Njia mpya ya matembezi inayoelekea kwenye 'lango la kuzimu' nchini Ireland

Chanzo cha picha, Yvone Gordon
Rathcroghan ni mojawapo ya maeneo ya kale zaidi ya kifalme barani Ulaya ambayo bado hayajafanyiwa utafiti wa kiakiolojia.
Njia hii mpya ya matembezi inawapa wasafiri fursa ya kutembelea maeneo hayo ya kihistoria, ikiwemo pango linalohusishwa na chimbuko la sherehe za Halloween.
Kutoka kileleni mwa kilima cha Rathcroghan, katika kaunti ya Roscommon nchini Ireland, mandhari inaenea hadi kwenye mashamba yenye nyasi, kuta za mawe pamoja na ng'ombe na kondoo wanaochungwa eneo hilo.
Ingawa eneo hilo linaweza kuonekana kama mashamba ya kawaida, ukilitazama kwa karibu unaweza kuona makumi ya miundo mikubwa ya ardhi yenye umbo la duara pamoja na vilima vya kale vya mazishi.
Hii ni kwa sababu Rathcroghan maana yake ni "ngome ya Cruachan" katika lugha ya Kiairishi, ni mojawapo ya maeneo ya kale na makubwa zaidi ya kifalme barani Ulaya ambayo bado hayajafanyiwa uchimbaji wa kiakiolojia.
Eneo hili lilikuwa mji mkuu wa kale wa jimbo la Connacht nchini Ireland, na lina mabaki 266 ya kihistoria yaliyoenea katika eneo la kilomita za mraba 6.5.
Mabaki hayo yanajumuisha ngome za duara za zama za Chuma mawe ya Ogham yaliyochongwa kwa maandishi ya kale ya Kiarishi, pamoja na visima vilivyokuwa vikitumika kwa shughuli za kidini.
Mojawapo ya maeneo yenye mafumbo makubwa zaidi ya Rathcroghan ni njia ya chini ya ardhi inayoingia ndani kabisa ya ardhi na kuvuka mpaka wa kihekaya unaotenganisha ulimwengu wa wanadamu na ulimwengu wa viumbe wa kiroho katika imani za Waselti au Celtic otherwolrd.
Eneo hilo linalojulikana kama "Lango la Kuzimu" la Ireland, linaaminika kuwa chimbuko la mila za kale ambazo baadaye zilibadilika na kuwa sherehe za Halloween.
"Ni eneo lenye kuvutia sana. Si maeneo mengi yanayoweza kujivunia kuwa na lango linaloelekea katika ulimwengu wa viumbe wa kiroho," anasema John Waddell, profesa mstaafu wa masuala ya akiolojia katika Chuo Kikuu cha Galway.

Chanzo cha picha, Alamy
Kwa kuwa makaburi na maeneo mengi ya kihistoria ya Rathcroghan yako ndani ya mashamba yanayomilikiwa na watu binafsi, kwa muda mrefu wageni wamekuwa na uwezo wa kufikia baadhi tu ya maeneo hayo kwa kutumia magari.
Hata hivyo, sasa njia mpya ya matembezi yenye urefu wa kilomita 13 imeanzinduliwa, ikiunganisha maeneo muhimu ya kihistoria katika eneo hilo kupitia njia ya mzunguko inayojulikana kama Rathcroghan Archaeological Walking Trail.
Njia hiyo inawapa wasafiri fursa mpya ya kutembelea eneo hilo na kuliona kwa mtazamo tofauti, huku wakielewa jinsi makaburi na maeneo hayo ya kale yalivyokuwa yameunganishwa.
Historia ya kidini na ulimwengu wa kiroho
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Historia ya Rathcroghan inaanzia miaka 5,500 iliyopita. Eneo hilo lilikuwa kitovu muhimu cha mikusanyiko ya sherehe za kimila, pamoja na karamu, maadhimisho ya misimu na hafla za kutawazwa kwa wafalme.
Eneo hilo pia limekuwa chimbuko la simulizi nyingi za ngano na imani za kale.
Hapa ndipo simulizi kuu la kitaifa la Ireland, The Táin Táin Bó Cúailnge (Uvamizi wa Ng'ombe wa Cooley), linapoanzia na kuishia.
Simulizi hilo, ambalo hulinganishwa na The Iliad ya Ugiriki ya kale, linaelezea uvamizi mkubwa ulioanzishwa na Malkia Medb wa Connacht, shujaa wa zama za Chuma (Iron Age) aliyetawala kutoka katika kasri lake lililokuwa karibu na eneo hilo.
"Rathcroghan ni eneo la kale la kifalme. Hatuizungumzii kasri lililojengwa katikati ya mandhari ya kawaida; tunazungumzia eneo ambalo watu walikusanyika kwa sababu mbalimbali kuadhimisha sherehe, sikukuu za mabadiliko ya misimu, ndoa, mikataba, vifo, mazishi na kutawazwa kwa mfalme," anasema Elaine Conroy, mwongoza watalii wa Rathcroghan na msaidizi wa utafiti.

Chanzo cha picha, Yvonne Gordon
Eneo hilo pia linachukuliwa kuwa takatifu. Rathcroghan ni mojawapo ya maeneo matatu makuu ya mazishi katika Ireland ya kale, ambako wafalme na machifu wa kwanza wa taifa hilo walizikwa. Hadi sasa, vilima 40 vya mazishi vimetambuliwa katika eneo hilo.
Takribani kilomita moja kusini-magharibi mwa kilima kikuu cha Rathcroghan kuna pango la Oweynagat, ambalo linaaminika kuwa makazi ya Mórrígan, mungu wa kike wa ulimwengu wa kiroho anayehusishwa na chimbuko la sherehe za Halloween.
Katika simulizi la The Táin, mungu huyo anaelezewa kuwa na uwezo wa kubadilisha umbo lake. Pia anahusishwa na sherehe za Samhain, zilizoashiria mwanzo wa majira ya baridi.
Kipindi hicho, kilichoanza tarehe 31 Oktoba, kiliaminika kuwa wakati ambapo pazia lililotenganisha ulimwengu wa wanadamu na ulimwengu wa viumbe wa kiroho lilikuwa jembamba zaidi. Katika kipindi hicho, Mórrígan pamoja na viumbe wake waovu waliaminika kutoka pangoni humo.
Kutokana na imani hiyo, watu walianza kuvaa mavazi ya kujificha ili kuzuia roho hizo zisiwatambue na kuwadhuru.
Kwa kawaida, inachukua takribani saa tatu kutembea njia hiyo yote.
Nilianza ziara yangu katika Kituo cha Wageni cha Rathcroghan, kilichopo katika kijiji cha Tulsk, kabla ya kuendesha gari kwa umbali wa kilomita nne hadi kwenye sehemu ya kuanzia njia hiyo katika kilima cha Rathcroghan.
Hapo ndipo njia mpya ya matembezi inapoanzia na kuishia, huku safari yangu ikielekea kwenye eneo linalojulikana kama "Lango la Kuzimu".
Njia mpya ya kutembelea Rathcroghan
Kilima cha Rathcroghan ndicho alama kubwa zaidi na inayofikika kwa urahisi katika eneo hilo. Ni muundo wa ardhi wenye upana wa mita 88 na urefu wa mita 5.5, ambao haujawahi kufanyiwa uchimbuzi wa kiakiolojia.
Hata hivyo, misingi ya majengo iliyogunduliwa kupitia uchunguzi wa kijiografia (geophysical surveys) inaashiria kuwa eneo hilo huenda lilitumika kwa shughuli mbalimbali za sherehe, ikiwemo kutawazwa kwa wafalme.

Chanzo cha picha, Yvonne Gordon
"Hapa ndipo palipokuwa kitovu cha Connacht," anasema Mike McCarthy, mwanaakiolojia na mtafiti katika Kituo cha Wageni na Urithi cha Rathcroghan, tunaposimama kwenye sehemu mpya ya kuanzia njia ya matembezi karibu na kilima cha Rathcroghan.
"Tunatembea katika eneo ambalo lilitumika kwa mikusanyiko, sherehe na shughuli za kutawazwa kwa wafalme. Pia tuko katikati ya eneo muhimu sana la kihistoria la mazishi ya kale, ambako wafalme wa Connacht walizikwa. Kwa hiyo, eneo hili halina tu historia na mabaki ya kiakiolojia, bali pia lina uhusiano na ngano, hekaya na fasihi."
Waddell, ambaye aliwahi kufanya utafiti wa moja kwa moja katika eneo la Rathcroghan, anasema mojawapo ya mambo yanayolifanya eneo hilo kuvutia ni jinsi lilivyojaa maana na imani za kale.
"Uchunguzi wa kijiografia uliofanywa katika kilima cha Rathcroghan umeonyesha kuwa eneo hilo lina historia tata sana, likiwa na miundo mbalimbali ya duara iliyozikwa ndani yake na mingine iliyojengwa juu yake. Lilikuwa eneo kubwa la kufanyia sherehe, huenda hata lilikuwa na ukumbi mkubwa wa duara uliojengwa kwa nguzo za mbao," anasema.
"Kinacholifanya eneo hili kuwa la kipekee ni mchanganyiko wa hekaya, ngano na mabaki ya kiakiolojia, vyote vikiwa vimehifadhiwa katika simulizi nyingi za kihistoria."

Chanzo cha picha, Yvone Gordon
Kutoka kwenye kilima hicho, ninaendelea kutembea pamoja na McCarthy kuelekea kwenye mojawapo ya ngazi nyingi mpya zilizowekwa kuvuka ukuta wa mawe, ili kuunganisha njia hiyo mpya na mashamba ambayo hapo awali hayakuruhusiwa kutembelewa na umma.
Baada ya kupita kwenye kilima kimoja cha mazishi kisicho na jina, muda mfupi baadaye tunafika Relignaree, eneo kubwa la duara lenye upana wa mita 110, linalojulikana kama "Makaburi ya Wafalme" (The Graveyard of Kings).
Bango jipya lililowekwa eneo hilo linaeleza kuwa mahali hapo hapakuwa tu makaburi ya kifalme, bali huenda pia palikuwa makazi ya watu wa tabaka la juu, yakiwa na ngome za duara na njia za chini ya ardhi.
Ng'ombe wamekuwa wakichunga katika eneo hili kwa maelfu ya miaka, na bado wanaendelea kufanya hivyo hadi leo. Katika matembezi yetu, tunakutana na kundi la ng'ombe wakiwa na ndama wao. McCarthy anasema watembea kwa miguu wanaweza pia kukutana na mifugo mingine pamoja na kondoo wadadisi njiani.
Kama McCarthy anavyoeleza, mifugo hiyo husaidia kuzuia nyasi na vichaka kuota na kufunika eneo hilo.
"Makaburi na miundo hii ya kihistoria bado ipo hapa kwa sababu ya shughuli za kilimo. Vinginevyo, mazingira ya asili yangekuwa yameifunika na kuimeza," anasema.
Wakulima wameweka hata vifaa vikubwa vya kujikuna kwa ajili ya ng'ombe ili kuzuia wanyama hao kutumia makaburi na miundo ya kale ya kiakiolojia kujikuna.
"Lango la Kuzimu"
Muda mfupi baadaye tunafika kwenye mstari wa miti na vichaka. Hapo, chini ya miti hiyo, kuna mtaro unaoonekana wa kawaida tu, lakini unaelekea kwenye eneo linalojulikana katika hekaya kama "Lango la Kuzimu".
Njia hiyo ya mwamba wa chokaa iko chini ya ardhi kwa kina cha mita saba na ina urefu wa mita 37. Ilitajwa katika maandishi ya watawa wa Waselti tangu karne ya tisa, na kwa muda mrefu imekuwa ikichukuliwa kuwa mojawapo ya njia kuu zinazoelekea katika ulimwengu wa viumbe wa kiroho ulimwengu wa kipekee ambao, kwa mujibu wa imani za kale, wanadamu walio hai wangeweza kuufikia.

Chanzo cha picha, Yvone Gordon
Ingawa kwa sasa pango hilo limefungwa kwa wageni kwa sababu za afya na usalama, kutokana na kiwango kikubwa cha hewa ya kaboni ndani yake, ninapiga magoti na kujiegemeza kwa mikono ili kutazama ndani ya lango la njia hiyo ya chini ya ardhi.
Lango hilo limezungukwa na jiwe la Ogham lililochongwa maandishi ya kale, linalokadiriwa kuwa la kati ya karne ya nne na ya nane.
Kutoka hapo, njia nyembamba ya mawe yenye urefu wa mita 10.5 inaelekea chini hadi kwenye pango la asili.
Picha iliyowekwa kwenye bango jipya la maelezo kwenye lango la pango hilo inaonyesha jinsi linavyoonekana chini ya ardhi. Bango hilo pia linaeleza kuwa pango hilo maarufu kwa sifa zake za kutisha lilichukuliwa kuwa mojawapo ya milango mikuu inayoelekea katika ulimwengu wa kiroho wa Ireland, unaojulikana kama Irish Otherworld.
Kwa mujibu wa imani za kale, ulimwengu huo wa kihekaya ndio mahali ambapo jamii za kabla ya Ukristo ziliamini jua lilikwenda usiku.
Tunapoendelea na matembezi yetu, tunafika kwenye eneo la Rathnadarve, lenye muundo wa duara wenye upana wa mita 115. Hapa ndipo mafahali wawili wanapokutana katika pambano la kufa au kupona mwishoni mwa simulizi la The Táin, simulizi kuu la kitaifa la Ireland.
Mbele zaidi, tunavuka barabara nyembamba ya mashambani na kuona bango lililofichika linaloelekeza kwenye kilima chenye nyasi. Limeandikwa: "Cruachan Connacht, eneo la kale la kifalme."
Hili ni eneo la Rathbeg, ambako bango jipya la maelezo linaonyesha kuwa palikuwa "Makaburi ya Wafalme".
Ingawa eneo hilo halijafanyiwa uchimbuzi wa kiakiolojia, tunafahamishwa kuwa huenda lilitumika kuwazika baadhi ya wanachama wa tabaka la juu la wapiganaji wa zama za Chuma, lililojulikana kama Aos Dána.
Nilikulia nchini Ireland nikisikia simulizi kuhusu Malkia Medb, na hata kuona picha zake kwenye noti za zamani za sarafu ya Ireland.
Kutembea katika eneo hili kunafanya simulizi hizo za kale kuwa halisi zaidi, kiasi kwamba ninaweza karibu kusikia milio ya kwato za mafahali wawili wa The Táin, magurudumu ya gari la Malkia Medb au mayowe ya kutisha ya Mórrígan.
Tofauti na kutembelea mnara au mnara wa kumbukumbu pekee, Rathcroghan inawapa wageni fursa ya kuzama katika historia ya eneo hilo na kuelewa jinsi mababu zetu walivyolitumia miaka 5,500 iliyopita.
"Watu wamezoea wazo kwamba baadhi ya makaburi na miundo ya kale yalikuwa maeneo ya kufanyia sherehe na ibada za kimila," anasema Waddell.
"Rathcroghan inatoa mtazamo kwamba mandhari yote ya eneo fulani yanaweza kuwa na umuhimu wa aina hiyo, kama sehemu zilizohifadhi kumbukumbu na shughuli za ibada za kale."



































