Teknolojia mpya ya kupata watoto bila tendo la ndoa wala IVF

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika muongo mmoja uliopita, nimetoa utabiri wa kijasiri kuhusu mustakabali wa tendo la ngono. Utabiri mmoja ulio wazi ni kwamba watu wataendelea kufanya tendo la ngono kwa miaka mingi ijayo, lakini kwa sababu tofauti: hawatakuwa wakilifanya tena kwa lengo kuu la kupata watoto.
Hii haimaanishi kwamba uzazi utakoma kabisa, bali inamaanisha kuwa teknolojia itabadilisha namna tunavyopata watoto. Huenda kukapatikana njia salama na rahisi zaidi za kuzaliana, na hivyo tendo la ngono kama tunavyolijua likawa limefikia ukingoni.
Hadi takriban karne moja iliyopita, wanadamu walitengeneza viinitete na watoto kwa njia ileile ya jadi ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa ya kubahatisha kupitia tendo la ngono.
Baadaye, baadhi walianza kutumia njia ya uingizaji mbegu bandia, na miaka 45 iliyopita, njia ya utungishaji nje ya mwili (IVF). Ingawa teknolojia hizi zimekuwa muhimu, bado zinahusisha mayai na mbegu za kiume za asili za binadamu.
Hata hivyo, kutokana na maendeleo ya teknolojia ya seli shina, hali hiyo itabadilika.
Hatua inayofuata ya mabadiliko itakuwa katika mfumo wa uundaji wa gameti kupitia seli za ngozi (IVG) yaani, kugeuza seli za ngozi kuwa seli shina zenye uwezo mkubwa wa kujibadilisha, kisha kuzigeuza kuwa mayai na mbegu za kiume.
Teknolojia ya IVG inasisimua sana kwa mamilioni ya wanandoa, lakini pia inaibua maswali magumu.
Kwa mfano, ikiwa tunaweza kutengeneza mayai kutoka kwenye seli za ngozi, watu wenye umri wa miaka 90 wanaweza kuwa wazazi wa kijenetiki. Vivyo hivyo, watoto wa miaka tisa, vijusi vilivyoharibika, au hata watu waliokufa miaka mingi iliyopita ambao seli zao ziligandishwa.
Pia, fikiria hili: vipi ikiwa tunaweza kutengeneza mbegu za kiume kutoka kwa seli za ngozi za wanawake, au mayai kutoka kwa wanaume?
Hili linaweza kuwa kweli hivi karibuni. Mnamo mwaka 2023, wanasayansi wa Japani walitangaza kuwa wametengeneza mayai ya kike kutokana na seli za ngozi za panya dume, na kwa kutumia mbegu za kiume za panya wa kawaida, walifanikiwa kuzalisha watoto wa panya.
Ili kuendeleza wazo hili, vipi kama tungetengeneza mayai na mbegu za kiume kutoka kwa mtu mmoja na kuzitumia kutengeneza viinitete?
Geuza yai hilo lililorutubishwa kuwa mtoto na una mtoto mwenye michango sawa ya kijenetiki kutoka kwa wazazi wanne - au wanane, au kumi na sita, au zaidi.
Kukua kwa teknolojia
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Teknolojia nyingine inayoweza kumaliza uzazi kama tunavyoujua ni uwezo wa kurekebisha DNA ya kijusi. Urekebishaji uliolengwa wa mfuatano fulani katika DNA ya seli umewezekana kutokana na nyenzo mpya ya kihistoria iliyovumbuliwa mwaka 2012, inayolenga mfuatano wa DNA wa CRISPR (Clustered Regularly Interspaced Short Palindromic Repeats).
Mnamo Novemba 2018, mwanasayansi wa China, He Jiankui, alitangaza kuzaliwa kwa mabinti wawili ambao viinitete vyao alivifanyia mabadiliko ya kijenetiki kupitia mfumo wa CRISPR mapema mwaka huo. Cha kusikitisha ni kwamba alifanya kazi hii kwa siri, kwa njia zilizokiuka maadili ya utafiti wa kibinadamu na sheria za China.
Mahakama ya China ilimhukumu kwenda jela miaka mitatu, wakati mahakama ya mtazamo wa kimataifa ilimshutumu kama muhalifu aliyevunja sheria.
(Watoto hao wawili wa kwanza sasa wana zaidi ya miaka mitano, lakini China haijawahi kutoa taarifa yoyote kuhusu afya yao au muundo wao wa kijenetiki.

Chanzo cha picha, Getty Images
Unapofanya mabadiliko kwenye DNA ya kiinitete katika hatua za awali, unabadilisha DNA katika kile kitakachokuwa seli zake zote ikiwemo seli za uzazi (mayai na mbegu za kiume).
Hivyo, unafanya mabadiliko ambayo yanaweza kurithishwa kwa vizazi vya kiinitete hicho bila kikomo.
Matumizi yanayowezekana zaidi ya teknolojia hii ya kubadilisha DNA ni kuzuia magonjwa au hali zinazosababisha ulemavu kwa watoto.
Matumizi ya kutisha zaidi ingawa hayana uwezekano mkubwa wa kutokea ni kuitumia kuunda 'watoto wa kipekee', ambao si tu watakuwa na uwezo wa hali ya juu, bali pia wataurithisha uwezo huo kwa watoto wao wenyewe.
Baadhi ya watu wanaamini kuwa hatupaswi kamwe kuruhusiwa kubadilisha DNA ya vizazi vyetu vijavyo, jambo ambalo linaweza kuwa na athari za kudumu; wengine wanaamini kuwa hatupaswi kuitumia kwa sasa, kwa sababu haijathibitishwa kuwa salama au yenye ufanisi.
Mnamo 2017, watafiti waliripoti kufanikiwa kuweka hai wanakondoo wachanga waliozaliwa wiki moja au mbili kabla ya wakati wao, wakiwa ndani ya mifuko ya plastiki iliyojaa maji maalum.
Hivi karibuni zaidi, Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Marekani (FDA) ilifanya mkutano wa hadhara ili kujadili iwapo, lini, na jinsi gani ya kuendesha majaribio ya mifuko hiyo ya uzazi ya bandia kwa watoto wachanga.
Vifaa hivi hutumika kuhifadhia watoto njiti (incubators) vya kiwango cha juu. Vinaweza kusogeza mbele uwezo wa mtoto njiti kuishi kwa wiki moja au mbili zaidi, kutoka (kwa kiwango kizuri zaidi) takriban wiki 22 za ujauzito hadi kufikia karibu wiki 20, lakini bado mtoto huyo angelazimika kutumia miezi minne na nusu akikua ndani ya mwili wa mwanamke.
Maendeleo haya yanaweza kuwa ya kustaajabisha kwa watoto wachanga njiti na wazazi wao, lakini hayataleta mabadiliko makubwa kwa wengi wetu.
Vipi kuhusu tumbo la uzazi la bandia ambalo linaweza kuchukua kiinitete cha siku sita au saba na kusaidia kikue kwa miezi tisa hadi kuwa mtoto mchanga mwenye afya njema?
Hilo halingetoa tu tendo la ndoa katika utengenezaji wa watoto, bali pia lingefuta ujauzito wenyewe. Baadhi ya watu wanaweza kulikaribisha hili, wakati wengine bila shaka watakuwa na hofu au mashaka.
Hayo yote huenda yasiwe ya kufikirika au yasiyowezekana katika siku za usoni za mbali. Eneo kuu la utafiti wa muda mrefu leo ni kutumia seli shina kukuza viungo vya binadamu.
Lengo kuu ni viungo muhimu kwa ajili ya upandikizaji kama vile figo, ini, na mioyo lakini ikiwa viungo hivyo vinaweza kukuzwa, kwa nini isiwezekane kwa tumbo la uzazi?
Wazia kiungo hicho, kilichokuzwa kutoka kwenye seli shina za mwanamke, kikiwa kimeunganishwa na mashine itakayotoa damu, sukari, oksijeni, na homoni zote muhimu, pamoja na mfumo wa kuchuja na kuondoa taka mwilini kisha ongeza kiinitete.
"Tumbo hili la uzazi lililo ndani ya sanduku" linaweza, walau kwa kinadharia, kuchukua nafasi ya tumbo la uzazi la mwanamke.
Lakini je, lifanyike hivyo? Watoto wetu na wajukuu wetu huenda wakahitaji kufanya uamuzi huo.
Hiki ni kipindi cha kustaajabisha kuwa katika fani ya tiba na biolojia. Ujuzi wetu unapanuka kwa kasi ya kushangaza. Uwezo wetu wa kutumia vizuri ujuzi huo unakua kwa kasi ndogo zaidi, lakini kwa uthabiti. Uelewa wetu juu ya madhara ya kutumia teknolojia mpya na makubaliano yetu kuhusu mipaka gani, kama ipo, inayopaswa kuwekwa unakua kwa kasi ndogo zaidi.
Kutengeneza watoto kwa njia ya bandia si ajabu, ingawa ni jambo la pekee kwa namna fulani. Nina uwezo wa kutoa ridhaa kwa utaratibu wa majaribio, nikikubali hatari zake kwa ajili ya kupata faida inayoweza kutokea kwangu binafsi au kwa ajili ya sayansi. Watoto hawawezi kutoa ridhaa; wala viinitete haviwezi.
Hiyo haimaanishi kwamba tusitumie kamwe teknolojia mpya katika uzazi, bali inamaanisha kuwa tunapaswa kuwa waangalifu sana kupima teknolojia hizo ili kuhakikisha kuwa ziko salama na zinafanya kazi vizuri kwa ajili ya watoto wenyewe.

































