'Jeshi la Lula':: Siri ya nguvu ya WhatsApp katika siasa za Brazil

    • Author, Julia Braun
    • Author, Rute Pina
    • Author, Luiz Fernando Toledo
    • Nafasi, BBC News Brasil
    • Akiripoti kutoka, London & São Paulo
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kundi la WhatsApp lililoanzishwa kuunga mkono kampeni ya kuchaguliwa tena kwa Luiz Inácio Lula da Silva linatajwa na washirika wake kuwa lilichangia mojawapo ya mabadiliko ya kushangaza zaidi katika siasa za Brazil za miaka ya karibuni.

Rais huyo wa mrengo wa kushoto alikuwa akionekana kupoteza nguvu katika kinyang'anyiro dhidi ya mpinzani wake wa mrengo wa kulia, Flávio Bolsonaro. Hata hivyo, ndani ya kipindi cha wiki tatu pekee, alifanikiwa kubadili mwelekeo wa kampeni na kurejesha ushindani katika uchaguzi huo.

Kuibuka kwa 'Jeshi la Lula'

Wakati wengi walikuwa na shaka kama Luiz Inácio Lula da Silva angeweza kubadili mwelekeo wa uchaguzi, chaneli ya WhatsApp iliyopewa jina la "Jeshi la Lula" iliibuka na kukua kwa kasi, hadi kufikia zaidi ya wafuasi milioni 10.8.

Ikiongozwa na Mbunge André Janones, chaneli hiyo iliwahamasisha wafuasi wa Lula kusambaza video za kampeni, kueneza ujumbe kwenye mitandao ya kijamii na kuwashawishi wapiga kura wapya kumuunga mkono.

Ukuaji wake wa haraka kati ya duru ya kwanza na ya pili ya uchaguzi ulivutia umakini mkubwa, hasa kwa kuwa ulionekana kubadilisha mwelekeo wa siasa za Brazil uliokuwa umejengeka kwa miaka mingi.

Kwa muda mrefu, makundi ya kihafidhina yaliyokuwa yakimuunga mkono Rais wa zamani Jair Bolsonaro yalionekana kuwa na ushawishi mkubwa zaidi katika uhamasishaji wa kisiasa mtandaoni, hususan kupitia majukwaa ya WhatsApp na Telegram. Hata hivyo, kuibuka kwa "Jeshi la Lula" kulionesha kuwa upande wa kushoto nao unaweza kutumia majukwaa hayo kwa ufanisi mkubwa katika kufikia na kuhamasisha wapiga kura.

Kuibuka kwa "Jeshi la Lula" kuliwapa matumaini wafuasi wengi kwamba mrengo wa kushoto nchini Brazil hatimaye ulikuwa umebuni njia ya kushindana na wapinzani wake katika uwanja wa kidijitali.

Mabadiliko hayo yalikuwa muhimu hasa kwa kuwa mitandao ya kijamii imekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Brazil tangu ushindi wa Jair Bolsonaro mwaka 2018, ambapo majukwaa kama WhatsApp yalitumika kwa kiwango kikubwa katika kampeni za kisiasa.

Ujumbe uliosambazwa kupitia "Jeshi la Lula" mara nyingi uliambatanishwa na maandishi, picha au video zilizoandaliwa tayari kwa ajili ya kusambazwa. Wafuasi walipewa majukumu mahususi ya kuyashiriki maudhui hayo kwa marafiki, familia na makundi mbalimbali ya WhatsApp ili kuongeza mwonekano wa kampeni ya Lula.

Mara kwa mara, kiongozi wa operesheni hiyo, Mbunge André Janones, aliwahamasisha wafuasi wake kusambaza kwa wingi video za kampeni au kuhakikisha lebo mpya za mitandao ya kijamii (hashtags) zinapata umaarufu.

Baadhi ya ujumbe wake ulisisitiza hali ya dharura na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka.

"Jamani, hili ni jambo la dharura!"

"Msilale bado."

"Hakuna kula kabla ya kazi hii kukamilika."

"Nina kazi moja zaidi kabla hamjaruhusiwa kupumzika."

Kauli hizo zililenga kuwahamasisha wafuasi kuendelea kuwa hai mtandaoni na kueneza ujumbe wa kampeni kwa kasi na upana zaidi.

Usiku wa kuamkia uchaguzi, André Janones aliendesha matangazo ya moja kwa moja yaliyodumu kwa saa 24, aliyoyapa jina la "matangazo ya kuleta mabadiliko", wakati kura za maoni zikiendelea kuonyesha kwamba Flávio Bolsonaro alikuwa mbele katika kinyang'anyiro hicho.

Mkakati huo ulionekana kuzaa matunda, licha ya wasiwasi kutoka kwa baadhi ya wanachama wa Chama cha Wafanyakazi (PT), ambao waliamini kuwa mtindo wa Janones wa kuibua mijadala na migogoro kwenye mitandao ya kijamii ungeweza kudhoofisha taswira ya utulivu na umakini ambayo walitaka kumjengea Luiz Inácio Lula da Silva.

Baada ya ushindi wake, Lula alimpongeza Janones hadharani katika hotuba yake, akimtaja kama "jenerali wetu" na kumshukuru kwa kile alichosema kuwa mchango wake wa kuhamasisha na kuinua morali ya wafuasi wa kampeni hiyo siku hadi siku.

Mitandao ya kijamii ilivyochangia kurejea kwa Lula

Hata hivyo, wataalamu wanasema ni vigumu kupima kwa usahihi athari za uhamasishaji wa kisiasa kupitia mitandao ya kijamii katika matokeo ya uchaguzi.

Ingawa washirika wa Lula wanaamini kuwa "Jeshi la Lula" lilichangia kurejea kwake kisiasa, mchambuzi wa siasa Denilde Holzhacker anasema mafanikio hayo yalitokana zaidi na mabadiliko ya mkakati wa kampeni.

Kwa mujibu wake, Lula hakutegemea kampeni za mtandaoni pekee, bali alizichanganya na uhamasishaji wa wananchi ngazi ya jamii. Kampeni hiyo pia ilirekebisha ujumbe wake na kuongeza juhudi za kuwafikia wapiga kura.

"Sifa ya Lula ni kwamba alitambua udhaifu wake na akabadilisha kabisa mtindo wake," anasema Holzhacker.

Kwa upande wake, mwanasosholojia Mayra Goulart anaamini kurejea kwa Lula kulitokana na mchanganyiko wa uhamasishaji wa mitandaoni na wa ana kwa ana.

"Ilikuwa mchanganyiko wa mitandao ya kijamii na uhamasishaji wa ngazi ya jamii," anasema.

Goulart anasema wafuasi wa Lula walifanikiwa kubadilisha hamasa ya mtandaoni kuwa ushiriki halisi wa kisiasa kwa kuwahamasisha watu kujitokeza kupiga kura na kuwashawishi wapiga kura ambao hawakuwa wameamua upande wa kuunga mkono.

Katika hotuba yake ya ushindi, Lula alisema uchaguzi huo ulimfunza mengi na kuahidi kuwapa wananchi nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika maamuzi ya serikali.

"Tutawapa wananchi nafasi kubwa zaidi ya kushiriki katika maamuzi, na mawasiliano ya kidijitali yatakuwa na nafasi kubwa zaidi katika serikali yangu."

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi