Maisha na safari ya kisiasa ya Tundu Lissu

.
Maelezo ya picha, Tundu Lissu
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Tundu Antiphas Mughwai Lissu ni miongoni mwa wanasiasa wenye misimamo mikali katika historia ya siasa za Tanzania.

Lissu ni mwanasheria aliyegeukia ubunge kupitia upinzani, na katika harakati zake za kisiasa amenusurika jaribio la mauaji, tukio lililosababisha akaishi uhamishoni akihofia usalama wake.

Mwanasheria huyo amejijengea nafasi ya kipekee katika siasa za upinzani Tanzania, akifahamika kwa kauli zake kali, hoja za kisheria na msimamo wake kuhusu masuala ya utawala na haki.

Safari yake ya kisiasa imepitia vipindi mbalimbali, kutoka kuwa mbunge na mwanasheria, hadi kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa CHADEMA na mgombea Urais.

Makuzi na Elimu

Lissu alizaliwa Januari 20, 1968, katika kijiji cha Mahambe, wilaya ya Ikungi, mkoani Singida, katika familia ya wakulima.

Alianza masomo yake katika Shule ya Msingi Mahambe kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari Ilboru jijini Arusha kwa kidato cha kwanza hadi cha nne, kisha akahamia Shule ya Sekondari Galanos, mkoani Tanga, kwa kidato cha tano na sita, akihitimu mwaka 1988.

Hata akiwa mwanafunzi, Lissu alijulikana kwa tabia ya kupinga uonevu na kutokukubali unyonge mbele ya mamlaka za shule.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alipata Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B), kisha akaendelea na masomo ya juu zaidi katika Chuo Kikuu cha Warwick nchini Uingereza, ambako alipata Shahada ya Uzamili katika Sheria (LL.M).

Kazi ya Sheria na Uanaharakati

Kabla ya kuingia bungeni, Lissu alijijengea jina kama mwanasheria wa masuala ya mazingira na haki za ardhi.

Alifanya kazi na Chama cha Wanasheria wa Mazingira (LEAT — Lawyers' Environmental Action Team) na Taasisi ya World Resources Institute, akishughulikia kesi za wananchi walionyang'anywa ardhi yao kwa ajili ya uwekezaji, hasa katika sekta ya madini.

Kwa miaka mingi amekuwa akijulikana kama mtetezi wa watu wa kawaida dhidi ya taasisi kubwa za kiserikali na kibiashara. Ameongoza pia Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), chama cha kitaaluma cha mawakili wa Tanzania Bara.

Kuingia Bungeni na Kambi ya Upinzani

Mwaka 2010, Lissu aligombea na kushinda ubunge wa jimbo la Singida Mashariki kupitia CHADEMA, nafasi aliyoishikilia hadi mwaka 2020.

Bungeni, alijulikana kama mwanasheria mkuu wa CHADEMA na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani, akijipambanua kwa uwezo wake wa kutumia takwimu na hoja za kisheria kuikosoa serikali, hususan wakati wa utawala wa Rais wa awamu ya tano, John Pombe Magufuli.

Msimamo wake mkali dhidi ya ufisadi na ukiukwaji wa haki za binadamu ulimfanya akamatwe mara kadhaa katika miaka hiyo, akishtakiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo uchochezi.

,

Shambulio la Risasi 2017 labadili maisha yake

Septemba 7, 2017, maisha ya Lissu yalibadilika. Akiwa nyumbani kwake eneo la Area D, jijini Dodoma, muda mfupi baada ya kutoka kikaoni bungeni, watu wasiojulikana wenye silaha walishambulia kwa risasi zaidi ya 30 gari lake, ambapo risasi 16 zilimpata katika sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo tumboni na miguuni.

Alipatiwa matibabu ya awali katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma kabla ya kusafirishwa usiku huohuo kwenda Hospitali ya Aga Khan, Nairobi.

Baadaye, Januari 2018, alihamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi, ambako alifanyiwa upasuaji zaidi ya mara 20. Hakuna aliyewahi kufikishwa mahakamani kwa shambulio hilo, jambo ambalo Lissu mwenyewe amekuwa akilalamikia mara kwa mara.

Kurejea, kugombea Urais, na uhamishoni

Baada ya zaidi ya miaka mitatu ya matibabu na kuishi uhamishoni, Lissu alirejea Tanzania Julai 2020 na kupokelewa na wafuasi wake kama shujaa, na kugombea urais kupitia CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Alishindwa na aliyekuwa Rais John Magufuli, huku akipata takriban asilimia 13 ya kura dhidi ya asilimia 84 za mshindi, matokeo aliyoyapinga akidai kuna udanganyifu mkubwa.

Baada ya uchaguzi, akihofia usalama wake, Lissu alikimbilia makazi ya Ubalozi wa Ujerumani jijini Dar es Salaam kabla ya kurejea uhamishoni.

Alirejea tena nchini mwaka 2023 na kuendelea na harakati za kisiasa akiwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA-Bara, akifanya mikutano ya hadhara nchi nzima akikosoa utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan, hasa kuhusiana na haki za binadamu na mkataba wa uendeshaji wa bandari na kampuni ya Dubai.

Katika kipindi hiki aliendelea kukamatwa mara kadhaa kwa madai ya kufanya mikutano isiyo halali.

Kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA

.
Maelezo ya picha, Lissu kwenye moja ya mikutano ya ndani ya CHADEMA wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama hicho uliomuingiza kuwa Mwenyekiti na kumbwaga Freeman Mbowe (kulia)

Januari 21, 2025, Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, akichukua nafasi ya juu zaidi katika chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania.

Akiwa kiongozi wa chama hicho, aliongoza kampeni ya "No Reforms, No Election" (Bila Mageuzi, Hakuna Uchaguzi), akitaka mabadiliko ya kikatiba na kiuchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, msimamo uliopelekea mvutano mkubwa kati yake na serikali.

Kesi ya Uhaini

Aprili 9, 2025, Lissu alikamatwa mjini Mbinga, Mkoani Ruvuma mara tu baada ya mkutano wa kisiasa, na siku iliyofuata akashtakiwa kwa kosa la uhaini, kosa lisilo na dhamana ambalo, likithibitika, hukumu yake ni adhabu ya kifo.

Alishtakiwa pia kwa makosa ya "kusambaza taarifa za uongo" chini ya sheria za makosa ya mtandao. Aprili 12, 2025, alizuiwa rasmi kugombea katika Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Tangu wakati huo amekuwa akishikiliwa mahabusu huku kesi yake ikiendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania mbele ya jopo la majaji watatu.

Katika mwenendo wa kesi hiyo, Lissu aliamua kujiwakilisha mwenyewe bila wakili, akihoji moja kwa moja mashahidi wa siri wa upande wa mashtaka.

Kesi imepitia hatua mbalimbali, ikiwemo mzozo wa kisheria uliofikishwa Mahakama ya Rufani, kabla ya kurejea Mahakama Kuu ambako, kufikia Novemva 2026, alikuwa akisubiri hukumu

Sifa yake ya Utata

Lissu anasifika kwa lugha kali na msimamo usiobadilika, sifa zinazompatia wafuasi wengi lakini pia kumfanya awe na wapinzani wakubwa.

Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini Tanzania wamemwelezea kama kiongozi mwenye shauku kubwa ya mabadiliko lakini asiye tayari kupokea njia mbadala tofauti na anavyoamini yeye mwenyewe.

Kwa miongo miwili, safari yake imeambatana na mfululizo wa kukamatwa, mashtaka, majeraha ya risasi, na kuishi uhamishoni, lakini pia kwa taswira ya kiuongozi anaonekana kuwa ni mtu asiyekata tamaa katika kile anachokiita 'mapambano ya demokrasia na utawala wa sheria nchini Tanzania'.

Imehaririwa na Ambia Hirsi