Watu wanaohitaji saa nne tu za usingizi

M
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Baadhi ya watu wanaweza kuishi vizuri kwa usingizi mfupi sana. Lakini si rahisi kujua kama wewe ni mmoja wao.

Aimee Pugh Bernard hajawahi kuhitaji usingizi mwingi. Kwa kawaida hulala saa nne usiku na kuamka karibu saa kumi unusu alfajiri.

"Nakuwa macho kabisa. Siwezi kusalia kitandani," anasema.

Bernard, profesa wa kinga mwilini katika Chuo Kikuu cha Colorado, wakati mwingine hupata saa tano tu za usingizi. Hata hivyo, bado huwa na nguvu siku inayofuata. Hufanya mazoezi, kumtembeza mbwa wake na kuanza kazi mapema asubuhi.

Kwa wengi, hali ni tofauti. Kwa mujibu wa Taasisi ya Kitaifa ya Usingizi ya Marekani, watu wazima wenye umri wa miaka 26 hadi 64 kwa kawaida huhitaji saa saba hadi tisa za usingizi kwa siku.

Tofauti hizi zimekuwa fumbo kwa muda mrefu. Hata hivyo, tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa vinasaba vina mchango mkubwa katika kuamua muda wa usingizi anaohitaji mtu.

Dalili za kwanza

Mwaka 2019, Bernard aligundua sababu inayoweza kueleza uwezo wake wa kulala kwa muda mfupi.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha California, San Francisco waligundua mabadiliko ya kijeni yanayohusishwa na muda wa usingizi. Watu wenye mabadiliko hayo hulala kwa saa nne hadi sita na nusu kwa usiku na huamka mapema.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Baada ya kupima damu yake, Bernard aligundua kuwa alikuwa miongoni mwao.

Hali hii ya kurithiwa inajulikana kama familial natural short sleep (FNSS). Tangu wakati huo, mabadiliko mengine kadhaa ya kijeni yanayohusishwa na hali hiyo yamegunduliwa.

Mojawapo ya maswali makubwa ni kwa nini watu wenye FNSS wanaonekana kuishi vizuri licha ya kupata usingizi mchache sana.

Utafiti unaonyesha kuwa baadhi ya tofauti hizi za kijeni zinaweza kuwakinga dhidi ya athari za ukosefu wa usingizi, ikiwemo matatizo ya kumbukumbu.

Katika majaribio ya wanyama, watafiti waligundua kuwa baadhi ya panya waliokuwa na mabadiliko hayo walionekana kulindwa dhidi ya matatizo ya kumbukumbu na walikuwa na uwezekano mdogo wa kupata dalili zinazofanana na ugonjwa wa Alzheimer.

Utafiti mwingine wa mapacha wawili ulionyesha kuwa pacha aliyekuwa na mabadiliko hayo ya kijeni alilala kwa saa moja chini kuliko ndugu yake, lakini alipata athari chache zaidi za kukosa usingizi.

.

Matumaini ya kutengeneza dawa

Wanasayansi wanaamini kwamba uelewa wa tofauti hizi za kijeni unaweza kusaidia kutengeneza dawa za kutibu matatizo ya usingizi au kuwasaidia watu kustahimili usingizi mchache.

Hata hivyo, watafiti wanasisitiza umuhimu wa kuelewa kwa usahihi jinsi mabadiliko hayo yanavyofanya kazi kabla ya kutumia maarifa hayo kutengeneza dawa.

Ingawa FNSS ni hali adimu, watafiti wanaamini kuwa kati ya asilimia 30 na 65 ya tofauti za muda wa usingizi kati ya watu zinaweza kuelezwa na vinasaba.

Mamii ya maeneo katika jenomu ya binadamu yamehusishwa na muda wa usingizi. Tofauti moja ya kawaida ya kijeni inaweza kuathiri muda wa usingizi kwa takribani dakika moja tu, lakini athari zake zikijumlishwa zinaweza kuwa kubwa zaidi.

Baadhi ya tafiti zimeonyesha kuwa watu wenye vinasaba vinavyohusishwa na usingizi mfupi wana hatari ndogo ya matatizo fulani yanayohusiana na ukosefu wa usingizi.

Hata hivyo, tafiti nyingine zimehusisha tofauti hizo za kijeni na hatari kubwa ya kukosa usingizi, uchovu, ADHD, mfadhaiko na kisukari aina ya pili.

Hii haimaanishi kwamba usingizi mfupi husababisha matatizo hayo, bali inaonyesha kwamba mwelekeo wa kijeni wa kulala kwa muda mfupi si kinga dhidi ya hatari zote za kiafya.

Taswira ya kuwa sawa

.

Jambo jingine ni kwamba watu wanaodhani wanafanya kazi vizuri kwa usingizi mchache si mara zote wana uwezo wa kutathmini hali yao kwa usahihi.

Utafiti mmoja ulionyesha kuwa watu waliolala saa nne au sita kwa usiku walizidi kufanya vibaya katika vipimo vya uwezo wa kufikiri kadri muda ulivyopita.

Hata hivyo, baada ya wiki mbili walihisi kuwa walikuwa na usingizi kidogo tu.

Watafiti wanasema mtu anaweza kuendelea kudhoofika kutokana na ukosefu wa usingizi huku akiwa hafahamu kiwango cha athari hiyo.

Kwa muda mrefu, tafiti za kijeni zinaweza kusaidia kubaini ni nani anayehitaji usingizi mchache kiasili na nani anayeonekana kuwa sawa lakini yuko katika hatari kubwa ya kuathirika.

Kwa Bernard, kugundua kuwa alikuwa na mabadiliko ya kijeni yanayohusishwa na FNSS kulimpa utulivu wa akili.

"Sasa nina jibu," anasema. "Najua kwamba, kijeni, hivyo ndivyo nilivyo, na ninapaswa kukikubali."

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi na kuhaririwa na Mariam Mjahid