Papa Leo XIV aanza ziara Amerika Kusini wiki tatu baada ya kufanyiwa upasuaji wa saratani ya mapafu
Papa Leo XIV anaanza ziara ndefu katika mataifa ya Amerika Kusini, wiki tatu tu baada ya kufanyiwa upasuaji wa saratani ya mapafu.
Ziara hiyo inajumuisha kile kinachotarajiwa kuwa kurejea kwake kwa furaha nchini Peru, ambako aliwahi kuhudumu kama kasisi kwa miaka mingi.
Vatican imesema hakuna hatua zozote za ziada zinazochukuliwa kuhusiana na afya ya Papa huyo. Imemtaja kuwa ni mtu mwenye umri wa miaka 71 aliyefanyiwa upasuaji, na si mtu mwenye tatizo la kiafya la kudumu.
Ni Papa Leo mwenyewe aliyefichua mwezi uliopita kuwa madaktari waligundua uvimbe kwenye mapafu yake wakati wa uchunguzi wa kawaida wa afya. Uvimbe huo uliondolewa pamoja na sehemu ya chini ya pafu lake la kulia. Baadaye, timu yake ya madaktari ilithibitisha kuwa saratani hiyo haikuwa imesambaa katika sehemu nyingine za mwili.
Katika mkutano na waandishi wa habari mjini Roma kabla ya safari hiyo, ambayo itamfikisha Uruguay, Argentina na Peru, msemaji wa Vatican alisema Papa Leo ana nguvu nyingi za kimwili na ana shauku kubwa kuhusu ratiba ya ziara hiyo.
Alisema ratiba hiyo ilithibitishwa binafsi na Papa bila kufanyiwa mabadiliko yoyote.
Ujumbe wa Vatican kupitia ziara hiyo ni kwamba tatizo la kiafya alilopata Papa lilikuwa la muda mfupi na sasa amerejea katika shughuli zake za kawaida, anasema Profesa Massimo Faggioli wa Chuo Kikuu cha Villanova, akizungumza na BBC.
Anasema Papa amekuwa na ratiba yenye shughuli nyingi tangu kurejea kazini baada ya upasuaji huo.
"Tumemwona katika siku hizi akitoa hotuba, akipokea wageni na kushiriki shughuli mbalimbali. Anaonekana kuwa katika hali nzuri sana. Hilo lilikuwa muhimu," amesema.
Ziara hiyo itaanzia Uruguay, ambako idadi ya Wakatoliki imepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka ya hivi karibuni. Nchi hiyo inatarajia kupokea ziara ya kwanza ya Papa baada ya takribani miongo minne.
Baadaye, Leo ataelekea Argentina, nchi alikozaliwa Papa Francis, mtangulizi wake.
Vatican imesema kuwa katika mataifa yote matatu, Papa atakutana na manusura wa unyanyasaji wa kingono uliofanywa na viongozi wa Kanisa Katoliki. Suala hilo lilitawala mjadala wakati wa ziara ya Papa Francis nchini Chile na Peru mwaka 2018.
Profesa Faggioli anaona ziara hiyo kama njia ya Papa Leo kuimarisha tena uhusiano wa upapa na Amerika Kusini baada ya kipindi cha Papa Francis, ambaye baadhi ya ziara zake katika eneo hilo zilikumbwa na changamoto.
Anaamini Papa Leo ana mtazamo mpana kuhusu umoja wa nchi za Amerika kama bara moja.
"Demokrasia zinakabiliwa na changamoto huko, kwa hiyo kuna mambo mengi anayoweza kuyazungumzia," anasema.
Hata hivyo, anasema swali kubwa ni lini Papa Leo atatembelea Marekani. Anasema hakuna shaka kuwa Papa anataka kufanya ziara hiyo, lakini bado haijulikani kama atakwenda wakati Donald Trump akiwa bado rais wa Marekani.
Soma pia: