Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Marekani yaidhinisha uuzaji wa makombora ya Patriot kwa Ukraine

Marekani imeidhinisha uuzaji wa makombora 500 aina ya Patriot kwa Ukraine, ambazo ni silaha muhimu za kujilinda dhidi ya mashambulizi ya anga ya Urusi.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Khamenei aagiza Iran kujibu mara moja tishio lolote, popote litakapotokea

    Tovuti rasmi ya Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mojtaba Khamenei, imeripoti kuwa katika mkutano na makamanda wa Jeshi la Iran, amewaamuru kuchukua hatua za haraka dhidi ya tishio lolote kutoka kwa maadui, bila kujali mahali linapotokea.

    Kiongozi huyo amenukuliwa akisema kuwa iwapo kutatokea shambulio jingine la kijeshi au la kigaidi, Iran itaamua wakati, aina na namna ya kujibu.

    Khamenei amesisitiza kuwa Iran itajibu mara moja na kwa nguvu kubwa tishio lolote linaloikabili, na kwamba mipaka ya kijiografia haitakuwa kikwazo katika kuchukua hatua hizo.

    Kiongozi huyo pia ametoa wito wa kuimarishwa zaidi kwa uwezo wa kutoa ulinzi wa jeshi la Iran, mifumo ya kijasusi na teknolojia za kisasa za kijeshi.

    Katika mkutano huo, maafisa waandamizi wa jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) pia walitoa taarifa kuhusu usalama wa taifa, hali ya mipakani na maandalizi ya ulinzi.

    Tangu baba yake kuuawa katika vita vya siku 40 na yeye kurithi nafasi ya Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu, Mojtaba Khamenei hajaonekana hadharani, wala hakuna sauti au video yake iliyowahi kutolewa hadharani.

    Soma pia:

  2. Misri yaonya kuhusu madhara zaidi iwapo vita kati ya Iran na Marekani vitaendelea.

    Misri imeonya kwamba ina "wasiwasi mkubwa" kuwa ongezeko jipya la uhasama katika vita vya Marekani na Iran litakuwa na madhara makubwa zaidi.

    Akizungumza katika mkutano wa usalama wa 'IISS Manama Dialogue' nchini Bahrain hii leo, Badr Abdelatty, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri amesema kuwa "awamu ya pili ya vita itakuwa hatari zaidi, yenye uharibifu mkubwa zaidi, na haitaleta suluhisho yoyote. Ni lazima tujifunze kutokana na yaliyopita."

    Kauli yake inajiri huku mazungumzo ya kupatanisha Marekani na Iran yanaoongozwa na Qatar yakiendelea hii leo mjini Doha.

    Hapo jana, ujumbe wa Qatar ulifanya mazungumzo ya muda mrefu na maafisa wa Iran mjini Tehran.

    Shirika la habari la Axios limeripoti kuwa, ikinukuu chanzo kimoja cha kidiplomasia, kuwa wapatanishi wa Qatar walikuwa wakiwasiliana mara kwa mara na Ikulu ya Marekani wakati wa mkutano huo uliochukua saa 12 hapo jana.

    Chanzo hicho kilisema: "Maendeleo chanya yamepatikana na majadiliano yanaendelea ili kuwezesha kuafikiwa kwa makubaliano kati ya Marekani na Iran."

    Soma pia:

  3. Serikali ya Yemen: Msaada wa Iran kwa Wahouthi unahatarisha usafiri baharini

    Serikali ya Yemen imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kulaani mashambulizi ya mara kwa mara ya kundi la Houthi kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Aden nchini humo, na kuchukua hatua za kulinda raia na miundombinu ya raia, na kuhakikisha kwamba vikwazo vya mauzo na usafirishaji wa silaha vinatekelezwa.

    Katika barua, Mwakilishi wa kudumu wa Yemen katika Umoja wa Mataifa Abdullah Al-Saadi alisema kwamba Wahouthi walilenga Uwanja huo wa ndege mnamo Oktoba 28 kwa makombora ya kibalistiki, katika shambulio alilolielezea kama la sita katika mwezi mmoja, akiongeza kuwa mashambulizi hayo yalihatarisha maisha ya wasafiri na wafanyakazi na kuvuruga safari nyingi za ndege.

    Serikali hiyo imesema inachukulia mashambulizi katika uwanja wa ndege wa kiraia kama "uhalifu wa kivita na tishio la moja kwa moja kwa maisha ya abiria, wafanyakazi wa ndege, na usalama wa shughuli za anga.”

    Al-Saadi amesisitiza kwamba kulenga vituo vya raia mara kwa mara "kunahitaji kuchukuliwa hatua za kimataifa zinazozidi kauli na lawama, inahitaji hatua za vitendo zinazohakikisha ulinzi wa viwanja vya ndege vya kiraia na kuwawajibisha wale waliohusika na mashambulizi.”

    Serikali ya Yemen pia imeishutumu Iran kwa kutoa msaada wa kijeshi kwa Wahouthi, msaada ambao inasema ‘uliwezesha kundi hilo kupanua mashambulizi yake kwa kutumia makombora ya kibalistiki, ndege zisizo na rubani na boti zenye vilipuzi, na kutishia usafiri katika Bahari ya Shamu, Mlango wa Bahari wa Bab al-Mandab na Ghuba ya Aden’.

    Soma pia:

  4. DRC yarekodi zaidi ya vifo 5,000 kutokana na Ebola

    Mamlaka nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zinasema kuwa virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo sasa vimesababisha zaidi ya vifo 5,000; hali inayozua wasiwasi kuhusu ukubwa na kuendelea kuenea kwa mlipuko huo.

    Katika ripoti iliyotolewa siku ya Ijumaa, Jopo la Rais kuhusu Ebola lilieleza kuwa jumla ya maambukizi 10,351 yaliyothibitishwa yamerekodiwa tangu mlipuko huo uanze, ikiwemo vifo vya watu 5,026.

    Maafisa wa afya pia waliripoti visa vipya 77 pamoja na vifo vingine 34 kutokana na Ebola.

    "Mkoa wa Ituri bado ndio kitovu cha mlipuko huo, ukichangia asilimia 71% ya visa vyote vilivyothibitishwa na asilimia 36.4% ya visa vipya vilivyothibitishwa kote nchini," ripoti hiyo ilisema.

    Mlipuko huo umeathiri mikoa minane kati ya mikoa 26 ya DRC.

    Mamlaka za afya zinasema wagonjwa 1,101 kwa sasa wanapokea huduma katika vituo vya matibabu, huku watu 2,788 wakipona kutokana na ugonjwa huo.

    Ingawa juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zinaendelea, ukosefu wa usalama katika maeneo ya mashariki mwa DRC yaliyoathiriwa na mlipuko huo umezidisha ugumu wa juhudiz za wahudumu wa afya.

    Katika baadhi ya maeneo, timu za kukabiliana na ugonjwa huo zimekabiliwa na vitisho na mashambulizi kutoka kwa watu wanaopinga hatua za kudhibiti Ebola.

    Soma pia:

  5. Saudi Arabia yazuia wasafiri kutoka Kenya kuingia nchini humo

    Saudi Arabia imesitisha safari za raia wake kwenda nchini Kenya, na pia imesimamisha utoaji wa aina zote za visa kwa wasafiri wanaotoka nchini humo na kupiga marufuku kuingia kwa raia wa Kenya nchini humo.

    Ufalme huo umesema umechukua hatua hiyo ili kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Ebola.

    Wasafiri waliokaa nchini Kenya au nchi zilizoathirika na Ebola kwa siku 21 watazuiwa kuingia Saudi Arabia

    Mamlaka za Saudi Arabia zimesema hatua hizo ni sehemu ya mkakati wa tahadhari wa kulinda raia, wakazi na wageni waliomo nchini humo.

    Mwezi Juni, Saudi Arabia ilisitisha safari za raia wake kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda na Sudan Kusini, pamoja na kuzuia wasafiri kutoka mataifa hayo kuingia nchini humo, kutokana na wasiwasi kuhusu Ebola.

    Soma pia:

  6. Wakenya wakabiliwa na gharama ya juu ya maisha, mfumuko wa bei ukiongezeka

    Bei za juu za mafuta na chakula nchini Kenya zimesababisha mfumuko wa bei kuongezeka hadi asilimia 7.3% mwezi Oktoba, kutoka asilimia 6.8% mwezi Septemba.

    Hili ndilo ongezeko kubwa zaidi katika kipindi cha miaka mitatu. Mara ya mwisho kwa mfumuko wa bei kuwa sawa na huu ilikuwa Julai 2023 (7.3%).

    Kwa mujibu wa shirika la takwimu nchini humo KNBS, ongezeko hilo limetokana na bei za juu za chakula, usafiri, maji na umeme.

    Kwa mfano, gharama za usafiri ziliongezeka kwa 17.1% kati ya Oktoba 2025 na Oktobam waka 2026.

    Aidha takwimu hizo zinaonyesha kwamba katika miezi michache iliyopita, mfumuko wa bei umekuwa ukiongezeka.

    Mwezi Juni, kiwango hicho kilikuwa 6.4%, Julai 6.5%, kisha kikaongezeka hadi 6.6% mwezi Agosti na 6.8% Septemba.

    Soma pia:

  7. Tetesi za Soka: Man United yammezea mate Fermin Lopez wa Barcelona

    Manchester United inamuwinda kiungo wa Barcelona Fermin Lopez, mwenye umri wa miaka 23, raia wa Hispania, huku klabu hiyo ikilenga kuimarisha safu yake ya ushambuliaji katika dirisha la usajili la Januari

    Beki wa Manchester United, Lisandro Martinez, anatarajiwa kuondoka kwenye klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu, huku Barcelona na Atletico Madrid zikionyesha nia ya kutaka kumsajili mchezaji huyo wa Argentina mwenye umri wa miaka 28.

    Wakati huo huo, Arsenal inammezea mate mshambuliaji wa Club Brugge, Nicolo Tresoldi.

    Klabu kadhaa za Ligi Kuu England zinamfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Minnesota United, Kelvin Yeboah, mwenye umri wa miaka 26 huku Everton ikiwa inaongoza katika mbio za kumsajili raia huyo wa Ghana.

    Nayo Manchester United inazidi kuonyesha nia ya kumsajili beki wa Fulham, Calvin Bassey, raia wa Nigeria mwenye umri wa miaka 26.

    Winga wa Nottingham Forest, Omari Hutchinson, raia wa England mwenye umri wa miaka 23, anayeichezea AC Milan kwa mkopo, anatarajiwa kurejea katika klabu yake msimu ujao wa majira ya kiangazi. AC Milan imeanza kuelekeza nguvu zake katika kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Endrick, raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 20.

  8. Rais Ruto na Putin wakubaliana kusitisha uajiri wa Wakenya katika jeshi la Urusi

    Kenya na Urusi zimekubaliana kusitisha uajiri wa raia wa Kenya kujiunga na jeshi la Urusi, kufuatia mazungumzo kati ya Rais William Ruto na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin mjini Moscow.

    Makubaliano hayo yaliyofikiwa baada ya wawili hao kufanya mkutano katika Ikulu ya Kremlin, yataifanya Kenya kutambuliwa kama nchi isiyoruhusiwa kuajiriwa raia wake kujiunga na jeshi la Urusi.

    Hatua hiyo inalenga kufunga njia zilizokuwa zikitumika kuwaandikisha Wakenya kupigana katika vita kati ya Urusi na Ukraine.

    Makubaliano hayo yameafikiwa huku kukiwa na wasiwasi kuhusu kuajiriwa kwa mamia ya Wakenya katika jeshi la Urusi.

    Rais William Ruto amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin amethibitisha kujitolea kwa nchi yake kusitisha uajiri wa Wakenya kujiunga na jeshi la Urusi.

    "Nilimshukuru Rais Putin kwa kuthibitisha kuwa Wakenya hawataendelea kuandikishwa katika jeshi la Urusi, kwa kuwa Kenya imeainishwa kama nchi isiyoruhusiwa kuwa chanzo cha uajiri wa wanajeshi," alisema Rais Ruto.

    Aidha, Ruto ametangaza kuteuliwa kwa afisa wa jeshi anayeshughulikia masuala ya ulinzi katika Ubalozi wa Kenya mjini Moscow, ili kuratibu kurejea nchini kwa Wakenya walioenda Urusi kupigana vita.

    Afisa huyo atashirikiana na Wizara ya Ulinzi ya Urusi kuratibu taratibu za kuwarejesha Wakenya hao, kushughulikia fidia zao na kuhakikisha wanarejea nchini salama.

    Soma pia:

  9. Qatar yaendeleza juhudi ya kuwa mpatanishi kati ya Marekani na Iran

    Mazungumzo ya kuwapatanisha Marekani na Iran yanaoongozwa na Qatar, yanaendelea hii leo mjini Doha.

    Hapo jana, ujumbe wa Qatar ulifanya mazungumzo ya muda mrefu na maafisa wa Iran mjini Tehran.

    Shirika la habari la Axios limeripoti kuwa, ikinukuu chanzo kimoja cha kidiplomasia, kuwa wapatanishi wa Qatar walikuwa wakiwasiliana mara kwa mara na Ikulu ya Marekani wakati wa mkutano huo uliochukua saa 12 hapo jana.

    Chanzo hicho kilisema: "Maendeleo chanya yamepatikana na majadiliano yanaendelea ili kuwezesha kuafikiwa kwa makubaliano kati ya Marekani na Iran."

    Juhudi hizi mpya za kidiplomasia zinafuatia barua kutoka kwa Makamu wa Rais wa Marekani, J.D. Vance, kwenda kwa Mohsen Rezaei, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, akitoa wito wa kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

    Mazungumzo hayo yanafanyika wakati baadhi ya wachambuzi wakionya kuwa iwapo Warepublican watapata kipigo kikubwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, Rais Donald Trump anaweza kuagiza operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya Iran.

    Soma pia:

  10. Maandamano mapya yatarajiwa Ufaransa, serikali ikiahidi kudumisha usalama

    Ufaransa imesema iko tayari kuwatuma polisi 70,000 kudumisha usalama, huku maandamano mengine yakitarajiwa kufanyika hii leo.

    Maandamano hayo yamechochewa na hasira za wananchi wanaolalamikia kupanda kwa gharama ya Maisha na huduma duni za serikali za utawala wa Rais Emmanuel Macron.

    Maandamano hayo ya kitaifa, yanayotarajiwa kufanyika hii leo, usiku wa sherehe za Halloween, yanakuja wiki mbili baada ya ghasia na uporaji wa mali kuwashtukizia vikosi vya usalama, na kusababisha uharibifu wa maduka, majengo ya umma na biashara katika miji mbalimbali nchini Ufaransa.

    Waziri wa Mambo ya Ndani Laurent Nunez ameahidi kutoruhusu hali kama hiyo kujirudia.

    "Kila mtu yuko tayari kuhakikisha tunachukua hatua kali dhidi ya jaribio lolote la kuvuruga amani," Nunez alisema katika mkutano na waandishi wa habari mapema wiki hii.

    Soma pia:

  11. Marekani yaidhinisha uuzaji wa makombora ya Patriot kwa Ukraine

    Marekani imeidhinisha uuzaji wa makombora 500 aina ya Patriot kwa Ukraine, ambazo ni silaha muhimu za kujilinda dhidi ya mashambulizi ya anga ya Urusi.

    Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ameonya kuwa huenda ikachukua "miaka kadhaa" kabla ya makombora hayo kufika nchini humo.

    Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imesema makombora hayo ya kisasa ya kuzuia mashambulizi ya angani, aina ya PAC-3, yana thamani ya dola bilioni 2.1 na kwamba gharama yake italipwa kikamilifu na washirika wa Ukraine barani Ulaya na Canada.

    Zelensky amerudia wito wake kwa Marekani kuharakisha kutoa mifumo yake ya makombora ya Patriot, ambayo ndiyo silaha pekee yenye uwezo wa kuzuia makombora hatari ya Urusi aina ya ballistic.

    Hatua hii ya hivi karibuni imekuja kufuatia mvutano kati ya Zelensky na Rais wa Marekani Donald Trump mapema mwezi huu, baada ya Marekani kulegeza vikwazo dhidi ya Urusi kama sehemu ya makubaliano ya kupata mafuta ya dizeli kutoka Urusi.

    Trump aidha alisema ni wakati mwafaka kwa Ukraine kupata kiongozi mpya ambaye anaweza kufanikisha makubaliano ya kumaliza vita na Urusi.

    Urusi ilianzisha uvamizi mkubwa nchini Ukraine mwezi Februari mwaka 2022, baada ya awali kuteka eneo la Crimea na baadhi ya maeneo ya Donbas mashariki mwa Ukraine.

    Soma pia:

  12. Hujambo na karibu kwenye matangazo yetu ya moja kwa moja Jumamosi ya leo