Moja kwa moja , Mashirika ya haki za binadamu yalaani hukumu ya Tundu Lissu

Shirika la Amnesty International limesema hukumu hiyo ni matokeo ya mchakato uliokosa haki tangu mwanzo.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Asha Juma

  1. Karua, Bobi Wine na Maraga wamtetea Lissu baada ya hukumu ya miaka minne

    .

    Viongozi kadhaa wa kisiasa na wanaharakati kutoka ukanda wa Afrika Mashariki wamekosoa hukumu ya kifungo cha miaka minne jela dhidi ya mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kumwondolea shtaka la uhaini lakini kumtia hatiani kwa kosa la uchochezi.

    Kiongozi wa People's Liberation Party (PLP) nchini Kenya, Martha Karua, alitaka Lissu aachiliwe huru mara moja, akisema kufutwa kwa shtaka la uhaini kunathibitisha kuwa hakukuwa na msingi wa kumshikilia gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja. Karua alieleza kuwa hukumu ya uchochezi na kifungo cha miaka minne ni ukiukwaji wa haki na inaibua maswali kuhusu mwenendo wa kesi hiyo.

    Karua pia alisema kuwa kesi dhidi ya Lissu inapaswa kutazamwa katika muktadha mpana wa kisiasa nchini Tanzania, hususan baada ya CHADEMA kuzuiwa kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2025. Alionya dhidi ya matumizi ya mashitaka ya jinai kama njia ya kudhoofisha wapinzani wa kisiasa na kupunguza ushindani wa kidemokrasia.

    Kwa upande wake, kiongozi wa Linda Mwananchi Movement (LMM) na Seneta wa Nairobi, Edwin Sifuna, alikaribisha uamuzi wa mahakama wa kumuondolea Lissu shtaka la uhaini, akisema hakupaswa kushtakiwa kwa kosa hilo tangu mwanzo. Sifuna alidai kuwa kosa pekee la Lissu lilikuwa kudai mageuzi katika mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi wa haki na wa uwazi.

    Naye kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, alisema kuondolewa kwa shtaka la uhaini ni ushindi dhidi ya kile alichokiita matumizi ya mfumo wa dola kutishia wapinzani wa kisiasa. Hata hivyo, alikosoa hukumu ya uchochezi, akidai kuwa shtaka hilo lilitumika kumweka Lissu gerezani kwa kuendelea kuitetea ajenda yake ya "No Reforms, No Election".

    Bobi Wine alisema hukumu hiyo inaonesha namna mifumo ya mahakama inaweza kutumiwa kuwanyamazisha viongozi wa upinzani wanaodai mageuzi ya kidemokrasia.

    Wakati huo huo, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga, alikosoa mwenendo wa kesi hiyo akisema mashitaka ya uhaini dhidi ya Lissu hayakuwa na msingi wa kisheria. Maraga alisisitiza kuwa wito wa mageuzi ya kikatiba, mikutano ya amani na kususia uchaguzi haupaswi kutafsiriwa kama uhaini.

    Aidha, mwanasheria na mwanaharakati wa Kenya Miguna Miguna alijiunga na viongozi wengine wa kikanda kulaani hukumu hiyo, akisema kutiwa hatiani kwa Lissu licha ya kuondolewa shtaka la uhaini kunazua maswali kuhusu haki na uhuru wa kisiasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

    Viongozi hao kwa pamoja wametoa wito wa kuheshimiwa kwa haki za kisiasa, uhuru wa kujieleza na ushindani wa kidemokrasia nchini Tanzania.

    Soma Zaidi:

  2. Mashirika ya haki za binadamu yalaani hukumu ya Tundu Lissu

    .

    Mashirika mbalimbali ya haki za binadamu yamekosoa hukumu ya kifungo cha miaka minne jela dhidi ya mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, baada ya Mahakama Kuu kumkuta na hatia ya kosa la uchochezi huku ikimuondolea shtaka la uhaini.

    Shirika la Amnesty International limesema hukumu hiyo ni matokeo ya mchakato uliokosa haki tangu mwanzo. Mkurugenzi wake wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Tigere Chagutah, alisema Lissu hakupaswa kukamatwa, kushtakiwa wala kutiwa hatiani.

    Kwa mujibu wa Amnesty, Lissu ametumia siku 577 akiwa mahabusu kutokana na kile shirika hilo linachodai kuwa matumizi ya haki zake za msingi kwa njia ya amani. Shirika hilo pia lilidai kuwa alinyimwa fursa ya kuwasiliana kwa siri na mawakili wake, jambo lililomlazimu kujitetea mwenyewe mahakamani.

    Amnesty ilidai pia kuwa matangazo ya moja kwa moja ya mwenendo wa kesi yalikatizwa, huku baadhi ya waangalizi wa kimataifa wa kesi hiyo wakikamatwa na baadaye kufukuzwa nchini. Aidha, ilisema Lissu alizuiliwa katika mazingira yasiyofaa na kuitaka Tanzania kufuta hukumu hiyo, kumuachilia huru bila masharti na kuheshimu haki za uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani.

    Kwa upande wake, Human Rights Watch (HRW) ilisema hukumu hiyo ni ishara ya kile ilichokiita ukandamizaji unaoendelea dhidi ya wapinzani wa kisiasa nchini Tanzania. Shirika hilo lilibainisha kuwa kesi ya Lissu ilizua wasiwasi wa haki za binadamu kutokana na ucheleweshaji wa mara kwa mara wa shauri hilo pamoja na madai kwamba alizuiwa kuwasiliana kwa faragha na mawakili wake.

    HRW ilizitaka mamlaka za Tanzania kuacha kutumia mfumo wa haki ya jinai dhidi ya wapinzani wa kisiasa na badala yake kuheshimu haki za kisiasa na uhuru wa kujieleza.

    Nalo Pan-African Solidarity Network (PASNet) limetaka kuachiliwa kwa Lissu mara moja na bila masharti, likisema hukumu hiyo imeibua maswali kuhusu haki ya usikilizwaji wa kesi na uhuru wa mahakama nchini Tanzania.

    PASNet ilidai kuwa Lissu alitiwa hatiani kwa kosa ambalo hakushtakiwa moja kwa moja nalo na kwamba hakupata fursa ya kutosha kujitetea. Shirika hilo pia lilieleza wasiwasi kuhusu afya yake, upatikanaji wa matibabu maalumu na athari za kuendelea kushikiliwa kwake kwa familia yake.

    Aidha, PASNet imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Afrika (AU) na Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu kuunda tume huru ya kimataifa kuchunguza madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaodaiwa kutokea baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa mwaka 2025.

    Mashirika hayo kwa pamoja yameitaka Tanzania kuheshimu haki za msingi za kisiasa na kuhakikisha mfumo wa sheria hautumiki kuwanyamazisha wakosoaji wa serikali na viongozi wa upinzani.

    Soma Zaidi Hapa:

  3. Hujambo. Karibu katika matangazo yetu mubashara mimi ni Asha Juma.