Shakahola: Mwana wa Mackenzie afichua ndugu zake bado wanalazimishwa kufunga
Mwana mkubwa wa kiongozi wa dhehebu tata nchini Kenya, Paul Mackenzie, anasema ndugu zake wadogo waliendelea kulazimishwa kufunga kula hadi wiki mbili zilizopita, licha ya baba yao kupatikana na hatia ya mauaji ya watu 191.
Dan Mackenzie, mwenye umri wa miaka 27, amesema aliripoti suala hilo kwa polisi, ambao waliwaokoa watoto wanane, wakiwemo ndugu zake watano wadogo, kutoka nyumbani kwa bibi yao na kuwapeleka katika kituo cha uokoaji.
“Kwa hakika walilazimishwa kufunga kwa sababu walinyimwa chakula kwa karibu siku tatu,” aliiambia BBC katika kipindi cha Newsday.
Siku ya Jumatatu, baba yake alipatikana na hatia ya kuwaua watoto 190 na mtu mzima mmoja waliokufa kwa njaa katika msitu wa Shakahola, karibu na pwani ya Kenya.
Mackenzie alikuwa amewaamuru wafuasi wa dhehebu lake kujinyima chakula wao pamoja na watoto wao hadi kufa, akidai kuwa wangekutana na Yesu.
Viongozi wengine 28 wa dhehebu hilo pia walipatikana na hatia ya mauaji.
Mackenzie amwita mwanawe msaliti baada ya hukumu
Dan amesema hukumu hiyo imewapa waathiriwa wa mkasa wa Shakahola afueni, huku akieleza kuwa alikutana kwa muda mfupi na baba yake baada ya mahakama kutoa uamuzi.
“Tumepata afueni kidogo sisi kama waathiriwa wa kilichotokea Shakahola, kwa sababu sasa kesi hii inafikia mwisho na amepatikana na hatia,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu mazungumzo yake na baba yake baada ya hukumu kutolewa, Dan alisema alipata nafasi ya kumsalimia wakati Mackenzie alipokuwa akipelekwa kwenye gari.
“Nilipata nafasi kidogo wakati akipelekwa kwa gari. Nikamsalimia na akaniambia kuwa ninamsaliti. Nikacheka tu kwa sababu sikuwa na la kumwambia,” amesema.
Dan amesema haelewi ni kwa nini baba yake alimwita msaliti, lakini anaamini huenda kauli hiyo inahusiana na hatua yake ya kuzungumza kuhusu yaliyotokea katika dhehebu hilo.
“Sijui anamaanisha nini. Pengine kuna kiapo kati ya mzazi na mtoto kwamba hapaswi kuzungumza ukweli, au sijui ni kiapo gani kinachofanya aone kwamba nimemsaliti,” amesema.
Dan, ambaye awali alikuwa akimtetea baba yake, amesema alikuja kuelewa ukubwa wa mkasa huo wakati wa kusikilizwa kwa kesi mahakamani.
Anasema pia alipitia maisha magumu akiwa mtoto ndani ya dhehebu hilo.
“Nilipokuwa na umri wa miaka 12, nililazimishwa kufunga kwa karibu wiki moja,” amesema.
Pia anakumbuka jinsi waumini wa kanisa hilo walivyokuwa wakimpiga kwa saa nyingi ili kumlazimisha kuhudhuria ibada alipokuwa mtoto.
Dan anasema aliondoka shuleni akiwa na umri wa miaka saba, kutokana na mafundisho ya dhehebu hilo yaliyopiga marufuku elimu na kueleza kuwa dawa za kisasa zilikuwa “uovu”.
Amesema aliamua kujitenga na maisha hayo mwaka 2018 au 2019, baada ya kuchoshwa na hali aliyokuwa akipitia. Kwa mujibu wake, baba yake alimnunulia pikipiki ili aweze kujitegemea.
Dan pia ameeleza kuhusu kifo cha ndugu yake mdogo zaidi, aliyekuwa na umri wa takriban mwaka mmoja na nusu, katika mkasa wa Shakahola.
Maisha ya Dan baada ya kujitenga na dhehebu
Kwa sasa Dan anaishi Malindi, katika pwani ya Kenya, ambako anajipatia kipato kwa kufanya kazi ya udereva wa bodaboda. Pia anawasaidia ndugu zake wadogo.
Amesema hajawahi kupata huduma za kisaikolojia licha ya kupitia matukio magumu akiwa mtoto na kupoteza ndugu yake katika mkasa huo.
Akizungumzia jinsi jamii inavyompokea licha ya uhalifu unaohusishwa na baba yake, Dan amesema baadhi ya watu walikuwa na hasira, lakini hawakumlaumu yeye moja kwa moja.
“Wananiona kila wakati na kusema, ‘Huyo ni baba yako, si wewe.’ Walikuwa na hasira na wakati mmoja walibomoa ukuta, lakini mimi hawakunigusa. Tumeendelea kuishi vizuri,” amesema.
Dan anasema alihisi pia kuwa na wajibu wa kuwaripoti wanafamilia ambao bado wanaamini mafundisho ya Mackenzie ili kuwaokoa ndugu zake wadogo.
“Nililazimika kumripoti bibi yangu,” amesema.
Amesema anatumaini hukumu hiyo itawapa faraja wale waliopoteza marafiki na jamaa zao.
Familia zilizopoteza watoto zafurahishwa na hukumu
Siku ya Jumatatu, Stephen Mwiti, mwenye umri wa miaka 48, ambaye alisema alipoteza watoto wake wote sita kutokana na dhehebu hilo, alikaribisha hukumu hiyo.
“Nina furaha kwamba watu wote wamepatikana na hatia,” aliiambia BBC nje ya mahakama.
Aliyekuwa mke wake ni miongoni mwa watu waliopatikana na hatia ya mauaji pamoja na Mackenzie.
Katika hukumu yake iliyochukua saa nane mjini Mombasa, Jaji Diana Mochache alisema wafuasi wa Mackenzie waliamini kuwa alikuwa “msemaji wa Yesu”.
Mmoja wa washtakiwa wenzake aliiambia mahakama kuwa Mackenzie alikuwa amesema mtu yeyote aliyekataa kufunga alipaswa kulazimishwa kwenda mbinguni “kwa mateke na makofi”.
Jaji huyo alisema mazishi yaliyofanyika katika msitu ambako dhehebu hilo lilikuwa na makao yake yalielezwa kuwa “harusi”, huku waliokufa wakisherehekewa kwa madai kuwa walikuwa “wamefunga ndoa na Yesu”.
Mackenzie anakabiliwa na kesi nyingine
Mackenzie na viongozi wengine wa dhehebu hilo pia wanakabiliwa na kesi tofauti zinazohusu ugaidi, itikadi kali na kunyima watoto haki ya kupata elimu.
Hukumu ya mauaji ndiyo uamuzi wa kwanza kuhusu mashtaka mazito zaidi dhidi ya mchungaji huyo, aliyekamatwa mwaka 2023 baada ya miili ya zaidi ya watu 400 kugunduliwa katika makaburi ya kina kifupi katika msitu wa Shakahola, karibu na pwani ya Kenya.
Mahakama inatarajiwa kutangaza adhabu yake tarehe 6 Novemba.
Pia unaweza kusoma: