Kwa miaka 9, adai kubakwa na mumewe na rafiki zake bila kujua

    • Author, Jonny Humphries
    • Nafasi, BBC News
    • Akiripoti kutoka, Manchester, Inglaterra
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Tahadhari: Habari hii ina maelezo ya ukatili wa kingono ambayo yanaweza kukusumbua.

Mwanamke mmoja aliyeamini kuwa hakuwa amefanya mapenzi kwa kipindi cha miaka tisa, kumbe bila kujua alikuwa akipewa dawa za usingizi na kubakwa mara kwa mara na mumewe pamoja na kundi la wanaume wengine walioalikwa, katika tukio lililoelezwa mahakamani nchini Uingereza.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, mumewe alikuwa akiishi maisha ya siri. Alikuwa akimpa mkewe mchanganyiko wa dawa uliomfanya apoteze fahamu kabisa, ili asiweze kutambua unyanyasaji aliokuwa akifanyiwa.

Mume huyo na wanaume wengine wanne tayari wamekiri makosa mbalimbali, lakini kesi ya washitakiwa wengine tisa wanaokataa mashtaka dhidi yao imeanza katika mahakama moja mjini Manchester, Uingereza.

Katika maelezo yake ya awali mahakamani, mwendesha mashtaka Louise Oakley alisema mwanamke huyo alikuwa na furaha, lakini maisha aliyoyafahamu yalimalizika pale polisi walipobisha hodi mlangoni mwa nyumba yake.

Kabla ya kesi kuanza, Jaji Maurice Greene aliwaonya wajumbe wa baraza la mahakama kuwa wajiandae kusikiliza ushahidi ambao unaweza kusababisha hisia za mshtuko na hasira.

Mwanzoni kabisa mwa kesi hiyo, upande wa mashtaka ulionyesha video zinazodaiwa kumwonyesha mwanamke huyo, mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, akibakwa na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji wa kingono akiwa amepoteza fahamu.

Oakley aliliambia baraza la mahakama kuwa mume huyo na mkewe walionekana kama wanandoa waliokuwa wakisubiri kwa hamu kustaafu. Walikuwa na shughuli nyingi, wakifurahia nyumba yao na bustani, wakikutana na familia na marafiki na kusafiri pamoja kwenda likizo nje ya nchi.

Hata hivyo, mwendesha mashtaka alisema mume huyo, ambaye pia ana umri wa zaidi ya miaka 60, alikuwa akichapisha picha na video mtandaoni tangu mwaka 2004, zikimuonyesha akimbaka na kumfanyia ukatili wa kingono mkewe ndani ya nyumba yao katika eneo la Stockport, Greater Manchester.

Jina la mume huyo limehifadhiwa kwa ajili ya kulinda haki ya mkewe ya kutotambulika.

"Huenda mkapata ugumu kufikiria namna unyanyasaji huu ungeweza kuwa mbaya zaidi, lakini ulikuwa hivyo," alisema Oakley mahakamani.

Mwendesha mashtaka alisema mume huyo alikuwa amepanga kwa miaka kadhaa kuwaalika wanaume nyumbani kwake ili kumbaka mkewe, lakini alianza kutekeleza mpango huo mwaka 2023.

Kwa mujibu wa upande wa mashtaka, wanaume hao "walijua vizuri kuwa mwanamke huyo hakuwa na fahamu, na ndiyo maana walikuwa hapo, ili kutumia mwili wake akiwa amepoteza fahamu."

Oakley alisema polisi walikamata simu ya mkononi ya mume huyo, iliyokuwa na siri zake nyingi na mawazo yake ya kikatili kuhusu ngono.

Wachunguzi waligundua zaidi ya picha na video milioni moja zilizokuwa zikihifadhi kumbukumbu za vitendo vya ukatili wa mume huyo.

Oakley alisema mafaili hayo yaliwapa polisi karibu mwongozo kamili wa namna mume huyo na wanaume tisa wanaoshtakiwa walivyokuwa wakitekeleza vitendo hivyo.

"Ukatili wake ulionekana kutokuwa na mipaka," alisema.

"Wao pia walikuwa wakiishi maisha ya siri. Wengine waliingia na kutoka katika makazi ya wanandoa hao usiku, kwa tahadhari na kimyakimya ili wasionekane wala kusikika, huku wengine wakijificha nyuma ya skrini za kompyuta au simu zao, bila shaka wakiamini kuwa wako salama."

Miongoni mwao ni Jonathan Kirk, 43, mhudumu wa huduma za dharura za afya; Philip Wild, 59, dereva wa teksi; Alan Keelan, 42, kocha wa soka la ridhaa; Mohammed Sabir, 28, mfanyakazi wa kampuni binafsi ya masuala ya ajira; Jordan Wallace, 31, mfanyakazi wa kampuni ya vifaa vya ujenzi; Richard Townsend, 37, fundi wa kufunga mabati ya chuma; na Robert Stewart, 70, mstaafu, ambao hawa walimgusa mwanamke huyo.

Washitakiwa wengine wawili, Daniel Rayner na David Graves, walielezwa kuwa walihusika katika unyanyasaji bila kumgusa moja kwa moja mwanamke huyo. Hawakutembelea nyumba yake, lakini wanatuhumiwa kuhamasisha vitendo hivyo au kusaidia kwa njia nyingine.

Oakley aliwaonya wajumbe wa baraza la mahakama kuwa upande wa utetezi unaweza kujaribu kurejelea baadhi ya mienendo ya kingono isiyo ya kawaida, kama vile kubadilishana wapenzi.

Pia, alisema wanaweza kudai kuwa picha hizo zilikuwa zimeandaliwa na kwamba mwanamke huyo alikuwa akijifanya amelala au amepoteza fahamu kama sehemu ya mchezo wa kimapenzi na mumewe.

"Vitendo walivyofanya wanaume hawa havikuwa kushiriki katika mienendo ya kingono isiyo ya kawaida na yenye ridhaa. Ulikuwa ubakaji na unyanyasaji wa kingono, bila shaka," alisema mwendesha mashtaka huyo.

Oakley alitoa mfano wa ujumbe uliotumwa na mmoja wa washitakiwa, Robert Stewart, mstaafu, kwa mume huyo saa kadhaa baada ya kudaiwa kumbaka mwanamke huyo Septemba 2025.

"Rafiki yangu, nimekuwa na hisia mbaya kuhusu jambo hilo siku nzima," mwendesha mashtaka aliusoma ujumbe huo.

"Futa picha zote kutoka kwenye simu yako na kadhalika, kwa sababu ni hatari sana. Kumbuka kilichompata yule mwanaume nchini Ufaransa."

"Unifute kwenye simu yako na katika maisha yako. Akigundua, litakuwa tatizo kubwa na mwisho wa ndoa yako; litaharibu maisha yako."

Oakley alisema kuwa "mwanaume wa Ufaransa" aliyetajwa katika ujumbe huo alikuwa akirejelea kesi maarufu ya Gisèle Pelicot, mwanamke aliyebakwa mara kwa mara na wanaume kadhaa baada ya kupewa dawa na mumewe.

'Ugonjwa wa akili na upotovu'

Upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa baada ya kukiri makosa, mume huyo alitoa maelezo kuhusu vitendo vyake na atatoa ushahidi katika kesi hiyo.

Aliwaambia waendesha mashtaka kuwa alianza kumfanyia mkewe unyanyasaji huo mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Mwanzoni, alisema alikuwa akimnyanyasa mkewe akiwa amepoteza fahamu na kuhifadhi picha hizo kwa ajili yake mwenyewe. Hata hivyo, baadaye alianza kuzisambaza katika maundi ya mitandao iliyoyokuwa na wanaume wengine wenye mawazo yanayofanana.

Oakley alisema katika mabadiliko aliyoyataja kuwa ya "ugonjwa na upotovu", wakati mwingine mume huyo alikuwa akijifanya kuwa mkewe katika mazungumzo ya mtandaoni, lakini aliacha tabia hiyo mapema.

Baraza la mahakama liliambiwa kuwa uchunguzi kuhusu unyanyasaji huo ulianza baada ya timu ya waandishi wa habari wa uchunguzi waliofanya kazi kwa siri kujiunga na kundi moja katika mtandao wa mawasiliano uliosimbwa wa Telegram, Oktoba 2025.

Inaelezwa kuwa washiriki wa kundi hilo walikuwa wanaume walichapisha na kutuma picha za wanawake walioonekana kupoteza fahamu, wakibakwa na kufanyiwa unyanyasaji wa kingono.

Kwa mujibu wa Oakley, mtumiaji mmoja wa kundi hilo alidai kuwa alimpa mkewe dawa na kumbaka, huku akiwaalika wanaume wengine kushiriki. Pia alisambaza picha za mwanamke huyo.

Namba ya simu iliyotumiwa na mtumiaji huyo ilibainika kuwa imesajiliwa kwa jina la mume wa mwanamke huyo. Hali hiyo iliwezesha polisi wa Greater Manchester kupata kibali cha kupekua makazi yao.

Oakley alisema baada ya maudhui yaliyokuwa kwenye simu hiyo kupakuliwa, polisi waligundua mafaili katika sehemu iliyokuwa imefungwa kwa usalama na kupewa jina la "visits" (ziara). Simu hiyo pia ilikuwa na programu za mawasiliano zilizotumiwa kuwasiliana na washitakiwa wengine.

Mwendesha mashtaka alisema wajumbe wa baraza la mahakama wataonyeshwa sehemu tu ya mafaili hayo, ingawa polisi wamechunguza kila moja.

Mume huyo alikiri mashtaka 62, yakiwemo ya ubakaji, kumpa mtu dawa kwa makusudi, kusambaza picha za faragha na unyanyasaji wa kingono.

Wanaume wengine wanne pia wamekiri makosa mbalimbali. Hao ni Keith Fotheringham, 59, kutoka Dundee, Scotland; Sean Peers, 38, kutoka Stockport; Graham Brougham, 74, kutoka Northwich, Uingereza; na Karl Lindsay, 55, kutoka Taunton, Uingereza.

Kesi dhidi ya washitakiwa wengine tisa bado inaendelea.