Marekani yafungua anga baada ya kusitisha safari za ndege nchini kote

Chanzo cha picha, Getty Images
Vyombo vya habari vya Marekani vinaripoti kuwa marufuku ya safari za ndege nchini kote imeondolewa.
Takribani saa nne baada ya safari za ndege kusimamishwa, mamlaka zimeruhusu ndege kurejea angani na kuendelea na safari zake.
Waziri wa Uchukuzi wa Marekani, Sean Duffy, amethibitisha kuwa anga la nchi hiyo limefunguliwa tena.
“Vituo vyetu vya udhibiti wa safari za ndege pamoja na mifumo yetu ya mawasiliano sasa vinafanya kazi. Saa 8:15 usiku kwa saa za Mashariki mwa Marekani, tulifungua tena anga,” amesema Duffy.
Hata hivyo, amesema kurejea kwa shughuli za usafiri wa anga katika hali ya kawaida kutategemea upatikanaji wa rasilimali zinazohitajika.
Duffy ameeleza kuwa itachukua muda kurekebisha athari zilizosababishwa na hitilafu hiyo.
Amesema tukio hilo limesababisha athari katika ratiba za safari za ndege, huku mamlaka zikifuatilia safari zilizopangwa kufanyika mwishoni mwa wiki ili kuhakikisha shughuli zinarejea katika hali ya kawaida.
Kutokana na hali hiyo, ucheleweshaji wa safari unatarajiwa kuendelea kwa siku kadhaa, huku baadhi ya abiria wakiendelea kukwama katika viwanja vya ndege.
Duffy: Mfumo wa Marekani wa kudhibiti safari za ndege ni wa zamani sana
Akielezea chanzo cha tatizo hilo, Duffy amesema kuwa saa 3:36 alasiri kwa saa za eneo husika, mifumo ya rada na mawasiliano katika vituo vya udhibiti wa safari za ndege nchini kote ilianza kukumbwa na hitilafu.
Baada ya mifumo ya mawasiliano kuanza kupokea taarifa zisizolingana kutokana na hitilafu katika vifaa vya kusambaza data (routers), Shirika la Usafiri wa Anga la Marekani (FAA) lilitoa amri ya kusimamisha safari za ndege nchini kote.
Duffy aliwaambia waandishi wa habari kuwa Marekani inatumia mfumo wa zamani sana wa kudhibiti safari za ndege.
Alifafanua kuwa vifaa hivyo vililemewa na kiasi kikubwa cha data, hali iliyosababisha kutokuwepo kwa uthabiti na usahihi wa taarifa zilizokuwa zikipokelewa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa Bunge la Marekani kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kuboresha mfumo huo na kujenga mfumo wa kisasa wa kudhibiti safari za ndege.
Pia unweza kusoma:



















