Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Trump atishia Iran huku jeshi la IRGC likilenga rada za Marekani Bahrain

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran limesema limelenga na kuharibu rada ya tahadhari ya mapema nchini Bahrain, likijibu shambulio la anga lililofanyika usiku wa manane katika eneo la Sirik.

Muhtasari

Trump atishia kuishambulia Iran

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Hitilafu ya Microsoft yaathiri mamilioni ya watu wanaotumia Microsoft 365

    Kampuni ya Microsoft imesema iko mbioni kurekebisha hitilafu kubwa ya kimataifa inayoripotiwa kuwaathiri mamilioni ya watumiaji, wakiwemo wale nchini Marekani, Japan, Singapore, Uingereza na Australia.

    Huduma kadhaa za kampuni hiyo, zikiwemo Teams, Outlook na programu yake ya akili unde (AI) Copilot, zimeathiriwa na matatizo ya muunganisho wa mtandao.

    Ni huduma zipi za Microsoft zilizoathirika?

    Watumiaji walioathirika huenda wasiweze kuingia au kutumia baadhi ya programu za Microsoft 365.

    Huduma ya Exchange Online ya Microsoft, inayojumuisha programu ya barua pepe ya Outlook, imeathirika na kuwafanya wateja wengi kushindwa kuitumia.

    Microsoft imesema baadhi ya watumiaji huenda pia wakashindwa kufungua faili fulani au kuona taarifa katika programu zao za kalenda.

    Microsoft imedokeza kuwa hitilafu hiyo huenda haijasababishwa na shambulio la kimtandao au cyberattack.

    Kulingana na tovuti ya Microsoft, zaidi ya watu milioni 430 duniani hutumia programu za Microsoft 365, ambazo ni huduma za usajili zinazojumuisha Outlook na Teams.

    Aidha, kampuni hiyo inasema kuwa zaidi ya asilimia 90 ya kampuni 500 kubwa zaidi duniani hutumia Copilot, programu yake ya akili unde (AI)

  2. Trump amwondoa Vance kwenye mazungumzo ya Marekani na Iran

    Jarida la Marekani la Politico limeripoti kuwa Rais Donald Trump, hapo jana alitangaza kumwondoa Makamu wa Rais J.D. Vance katika jukumu lake la kusimamia mazungumzo ya Marekani na Iran.

    Hatua hiyo, kulingana na Politico, imechukuliwa baada ya Vance kuhusisha kushindwa vibaya kwa chama cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula wiki iliyopita na vita vya Iran.

    Donald Trump aliandika ujumbe kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social, akimtaka J.D. Vance kuelekeza nguvu zake katika kukabiliana na madai ya ufisadi na uhalifu katika miji na majimbo yanayoongozwa na chama cha Democratic.

    Trump aliongezea kuwa Washington "haihitaji kufikia makubaliano na Iran."

  3. Hakuna kitakachosalia Iran iwapo watawalenga viongozi wa Marekani -Trump

    Katika mahojiano na shirika la habari la Salem News, alipoulizwa kuhusu uwezekano wa kutumia tena nguvu za kijeshi dhidi ya Iran na iwapo angesita kuchukua hatua hiyo, Rais wa Marekani Donald Trump alijibu kuwa akiona mwelekeo wa mambo unabadilika, atachukua hatua bila kusita.

    "Ikiwa nitaona mambo yanaelekea upande tofauti, nitafanya hivyo. Huenda nikafanya hivyo hata sasa hivi. Bila kusita hata kidogo," alisema Trump .

    Alipoulizwa iwapo kuendelea kuwepo kwa serikali ya Iran madarakani hadi atakapomaliza muhula wake katika Ikulu ya White House kutamaanisha ameshindwa katika vita hivyo, Trump alijibu, "Ndiyo, huo utakuwa ni ushindi wa Iran na kushindwa upande wangu.”

    Akijibu swali kuhusu hatua ambayo Washington ingechukua iwapo Iran ingemuua kiongozi wa ngazi ya juu wa Marekani, Trump alisema, "Basi hakutakuwa na chochote kitakachosalia kwao."

    Aidha, Iran imetishia kuwa iwapo itashambuliwa tena kijeshi, haitafungia mipaka ya mzozo huo katika eneo la Mashariki ya Kati pekee, bali itashambulia kambo zote za kijeshi za Marekani zilizo bara Asia na Ulaya.

  4. Naweza kuharibu miundombinu yote ya Iran ndani ya siku tatu - Trump

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Saudi Arabia, Qatar, Falme za Kiarabu na mataifa mengine ya Ghuba yamemuomba asitishe kwa sasa kutekeleza mashambulizi makubwa dhidi ya Iran.

    Trump amedai kuwa kama si ombi hilo, angeweza kuharibu miundombinu ya nishati ya Iran, madaraja na viwanda vyake ndani ya siku tatu.

    Katika mahojiano aliyoyafanya hapo jana, Trump alisema ana uwezo wa kumaliza vita hivyo, lakini kutokana na ombi la washirika wa Marekani katika eneo hilo, ameendelea kuiwekea Iran shinikizo la kiuchumi na kijeshi.

    "Saudi Arabia imeniomba niache hali iendelee kama ilivyo kwa muda fulani," alisema Trump.

    Alipoulizwa iwapo angefanya mashambulizi zaidi dhidi ya Iran kama asingepokea maombi hayo, Trump alijibu, "Ndiyo, ningefanya hivyo."

    Rais huyo wa Marekani alikiri kuwa hadi sasa Washington imejizuia kwa kiasi kikubwa kulenga miundombinu ya nishati na madaraja nchini Iran.

    "Ndani ya siku moja, vyanzo vyao vya nishati vitakuwa vimeharibiwa. Ndani ya siku moja, madaraja yao yatakuwa yameharibiwa, na ndani ya siku moja, uwezo wao wa uzalishaji viwandani utakuwa umeharibiwa. Mambo hayo yatachukua siku tatu pekee," alisema.

    Trump pia alikiri kuwa kupanda kwa bei ya petroli kufuatia vita hivyo kulichangia kushindwa kwa chama cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula.

    Hata hivyo, alitetea uamuzi wake wa kuishambulia Iran.

  5. Tetesi za soka Ulaya: Man United na Man City zapigana vikumbo kwa Malo Gusto

    Manchester United na Manchester City wanajiandaa kuwania saini ya beki wa Chelsea na timu ya taifa ya Ufaransa, Malo Gusto, mwenye umri wa miaka 23. (Talksport)

    Liverpool wamemuweka katika orodha ya wachezaji wanaowafuatilia beki wa Brighton, Luka Vuskovic, mwenye umri wa miaka 19, kwa ajili ya usajili wa majira yajayo ya kiangazi. Hata hivyo, Brighton wanadaiwa kumuwekea thamani ya takribani pauni milioni 80. (Florian Plettenberg)

    Fulham wanaongoza katika mbio za kuwania saini ya winga wa Real Betis ya Hispania, Rodrigo Riquelme, mwenye umri wa miaka 26. (Teamtalk)

    Everton wanaweza kujaribu kumsajili kiungo wa Tottenham Hotspur, Conor Gallagher, mwenye umri wa miaka 26, iwapo klabu hiyo ya kaskazini mwa London itaamua kumuuza katika dirisha la usajili la Januari. (Football Insider)

    PSV Eindhoven ya Uholanzi imeanza mazungumzo na Napoli kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ubelgiji, Kevin De Bruyne, mwenye umri wa miaka 35, katika dirisha la Januari. (Il Mattino – kwa Kiitaliano)

    Kiungo wa AC Milan, Youssouf Fofana, mwenye umri wa miaka 27, ambaye kwa sasa yuko kwa mkopo Sevilla, anafuatiliwa na Tottenham Hotspur na Juventus. (Calciomercato – kwa Kiitaliano)

    Kocha wa Charlotte FC ya Marekani, Dean Smith, anataka kuungana tena na kiungo mshambuliaji Jack Grealish, mwenye umri wa miaka 31, ambaye aliwahi kufanya naye kazi Aston Villa. Hata hivyo, mshahara wa mchezaji huyo wa kimataifa wa England, ambaye kwa sasa yuko Everton kwa mkopo akitokea Manchester City, unaweza kuwa kikwazo katika mpango huo. (Football Insider)

    Mshambuliaji wa Monaco na timu ya taifa ya Marekani, Folarin Balogun, mwenye umri wa miaka 25, anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji wanaolengwa na Mauricio Pochettino kwa ajili ya usajili wake wa kwanza akiwa kocha wa Manchester United. Balogun aliwahi kukaribia kujiunga na Everton siku ya mwisho ya dirisha la usajili majira yaliyopita. (Teamtalk)

    Leeds United ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia mshambuliaji wa Middlesbrough na timu ya taifa ya England chini ya miaka 21, Will Lankshear, mwenye umri wa miaka 21. Mchezaji huyo amekuwa katika kiwango kizuri tangu alipojiunga na Middlesbrough akitokea Tottenham Hotspur katika dirisha la usajili la majira ya kiangazi. (Football Insider)

    Newcastle United na Sunderland zinafuatilia maendeleo ya kiungo wa Sheffield United na timu ya taifa ya England chini ya miaka 21, Sydie Peck, mwenye umri wa miaka 22, ambaye anatajwa kuwa na kipaji kikubwa. (Teamtalk)

    Tottenham Hotspur inafikiria kuvunja mkataba wa mkopo wa winga wake Mikey Moore, mwenye umri wa miaka 19, anayeichezea Cologne ya Ujerumani. Hatua hiyo inaweza kumfungulia njia ya kurejea Rangers ya Scotland katika dirisha la Januari. (Teamtalk)

    Barcelona haina mpango wa kumuuza kiungo wake Gavi, mwenye umri wa miaka 22, licha ya kuwepo kwa taarifa za Bayern Munich na Napoli kutaka kumsajili kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania. (Marca – kwa Kihispania)

  6. Iran yashambulia kituo cha kijeshi cha Marekani Bahrain

    Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), katika taarifa iliyotolewa leo asubuhi,imesema kuwa, "imelenga na kuharibu" rada ya kutoa tahadhari za mapema ya majeshi ya Marekani nchini Bahrain, ikiwa kama jibu la shambulio la anga la ambalo Marekani ilitekeleza eneo la Sirik.

    Katika taarifa hiyo, IRGC imesema, "Hili ni onyo kali kwa adui kusitisha vitendo vyake vya uchochezi angani na na kujaribu kupitisha mafuta kimagendo katika Mlango-Bahari wa Hormuz.”

    “Endapo ukiukaji wa mipaka na uchokozi huo utajirudia, kikosi cha anga cha IRGC kiko tayari kwa makabiliano yasiyo na mipaka.”

    Saa moja kabla ya kutolewa kwa tangazo hilo, mashirika ya habari ya Iran yalikuwa yameripoti shambulio la anga katika eneo la Sirik.

    Baadaye, jeshi la IRGC ,lilithibitisha shambulio hilo na kusema kuwa mnara wa mawasiliano katika eneo hilo, lililoko karibu na pwani ya Ghuba ya Uajemi, ulikuwa miongoni mwa maeneo yaliyolengwa katika mashambulizi hayo.

  7. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Ijumaa ya leo