Ndugu waliotelekezwa wakiwa wachanga ndani ya mifuko wakutana tena

Mkusanyiko wa picha unaowaonyesha David McBride na Helen Ward wakiwa watoto na watu wazima. Upande wa kushoto kuna picha ya gazeti ya rangi nyeusi na nyeupe inayomwonyesha mtoto David akiwa amefungwa kwenye blanketi. Katikati, David na Helen wakiwa watu wazima wamekaa pamoja nje, wakitabasamu kuelekea kwenye kamera. Upande wa kulia kuna picha ya gazeti ya rangi nyeusi na nyeupe inayomwonyesha mtoto Helen akiwa amelala kwenye kitanda cha watoto.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 8

"Nilipatikana ndani ya begi la kitambaa chenye michoro ya miraba, nikiwa nimevalishwa nguo za bluu"

David McBride alilelewa katika familia yenye upendo na malezi mema jijini Belfast, Ireland Kaskazini. Tangu akiwa mdogo, alijua kuwa alikuwa mtoto wa kuasiliwa.

Hata hivyo, hakutambua jinsi ambavyo taarifa kuhusu asili yake zilivyokuwa chache hadi alipokuwa na umri wa miaka 15. Wakati huo, alituma maombi ya kupata cheti chake cha kuzaliwa ili aweze kujiunga na jeshi.

Cheti hicho kilikuwa karibu tupu. Majina ya wazazi wake wa kumzaa yalionyeshwa kuwa hayajulikani, hali kadhalika mahali alipozaliwa na hata tarehe yake ya kuzaliwa.

Baba yake mlezi alimweleza machache aliyoyafahamu. David alikuwa mtoto aliyeokotwa baada ya kutelekezwa. Akiwa mchanga, alipatikana ameachwa kwenye kiti cha mbele cha gari lililokuwa limefunguliwa milango.

Mtoto mdogo anaonekana katika picha ya karibu ya mtindo wa zamani, ya rangi nyeusi na nyeupe; ameelekeza uso wake kwenye kamera na amevaa koti au sweta yenye michoro ya miraba juu ya shati lenye kola na tai. Nyuma yake kuna ukuta wa mawe au matofali wenye muundo wa kipekee.
Maelezo ya picha, David McBride alikuwa na utoto wenye furaha akiwa na wazazi wake wa kulea.

David na baba mlezi waliamua kwa pamoja kuanza kuchunguza historia yake. Walianza kwa kutafuta taarifa katika maktaba ya umma ya eneo lao, wakisoma kwa makini makala na taarifa zilizokuwa zimechapishwa kwenye magazeti.

Wakati David alipopatikana, kisa chake kiliripotiwa sana na vyombo vya habari kwa sababu visa vya watoto wachanga kutelekezwa vilikuwa nadra sana nchini Ireland Kaskazini wakati huo.

David anaeleza kuwa wakati huo kanisa lilikuwa likitoa msaada au angalau makazi kwa wanawake na watoto wao wachanga, hasa wale waliozaliwa nje ya ndoa.

"Endapo mwanamke angepata ujauzito nje ya ndoa, jamii ilimtenga. Tatizo lilikuwa tabia ya kuficha kila kitu," anasema.

Makala za magazeti hazikuwapa taarifa nyingi, lakini zilimsaidia kufahamu kuwa alikuwa ametunzwa vizuri.

"Nilikuwa nalishwa vizuri na kutunzwa ipasavyo."

Alikisia kuwa huenda mama yake alikuwa msichana mdogo aliyekuwa na hofu wakati alipomtelekeza. Hivyo, aliamua kujaribu kumtafuta.

Ndugu waliounganishwa na mifuko yenye michoro ya miraba

Mwanamume na mwanamke (David na Helen) wamesimama bega kwa bega nje, katika eneo linaloonekana kuwa mtaa wa makazi. Wote wawili wanatabasamu huku wakitazama moja kwa moja kwenye kamera, na mkono wa David umewekwa juu ya bega la Helen. David amevaa sweta ya bluu yenye kofia, ana nywele fupi na ndevu. Helen ana nywele ndefu nyeusi na amevaa jaketi la jinsi la rangi ya bluu hafifu juu ya vazi la ndani la rangi ya bluu iliyopauka; pia anaonekana akiwa na mkoba mdogo wenye michoro unaoning'inia begani mwake.
Maelezo ya picha, David na Helen wote walipatikana wakiwa watoto wachanga, wakiwa wamefungwa kwa namna inayofanana.

Miaka ilipita, lakini licha ya juhudi zake za kutafuta familia yake na hata kushiriki katika kipindi cha BBC kuhusu watoto waliotelekezwa wakiwa wachanga, David hakupata majibu mengi.

Hatimaye, kwa kutiwa moyo na dada yake wa kulelewa, aliamua kufanya kipimo cha vinasaba (DNA).

Matokeo yake yalibadilisha kila kitu. Aligundua kuwa alikuwa na dada yake wa kumzaa.

"Nilifurahia sana... ilikuwa kana kwamba Krismasi ilikuwa imewadia," anasema.

Dada huyo aliitwa Helen Ward. Hata hivyo, badala ya kumpa majibu kuhusu mama yao, Helen naye alikuwa na maswali mengi, kwani pia alikuwa ametelekezwa akiwa mchanga.

"Nilipatikana ndani ya begi la kijani lenye michoro ya miraba, kwenye kibanda cha simu," anasema Ward. "Jambo la kwanza nililofikiria ni kwamba sisi ni ndugu waliookotwa ndani ya mifuko yenye michoro ya miraba."

Mwanamke aliyevaa blauzi nyekundu angavu na mkufu (Helen) amesimama nje mbele ya mimea mingi ya kijani, akiwa ameshikilia kipande kikubwa cha gazeti katika usawa wa kifua chake. Kipande hicho kina picha ya mtoto mchanga na kichwa cha habari kinachoonekana wazi, “MTOTO ALIYENYIMWA UTAMBULISHO”, pamoja na maandishi mengine ya gazeti yanayosomeka kwa sehemu.
Maelezo ya picha, Alipopata watoto, Helen alitaka kujua zaidi kumhusu mama yake mwenyewe.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hata hivyo, hawakuwa pacha.

Walizaliwa kwa tofauti ya miaka saba na kupatikana katika maeneo tofauti, kila mmoja upande wake wa mpaka kati ya Ireland Kaskazini na Jamhuri ya Ireland.

Licha ya hayo, kulikuwa na mambo mengi yanayofanana katika simulizi zao.

"Nilipatikana na dereva wa lori," anasema Ward. "Ndani ya begi kulikuwa na chupa yenye maziwa ya uvuguvugu na nguo za kubadilisha. Nilikuwa nimevalishwa vizuri na kufunikwa kwa nguo za kutosha kunipa joto."

Kama David, Helen alikulia katika familia ya walezi iliyompa upendo na malezi mazuri. Hata hivyo, alipokuwa mama mwenyewe, alihisi haja ya kutafuta taarifa kuhusu mama yake mzazi.

Aliwasiliana na mfanyakazi wa ustawi wa jamii katika eneo alilopatikana na kuonyeshwa cheti cha kuzaliwa kilichofanana na kile ambacho David alikuwa amekipata miaka mingi iliyopita.

Cheti hicho kilionyesha kuwa mama na baba yake hawakujulikana, huku maelezo yakisema mtoto alipatikana akiwa ametelekezwa kwenye kibanda cha simu.

"Nilihuzunika sana. Unakuwa na maswali mengi, lakini ni vigumu sana kupata majibu," anasema.

Katika miaka iliyofuata, Helen naye aliendelea na juhudi za kutafuta familia yake. Alisimulia kisa chake katika kipindi cha redio kilichowapa wasikilizaji nafasi ya kupiga simu, na hatimaye akawapata polisi aliyeshughulikia kesi yake mwaka 1969 pamoja na dereva wa lori aliyemkuta kwa mara ya kwanza.

Hata hivyo, ni baada ya rafiki yake kumnunulia kifaa cha kupima DNA nyumbani ndipo alipompata kaka yake aliyekuwa amempoteza kwa miaka mingi.

"Haikuaminika. Nilikuwa najibana ili kuhakikisha kuwa sikuwa naota," anasema.

Walipokutana ana kwa ana na kutambua kufanana kwa baadhi ya maumbile yao, hisia zilikuwa nyingi kiasi cha kuwashinda.

"Unajaribu kuelewa kila kitu kinachotokea. Una mambo mengi sana ya kusema kiasi kwamba unahisi utapasuka," anakumbuka Helen.

"Mara tu tulipokutana, tulihisi kana kwamba kila kitu kilichokuwa kimetuzunguka kilitoweka," anasema David.

Safari ya kuwatafuta wazazi wao

Hata hivyo, wakati safari moja ya kutafuta majibu ilipofikia mwisho, nyingine ilianza. Safari hii walitaka kuwafahamu wazazi wao.

Hatimaye, waligundua kuwa mama yao alikuwa amefariki akiwa na umri wa miaka 90, muda mfupi tu kabla ya wao kukutana. Baba yao alikuwa amefariki miaka kadhaa mapema.

Licha ya kutoweza kukutana na wazazi wao, waliweza kuunganisha baadhi ya vipande vya historia ya familia yao.

Watu wazima wawili (David na Helen) wamesimama bega kwa bega mbele ya mti mkubwa wa Krismasi uliopambwa, wakiwa wameelekeza nyuso zao kwenye kamera na wamevaa mavazi ya kawaida ya rangi nyeusi; David amevaa sweta nyeusi na suruali ya jeans, huku Helen akiwa amevaa blauzi nyeusi na sketi yenye michoro. Kwenye mti huo kuna taa ndogo za mapambo pamoja na mipambo ya duara ya rangi nyekundu na dhahabu.
Maelezo ya picha, David anasema jitihada zao za kutafuta majibu kutoka kwa wazazi wao 'hazikuwa zimepangwa kutokea'

Hata hivyo, wakati safari moja ya kutafuta majibu ilipofikia mwisho, nyingine ilianza. Safari hii walitaka kuwafahamu wazazi wao.

Hatimaye, waligundua kuwa mama yao alikuwa amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 90, muda mfupi tu kabla ya wao kukutana. Baba yao alikuwa amefariki miaka kadhaa mapema.

Licha ya kutoweza kukutana na wazazi wao, waliweza kuunganisha baadhi ya vipande vya historia ya familia yao.

"Mama yetu alikuwa mwanamke wa mashambani, huku baba yetu akiwa mtu wa mjini. Mama alikuwa mdogo kwake kwa miaka mingi. Tamaa ya maisha ya mjini ilimfanya ahame kutoka pwani ya magharibi ya Ireland na kwenda Dublin. Baba yetu alikuwa kiongozi wa bendi mjini Dublin. Inaonekana walikutana wakati mama alipokuwa akienda kwenye kumbi za dansi. Uhusiano wao wa kimapenzi uliendelea kwa miaka 40 au zaidi," anasema David.

David anaamini kuwa uhusiano huo uliodumu kwa muda mrefu unaashiria kuwa wazazi wake walipendana. Hata hivyo, ulikuwa uhusiano wenye changamoto nyingi.

Baba yao alikuwa ameoa na pia alikuwa Mprotestanti, huku mama yao akiwa Mkatoliki.

Wakati huo, jamii ya Ireland ilikuwa imegawanyika kwa misingi ya dini na bado ilikuwa na mitazamo mikali kuhusu masuala ya kijamii. David anaamini kuwa wazazi wake walivunja miiko mingi ya jamii.

"Mkatoliki na Mprotestanti. Mtoto kuzaliwa nje ya ndoa... walikuwa na nafasi gani ya kufanikiwa?" anauliza.

Siri nyingine ya familia yafichuka

Watu wazima watatu wamesimama bega kwa bega mbele ya mti mkubwa wa Krismasi uliopambwa ndani ya nyumba, wakiwa wameelekeza nyuso zao kwenye kamera. John, aliye upande wa kushoto, amevaa shati lenye rangi angavu na zipu kifuani pamoja na suruali ya jeans; katikati, Helen amevaa koti la rangi nyeusi juu ya vazi la rangi angavu; na David, aliye upande wa kulia, amevaa sweta ya rangi nyeusi na suruali. Mti huo umepambwa kwa maua meupe, mapambo ya rangi ya dhahabu na fedha, utepe, na taa.
Maelezo ya picha, John (kushoto), Helen (katikati) na David (kulia) sasa wanasherehekea familia ambayo hawakujua kamwe kuwa wanayo.

Hata hivyo, kulikuwa na tukio lingine la kushangaza zaidi.

Helen alikumbuka simulizi alilowahi kulisoma wakati wa miaka yake ya utafiti, na likamfanya ajiulize iwapo huenda alikuwa na kaka mwingine.

"Simulizi hilo lilihusu mtoto mchanga aliyepatikana mwaka 1965 ndani ya kibanda cha simu. Alikuwa ndani ya begi pamoja na chupa yenye maziwa ya uvuguvugu. Hivyo, vipande vyote vya historia yake vilikuwa sehemu ya simulizi langu na la David pia," anasema.

Mwanamke mmoja kijana aliyekuwa akiishi Australia alitazama kipindi cha televisheni ambacho David na Helen walishiriki kusimulia safari yao ya kutafuta familia. Kipindi hicho kilimfanya aanze kujiuliza zaidi kuhusu baba yake mzazi, John, aliyekuwa na asili ya Ireland.

Baadaye ilibainika kuwa John alikuwa kaka yao, hivyo watatu hao walikuwa ndugu wa tumbo moja.

"Yeye ndiye aliyekuwa mtoto wa katikati," anaeleza Helen. "Tulipoketi pamoja kwa mara ya kwanza, ilikuwa kama ndoto. Unaitazama familia yako na ghafla maswali elfu moja yanajitokeza tena. Lakini kwa wakati huo, ilikuwa furaha isiyoelezeka."

Picha tatu tofauti za kireasmi, zenye rangi nyeusi na nyeupe, zinawaonyesha ndugu hao watatu wakiwa bado watoto. Katika picha ya upande wa kushoto, John amevaa shati, tai, na sweta, huku akitabasamu kwa upana kuelekea kwenye kamera. Ana umri wa takriban miaka 4. Katikati, yupo Helen mwenye umri wa miezi 6 hadi 12; amevaa gauni lenye mapambo ya kushonwa na anaonekana kuwa na sura ya umakini mkubwa. Upande wa kulia, David ana tabasamu la utundu usoni, likionyesha mapengo ya meno. Kola ya vazi lake ina mapambo ya kushonwa.
Maelezo ya picha, John Dowling, Helen Ward, na David McBride wakiwa watoto wachanga

Hata hivyo, maswali ambayo hayajapata majibu na kile Helen anachokiita mazungumzo ambayo hayakuwahi kufanyika na wazazi wao, yameacha pengo ambalo wanakiri huenda lisijazwe kamwe.

Licha ya yote hayo, Helen na David wanasema hawawezi kumhukumu mama yao kwa maamuzi aliyoyafanya.

"Lazima ilikuwa hali ya kutisha kwake kuwatelekeza watoto wake watatu, muda mfupi tu baada ya kuwabeba tumboni na kuwazaa," anasema Helen.

David anakumbuka kutazama video ya mama yao akiwa mzee, akishikilia mwanasesere na kukataa kuuachia.

"Hujiuliza iwapo, akikaribia kufariki, akili yake ilikuwa ikimwambia: 'Huyu ni mtoto wangu. Nimepoteza watoto watatu na sitakubali mninyang'anye hata huyu,'" anasema David.