Wachezaji 5 ambao soka limekatisha uhai wao

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Soka ni mchezo unaounganisha mamilioni ya watu duniani, lakini wakati mwingine furaha ya mashabiki hugeuka kuwa huzuni kubwa pale mchezaji anapoanguka uwanjani na kushindwa kuamka tena. Katika historia ya mchezo huo, wapo wachezaji waliopoteza maisha wakiwa wanatekeleza kile wanachokipenda zaidi, kucheza mpira wa miguu.

Kifo cha hivi karibuni cha mshambuliaji wa Tenerife, Jesus de Miguel, kimeibua tena kumbukumbu za matukio mengine ya kusikitisha yaliyowahi kutokea katika viwanja vya soka duniani.

De Miguel, mwenye umri wa miaka 30, alifariki Jumanne, Novemba 3, 2026, baada ya kupata majeraha makubwa katika mchezo wa Ligi Daraja la Pili nchini Hispania dhidi ya FC Andorra. Alipata majeraha hayo baada ya kugongana vikali na kipa wa wapinzani, Jesus Owono.

Tukio hilo linamuweka De Miguel katika orodha ya wachezaji waliopoteza maisha kutokana na matukio yaliyotokea wakati wa mchezo. Hizi ni simulizi za wachezaji wengine wanne ambao vifo vyao viliutikisa ulimwengu wa soka.

5. Juan Izquierdo (2024)

Juan Izquierdo alikuwa beki wa kati wa klabu ya Nacional ya Uruguay. Alipoteza maisha Agosti 27, 2024, akiwa na umri wa miaka 27, baada ya kujiskia vibaya ghafla wakati wa mchezo wa Copa Libertadores dhidi ya Sao Paulo ya Brazil.

Tukio hilo lilitokea Agosti 22, 2024, katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo. Izquierdo alianguka uwanjani baada ya kupata hitilafu ya mapigo ya moyo, hali iliyohitaji apelekwe hospitalini kwa matibabu ya haraka.

Licha ya juhudi za madaktari, hali yake iliendelea kuwa mbaya kwa siku zilizofuata. Baada ya siku tano za kupatiwa matibabu, alifariki kutokana na kusimama kwa moyo na mfumo wa upumuaji, hali iliyohusishwa na hitilafu ya mapigo ya moyo.

Kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwa familia na klabu yake, hasa ikizingatiwa kuwa mtoto wake wa pili alikuwa amezaliwa siku 10 tu kabla ya tukio hilo. Nacional ilieleza kifo chake kuwa ni pigo lisiloweza kufidiwa.

4. Phil O'Donnell (2007)

Phil O'Donnell alikuwa nahodha wa klabu ya Motherwell ya Scotland na kiungo mwenye uzoefu aliyewahi pia kuchezea Celtic na Sheffield Wednesday. Alifariki Desemba 29, 2007, akiwa na umri wa miaka 35, baada ya kuanguka uwanjani wakati wa mchezo dhidi ya Dundee United.

Tukio hilo lilitokea katika dakika za mwisho za mchezo ambao Motherwell ilikuwa ikiongoza kwa mabao 5-3. O'Donnell alikuwa akijiandaa kutolewa nje na kocha wake wakati alipoanguka ghafla kabla ya mabadiliko hayo kukamilika.

Wahudumu wa afya walimfanyia huduma ya kwanza uwanjani kwa takribani dakika tano kabla ya kupelekwa kwenye gari la wagonjwa lililokuwa likisubiri nje ya uwanja. Hata hivyo, hakunusurika, huku chanzo cha kifo chake kikitajwa kuwa kushindwa kwa moyo.

Kifo cha nahodha huyo kilisababisha huzuni kubwa katika soka la Scotland, kiasi cha baadhi ya michezo kuahirishwa. Kocha wake, Mark McGhee, alimuelezea kama mtu mwenye weledi, uadilifu na uaminifu wa hali ya juu, ndani na nje ya uwanja.

3. Antonio Puerta (2007)

Antonio Puerta alikuwa mmoja wa wachezaji wenye vipaji vilivyoanza kung'ara katika soka la Hispania. Akiwa na klabu ya Sevilla, alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la UEFA mwaka 2007, lakini miezi michache baadaye maisha yake yakakatishwa na tatizo la moyo.

Agosti 25, 2007, katika mchezo wa La Liga dhidi ya Getafe, Puerta alianguka uwanjani baada ya kupata tatizo la moyo. Alipatiwa huduma ya kwanza na baadaye kupelekwa hospitalini, lakini hali yake iliendelea kuwa mbaya.

Baada ya siku tatu, alifariki akiwa na umri wa miaka 22 kutokana na kushindwa kwa viungo mbalimbali vya mwili kufuatia kusimama kwa moyo kwa muda mrefu.

Kifo chake kiliwagusa sana wachezaji na mashabiki, akiwemo Sergio Ramos, ambaye alikuwa rafiki yake. Ramos aliendelea kumuenzi Puerta kwa kuvaa jezi yenye ujumbe maalumu wa kumkumbuka na baadaye kuchora 'tatoo' au alama ya kumbukumbu yake mwilini.

2. Cristiano Junior (2004

Mchezaji huyo raia wa Brazil mwenye umri wa miaka 25, ambaye wakati huo alikuwa mwanasoka anayelipwa mshahara mkubwa zaidi nchini India, aligongana na kipa wa timu pinzani alipofunga bao akiwa na klabu yake ya Dempo, dakika 12 kabla ya mchezo wa fainali ya Kombe la Federation Cup la mwaka 2004 kumalizika, mjini Bangalore.

Junior, ambaye alihamia India kwa lengo la kupata fedha za kutosha ili kumjengea mama yake nyumba katika nchi yao ya Brazil, alianguka chini na kupoteza fahamu. Alipata msaada wa haraka kutoka kwa mshambuliaji mwenzake wa klabu hiyo, Santi Martins, raia wa Nigeria.

Martins alibaki pembeni yake hadi ambulensi ilipomchukua na kumpeleka hospitalini. Hata hivyo, Junior alitangazwa kuwa amefariki dunia mara tu alipowasili hospitalini, baada ya kupata mshtuko wa moyo uliosababisha moyo kusimama.

"Mchezo uliendelea. Tulicheza dakika 12 zilizobaki, tukapokea kombe na tukaambiwa kuhusu kifo cha Cristiano tulipofika hospitalini. Tulivunjika moyo na kushindwa kujizuia," alisema Stanley Colaco, aliyekuwa nahodha wa klabu hiyo, katika mahojiano na gazeti la Times of India mwaka 2021.

1. Marc-Vivien Foé (2003)

Marc-Vivien Foé alikuwa kiungo wa timu ya taifa ya Cameroon aliyewahi pia kuchezea klabu za Manchester City, West Ham United na Lyon. Alifariki Juni 26, 2003, akiwa na umri wa miaka 28, katika moja ya matukio yaliyotikisa zaidi historia ya soka la kimataifa.

Tukio hilo lilitokea wakati Cameroon ilipokuwa ikicheza dhidi ya Colombia katika nusu fainali ya Kombe la Mabara (FIFA Confederations Cup) mjini Lyon, Ufaransa. Foé alianguka ghafla katikati ya mchezo baada ya kupata hitilafu ya moyo.

Wahudumu wa afya walimkimbilia na kujaribu kumuokoa kwa kumpa huduma ya kupumua kwa msaada na oksijeni. Juhudi za kurejesha mapigo ya moyo wake ziliendelea kwa takribani dakika 45, lakini hazikufanikiwa. Baadaye alitangazwa kufariki.

Kifo cha Foé kilichochea mabadiliko katika namna wachezaji wanavyofanyiwa uchunguzi wa matatizo ya moyo na jinsi timu zinavyojiandaa kukabiliana na dharura za kiafya uwanjani. Mafunzo ya huduma ya kwanza ya CPR na matumizi ya vifaa vya kurejesha mapigo ya moyo (defibrillators) yalipata umuhimu mkubwa zaidi katika soka duniani.