Ni nani anatoa vitisho vya mabomu vinavyotikisa safari za ndege Ulaya?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Tahadhari za bomu zilikuja kwa kasi, zikilenga shirika moja la ndege baadaye uwanja mmoja wa ndege baada ya mwingine.

Katika karibu visa vyote, isipokuwa uwanja wa ndege wa Heathrow jijini London, tahadhari hizo zilichukuliwa kuwa za kuaminika kiasi cha kusababisha ndege zilizohusika kubadili njia zake, au hata katika kisa cha Italia, ndege za kivita kurushwa angani ili kuisindikiza ndege iliyokuwa ikilengwa.

Baadaye tahadhari hizo zote zilibainika kuwa za uongo.

Matukio haya ya uongo yanayolenga mashirika ya ndege, yaliyotokea kwa wakati mmoja na kwa uratibu, imesababisha baadhi ya watu kuanza kuituhumu Urusi.

Baada ya mfululizo wa mashambulizi ya kimtandao na kuonekana kwa ndege zisizo na rubani katika maeneo nyeti mapema mwaka huu, katika siku chache zilizopita, wadukuzi wamekuwa wakidhibiti kwa mbali mifumo ya majokofu ya maduka makubwa, pamoja na mfumo wa benki ya damu.

Pia kumekuwa na tukio la kutia wasiwasi katika mpaka wa Poland na Urusi.

Aidha, mwezi Agosti, shambulizi la ndege isiyo na rubani lililolenga uwanja wa ndege wa Leipzig Halle nchini Ujerumani lilimfanya waziri wa mambo ya ndani wa nchi hiyo kuilaumu Moscow hadharani.

Je, Urusi ndiyo inayohusika na matukio haya?

Kuna wengi wanaodai kuwa, kwa kutegemea ushahidi wa kimazingira pekee, huenda haya yakawa ni mfano mwingine wa kile kinachojulikana kama vita vya mseto (hybrid warfare), vita vya eneo la kijivu (grey zone) au vita vilivyo chini ya kiwango cha uchokozi kinachotambulika rasmi (sub-threshold warfare).

Hivi ni vitendo vinavyolenga kuharibu miundombinu au kuvuruga jamii ya nchi fulani, lakini mara nyingi hufanywa kwa siri, bila wahusika kujulikana au kuwajibika, na kwa namna inayofanya iwe vigumu kuthibitisha waliohusika.

Pia, vitendo hivyo hubaki chini ya kiwango kinachoweza kuchochea utekelezaji wa Kifungu cha 5 cha mkataba wa NATO, ambacho kinaweka msingi wa nchi wanachama kusaidiana kijeshi iwapo mmoja wao atashambuliwa.

Kwa hakika, Moscow imekasirishwa sana na NATO kutokana na kuiunga mkono Ukraine na, kwa kufanya hivyo, kuvuruga mipango ya Kremlin ya kuiteka nchi hiyo na kwa vitendo kuondoa uhuru wake wa kujitawala.