Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Usinidharau kwa sababu ya jinsi ninavyozungumza'
- Author, Na Asha Juma
- Nafasi, BBC, Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Hebu fikiria ukiwa na jambo muhimu la kusema, lakini kila neno linalotoka mdomoni mwako linahitaji muda zaidi ili kueleweka.
Kwa wengi, kuzungumza ni jambo la kawaida. Lakini kwa Maryanne Wangari na kila mazungumzo yamekuwa safari ya uvumilivu, ujasiri na kujikubali.
Maryanne alianza kuishi na changamoto ya matamshi akiwa na umri wa mwaka mmoja baada ya kuugua ugonjwa uliomlaza hospitalini kwa muda mrefu.
"Mimi mwenyewe sikujua nilikuwa na tatizo. Nilielezwa na mama na bibi yangu. Walisema nilianza kuugua nikiwa na mwaka mmoja," anasimulia.
Anasema kabla ya hapo alikuwa mtoto wa kawaida kama wengine.
Baada ya kutoka hospitalini, maisha yaliendelea. Alianza shule kama watoto wengine, lakini safari yake ya kujifunza kuwasiliana ilikuwa tofauti.
"Nilijifunza kuzungumza kwa kuwaangalia na kuwasikiliza watoto wengine. Taratibu nikaanza kuzoea kuwasiliana kama wao."
'Watu hufikiri hatuelewi'
Licha ya kuzungumza kwa shida, Maryanne anasema changamoto yake haiko katika kufikiri au kuelewa.
"Watu wengi wanafikiri mtu anayezungumza polepole haelewi mambo. Hiyo si kweli. Tunaelewa kila kitu. Tuna mawazo, ndoto na hisia kama watu wengine."
Anasema jambo ambalo amekuwa akilitamani zaidi ni watu kumpa muda wa kujieleza badala ya kumhukumu kabla hajamaliza kuzungumza.
"Ningependa watu wanisikilize kwa uvumilivu. Wasinicheke au kunidharau kwa sababu ya namna ninavyozungumza."
Maumivu ya kutoeleweka
Ingawa anasema wengi wa familia yake walimkubali na kumpa ushirikiano, si kila mtu amekuwa na uelewa huo.
Wakati mwingine, hali hiyo humwathiri kihisia.
"Nikiumizwa au nikikasirishwa napenda kujitenga na watu. Nakaa peke yangu nikifikiria mpaka hasira ziishe," Maryanne anasema.
Hata hivyo, anasema hajawahi kufikiria kukata tamaa.
"Sijawahi kukata tamaa. Imani yangu ndiyo inanipa nguvu ya kuendelea kila siku. Nikiweka Mungu mbele naamini ninaweza kufanya chochote."
TikTok, Facebook na maisha ya vijana
Kama vijana wengi wa kizazi chake, Maryanne pia anapatikana kwenye mitandao ya kijamii.
Anatumia TikTok, Facebook na WhatsApp kuwasiliana na watu na kushiriki ujumbe mbalimbali.
"Napenda kuweka video TikTok. Pia huwahamasisha watu na kuzungumzia haki za watoto."
Lakini mitandao hiyo pia imeleta changamoto zake.
Anasema amewahi kukutana na watu waliotaka kumdhalilisha au kumcheka kwa sababu ya hali yake.
"Wakati mwingine nikiona mtu anataka kunidharau, najiondoa kwenye mazungumzo au natoka kwenye mtandao kwa muda."
Badala ya kushindana na wanaomdhihaki, anachagua kulinda amani yake.
"Sipendi mabishano. Huwa nafanya mambo mengine mpaka nipate utulivu."
'Rafiki yangu alichukua mchumba wangu'
Licha ya changamoto ya matamshi, Maryanne amesema pia amepitia maumivu ya kawaida ambayo vijana wengi hukutana nayo.
Anasema aliwahi kuwa kwenye mahusiano yaliyovunjika baada ya rafiki yake kuhusika na mtu aliyekuwa naye.
"Nilichukulia hilo kama somo la maisha. Niliamua kuendelea mbele na kujijenga."
Kwa sasa, anasema kipaumbele chake ni kutafuta kazi na kujitegemea.
Anapenda kutengeneza kazi za mikono, hususan shanga, na anaamini siku moja kipaji hicho kitamsaidia kujisimamia kiuchumi.
Wataalamu wanasemaje?
Mtaalamu wa tiba ya usemi aliyefuatilia mazungumzo ya Maryanne anasema changamoto yake si ya uelewa.
"Anaelewa vizuri mazungumzo yanayoendelea. Changamoto yake kubwa ni katika kujieleza kutokana na udhaifu au changamoto ya uratibu wa misuli inayohusika katika kutoa sauti na matamshi."
Mtaalamu huyo anafafanua kuwa ubongo hupanga taarifa na kuzituma kwa misuli ya ulimi, midomo, taya na koo ili kuzalisha sauti.
Iwapo misuli hiyo haitafanya kazi kwa uratibu unaotakiwa, mtu anaweza kupata shida ya kutoa maneno kwa ufasaha licha ya kuelewa kila kitu.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, hali kama hiyo inaweza kuboreshwa kupitia tathmini na mazoezi ya tiba ya usemi, hasa iwapo itagunduliwa mapema.
Ujumbe wake kwa jamii
Maryanne anasema jambo kubwa analotamani ni kuona jamii ikibadilisha mtazamo wake kuhusu watu wanaozungumza tofauti.
Anataka waonekane kama watu wenye uwezo sawa na wengine, badala ya kuhukumiwa kwa namna wanavyozungumza.
"Wasimdharau mtu anayezungumza tofauti. Usikubali maneno ya watu yakuvunje moyo. Jiamini jinsi ulivyo."
Anasema ingawa sauti yake inaweza kuchukua muda zaidi kusikika, ndoto zake hazijawahi kupungua.
Na huo ndiyo ujumbe anaotaka dunia isikie.
"Tunaelewa kila kitu. Tunahitaji tu muda kidogo zaidi kujieleza."
Imehaririwa na Ambia Hirsi