Siri zako ziko salama mikononi mwa AI?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kusambaratika kwa kampuni changa ya akili mnemba (AI) ya Character.AI kumeibua swali muhimu ambalo mara nyingi halijadiliwi: Taarifa zako binafsi ziko salama kiasi gani wakati kampuni inayozihifadhi inapofilisika, kuuzwa au kufungwa kabisa?

Nilipofungua akaunti kwenye jukwaa hilo wiki iliyopita, ujumbe wa kwanza nilioupokea ulikuwa wa kuvutia wateja. Chatbot iliyojiita "Jessica" ilijitambulisha kama msichana ambaye wazazi wake hawapo nyumbani, kisha ikapendekeza mazungumzo ya kimahaba. Nilijibu kwa kusema: "Asante, sina nia hiyo."

Nilikataa mwaliko wa Jessica, lakini mamilioni ya watu wengine, wakiwemo watoto, wamejenga mahusiano ya karibu na chatbots za kampuni hiyo.

Kwa wataalamu wa faragha, hatari zinazotokana na hali hii zinapaswa kukutia wasiwasi hata kama hujawahi kutumia Character.AI. Wanaonya kuwa huenda hii ikawa ishara ya changamoto kubwa zaidi inayokuja katika sekta ya AI.

Habari njema ni kwamba kuna hatua rahisi unazoweza kuchukua ili kulinda faragha yako.

Tatizo ni kwamba baadhi ya wataalamu wanahisi sekta ya AI kuwa katika "kiputo", ambapo gharama za kutengeneza na kuendesha mifumo ya AI ni kubwa kiasi kwamba baadhi ya kampuni huenda zisifanikiwe kupata na faida.

Kiputo hicho kikipasuka, kampuni nyingi za AI zinaweza kulazimika kuunganishwa na nyingine au kufungwa kabisa. Endapo hilo litatokea, taarifa ambazo mamilioni ya watu wameingiza katika mifumo ya AI zinaweza kuuzwa au kuhamishwa kwa kampuni nyingine, na huenda watumiaji wasijue hatima yake.

Uuzaji wa taarifa za watumiaji wakati kampuni inapofilisika si jambo jipya, lakini AI imeongeza ukubwa wa hatari hiyo kwa sababu ya kiasi kikubwa cha taarifa binafsi na nyeti zinazokusanywa na mifumo hiyo.

"Watu wanapozungumza na chatbot, mara nyingi hushiriki taarifa binafsi na nyeti sana," anasema Callie Schroeder, mkurugenzi wa programu ya AI na Haki za Binadamu katika Electronic Privacy Information Center (EPIC).

Fikiria ni mambo gani mtu angeweza kumweleza "Jessica" kama mazungumzo hayo yangeendelea kwa muda mrefu zaidi.

Schroeder anaonya kuwa hata wale wasioutumia AI bado wanaweza kuathiriwa.

"Hata kama hutumii AI, bado uko kwenye hatari kwa sababu watumiaji wengine hushiriki taarifa zinazowahusu marafiki na wanafamilia wao. Mtu anaweza kusimulia hisia zake kuhusu mama yake au kueleza jambo aliloambiwa na rafiki yake, na kwa kufanya hivyo anakuwa ametoa taarifa kuhusu mtu ambaye hajawahi kutumia huduma hiyo."

Hii ina maana kwamba hatari za faragha haziwahusu watumiaji wa AI pekee. Kwa namna moja au nyingine, karibu kila mtu anaweza kuathiriwa.

Roboti zinapoanza kuzungumza

Baada ya kutangaza kufilisika, Character.ai ilikubali kuuza baadhi ya mali zake kwa Disney kwa dola milioni 20. Mkataba huo haujumuishi data za watumiaji, hivyo mazungumzo ya watumiaji hayatakuwa sehemu ya makubaliano hayo.

Hata hivyo, nyaraka za mahakama zinaonyesha kuwa kampuni hiyo inaweza kuuza data kwa wanunuzi wengine, jambo lililozua wasiwasi miongoni mwa watetezi wa faragha pamoja na maafisa wa Marekani.

Muungano wa mawakili wakuu wa majimbo 40 uliwasilisha ombi mahakamani ukitaka sheria zinazolinda usalama na faragha za watoto zitekelezwe. Lakini baadhi ya wataalamu wa sheria wanaamini kuwa hatua hizo zinaweza kuwa na ufanisi mdogo.

Melissa Jacoby, profesa wa sheria katika Chuo Kikuu cha North Carolina, anasema kuwa bila sheria kali zaidi za faragha nchini Marekani, mamlaka zina uwezo mdogo wa kuzuia matumizi ya data hizo.

Makampuni mengi huahidi kupitia sera zao za faragha kueleza taarifa wanazokusanya na jinsi zinavyotumiwa. Hata hivyo, sera hizo mara nyingi huwa na vighairi vinavyoruhusu matumizi tofauti ya taarifa katika mazingira maalumu.

Kwa mujibu wa Callie Schroeder:

"Kufilisika mara nyingi ni mojawapo ya vighairi hivyo. Hilo ni hatari kubwa, kwa sababu kampuni inapofilisika, kinga nyingi ulizodhani zinakulinda huenda zisitumike tena."

Baadhi ya maeneo, kama Umoja wa Ulaya, yana sheria kali zaidi za faragha. Hata hivyo, hata huko data inaweza kuuzwa wakati wa mchakato wa kufilisika. Mara nyingi mnunuzi hutakiwa kufuata masharti ya sera ya awali ya faragha, lakini bado anaweza kuwa na uhuru mkubwa wa kuitumia data hiyo.

Katika sera yake ya faragha, Character.ai inaeleza kuwa data za watumiaji zinaweza kutumika kuboresha huduma, kufundisha mifumo ya akili bandia, kuendeleza algoriti na kuunda wasifu kwa ajili ya matangazo yanayolengwa. Hivyo, mnunuzi yeyote wa data hiyo anaweza kurithi haki hizo.

"Hayo ndiyo mambo yanayonitia wasiwasi zaidi. Kwa kuzingatia unyeti wa taarifa zinazokusanywa na kampuni kama hizi, matokeo yake yanaweza kuwa ya kutisha," anasema Schroeder.

Wasiwasi huo umeongezwa na madai yaliyowahi kuelekezwa kwa Character.ai. Miongoni mwao ni tuhuma kwamba chatbot ya kampuni hiyo ilimshawishi kijana mmoja kuwadhuru wazazi wake kutokana na vizuizi vya muda wa matumizi ya kifaa.

Pia kulikuwa na kesi ya mvulana mwenye umri wa miaka 14 aliyefariki kwa kujiua, huku ikidaiwa kuwa alikuwa amehamasishwa kufanya hivyo na mfumo wa akili bandia wa kampuni hiyo. Ujumbe huo, pamoja na kiasi kikubwa cha data nyingine za watumiaji, unaweza kuishia mikononi mwa kampuni ambazo watumiaji hawazifahamu.

Katika kujibu wasiwasi huo, msemaji wa Character.ai alisema kampuni hiyo imefikia makubaliano katika kesi husika na inaendelea kushirikiana na familia kuboresha usalama wa bidhaa zake. Hata hivyo, hakujibu maswali mahususi kuhusu faragha ya watoto.

Msemaji huyo aliongeza kuwa katika mwaka uliopita kampuni imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha usalama wa vijana wanaotumia huduma zake za akili bandia na itaendelea kuhimiza viwango kama hivyo katika sekta nzima.

Kwa Schroeder, Character.ai inaweza kuwa mwanzo tu.

"Kiasi kikubwa cha taarifa kinachoshikiliwa na kampuni za AI ni mali yenye thamani kubwa katika kesi za kufilisika. Bila kuwepo kwa sheria zaidi, nina wasiwasi kuhusu namna data hiyo itakavyotumiwa, nani ataipata na hatari zinazoweza kuwakabili watumiaji," anasema.

Unaweza kufanya nini?

Jibu fupi ni hili: futa data zako.

Character.ai imeeleza katika nyaraka zake za kufilisika jinsi watumiaji wanavyoweza kuomba data zao zifutwe.

Ingawa sheria mara nyingi hazilazimishi makampuni kutoa chaguo la kufuta data, mengi hutoa huduma hiyo kwa hiari ili kurahisisha usimamizi wa taarifa za watumiaji.

Ushauri muhimu ni kutambua huduma zinazohifadhi taarifa nyeti kukuhusu. Ikiwa huzitumii tena, chukua muda kufuta akaunti hizo pamoja na data inayohusiana nazo.

Njia za kufuta data hutofautiana kati ya huduma na huduma, lakini mara nyingi taarifa hizo hupatikana kwenye sehemu ya mipangilio ya faragha au sera ya faragha ya kampuni husika.

Iwapo huwezi kupata maelekezo hayo, wasiliana na huduma kwa wateja. Na kama unapata ugumu wa kuelewa hatua za kufuata, unaweza hata kuomba maelekezo kutoka kwa chatbot ya kampuni husika.

Lakini kuna tahadhari moja muhimu:

Hakikisha unathibitisha kwa makini majibu unayopewa.

Kwa namna fulani, hiyo ndiyo mojawapo ya kejeli kubwa za enzi ya akili bandia: wakati mwingine unaweza kuhitaji msaada wa AI ili kujilinda dhidi ya hatari zinazoweza kusababishwa na AI yenyewe.