CHADEMA yampa Lissu tumaini jipya, yatangaza mpango wa rufaa na dhamana

Chanzo cha picha, AFP
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza mpango wa kukata rufaa kupinga hukumu ya kifungo cha miaka minne jela iliyotolewa dhidi ya Mwenyekiti wake wa Taifa, Tundu Lissu, huku kikikusudia pia kuwasilisha maombi ya dhamana ili aweze kuachiwa wakati rufaa yake ikiendelea kusikilizwa.
Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Dk. Rugemeleza Nshala, alitangaza mpango huo Ijumaa, Novemba 6, 2026, muda mfupi baada ya Mahakama Kuu ya Dar es Salaam kumtia hatiani Lissu kwa kosa la uchochezi, lakini kumwachia huru katika shtaka la uhaini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam, Dk. Nshala alisema Lissu ameeleza nia ya kupinga hukumu hiyo na kwamba timu ya mawakili inaanza maandalizi ya kuwasilisha rufaa.
Alithibitisha pia kuwa CHADEMA itawasilisha maombi ya dhamana kwa ajili ya Lissu wakati rufaa yake ikiendelea, akieleza kuwa kwa mujibu wa msimamo wa timu ya mawakili wa chama hicho, kosa la uchochezi lina dhamana. Hata hivyo, ombi hilo litasubiri uamuzi wa mahakama husika.
Chadema yapinga ukali wa hukumu
Dk. Nshala alieleza kutoridhishwa na urefu wa kifungo alichopewa Lissu, akibainisha kuwa tayari amekuwa mahabusu kwa siku 577 tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025.
Alisema kuwa muda huo aliokaa mahabusu, ukijumuishwa na kifungo cha miaka minne alichohukumiwa, unafanya jumla ya muda wake wa kukaa kizuizini kufikia takribani miaka mitano.
"Adhabu ya juu kabisa kwa kosa la uchochezi ni miaka mitano. Tayari amekaa mahabusu mwaka mmoja na miezi saba, halafu sasa amehukumiwa miaka minne. Ukiunganisha muda aliokaa mahabusu na kifungo hiki, inakuwa miaka mitano," alisema Dk. Nshala.
Alieleza kuwa CHADEMA haijaridhishwa na adhabu hiyo, hasa ikizingatiwa kuwa mahakama imemuachia huru Lissu katika shtaka la uhaini.
Mapambano ya kisheria yaingia awamu mpya
Dk. Nshala alisema chama kitashauriana na Lissu pamoja na timu ya mawakili ili kuandaa hoja za kisheria zitakazotumika kupinga hukumu hiyo.
Alisisitiza kuwa CHADEMA itafuatilia hatua zote za kisheria, ikiwemo rufaa na maombi ya dhamana, huku ikiendelea kusisitiza umuhimu wa kuheshimiwa kwa utawala wa sheria.
Lissu alikamatwa Aprili 2025 kufuatia matamshi aliyoyatoa katika mkutano wa kisiasa, ambapo upande wa mashtaka ulimtuhumu kuhamasisha wafuasi kuvuruga uchaguzi mkuu wa nchi.
Kiongozi huyo wa upinzani alikanusha tuhuma hizo, akieleza kuwa matamshi yake yalikuwa sehemu ya kampeni ya kisiasa ya kudai mageuzi ya uchaguzi na katiba.
Ijumaa, jopo la majaji watatu lililoongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru lilimuachia huru Lissu katika shtaka la uhaini baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha nia ya kumtisha au kuishinikiza Serikali, jambo lililotajwa kuwa sehemu muhimu ya kosa hilo.
Hata hivyo, mahakama ilimtia hatiani katika shtaka mbadala la uchochezi na kumhukumu kifungo cha miaka minne jela.
Lissu aendelea kubaki gerezani
Licha ya kuachiwa huru katika shtaka la uhaini, Lissu alirejeshwa gerezani baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo.
Kesi hiyo imeendelea kuvuta hisia za viongozi wa upinzani, wanaharakati na mashirika ya kimataifa yanayotetea haki za binadamu.
Shirika la Amnesty International ni miongoni mwa taasisi zilizokosoa hukumu hiyo na kutaka Lissu aachiwe huru mara moja bila masharti.
Suala hilo limeibua mjadala mpana kuhusu hali ya demokrasia, uhuru wa kisiasa, mageuzi ya uchaguzi na nafasi ya vyama vya upinzani nchini Tanzania.
Kwa sasa, macho ya Watanzania na jumuiya ya kimataifa yanaelekezwa katika hatua zinazofuata za kisheria, huku CHADEMA ikiweka wazi kuwa kipaumbele chake ni kupinga hukumu hiyo na kutafuta kuachiwa kwa mwenyekiti wake.






























