Afrika: Je, huu ndio mwanzo wa kujitegemea kiuchumi?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Kuanzia ujenzi wa kiwanda kipya cha kusafisha dhahabu nchini Ethiopia hadi mpango wa kujenga kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta nchini Kenya chenye thamani ya mabilioni ya dola, nchi nyingi za Afrika zinazidi kujaribu kuongeza thamani ya rasilimali zake kwa kuzichakata ndani ya nchi badala ya kuziuza zikiwa ghafi.

Mabadiliko haya ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha viwanda vya ndani, kutengeneza ajira na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje baada ya kusindikwa kwa kutumia rasilimali za Afrika.

Nchini Ethiopia, kiwanda cha kusafisha dhahabu kinachogharimu zaidi ya dola milioni 50 kinatarajiwa kuiwezesha nchi hiyo kuchakata dhahabu yake ndani ya nchi kabla ya kuiuza katika masoko ya kimataifa.

Serikali ya Ethiopia pia imeshirikiana na bilionea kutoka Nigeria, Aliko Dangote, katika mradi wa kujenga kiwanda cha kuzalisha mbolea. Wakati huohuo, ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta linalounganisha Ethiopia na Djibouti umeanza. Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya dola milioni 660 unatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa mafuta kutoka bandari ya Djibouti hadi Ethiopia.

Kwa upande mwingine, Kenya inaendelea na mipango ya kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta kinachokadiriwa kugharimu takriban dola bilioni 16. Kikikamilika, kitakuwa cha kwanza cha aina hiyo katika Afrika Mashariki.

Miradi hii inaashiria mwelekeo mpya ambapo nchi za Afrika hazitaki kutegemea uchimbaji na uuzaji wa rasilimali pekee, bali zinataka pia kuendeleza viwanda vinavyoweza kuzalisha bidhaa zenye thamani kubwa zaidi.

'Afrika lazima ijenge mustakabali wake yenyewe'

Ni nadra kuzungumzia azma hii bila kumtaja Aliko Dangote, mmoja wa wawekezaji wakubwa barani Afrika.

"Hatuwezi kujenga Afrika yenye nguvu zaidi ikiwa tutaendelea kuwategemea wengine," alisema Dangote.

"Mtu kutoka nje ya Afrika hatakuja kutujengea Afrika bora zaidi. Ni sisi Waafrika wenyewe tunaoweza kufanya hivyo."

Dangote, ambaye uwekezaji wake umeenea katika sekta mbalimbali zikiwemo saruji, nishati, mbolea na usafirishaji, anahusika katika baadhi ya miradi mikubwa inayolenga kukuza viwanda barani humo.

Anaamini kuwa nchi za Afrika zinapaswa kuchakata rasilimali zake ndani ya nchi badala ya kuuza malighafi nje bila kuziongezea thamani, kisha kununua bidhaa zilizotengenezwa kutokana na rasilimali hizo kutoka mataifa mengine.

"Ni wakati wa Afrika kuamka kutoka usingizini na kuelekeza nguvu katika kuendeleza uchumi wake," alisema.

Hata hivyo, Dangote anasema vikwazo vya biashara bado ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazozuia ukuaji wa uchumi wa bara hilo.

"Changamoto kubwa katika maendeleo ya uchumi wa Afrika ni vikwazo vinavyozuia usafirishaji wa watu, bidhaa na huduma kati ya nchi za Afrika. Ninatumai kuwa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika utasaidia kutatua tatizo hili," alisema.

Juhudi za kuongeza thamani ya rasilimali

Wataalamu wanasema juhudi za kuongeza thamani ya rasilimali kwa kuzichakata ndani ya nchi si jambo jipya.

Dkt Marit Kitaw, mtaalamu wa sera za uchimbaji madini katika Kitengo cha Masuala ya Kiuchumi cha Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika, anahusisha mwelekeo huu na kuanzishwa kwa Dira ya Afrika kuhusu Madini mwaka 2009 (Africa Mining Vision).

Mpango huo ulilenga kushughulikia changamoto ya muda mrefu: licha ya nchi nyingi za Afrika kuwa na utajiri mkubwa wa madini, mapato yatokanayo na uchimbaji wake hayajachochea maendeleo mapana ya viwanda wala kuboresha kwa kiwango kikubwa maisha ya wananchi.

Mwendia Nyaga, mshauri wa masuala ya nishati, anasema ongezeko la idadi ya watu barani Afrika pia linazifanya serikali kutafuta njia mpya za kukuza uchumi na kutengeneza ajira.

Mamilioni ya vijana wanapoingia katika soko la ajira kila mwaka, nchi zinakabiliwa na shinikizo la kupanua fursa za kiuchumi na kujenga viwanda vinavyoweza kuajiri watu wengi.

"Kwa miaka mingi, nchi zinazoendelea zimekuwa zikisafirisha malighafi nje ya nchi na baadaye kuagiza bidhaa zilizotengenezwa kutokana na malighafi hizo," alisema Nyaga.

"Wazo la kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa kuzalisha bidhaa hizo ndani ya nchi halijapewa kipaumbele kwa kiwango kikubwa. Mabadiliko ya sera tunayoyaona sasa yanaweza kusaidia kubadili mwenendo huu."

Kutoka kuchimba dhahabu hadi kuisafisha ndani ya nchi

Dhahabu ni mojawapo ya mifano inayoonyesha juhudi za nchi za Afrika kupanua shughuli za kiuchumi zinazohusiana na rasilimali zake.

Kuanzia Afrika Kusini na Ghana hadi Uganda, Burkina Faso na Ethiopia, nchi mbalimbali zinawekeza katika viwanda vya kusafisha dhahabu ndani ya nchi badala ya kusafirisha dhahabu ghafi kwenda nje ili ichakatwe huko.

Kwa sasa, nchi 14 za Afrika zina viwanda vya kusafisha dhahabu.

Kiwanda cha Rand Refinery nchini Afrika Kusini ndicho kikubwa na cha zamani zaidi barani humo. Tangu kilipoanzishwa mwaka 1920, kimesafisha takriban theluthi moja ya dhahabu yote duniani.

Ethiopia ni miongoni mwa nchi za hivi karibuni kujiunga na orodha hiyo.

Kiwanda cha Ethiopia National Precious Metals Refinery, kilichopo katika eneo la viwanda la Bole Lemi mjini Addis Ababa, kinatarajiwa kusafisha dhahabu kwa ajili ya soko la ndani na masoko ya kimataifa.

Maafisa wanasema kikifanya kazi kwa uwezo wake kamili, kiwanda hicho kitaweza kusafisha hadi tani 600 za dhahabu kwa mwaka.

Dkt Marit anasema manufaa ya mradi huo hayaishii katika mapato yatokanayo na mauzo ya nje.

"Mradi huu utatengeneza ajira zaidi kwa vijana na wanawake, kusaidia kukuza ujuzi wa ndani, na kurahisisha upatikanaji wa teknolojia na maarifa ya kisasa," anasema.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa kuwa na viwanda vya kusafisha madini pekee hakutabadilisha uchumi wa Afrika. Nchi zinahitaji kujenga mifumo mipana ya viwanda inayotumia rasilimali zilizopo kuzalisha bidhaa mbalimbali.

Dkt Marit anatoa mfano wa akiba ya miamba ya fosfeti nchini Ethiopia. Anasema badala ya kusafirisha fosfeti ikiwa ghafi, nchi hiyo inaweza kuitumia kuzalisha mbolea ndani ya nchi. Hatua hiyo ingeongeza thamani ya rasilimali hiyo na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje.

Ethiopia imeanza mipango ya kujenga kiwanda cha mbolea nchini Somaliland kwa ushirikiano na kampuni ya Dangote Group.

Kwa nchi ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea mbolea kutoka nje, mradi huo unaonyesha namna rasilimali za asili zinavyoweza kuunganishwa na shughuli za viwanda ili kuzalisha bidhaa zenye thamani zaidi.

Mchumi Marid Tulu anasema usalama wa chakula, uzalishaji wa nishati na maendeleo ya viwanda vinazidi kuhusiana kwa karibu.

Anabainisha kuwa kadiri Afrika inavyopanua uzalishaji wa nishati na kujenga miundombinu ya kiuchumi, ndivyo nchi zake zitakavyokuwa na uwezo mkubwa wa kusimamia rasilimali zake na kuendeleza viwanda vinavyozalisha bidhaa zenye thamani kubwa.

Kwa nini ushirikiano wa kiuchumi kikanda ni muhimu?

Wataalamu wanaamini kuwa juhudi za kuendeleza viwanda barani Afrika zitafanikiwa zaidi ikiwa nchi zitashirikiana badala ya kila moja kujaribu kujenga viwanda vyake bila kuzingatia fursa zilizopo katika nchi jirani.

Dkt Marit anasema masoko ya kikanda yana nafasi muhimu katika kufanikisha azma hiyo.

Anauliza: "Ikiwa Ethiopia ina kiwanda cha kusafisha dhahabu, kwa nini Tanzania itumie fedha nyingi kujenga kingine kuanzia mwanzo?"

Kwa mujibu wake, Tanzania inaweza badala yake kupeleka dhahabu yake Ethiopia ili isafishwe huko. Anaongeza kuwa kuna haja ya kuimarisha ushirikiano wa masoko, kugawana miundombinu na kuvutia wawekezaji.

Mifano ya ushirikiano wa aina hiyo tayari inaonekana katika baadhi ya maeneo ya bara hilo.

Kusini mwa Afrika, Ukanda wa Lobito unaunganisha Angola, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia reli na bandari, kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wa madini na bidhaa nyingine.

Katika Afrika Mashariki, mradi wa Ukanda wa LAPSSET unaohusisha Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini ni miongoni mwa mipango mikubwa ya miundombinu inayolenga kuimarisha muunganiko wa kiuchumi katika eneo hilo.

Wanaounga mkono miradi hiyo wanasema inaweza kupunguza gharama za usafirishaji, kurahisisha upatikanaji wa masoko na kuimarisha biashara kati ya nchi.

Hata hivyo, wataalamu wanaonya kuwa bado kuna changamoto kubwa zinazoweza kuchelewesha maendeleo ya viwanda barani Afrika.

Miundombinu isiyotosheleza, ugumu wa kupata mitaji, uhaba wa umeme na vikwazo vya biashara vinaendelea kuathiri uzalishaji katika nchi nyingi.

Nyaga anasema kubadilisha mfumo wa zamani wa uchumi, ambao kwa muda mrefu umeegemea mauzo ya malighafi na uagizaji wa bidhaa zilizochakatwa, kutahitaji muda.

Hata hivyo, anaona idadi kubwa ya watu na soko la watumiaji linalopanuka kuwa fursa muhimu kwa Afrika.

"Fursa yetu kubwa zaidi ni watu wetu. Tuna nguvu kazi, uchumi unaokua kwa kasi na soko la watumiaji linalopanuka. Hii ni fursa kubwa sana," anasema.

Sasa serikali, wawekezaji na watunga sera barani Afrika wanazidi kujiuliza iwapo mfumo wa kuuza rasilimali ghafi na kuagiza bidhaa zilizochakatwa bado ndio njia bora ya kuendeleza uchumi wa bara hilo.

Mafanikio ya mabadiliko haya yatategemea upatikanaji wa mitaji, kuboreshwa kwa miundombinu, kuimarishwa kwa ushirikiano wa kikanda na utekelezaji madhubuti wa sera za maendeleo.