Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Wahouthi waua 53 katika shambulizi dhidi ya kambi ya kijeshi

Video zilizothibitishwa na shirika la habari la Reuters zinaonyesha watu waliojeruhiwa na miili yenye damu ikiwa imetapakaa ardhini katika eneo hilo la mkoa wa Shabwa.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula & Mariam Mjahid

  1. Tetesi za Soka Ulaya: Beki huyu wa Hispania kutua Getafe?

    Beki mkongwe wa Hispania na Real Madrid, Sergio Ramos (40), huenda akajiunga na klabu ya Getafe ya Madrid baada ya kuwa mchezaji huru. (Sport)

    Bournemouth imeweka dau la zaidi ya pauni milioni 100 kwa kiungo wa England Alex Scott (23), anayewaniwa na Chelsea na Liverpool. (Football Insider)

    Kiungo wa Ujerumani Florian Wirtz (23) hana mpango wa kuondoka Liverpool, licha ya taarifa zinazomhusisha na Chelsea, inayofundishwa na kocha wake wa zamani wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso. (CaughtOffside)

    Tottenham Hotspur inaendelea kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Eintracht Frankfurt, Younes Ebnoutalib (23). (TeamTalk)

    Newcastle United imeimarisha ufuatiliaji wake kwa kiungo chipukizi wa Valencia, David Otorbi (19). (Marca)

    Tottenham pia inamwania kiungo wa Japan Yuito Suzuki (24) wa Freiburg, huku kocha Roberto De Zerbi akilenga kuongeza nguvu kikosini. (Fussball News kupitia CaughtOffside)

    Barcelona inamfuatilia beki wa Benfica, Daniel Banjaqui (18), lakini inakabiliwa na ushindani kutoka Newcastle United na Manchester United. (Ekrem Konur)Barcelona na Real Madrid zinachuana kuwania saini ya beki wa Stuttgart, Finn Jeltsch (20), huku Liverpool nayo ikifuatilia maendeleo yake. (Sport)Arsenal na Tottenham zinaendelea kumfuatilia beki chipukizi wa Barcelona, Xavi Espart (19), ingawa kipengele chake kikubwa cha kuachiliwa kinaweza kufanya uhamisho wake kuwa mgumu. (CaughtOffside)

    Soma zaidi:

  2. Misri kutoa msaada wa kijeshi kwa Saudi Arabia kudhibiti Wahouthi

    Misri imesema iko tayari kuipa Saudi Arabia msaada unaohitaji, ili kulinda usalama na kudumisha amani.

    Hatua hiyo huenda ikachochea mvutano zaidi, katika vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, huku waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen wakizidisha mashambulizi dhidi ya Saudi Arabia.

    Rais wa Misri, Abdel Fattah al-Sisi, ameliomba bunge la taifa hilo kuitisha kikao cha dharura ili kuidhinisha jeshi la nchi hiyo, ambalo ni miongoni mwa majeshi makubwa zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu, kusaidia kulinda mshirika wake wa karibu, iwapo Saudi Arabia itaomba msaada huo.

    Bunge hilo litapiga kura kuhusu ombi hilo siku ya Jumapili, huku majadiliano yakitarajiwa kuendelea.

    Msaada wowote wa kijeshi kutoka Misri kwa Saudi Arabia unaweza kuashiria kuongezeka kwa kiwango cha majeshi yanayopigana vita hivyo vinavyoendelea kati ya waasi wa Kihouthi na Saudi Arabia.

    Katika siku za hivi karibuni, waasi wa Kihouthi wameishambulia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Riyadh pamoja na kampuni ya mafuta inayomilikiwa na serikali ya Saudi Arabia, Saudi Aramco, huku mapigano mapya yakizuka kati ya Wahouthi na vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia.

    Soma pia:

  3. Ndege ya Austrian Airlines yatua kwa dharura Bulgaria baada ya tishio la bomu

    Ndege ya shirika la Austrian Airlines iliyokuwa ikisafiri kutoka Israel kuelekea Austria, imelazimika kubadili njia na kutua nchini Bulgaria ghafla, baada ya taarifa za tishio la bomu ndani ya ndege hiyo kutolewa.

    Ndege hiyo aina ya Airbus A320, ilikuwa ikisafiri kutoka Tel Aviv nchini Israel, kuelekea Vienna jana usiku, lakini ilitua kwa dharura katika mji wa Sofia, ambako abiria walitolewa ndani ya ndege hiyo, hii ni kulingana na taarifa iliyotolewa na Wizara ya Uchukuzi ya Bulgaria.

    Jeshi la anga la Bulgaria lilituma ndege ya kivita aina ya MiG-29 kuisindikiza ndege hiyo, hadi ilipotua.

    Hakuna majeruhi walioripotiwa, na uchunguzi umeanzishwa kuhusu tukio hilo.

    Tukio hilo linajiri mwezi mmoja tu, baada ya rubani mmoja kujaribu kuteka nyara ndege ya Flydubai, iliyokuwa ikielekea Tel Aviv kwa kumshambulia rubani mkuu. Hata hivyo, wafanyakazi wa ndege hiyo pamoja na abiria walifanikiwa kumdhibiti mshambuliaji huyo, na ndege hiyo ikatua salama nchini Saudi Arabia.

    Vyombo vya habari vya Bulgaria na Israel viliripoti kuwa kulikuwa na tishio la bomu kwa ndege hiyo.

    Shirika la Austrian Airlines limethibitisha kuwa tishio hili liliondolewa, bila kutoa maelezo zaidi. Msemaji wa shirika hilo aliliambia shirika la habari la AFP kuwa kulikuwa na abiria 51 na wahudumu sita ndani ya ndege hiyo.

    Soma pia:

  4. Mchungaji Paul Mackenzie kusomewa hukumu katika mauaji ya Shakahola

    Mchungaji mwenye utata kutoka nchini Kenya, anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji ya watoto 191, katika mojawapo ya matukio mabaya zaidi yanayohusishwa na madhehebu ya kidini katika historia, anatarajiwa kusomewa hukumu yake hii leo.

    Mchungaji Paul Mackenzie anadaiwa kuwaongoza mamia ya wafuasi wake katika msitu mmoja pwani ya Kenya, na kuwashawishi kufunga hadi kufa ili wakutane na Yesu.

    Aidha mchungaji huyo pia aliwashawishi wafuasi wake kukataa matibabu ya kisasa na hata elimu.

    Katika mahubiri yake, mara nyingi alionya kuwa mwisho wa dunia ulikuwa umekaribia na kwamba shetani alikuwa ameingia katika maisha ya kisasa.

    Mwaka wa 2023, polisi waligundua miili iliyokuwa imeoza ya wafuasi wake zaidi ya 400 katika msitu wa Shakahola, pwani ya Kenya, hali iliyochochea uchunguzi kufanywa na kufunguliwa kwa kesi mahakamani.

    Mackenzie amekanusha mashtaka yote dhidi yake, akidai kuwa hakuwalazimisha wafuasi wake kufunga hadi kufa.

    Polisi bado wanafanya vipimo vya vinasaba vya DNA ili kutambua mabaki ya waliofariki kabla ya familia zao kuruhusiwa kuyazika.

    Soma pia:

  5. Visa vya Ebola vyaongezeka nchini Kenya na kufikia nane

    Kenya imethibitisha kisa kipya cha ugonjwa wa Ebola, na kupelekea jumla ya visa vya maambukizi kufikia nane.

    Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini Kenya, Dkt. Patrick Amoth, aliambia kituo cha televisheni cha Citizen TV hapo jana kuwa Wizara ya Afya iliwapima watu 38 na mmoja hapo jana na mmoja wao akapatikana na virusi vya Ebola vya aina ya Bundibugyo.

    Kisa hiki kipya ni cha mhudumu anayewahudumia wagonjwa waliokuwa wamewekwa karantini.

    Amoth amesema mgonjwa huyo ametengwa na anapokea matibabu maalumu, ambayo yametolewa kwa wagonjwa wengine saba waliopatikana na virusi hivyo.

    Wagonjwa waliothibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Ebola, wamekuwa wakipokea matibabu aina ya ‘Monoclonal Antibodies’, ambayo kitaalamu ni aina yap rotini ambayo husaidia mwili kuwa na kinga Zaidi ya kupambana na maambukizi. Kulingana na Dkt Amoth, wagonjwa hao wanaopokea aina hiyo ya matibabu wamekuwa wakiendelea vyema na kupata nafuu.

    Kisa hicho kipya kinajiri siku tu moja baada ya Kenya kutangaza visa vingine vinne vipya vya Ebola, vikiwemo vya mwanaume aliyekuwa na uhusiano wa karibu wa kifamilia na mgonjwa wa kwanza nchini humo, pamoja na wahudumu watatu wa afya waliomhudumia alipokuwa hospitalini.

    Amoth pia ametuliza hofu kuhusu kuenea kwa ugonjwa huo katika jamii, akisema uwezekano wa watu waliowekwa karantini kueneza virusi hivyo kabla ya kutengwa ulikuwa mdogo.

    “Walianza kuonyesha dalili baadaye sana, siku ya tisa au ya kumi. Kwa hiyo, wakati walipokuwa katika jamii, hawakuwa na dalili zozote. Hivyo, uwezekano wa kumwambukiza mtu mwingine ulikuwa mdogo sana,” alisema Amoth.

    Kenya ilithibitisha kisa chake cha kwanza cha Ebola tarehe sita mwezi Oktoba. Mgonjwa wa kwanza alikuwa mwanaume aliyekuwa akiishi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

    Aidha, kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya Ebola nchini Kenya, mkutano mkuu wa Kilimo wa Africa International Agricultural Expo 2026 (AIAE), uliokuwa ufanyike katika jumba la KICC nchini Nairobi, umehairishwa hadi mwaka ujao.

    Soma pia:

  6. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumatatu ya leo