Urusi yaishambulia Kyiv kwa makombora licha ya kukubali kushiriki katika mazungumzo ya amani
Mji mkuu wa Ukraine, Kyiv, umeshambuliwa kwa makombora saa chache baada ya Urusi kusema kuwa iko tayari kurejea katika meza ya mazungumzo ya amani, na hata Rais wa Marekani Donald Trump kusema kuwa dunia iko karibu kumaliza vita hivyo.
Nyumba kadhaa zililengwa wakati wa shambulio hilo jana usiku, na kusababisha watu sita kujeruhiwa, kulingana na taarifa iliyotolewa na Meya wa Kyiv, Vitaliy Klitschko.
Shambulio hilo la Urusi, limetokea wakati kumekuwa na juhudi mpya za kidiplomasia zinazoongozwa na wajumbe wa Donald Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner.
Witkoff alikutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini St Petersburg hapo jana, siku moja tu baada ya kukutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.
Mazungumzo ya awali ya pande hizo tatu yalikuwa yamesitishwa mwezi Februari, na tangu wakati huo Urusi imekuwa ikiongenza mashambulizi yake huku Ukraine ikikabiliwa na upungufu wa makombora ya kuzuia mashambulizi yaliyokuwa yakitolewa na nchi za Magharibi.
Haijabainika wazi ni mapendekezo gani hasa ambayo Witkoff aliwasilisha kwa Putin hapo jana.
Hata hivyo, Mshauri wa Putin, Yuri Ushakov, alisema mapendekezo yaliyowasilishwa hayakuwa na manufaa makubwa.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mazungumzo hayo hapo jana katika mji wa St Petersburg, Yuri Ushakov alisema kuwa duru nyingine ya mazungumzo inaweza kufanyika tarehe 10 mwezi Novemba mjini Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Soma pia: