Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Aphrodite: Mungu wa kike aliyebadilisha namna mwili wa mwanamke unavyooneshwa katika sanaa
Kazi za sanaa zinazomwonyesha Aphrodite, mungu wa kike wa kale wa Kigiriki anayehusishwa na mapenzi na uzuri, zimechukuliwa kwa muda mrefu kuwa zisizofaa kutokana na kuonyesha mwili wa mwanamke kama chombo cha kutazamwa. Ni kwa jinsi gani amekuwa mmoja wa watu wenye utata mkubwa zaidi katika historia ya sanaa?
Uchi wa Aphrodite au Venus, kama alivyokuwa akiitwa na Warumi wa kale umekuwa ukizua mijadala kwa karne nyingi.
Mwaka wa 1880, mwandishi Mark Twain alielezea mchoro wa Titian wa Venus of Urbino 1534 kuwa "mchoro wa kuchukiza, wa kudharauliwa na usio na maadili kuliko yote duniani."
Mwaka 1914, mwanaharakati wa haki za wanawake, Mary Richardson, alikata kwa kisu mchoro wa Diego Velázquez uitwao Venus of Rokeby takriban mwaka unaotabiriwa kuchorwa kati ya mwaka 1647–1651, angalau mara tatu katika eneo la kifua. Mchoro huo ulikuwa katika Jumba la Makumbusho la Taifa la Sanaa la London
"Nilichukizwa na jinsi wanaume waliokuwa wakitembelea jumba hilo walivyokuwa wakikodolea macho mchoro huo siku nzima," alieleza baadaye.
Maonyesho mapya yanayoitwa Aphrodite: The Making of a Goddess katika Jumba la Makumbusho la Ashmolean jijini Oxford, yanachunguza historia ya mungu huyo wa kike. Maonyesho hayo yanasaidia kuelewa jinsi alivyogeuka kuwa chanzo cha mijadala na utata katika jamii.
Kuna matoleo mawili ya simulizi kuhusu asili yake, moja la kimitholojia na jingine linalozingatia historia halisi. Hata hivyo, hakuna kati ya simulizi hizo linaloashiria kuwa angekuja kuwa chanzo cha mijadala mikubwa.
Katika simulizi la kimitholojia, hadithi inaanza pale Cronus alipomkata baba yake Uranus sehemu za siri na kuzitupa baharini. Mapovu yakaanza kutanda na kuchemka juu ya maji, na kutoka humo Aphrodite akatokea akiwa tayari amekamilika.
Simulizi la kihistoria kuhusu kuzaliwa kwa Aphrodite pia lina mizizi yake katika kisiwa cha Cyprus, ambako alionekana kama mungu wa kike karibu mwaka 1200 kabla ya Kristo.
Ingawa alikuwa mungu mpya katika mkusanyiko wa miungu wa kale, alionyesha sifa zinazodhaniwa kuwa zilitokana na miungu ya zamani ya Mashariki ya Kati, kama vile Ishtar, Astarte na Hathor.
Kwa mujibu wa Anja Ulbrich, msimamizi wa maonyesho katika Jumba la Makumbusho la Ashmolean, miungu hiyo ya kike ya kale ilikuwa na sifa kuu za "ujinsia, mapenzi na uzazi", lakini kila mmoja alikuwa na majukumu mengine mbalimbali.
Hali ilikuwa hivyo pia kwa Aphrodite. Katika siku zake za mwanzo, hakuwa tu mungu wa kike wa mapenzi ya kimahaba, bali pia alihusishwa na aina zote za mapenzi ya kimwili na uzazi, katika ulimwengu wa wanyama, mimea na binadamu.
Pia alikuwa na sura nyingine za tabia yake ambazo huenda hazifahamiki sana. Alishiriki katika Vita vya Trojan, na upande huo wa kivita wa tabia yake uliifanya hata jeshi la wanamaji la Ugiriki ya kale kumheshimu.
Aphrodite anaweza pia kudai kuwa ndiye mwanzilishi wa ustaarabu wa Roma. Kwa mujibu wa simulizi za mitholojia, alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwana wa mfalme wa Trojan, Anchises. Mwana wao, Aeneas, alikimbilia Italia baada ya kuanguka kwa mji wa Troy, na inasemekana kuwa wazao wake ndio walioanzisha mji wa Roma.
Baada ya kujitokeza kwa mara ya kwanza nchini Cyprus katika karne ya 13 kabla ya Kristo, Aphrodite alivutia watu wengi na ibada yake ikaenea katika maeneo mbalimbali ya Ugiriki ya kale. Lakini ni nini kilichomfanya avutie kiasi hicho?
"Uzazi, mapenzi na kuendeleza kizazi ni mambo yanayohusu binadamu wote, bila kujali tamaduni zao," anaeleza Ulbrich. "Moja ya majina yake ni 'Pandemos', linalomaanisha mungu wa kike wa wote. Hahusishwi tu na wapiganaji au wanawake; mapenzi yanamgusa kila mtu na kila kitu. Yameenea katika nyanja zote za maisha."
Aina mpya ya uchi
Hadi kufikia wakati huo, hakukuwa na jambo lolote lililozua utata. Kwa karne nyingi, wasanii hawakujaribu kumtofautisha Aphrodite na miungu mingine ya kike ya Mlima Olympus. Katika kazi zake za awali za sanaa, kwa kawaida hakuonyeshwa akiwa uchi, na hakuwahi kuoneshwa katika mikao ya kimvuto inayohusishwa naye leo.
Hata hivyo, karibu mwaka 350 kabla ya Kristo , mchoro wa sanamu ulitokea na kubadilisha kila kitu.
Sanamu ya Aphrodite wa Knidos, iliyochongwa na Praxiteles takriban mwaka 350 Kabla ya Kristo, ilikuwa ya kwanza katika Ugiriki ya kale kumuonesha mwanamke akiwa uchi kabisa.
Sanamu hiyo ya awali haipo tena, lakini tunaweza kupata picha ya jinsi ilivyokuwa kupitia nakala zilizotengenezwa baadaye na Waroma, kama vile Venus wa Capitoline takriban mwaka 160 Kabla ya Kristo.
Kabla ya Praxiteles, ni miili ya wanaume pekee iliyokuwa ikioneshwa ikiwa uchi. "Kuonesha na kusifu uzuri wa mwili wa mwanaume kupitia uchi lilikuwa jambo la kawaida tangu karne ya saba au ya sita kabla ya Kristo," anaeleza Ulbrich.
Kwa hiyo, Praxiteles aliamua kutumia mtazamo huo huo kuonesha uzuri wa mwili wa mwanamke.
Uchi wa Aphrodite ulikuwa wa aina tofauti. Ukiitazama kwa makini, unaweza kuona jinsi ulivyotofautiana na namna miili ya wanaume ilivyooneshwa ikiwa uchi katika sanamu za Ugiriki ya kale. Tofauti hiyo inaonekana hasa katika lugha ya mwili.
Katika sanamu ya Praxiteles, Aphrodite anaoneshwa akiwa anaoga. Anaonekana mwenye haya na aliye katika hali ya kujihisi hana kinga, akijaribu kufunika mwili wake kwa sababu ya staha au aibu. Hii ni tofauti na sanaa ya Ugiriki ya kale, ambamo miili ya wanaume iliyooneshwa uchi kila mara iliwasilishwa kwa kujiamini na kuonesha ushujaa.
Kama anavyoeleza Ulbrich, "Hii inatokana hasa na namna anavyooneshwa katika simulizi za mitholojia, ambako muda mwingi huutumia kuoga na kutunza uzuri wa mwili wake."
Hata hivyo, katika kazi ya Praxiteles, mikono ya Aphrodite imeachana kidogo na mwili wake. Hali hii inamwezesha mtazamaji, kutegemea upande anaoutazama, kupata taswira ya sehemu za mwili wake ulio uchi. Ni kazi ya sanaa inayomwalika mtazamaji kuitazama kwa karibu na kuchochea udadisi wake wa kimwili na kihisia.
Mbinu hizi mpya za kisanii zilizua mijadala mikali katika karne zilizofuata. Mkao aliouchukua Aphrodite katika sanamu hiyo hata ulipewa jina maalumu: Venus Pudica Venus mwenye haya.
Ulbrich anasema sanamu ya Aphrodite wa Knidos ilikuwa "ya kimapinduzi". Kabla ya Praxiteles, Aphrodite alitambulika katika sanamu kupitia mavazi mbalimbali, vito au alama nyingine zilizohusishwa naye. Lakini baada yake, anaeleza, "uchi kwa namna fulani ukachukua nafasi hiyo".
Ni muhimu kukumbuka kuwa mwili wa uchi ni jambo la kawaida kabisa kimaumbile, na si lazima uwe chanzo cha utata. Kilichomfanya Aphrodite aonekane kuwa na taswira ya uchochezi katika mitazamo ya nyakati zilizofuata haikuwa ukweli kwamba alikuwa uchi, bali namna mwili wake ulivyooneshwa ili kuvutia macho ya mtazamaji. Kwa njia hiyo, aligeuzwa kuwa kitu cha kutamanika.
Sanamu ya awali ya Praxiteles ilikuwa chanzo kikubwa cha msukumo kiasi kwamba wachongaji wa Waroma waliitengeneza upya mara maelfu. Venus wa Capitoline ni mojawapo ya mifano maarufu ya nakala hizo.
Sanamu ya Venus Pudica ilianzisha mtazamo mpya wa kuuwasilisha mwili wa mwanamke katika sanaa. Mtazamo huo ulienea katika maeneo yaliyokuwa chini ya utawala wa Dola la Roma, hususan Ulaya, Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.
Kuzaliwa upya kwa Aphrodite katika sanaa ya kimahaba
Hata hivyo, ushawishi huu haukuishia katika ulimwengu wa kale. Katika kipindi cha Mwamko wa Sanaa au Renaissance, wasanii walianza kutafuta na kunakili sanamu za kale za Kigiriki na Kirumi kwa ari ambayo haikuwa imeonekana kwa takriban miaka elfu moja.
Mojawapo ya sanamu zilizopewa heshima kubwa ilikuwa ile ya Venus mwenye haya. Hivyo, Aphrodite, katika taswira yake ya uchi, yenye mvuto na staha kama ilivyobuniwa na Praxiteles, alizaliwa upya kupitia kazi za wasanii kama Masaccio, Botticelli, Raphael na Titian, ambao baadaye walikuja kuwa miongoni mwa majina makubwa katika historia ya sanaa.
Ingawa baadhi ya wasanii walitumia mkao huo kumwonesha Aphrodite, wengine wengi waliutumia kuonesha wahusika wengine wa kike. Sanamu hiyo pia iliwapa wasanii wengine msukumo wa kubuni mikao mipya, wakizingatia kanuni ileile ya msingi: kuonesha uchi kwa kiasi na kwa staha.
Hivyo, kupitia kurudiwa mara kwa mara kwa taswira ya Venus mwenye haya (Venus Pudica) katika kazi za wasanii mbalimbali, mwanamke aliyeoneshwa kama kitu cha kutamaniwa akawa sehemu isiyoweza kufutika katika historia ya sanaa.
Katika kipindi cha Baroque, wasanii Rubens na Velázquez waliendeleza tena taswira hiyo. Baadaye, katika karne ya 19, ilihuishwa na Cabanel na Manet, kisha katika karne ya 20 na Modigliani pamoja na Yves Klein. Hasira zilizooneshwa na Mark Twain na Mary Richardson zilikuwa sehemu ya mwitikio dhidi ya historia hii ya kumwasilisha Aphrodite kwa mtazamo wa kimahaba na kimwili.
Anja Ulbrich aliiambia BBC kuwa mungu huyo wa kike amekuwa akioneshwa kwa mitazamo mbalimbali, na kwamba sanamu ya Praxiteles haipaswi kuchukuliwa kuwa ndiyo taswira pekee au ya mwisho ya kumwakilisha.
Miongoni mwa kazi za sanaa zinazooneshwa katika jumba la makumbusho la Ashmolean, kuna sanamu iliyotengenezwa Northumberland, inayomwonesha Aphrodite akiwa anaoga. Akizungumzia sanamu hiyo iliyoko mbali sana na eneo la Bahari ya Mediterania, Anja Ulbrich alisema huku akitabasamu: "Anaonekana kana kwamba amekerwa kidogo na baridi."
Katika miaka ya hivi karibuni, na nje ya ushawishi wa Praxiteles, Aphrodite amekuwa akioneshwa kwa mtazamo tofauti, wakati mwingine hata kama ishara ya ukombozi wa wanawake.
Mwaka 2023, Beyoncé alifungua tamasha lake kwa kuingia jukwaani akiwa ndani ya gamba kubwa la chaza, huku akiwa amevalia gauni lililopambwa kwa michoro iliyoakisi mkao wa mikono ya Venus mwenye haya.
Wasanii wengine kama Björk, Lady Gaga, Kylie Minogue na kundi la Bananarama pia wametunga nyimbo zinazomhusu mungu huyo wa kike.
Kama ishara ya uzuri usio na kifani na mvuto wa kimapenzi, Aphrodite amekuwa akibadilishwa na kutafsiriwa upya ili kuendana na matarajio ya watu wanaomwangalia kwa kipindi cha miaka 3,000. Huu ni muda mrefu wa kushangaza kwa mungu wa kike wa Ugiriki ya kale.
Jambo jingine la kushangaza ni kwamba sanamu moja tu, yaani Aphrodite wa Knidos, iliyochongwa na Praxiteles, imekuwa na ushawishi mkubwa katika namna tunavyoutazama uchi.
Hakuna dalili kwamba ushawishi wake katika maisha ya binadamu unakaribia kupungua, wala kwamba mijadala na utata anaouzua vitakoma hivi karibuni. Suala la uzuri na namna unavyotazamwa litaendelea kuwa muhimu, na daima litakuwa mada ya mijadala inayoakisi mabadiliko ya mitazamo ya jamii kadiri muda unavyopita.
"Kutegemea mazingira, watu wamekuwa wakimpa maana wanayoihitaji au wanayoitaka," anaeleza Ulbrich. "Ana uwezo mkubwa sana wa kuwakilishwa kwa namna mbalimbali, unajua."