimapenzi.
Lakini kulikuwa na jambo ambalo Boursicot hakulijua. Shi alikuwa mwanamume aliyekuwa akicheza nafasi za wanawake katika opera na alikuwa akifanya kazi kama mtoa taarifa kwa idara za ujasusi za China.
Boursicot aliamini kuwa Shi alikuwa mwanamke na kwamba walikuwa wamepata mtoto pamoja.
Akiwa na nia ya kulinda kile alichoamini kuwa familia yake, alikabidhi nyaraka 30 za siri za kidiplomasia za Ufaransa kwa China kati ya mwaka 1977 na 1979.
Udanganyifu huo ulidumu kwa miaka mingi hadi mwaka 1983, wawili hao walipokamatwa mjini Paris.
3. Clayton Lonetree: Mlinzi wa ubalozi aliyeingia kwenye mtego
Wakati wa Vita Baridi, Clayton Lonetree alikuwa mwanajeshi wa Marekani aliyelinda ubalozi wa nchi hiyo mjini Moscow.
Lakini kazi yake ya ulinzi ilimweka katika mazingira ambayo baadaye yangemletea matatizo makubwa.
Alianzisha uhusiano wa kimapenzi na Violetta Sanni, mwanamke wa Kisovieti aliyekuwa akifanya kazi kama mkalimani ndani ya ubalozi huo.
Baadaye, Sanni alimtambulisha kwa mtu aliyemwita ''mjomba wake''. Lakini mtu huyo alikuwa afisa wa ngazi za juu wa KGB, shirika la ujasusi la Sovieti.
Kutokana na uhusiano huo, Lonetree alitoa taarifa nyeti kuhusu usalama wa majengo ya kidiplomasia ya Marekani mjini Moscow na Vienna.
Taarifa hizo zilihusisha ramani za majengo, mipango ya ulinzi na njia za dharura za kuwahamisha watu kupitia majengo ya kidiplomasia ya Marekani yaliyoko Moscow na Vienna.
Mwaka 1987, alihukumiwa kwa ujasusi na kuwa mwanajeshi wa kwanza wa Kikosi cha Wanamaji cha Marekani kuhukumiwa kwa kosa hilo.
4. James Hudson: Video iliyozua mgogoro wa kidiplomasia
Mwaka 2009, James Hudson alikuwa Naibu Balozi Mkuu wa Uingereza katika mji wa Yekaterinburg nchini Urusi.
Lakini ghafla, maisha yake ya kikazi yaligeuka kuwa kashfa baada ya video ya faragha iliyodaiwa kumuonyesha akiwa na wanawake wawili kuchapishwa katika tovuti za habari za Urusi.
Video hiyo ya dakika nne iliitwa The Adventures of Mr Hudson in Russia.
Tukio hilo lilizua maswali kuhusu iwapo mwanadiplomasia huyo alikuwa ametegwa na vyombo vya usalama vya Urusi.
Ingawa haikuthibitishwa rasmi kuwa video hiyo ilikuwa sehemu ya operesheni ya ujasusi, kuchapishwa kwake kulizua mgogoro mkubwa na Hudson hatimaye alijiuzulu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza.
5. Majasusi wa Romeo wa Markus Wolf: Mtandao wa ujasusi wa Ujerumani Mashariki

Chanzo cha picha, EPA
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Fikiria mtu anaanzisha uhusiano na wewe, anakujali, anakusikiliza na baada ya muda mnakuwa karibu sana.
Lakini kumbe, tangu mwanzo, lengo lake halikuwa mapenzi. Alikuwa anataka kufikia taarifa za siri unazozifahamu kupitia kazi yako.
Hiyo ndiyo ilikuwa mbinu iliyotumiwa na maafisa wa ujasusi wa Ujerumani Mashariki wakati wa Vita Baridi.
Markus Wolf, aliyekuwa mkuu wa idara ya ujasusi wa nje ya shirika la Stasi, alitumia maafisa wa kiume waliokuwa wamepewa jina la Romeo spies.
Maafisa hao walipewa jukumu la kuanzisha mahusiano ya kimapenzi na wanawake waliokuwa wakifanya kazi kama makatibu na wasaidizi katika taasisi za serikali ya Ujerumani Magharibi.
Baada ya kupata imani ya wanawake hao, waliweza kuwashawishi kutoa taarifa za siri walizoweza kuzifikia kupitia kazi zao.
Mahusiano hayo yaliwawezesha maafisa wa Ujerumani Mashariki kunakili kwa utaratibu nyaraka za siri za NATO, mawasiliano ya Wizara ya Mambo ya Nje na mipango ya ulinzi, bila mashirika ya ujasusi ya nchi za Magharibi kugundua kwa urahisi kilichokuwa kikiendelea.
Je, mapenzi yanaweza kuwa silaha ya ujasusi?
Visa hivi vinaonyesha jinsi mahusiano ya karibu yalivyoweza kutumiwa katika operesheni za kutafuta taarifa za siri hasa za makampuni makubwa na pia nchi.
Na katika baadhi ya mazingira, mtu aliyedhani amepata mwenzi wa maisha kumbe alikuwa sehemu ya mchezo mkubwa wa kijasusi ambao nia ni kupata taarifa ambazo ni vigumu kuzipata kwa mazingira ya kawaida.
Mtafiti wa masuala ya ujasusi Henry Schlesinger akizungumza katika mahojiano na mwanahistoria wa ujasusi Andrew Hammond kwenye kipindi cha SpyCast alisema, "Mitego ya mapenzi hutumia mbinu hiyo hiyo ya ujasusi, lakini ni operesheni ngumu zaidi kwa sababu inahusisha binadamu na mahusiano yao ya karibu."
Imetayarishwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Yusuph Mazimu


































