Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , Vita vya Iran ni kama vimekwisha - Trump

Akizungumza na wanahabari katika Ikulu ya White House, Trump amesema kuwa uwezekano wa Marekani kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Iran ni "mdogo sana".

Muhtasari

Trump aashiria kumalizika kwa vita dhidi ya Iran

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula

  1. Trump: FBI inachunguza uhusiano wa mkuu wa Nvidia na jasusi wa China

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) linafanya uchunguzi kuhusu uhusiano kati ya afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Nvidia na mwanamke anayedaiwa kuwa jasusi wa China.

    Trump amesema amezungumza na Jensen Huang, afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Nvidia, kufuatia taarifa ambayo Marekani inaamini kuwa Huang alikuwa mlengwa wa operesheni ya kijasusi ya China.

    "Nilimuuliza Je, ulikuwa na habari yoyote kwamba alikuwa jasusi?' Akajibu, 'Sikuwa na habari yoyote kwamba alikuwa jasusi', na kwa kweli namwamini," Trump aliwaambia waandishi wa habari.

    Beijing imekanusha madai kwamba Huang alikuwa mlengwa wa operesheni ya kijasusi, huku Wizara ya Mambo ya Kigeni ya China ikisema madai hayo "hayana msingi wowote, ni ya kuichafua na kuipaka matope China".

    Kampuni ya Nvidia, imeagiza uchunguzi huru kuhusu sakata linalomhusisha Alice Huang, anayedaiwa kuwa jasusi wa China.

    Aidha kampuni hiyo imeongezea kuwa haina sababu ya kuamini kuwa siri za kampuni hiyo au usalama wa taifa uliathiriwa.

    Nvidia ni kampuni ya pili kwa ukubwa wa thamani duniani baada ya Apple. Kampuni hiyo hutengeneza chipu za kompyuta ambazo zimekuwa sehemu muhimu ya teknolojia ya akili unde (AI).

  2. Mazungumzo ya amani Ukraine yaanza upya, pande zote zikilegeza misimamo yao

    Wapatanishi wa Marekani wamesema kuwa Moscow na Kyiv zimeonyesha kulegeza makali yao, katika mazungumzo kuhusu suala la nani atadhibiti maeneo ya mashariki mwa Ukraine baada ya vita.

    Kauli hizo zimetolewa siku moja kabla ya kuanza kwa mazungumzo ya kwanza, yanayolenga kumaliza vita vya Ukraine.

    Maafisa waandamizi kutoka Moscow, Kyiv na Washington wanakutana mjini Abu Dhabi, vita vya Ukraine vikikaribia kuingia mwaka wa tano sasa.

    Jared Kushner, mkwe wa Rais Donald Trump, pamoja na mjumbe maalumu Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, wamesema mazungumzo hayo yanalenga kushughulikia "masuala ya usalama baada ya vita" kwa Urusi na Ukraine.

    "Sehemu muhimu ya mchakato huu ni kuhimiza pande zote kuanza kufikiria kwa uzito kuhusu kitakachotokea baada ya vita," Kushner aliandika kwenye mtandao wa X.

    Hata hivyo, misimamo ya Moscow na Kyiv kuhusu namna ya kumaliza vita hivyo bado unatofautiana pakubwa.

    Mojawapo ya maeneo muhimu yanayozua mzozo ni eneo la Donetsk, mashariki mwa Ukraine, ambalo kwa sasa sehemu kubwa linadhibitiwa na Urusi.

  3. Tetesi za usajili: Atletico Madrid yamtaka Zubimendi wa Arsenal

    Kiungo wa Arsenal na timu ya taifa ya Hispania, Martin Zubimendi, 27, ametajwa kuwa mmoja wa wachezaji wanaoweza kujiunga na Atletico Madrid katika dirisha dogo la usajili la Januari. (Sport)

    Mustakabali wa mshambuliaji Viktor Gyokeres wa Sweden na kiungo Mikel Merino wa Hispania katika klabu ya Arsenal nao mguu ndani mguu nje, huku klabu hiyo ikitafuta namna ya kuweka sawa matumizi yake ya fedha. (AS)

    Hata hivyo, Arsenal imepiga hatua katika mazungumzo ya kuongeza mikataba ya nahodha wake Martin Odegaard, 27, beki Jurrien Timber, 25, na kiungo Declan Rice, 27. Makubaliano ya wachezaji hao watatu yanatarajiwa kukamilika kabla ya Januari. (Teamtalk)

    Leeds United inapanga kuongeza kasi ya mazungumzo ya kumpa mkataba mpya mshambuliaji Dominic Calvert-Lewin, 29, utakaomuweka klabuni hapo hadi mwaka 2030. (Teamtalk)

    Beki wa Aston Villa na timu ya taifa ya Uholanzi, Ian Maatsen, 24, yuko katika hatua za mwisho kusaini mkataba mpya na klabu hiyo. (Football Insider)

    Everton ni miongoni mwa klabu kadhaa za Ulaya zinazovutiwa na winga wa Flamengo na timu ya taifa ya Brazil, Samuel Lino, 26. (Four Four Two)

    Manchester United na Liverpool zimeonyesha nia ya kumsajili beki wa Juventus na timu ya taifa ya Italia, Andrea Cambiaso, 26. (TuttoJuve)

    Barcelona imeonyesha nia ya kumsajili beki wa Bayern Munich, Jonathan Tah, 30. Hata hivyo, mabingwa hao wa Ujerumani hawana mpango wa kumuuza mchezaji huyo, ambaye pia hana nia ya kuondoka klabuni hapo. (Sky Sports Germany)

    Bayern Munich inajiandaa na uwezekano wa kustaafu kwa kipa wake Manuel Neuer, 40, mwishoni mwa msimu huu. Klabu hiyo inawafikiria Loris Karius, 33, wa Schalke 04 na Bernd Leno, 34, wa Fulham kama chaguo mbadala kuongeza ushindani ama kuwa mbadala wa Jonas Urbig, 23. (Sky Sports Germany)

    Nchini Italia, Napoli inapanga kumsajili mshambuliaji chipukizi wa Monza, Gustavo Varela, 21, raia wa Ureno, ambaye pia anawaniwa na vilabu vingine kadhaa. (Gazzetta dello Sport)

  4. Trump atangaza vita dhidi ya Iran vimekwisha kijeshi baada ya kukutana na Waziri Mkuu wa Qatar

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa vita dhidi ya Iran "kwa upande wa kijeshi vimekwisha", na kuelezea kuwa wamepiga hatua, katika mazungumzo ya kumaliza mzozo huo eneo la Mashariki ya Kati.

    "Tutadumisha hali ilivyo sasa,na tunafanya hivyo kwa ombi la nchi jirani za Iran."

    Akizungumza na wanahabari katika Ikulu ya White House, Trump alisema kuwa uwezekano wa Marekani kuanzisha tena mashambulizi dhidi ya Iran ni "mdogo sana".

    Aidha, alionya kuwa Marekani iko tayari kijeshi kuchukua hatua iwapo hali itabadilika.

    Maafisa wa Iran wamekuwa wakitilia shaka mara kwa mara kauli za rais huyo wa Marekani kuhusu uwezekano wa kumaliza mzozo huo.

    Alipoulizwa kwa nini hatangazi rasmi kumalizika kwa vita hivyo, Trump alisema baadhi ya washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba ya Uajemi bado wanaweza kukabiliwa na mashambulizi ya Iran.

    "Tuna washirika wazuri sana huko na tunapaswa kuhakikisha wapo salama," alisema Trump.

    Trump alikutana na Waziri Mkuu wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman Al Thani, katika Ofisi ya Oval ya Ikulu ya White House hapo jana, ambapo walijadiliana kuhusu kumaliza vita vya Iran.

    Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, waziri mkuu wa Qatar alisema alifanya mazungumzo chanya na Trump pamoja na Makamu wa Rais JD Vance kuhusu kufikia makubaliano na kurejesha amani katika eneo hilo.

    Saudi Arabia, Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) ni miongoni mwa washirika wa Marekani katika eneo la Ghuba ambao wamekabiliwa na mashambulizi ya Iran wakati wa vita. Pia, tishio la mashambulizi limeathiri pakubwa usafiri wa anga katika eneo hilo.

    Trump amekuwa akiashiria kupunguza makali ya mzozo na Iran tangu chama chake cha Republican kishindwe katika uchaguzi wa katikati ya muhula uliofanyika Novemba 3.

  5. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja Jumanne ya leo