Je, mwisho wa dunia ni Novemba 13, 2026? Utabiri wa zamani ulioibuka tena

h
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kadri tarehe hii inavyokaribia, hofu kuhusu "mwisho wa dunia" imeanza kujadiliwa tena kwa wingi kwenye mitandao ya kijamii na vyombo mbalimbali vya habari.

Tarehe hiyo inahusishwa na utafiti wa kisayansi uliochapishwa miaka 66 iliyopita ambao ulijaribu kutathmini mustakabali wa idadi ya watu duniani.

Utafiti huo uliandikwa na watafiti watatu na kuchapishwa katika jarida la sayansi la Marekani la tarehe 4 Novemba 1960, ukiwa na mada: "Doomsday: Friday, 13 November".

Katika utafiti wao, watafiti walisema kwamba ikiwa idadi ya watu duniani ingeendelea kuongezeka kwa kasi ileile waliyoiona katika takwimu za karibu miaka 2,000 iliyopita, basi kwa mujibu wa hesabu zao za kinadharia, idadi ya binadamu ingefikia kiwango kisicho na kikomo kufikia Novemba 2026.Hata hivyo, je, watafiti hao walikuwa wakizungumzia kutoweka kwa binadamu?

Na je, tarehe hiyo ina umuhimu wowote wa kisayansi unaoashiria janga la kimataifa au tukio linaloweza kusababisha maisha duniani kutoweka?

Jibu kwa kifupi ni hapana.

Kwa kweli, utafiti huo ulikuwa ukitumia mfano wa kihisabati kuonyesha kwamba ongezeko la idadi ya watu haliwezi kuendelea milele kwa kasi ileile. Watafiti hawakutabiri kwamba dunia ingefikia mwisho au kwamba binadamu wangetoweka Novemba 2026.

Badala yake, walionyesha kuwa endapo mwelekeo wa ongezeko la watu ungeendelea bila mabadiliko, mfumo huo ungekuwa hauwezekani kudumishwa na hivyo kulazimika kubadilika kabla ya kufikia hatua hiyo.

Kwa miongo iliyofuata, viwango vya kuongezeka kwa idadi ya watu duniani vilianza kupungua katika maeneo mengi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na maendeleo ya huduma za afya, elimu, ukuaji wa uchumi na mabadiliko ya kijamii. Hivyo, makadirio ya awali yaliyotokana na mfano huo wa kihisabati hayakutimia.

Kwahiyo, hakuna ushahidi wa kisayansi unaoonyesha kwamba Novemba 2026 itakuwa tarehe ya mwisho wa dunia, au kwamba kuna tukio maalum la kimataifa linalotarajiwa kusababisha kutoweka kwa maisha ya binadamu duniani.

Mjadala unaozungumziwa sasa unatokana zaidi na tafsiri potofu za utafiti wa zamani kuliko utabiri halisi wa kisayansi kuhusu mustakabali wa sayari yetu.

Taarifa hizi zilianzia wapi?

f
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Asili ya utafiti huu inaanzia kwa mwanafizikia Heinz von Foerster, mzaliwa wa Austria aliyekuwa na uraia wa Marekani.

Alifanya utafiti huo kwa kushirikiana na watafiti wengine wawili, Patricia Mora na Lawrence Amiot. Wote watatu walikuwa wanachama wa Idara ya Uhandisi wa Umeme katika Chuo Kikuu cha Illinois nchini Marekani.

Watafiti hao walitumia takwimu za kihistoria za makadirio ya idadi ya watu duniani. Takwimu hizo zilikuwa na makadirio 24 yaliyokusanywa kuanzia mwanzoni mwa mwaka wa kwanza wa Kalenda ya Kikristo (AD) hadi mwaka 1958. Lengo lilikuwa kuelewa jinsi idadi ya watu ilivyoongezeka katika historia.

Watafiti hawakutegemea dhana kwamba idadi ya watu duniani inaongezeka kwa kasi ileile kila mwaka. Badala yake, walibuni modeli ya kihisabati iliyotumia dhana ya ukuaji wa idadi ya watu unaoongezeka kwa kasi, inayojulikana kama Hyperbolic Growth.

Katika mfumo huu, si tu kwamba idadi ya watu inaongezeka, bali kasi ya ongezeko hilo pia inaendelea kuongezeka kadiri muda unavyopita.

Modeli hiyo ilijengwa kwa msingi wa wazo kwamba uwezo wa binadamu kushirikiana, kusaidiana na kuunda mahusiano na wengine husaidia kukabiliana na baadhi ya changamoto za mazingira.

Hali hiyo huongeza uwezo wa binadamu kuishi na kuzaliana.

Baada ya kutumia mlinganyo huo wa kihisabati katika takwimu za kihistoria, watafiti walihitimisha kwamba mfumo wao ungefikia hatua inayojulikana kama singularity yani hatua ya kinadharia ambapo, kwa mujibu wa mlinganyo wa kihisabati, ongezeko la idadi ya watu linafikia kiwango kisicho na ukomo ifikapo mwaka 2026. Walikadiria kuwa hatua hiyo ingefikiwa katikati ya Novemba 2026.

Hivyo, tarehe ya Novemba 13, 2026, ikawa sehemu ya kichwa cha utafiti huo. Kwa mujibu wa modeli hiyo, idadi ya watu duniani ingefikia kiwango cha kinadharia cha "kutokuwa na ukomo" iwapo masharti na hali zilizotumika katika hesabu hizo zingeendelea bila kubadilika.

Utabiri wa mwisho wa dunia

Kwa mtazamo wa kwanza, kichwa cha utafiti huo kinaweza kuonekana kama utabiri wa mwisho wa dunia, lakini maana yake halisi ni tofauti kabisa.

Watafiti hawakutabiri kwamba jiwe kubwa kutoka angani lingeigonga Dunia, kwamba Jua lingelipuka, au kwamba matetemeko ya ardhi na milipuko ya volkano vingesababisha maangamizi makubwa. Wala hawakutaja tarehe ambayo binadamu wangetoweka kutokana na janga la kiasili.

Kwa hakika, walitumia dhana ya "doomsday" yani mwisho wa dunia, kuelezea hatua ya kinadharia ya kihisabati ambapo idadi ya watu ingekuwa isiyo na ukomo kulingana na mlinganyo wao. Hata hivyo, hali hiyo haiwezekani katika ulimwengu halisi.

Kwa maneno mengine, dhana ya idadi ya watu kuwa "isiyo na ukomo" haimaanishi kwamba idadi ya watu duniani itafikia kiwango hicho kwa uhalisia. Ni matokeo ya kihisabati yanayopatikana wakati wa kufanya makadirio ya baadaye kwa kudhani kwamba masharti yote yaliyotumika katika hesabu hizo yataendelea kuwepo bila mabadiliko.

Uchambuzi wa utafiti wa awali unaonyesha kwamba watafiti walitambua kuwa mfumo huo hauwezi kutumika kwa usahihi bila kuzingatia athari za mazingira, rasilimali na hali nyingine zinazoizunguka jamii.

Haya ni mambo yanayoweza kuathiri viwango vya uzazi na vifo, na hivyo kubadilisha mwelekeo wa ongezeko la idadi ya watu.

Kuna uhusiano gani na makala ya Michel Tecla ya 1964?

H

Gazeti la Misri la Waddani pia lilichapisha picha ya makala ya zamani iliyokatwa kutoka kwenye gazeti, yenye tarehe ya Novemba 29, 1964. Makala hiyo ilisainiwa na mwandishi aliyejulikana kwa jina la Michel Tecla, na kichwa chake cha habari kilidai kuwa dunia ingeangamia Novemba 13, 2026.

Baadaye, vyombo vingine vya habari nchini Misri vilichapisha tena picha ya makala hiyo ya zamani, na kusababisha simulizi hiyo kuibuka tena baada ya zaidi ya miaka 60.

Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha kati ya maandishi yaliyochapishwa gazetini na utafiti wa awali wa kisayansi.

Utafiti kuhusu tarehe ya Novemba 13, 2026, ulichapishwa mwaka 1960 na Von Foerster pamoja na watafiti wenzake wawili, si Michel Tecla.

Vyombo vya habari vilivyoripoti suala hili hivi karibuni pia vimeelezea maudhui ya makala ya Tecla kwa namna tofauti.

Baadhi ya taarifa zimehusisha maandishi hayo na utafiti kuhusu ongezeko la idadi ya watu, huku nyingine zikirejelea nadharia zinazohusiana na shughuli za Jua, mabadiliko ya tabianchi na majanga ya kiasili.

Kwahiyo, si sahihi kuzichukulia dhana hizo zote kama sehemu ya nadharia moja ya kisayansi, au kudai kuwa ni matokeo ya utafiti wa Von Foerster, hadi pale maandishi kamili ya makala ya awali yatakapopatikana na kulinganishwa na maudhui ya utafiti huo wa kisayansi.

Shughuli za sayari

d

Baadhi ya taarifa za vyombo vya habari zilizohusisha makala ya Michel Tecla pia zimedai kuwa kutakuwa na shughuli zisizo za kawaida za Jua Novemba 13, 2026.

Taarifa hizo zilizua hofu kwamba hali hiyo inaweza kusababisha hitilafu katika sehemu ya sumaku kwenye Dunia na majanga ya kiasili.

Hata hivyo, ni muhimu kutofautisha kati ya dhoruba za jua zinazotokea kwa uhalisia na madai kwamba dhoruba hiyo itatokea katika tarehe maalumu.

Shughuli za jua ni jambo la kawaida linalofahamika kisayansi. Jua hupitia mizunguko ambayo kiwango cha shughuli zake hubadilika.

Katika mizunguko hiyo, wakati mwingine hutokea milipuko mikubwa ya nishati na miale ya jua, ambayo inaweza kuathiri eneo la sumaku la Dunia.

Dhoruba kali zinazowezwa kusababishwa na jua zinaweza kuvuruga mifumo ya mawasiliano, satelaiti na mifumo ya urambazaji. Pia zinaweza kuathiri mifumo ya usambazaji wa umeme.

Hata hivyo, hatari hizo hazimaanishi kuwa jua litaiangamiza Dunia katika tarehe maalumu.

Utafiti kuhusu ongezeko la idadi ya watu uliochapishwa katika jarida la Science la mwaka 1960 halikuwasilisha ushahidi wowote unaohusisha tarehe ya Novemba 13, 2026, na shughuli za jua au majanga yanayohusiana na matukio ya chini ya ardhi na hali ya hewa.

Imetafsiriwa na Elizabeth Kazibure na kuhaririwa na Mariam Mjahid