Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashujaa waliotikisa utawala wa kikoloni na kuibadili historia ya Kenya
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Kila mwaka Oktoba 20, Kenya huadhimisha Siku ya Mashujaa, siku ya kitaifa ya kuwakumbuka watu waliochangia katika historia na maendeleo ya taifa, wakiwemo wale waliopigania uhuru dhidi ya utawala wa kikoloni wa Uingereza.
Kabla ya Kenya kupata uhuru Desemba 12, 1963, watu kutoka jamii mbalimbali walipinga utawala huo kwa njia tofauti. Baadhi walipigana kwa silaha, wengine walihamasisha jamii zao kupinga sera za kikoloni, huku wengine wakitumia harakati za kisiasa kudai haki na kujitawala.
Mapambano hayo yalichochewa na masuala mbalimbali, yakiwemo uporaji wa ardhi, kodi za kikoloni, kazi za lazima na kuingiliwa kwa mifumo ya maisha na uongozi wa jamii za wenyeji.
Katika kuadhimisha Siku ya Mashuja makala hii inaangazia mashujaa sita ambao maisha na mapambano yao yanaangazia sura tofauti za safari ndefu ya Kenya kuelekea uhuru.
1. Koitalel Arap Samoei: Kiongozi aliyepinga upanuzi wa utawala wa Uingereza
Koitalel Arap Samoei alikuwa kiongozi wa Wanandi aliyeongoza upinzani dhidi ya kuenea kwa utawala wa kikoloni wa Uingereza katika eneo la Nandi mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20.
Wanandi walipinga kuingiliwa kwa ardhi zao na juhudi za Uingereza za kujenga reli na kupanua udhibiti wake katika eneo hilo.
Koitalel, ambaye pia alikuwa na nafasi muhimu ya kiroho na kijamii katika jamii yake, aliongoza upinzani huo kwa miaka kadhaa.
Mwaka 1905, aliuawa na maafisa wa kikoloni katika mazingira yanayohusishwa na mkutano uliokuwa umepangwa kwa ajili ya mazungumzo.
Kifo chake kilikuwa pigo kwa upinzani wa Wanandi, ingawa kilitokea karibu miongo sita kabla ya Kenya kupata uhuru.
Urithi wake unaonyesha kuwa upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni haukuanza na Mau Mau pekee. Jamii mbalimbali zilikuwa zimeanza kupinga upanuzi wa mamlaka ya Uingereza mapema zaidi.
2. Mekatilili wa Menza: Mwanamke aliyehamasisha jamii kupinga ukoloni
Mekatilili wa Menza ni miongoni mwa wanawake wanaokumbukwa kwa nafasi yao katika upinzani wa mapema dhidi ya utawala wa kikoloni nchini Kenya.
Alikuwa kiongozi wa jamii ya Wagiriama katika eneo la Pwani na alipinga sera za kikoloni zilizohatarisha ardhi, utamaduni na mifumo ya maisha ya jamii yake.
Miongoni mwa malalamishi ya Wagiriama yalikuwa kodi zilizowekwa na utawala wa kikoloni, kazi za lazima na kuingiliwa kwa maeneo yao ya jadi.
Mekatilili alitumia hotuba, mikusanyiko ya jamii na mila za Wagiriama kuhamasisha wananchi kupinga sera hizo.
Mwaka 1913, alikamatwa na kupelekwa uhamishoni Kisii, mbali na nyumbani kwake Pwani. Hata hivyo, simulizi za kihistoria zinasema alitoroka na kurejea katika eneo lake.
Upinzani aliouongoza unaonyesha nafasi ambayo wanawake walikuwa nayo katika kupinga ukoloni, licha ya kwamba historia ya mapambano ya uhuru mara nyingi imeangazia zaidi viongozi wanaume.
Mekatilili anabaki kuwa ishara ya ujasiri na utetezi wa ardhi, utamaduni na haki za jamii yake.
3. Otenyo Nyamaterere: Mpiganaji aliyepinga utawala wa kikoloni Kisii
Otenyo Nyamaterere ni mmoja wa mashujaa wanaokumbukwa katika historia ya upinzani wa Abagusii dhidi ya utawala wa kikoloni wa Waingereza mwanzoni mwa karne ya 20. Wakati huo, jamii za eneo la Gusiiland zilikuwa zikikabiliwa na kuenea kwa mamlaka ya kikoloni, hali iliyohusisha kuchukuliwa kwa ardhi, mifugo na kuingiliwa kwa mifumo yao ya kijamii na kiutamaduni.
Otenyo alijitokeza kuwa miongoni mwa walioongoza upinzani huo. Anatajwa katika simulizi za kihistoria kwa kumshambulia kwa mkuki Geoffrey Northcote, afisa wa kikoloni wa Uingereza, kitendo kilichomfanya kuwa ishara ya ujasiri na mapambano dhidi ya ukoloni miongoni mwa Waabagusii.
Baadaye alikamatwa na kuuawa mwaka 1908, lakini jina lake liliendelea kuishi katika kumbukumbu za jamii kama mfano wa watu waliokataa kusalimu amri mbele ya utawala wa kikoloni.
Ingawa mapambano yake yalitangulia harakati za kisiasa zilizokuja kufanikisha uhuru wa Kenya miongo kadhaa baadaye, hadithi yake inadhihirisha namna ambavyo jamii mbalimbali zilivyoonyesha upinzani kwa njia tofauti katika kutetea ardhi, uhuru na maisha yao. Leo, Otenyo Nyamaterere anakumbukwa kama mmoja wa mashujaa wa mwanzo waliothubutu kusimama dhidi ya ukoloni katika eneo la Kisii.
4. Harry Thuku: Mwanaharakati aliyesaidia kuendeleza upinzani wa kisiasa
Harry Thuku alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa harakati za kisiasa za Waafrika zilizopinga sera za kikoloni katika miaka ya mwanzo ya karne ya 20.
Alipinga masuala yaliyowaathiri Waafrika, yakiwemo kazi za lazima, mishahara duni na sera zilizowabagua katika maeneo mbalimbali ya maisha.
Mwaka 1922, kukamatwa kwake kulichochea maandamano makubwa jijini Nairobi. Watu walikusanyika kupinga hatua hiyo na kudai aachiliwe.
Maandamano hayo yaliishia katika umwagikaji wa damu baada ya vikosi vya kikoloni kuwafyatulia risasi waandamanaji.
Thuku alizuiliwa kwa miaka kadhaa. Baadaye aliendelea kushiriki katika shughuli za kisiasa, ingawa misimamo na ushiriki wake vilibadilika kadiri harakati za kitaifa zilivyoendelea.
Umuhimu wake katika historia ya Kenya ni kuonyesha jinsi upinzani ulivyoanza kuchukua sura ya kisiasa na kuhamasisha watu wengi zaidi kudai mabadiliko.
5. Dedan Kimathi: Kiongozi wa mapambano ya Mau Mau
Dedan Kimathi ni mmoja wa majina yanayohusishwa zaidi na mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa kikoloni nchini Kenya.
Alikuwa kiongozi muhimu wa Mau Mau, harakati iliyohusisha mapambano ya silaha dhidi ya serikali ya kikoloni katika miaka ya 1950.
Mau Mau ilipata uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa baadhi ya Waafrika waliokuwa wameathiriwa na kupokonywa kwa ardhi, ubaguzi na masharti magumu ya utawala wa kikoloni.
Mwaka 1952, serikali ya kikoloni ilitangaza hali ya hatari na kuanzisha operesheni dhidi ya watu waliotuhumiwa kuhusika na Mau Mau.
Kimathi aliendelea kuongoza wapiganaji msituni hadi alipokamatwa mwaka 1956.
Alihukumiwa kifo na kunyongwa mwaka 1957.
Mapambano ya Mau Mau yalikuwa na gharama kubwa kwa pande mbalimbali, yakiwemo vifo, kuzuiliwa kwa watu wengi na mateso yaliyotokana na hatua za serikali ya kikoloni.
Hata hivyo, harakati hizo ziliongeza shinikizo kwa serikali ya Uingereza na zikawa sehemu muhimu ya historia iliyotangulia uhuru wa Kenya.
Kimathi anabaki kuwa ishara ya mapambano ya silaha na gharama ambayo baadhi ya Wakenya walilipa katika harakati za kupinga ukoloni.
6. Achieng Oneko: Mwanasiasa aliyedai uhuru kupitia harakati za kitaifa
Ramogi Achieng Oneko alikuwa miongoni mwa viongozi wa harakati za kitaifa waliodai kujitawala kwa Kenya.
Alikuwa mwanachama wa Kenya African Union (KAU), chama kilichotetea haki za Waafrika na kutaka mabadiliko ya mfumo wa kisiasa wa kikoloni.
Mwaka 1952, Oneko alikamatwa pamoja na Jomo Kenyatta, Bildad Kaggia, Fred Kubai, Paul Ngei na Kung'u Karumba. Kundi hilo lilijulikana kama Kapenguria Six.
Viongozi hao walikabiliwa na kesi iliyohusishwa na madai ya kuunga mkono Mau Mau. Kenyatta alikuwa mmoja wa viongozi waliotuhumiwa kuhusika na harakati hizo.
Kesi na kuzuiliwa kwa viongozi hao vilikuwa sehemu ya juhudi za serikali ya kikoloni za kukandamiza harakati za kisiasa na upinzani wakati wa hali ya hatari.
Oneko aliachiliwa baada ya miaka kadhaa ya kuzuiliwa na baadaye alishiriki katika siasa za Kenya huru.
Historia yake inaonyesha kuwa mapambano ya uhuru hayakuhusisha wapiganaji wa msituni pekee. Viongozi wa vyama na wanaharakati wa kisiasa pia walichangia katika safari ya kuelekea kujitawala.
Mashujaa wa uhuru walikuwa wengi zaidi ya majina sita
Kutoka kwa Koitalel Arap Samoei na Mekatilili wa Menza hadi Dedan Kimathi na Achieng Oneko, historia ya Kenya inaonyesha kuwa upinzani dhidi ya ukoloni ulipitia vipindi tofauti na ulihusisha mbinu mbalimbali.
Baadhi ya mashujaa walipigana kwa silaha, wengine walihamasisha jamii zao, huku wengine wakitumia harakati za kisiasa kudai haki na kujitawala.
Wakati huo huo, maelfu ya watu ambao majina yao hayajaandikwa kwa kina katika vitabu vya historia walishiriki katika mapambano hayo, wakitoa msaada kwa wapiganaji, kushiriki maandamano au kukabiliana na athari za utawala wa kikoloni.
Kenya ilipata uhuru Desemba 12, 1963, baada ya miaka mingi ya upinzani, mazungumzo na mabadiliko ya kisiasa.
Kwa hiyo, kuadhimisha Mashujaa Day si kukumbuka watu maarufu pekee. Ni pia kutambua mchango wa wanawake na wanaume kutoka jamii mbalimbali ambao walipinga ukoloni na kusaidia kuweka msingi wa taifa huru.
Historia yao inatukumbusha kuwa uhuru haukupatikana kutokana na juhudi za mtu mmoja au kundi moja pekee, bali kutokana na mchango wa watu wengi katika nyakati tofauti.
Na ndiyo maana, kila Oktoba 20, Kenya ina nafasi ya kutafakari upya maana ya ushujaa, kujitolea na mchango wa watu katika kujenga taifa.