Trump aidhinisha viza kwa mama wa kijana Mghana aliyeuawa Marekani
Rais wa Marekani Donald Trump amekubali kutoa viza kwa mama wa kijana Mghana, Javits Frimpong, aliyeuawa kwa kupigwa risasi katika eneo la Bronx, New York, ili aweze kusafiri kwenda Marekani kumuaga mwanawe.
Hatua hiyo imekuja baada ya mazungumzo ya simu kati ya Meya wa New York, Zohran Mamdani, na Trump.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, Mamdani alisema mama huyo anastahili kupata fursa ya kumuomboleza mwanawe ana kwa ana.
Doris Adu Gyamfi, mama wa kijana huyo, anayeishi Kumasi nchini Ghana, anatarajiwa kuwasili Accra kwa ajili ya kuanza mchakato wa kupata viza.
Frimpong, mwenye umri wa miaka 15, alipigwa risasi na kuuawa Alhamisi asubuhi alipokuwa njiani kuelekea shuleni.
Polisi wanasema bado wanawatafuta washukiwa watatu waliotoroka baada ya tukio hilo, huku picha za kamera za usalama zikionyesha kijana huyo akijaribu kukimbia kuokoa maisha yake.
Serikali ya Ghana imelaani mauaji hayo na kuitaka Marekani kufanya uchunguzi wa kina ili kuhakikisha wahusika wanawajibishwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, amesema serikali itaendelea kulinda na kutetea maslahi ya raia wake popote walipo.
Mauaji hayo yamezua maombolezo makubwa katika jamii ya Waghana wanaoishi Bronx. Hadi sasa, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.