Je, mwelekeo mpya wa Marekani utaibadilisha Iran na Mashariki ya Kati?

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
Katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, chama cha Democratic kilifanikiwa kupata wingi wa viti katika mabunge yote mawili ya Congress, yaani Seneti na Bunge la Wawakilishi, na kuchukua udhibiti wa Congress katika kipindi kilichosalia cha urais wa Donald Trump.
Ushindi wa Democrats umekuwa pigo kubwa kwa rais wa taifa hilo.
Donald Trump amekiri kuwa vita dhidi ya Iran pamoja na kupanda kwa gharama ya maisha vilichangia kushindwa kwa wagombea wengi wa chama cha Republican.
Makamu wa Rais wa Marekani, J.D. Vance, pia alizungumzia suala la vita "Sababu iliyotufanya tushindwe ni vita."
Ila matokeo hayo ya uchaguzi wa katikati ya muhula yanamaanisha nini kwa mataifa mengine duniani, kuanzia vita vya Ukraine, Mashariki ya Kati hadi uhusiano wa kibiashara na China.
Vita vya Iran vimesababisha ongezeko kubwa la gharama za maisha kwa Wamarekani, ikiwemo kupanda kwa bei ya petroli.
Wakati wa kampeni zake za kuwania kuchaguliwa tena mwaka 2024, Trump aliahidi kushusha bei ya petroli hadi chini ya dola mbili kwa galoni moja. Hata hivyo, wastani wa bei ya petroli kufikia mwezi Oktoba ulikuwa dola 4.31 kwa galoni moja au lita tatu.
Pia aliahidi kutoanzisha vita vipya iwapo angerudi katika Ikulu ya White House.
Lakini siku moja kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula, Marekani ilianzisha mashambulizi mapya katika kisiwa kimoja nchini Iran. Trump aliwaambia waandishi wa habari kuwa hajutii kuanzisha vita hivyo.
Akijibu matokeo ya uchaguzi huo, Mohammad Baqer Qalibaf alisema kuwa wananchi wa Marekani "wamesema hawataki vita."
Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mojtaba Khamenei, alitangaza katika taarifa yake kwamba hatarajii sera za Marekani kubadilika kufuatia matokeo hayo ya uchaguzi.
Trump pia alisema katika mahojiano na CBS News, mshirika wa BBC nchini Marekani, kwamba mzozo huo "utaisha nitakaposema umeisha."

Chanzo cha picha, Fars News Agency / Handout/Anadolu via Getty Images
Kulingana na Mojtaba Khamenei, kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema kuwa wale wanaodhani mabadiliko katika sera za Marekani yataondoa "uadui wa Marekani dhidi ya Iran" wamekosea pakubwa.
Bw. Khamenei pia ameonya kuwa iwapo Marekani itaishambulia tena Iran, jibu la Iran litakuwa "katika kiwango kikubwa zaidi."
Kiongozi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu, aliyemrithi baba yake Ali Khamenei baada ya kuuawa katika mashambulizi ya Marekani na Israel mwezi Februari, bado hajaonekana hadharani.
Nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kinadharia, kushindwa kwa Trump kungeweza kutafsiriwa katika kipindi kingine kuwa pigo kwa nchi za Kiarabu zilizoko Ghuba ya Uajemi.
Rais wa Marekani pamoja na familia yake wana uhusiano wa karibu, wa kibinafsi na kibiashara na nchi nyingi za eneo la Ghuba.
Kuna uwanja wa gofu unaomilikiwa na kampuni ya Trump International mjini Dubai.
Qatar imemzawadia ndege yenye thamani ya dola milioni 400, huku Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar na Saudi Arabia zikiwekeza kwa pamoja mabilioni ya dola katika kampuni ya Affinity Capital inayomilikiwa na Jared Kushner, mkwe wa Donald Trump.
Trump pia aliichagua Riyadh kuwa kituo chake cha kwanza cha ziara za nje alipokuwa rais kwa muhula wake wa kwanza mwaka 2017.
Uhusiano wa Saudi Arabia na mtangulizi wake wa chama cha Democratic, Joe Biden, ulikuwa na mvutano mkubwa.
Viongozi wa nchi za Ghuba pia walikuwa na mashaka na rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, kwa kushindwa kumchukulia hatua Rais wa Syria wakati huo, Bashar al-Assad.
Hata hivyo, vita dhidi ya Iran vilivyoanza mwaka huu vimebadilisha mtazamo wao kuhusu Trump.
Kama mchambuzi mmoja alivyosema, "Trump aliichoma Ghuba ya Uajemi kwa moto" na bado kuna wasiwasi kwamba anaweza kuanzisha tena vita hivyo.
Hofu hiyo inatokana na uwezekano wa Iran kujibu kwa kulenga miundombinu muhimu ya nchi za eneo hilo, jambo linaloweza kusababisha uharibifu mkubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images


































