Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja , EU na Marekani zalaani hukumu ya Tundu Lissu

Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Bunge la Ulaya, David McAllister, amelaani uamuzi wa mahakama, akisema kumwandama mwanasiasa wa upinzani ni shambulizi la moja kwa moja dhidi ya misingi ya demokrasia na haki ya msingi ya kutoa maoni yanayopinga msimamo wa mamlaka.

Muhtasari

Moja kwa moja

Na Mariama Mjahid

  1. EU na Marekani zalaani hukumu ya miaka minne jela kwa Tundu Lissu

    Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kigeni ya Bunge la Ulaya, David McAllister, amezitaka mamlaka za Tanzania kumwachilia mara moja na bila masharti mwanasiasa wa upinzani Tundu Lissu, kufuatia kupatikana na hatia kwa shtaka la uchochezi.

    Katika taarifa yake, McAllister amesema kumchukulia hatua kiongozi wa upinzani kwa misingi ya kisiasa ni shambulizi la moja kwa moja dhidi ya misingi ya demokrasia na haki ya msingi ya kutoa maoni yanayopinga msimamo wa serikali.

    McAllister amekosoa pia uamuzi wa kumfungulia Lissu shtaka la uhaini kutokana na matamshi aliyotoa katika mkutano wa kisiasa kuhusu kuvuruga uchaguzi, akisema hatua hiyo ni kizuizi kisicho na uwiano dhidi ya uhuru wa kujieleza.

    Bunge hilo limesema kesi dhidi ya Lissu imekuwa na misukumo ya kisiasa na kukosoa kuzuiliwa kwake kwa zaidi ya siku 500. Kundi Kazi la Umoja wa Mataifa kuhusu Uwekaji Kizuizini Kiholela pia lilitaja kuzuiliwa kwake kuwa ni kwa njia isiyo halali.

    Novemba 27, 2025, Bunge la Ulaya lilipitisha azimio la kulaani kuzuiliwa kwa Lissu, likiitaka serikali ya Tanzania kumwachilia mara moja na bila masharti.

    McAllister amesisitiza tena wito huo, huku Bunge la Ulaya likizitaka mamlaka za Tanzania kuheshimu misingi ya demokrasia, kulinda haki ya wananchi kutoa maoni yao na kuhakikisha Lissu anaachiliwa huru.

    Umoja wa Ulaya Katika taarifa tofauti, Umoja wa Ulaya umesema unaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kesi hiyo, huku ukirejelea tathmini ya Kundi Kazi la Umoja wa Mataifa kuhusu Uwekaji Kizuizini Kiholela iliyobaini kuwa kuzuiliwa kwa Lissu hakukuwa na msingi wa kutosha wa kisheria na kulikuwa na dosari kubwa katika kuhakikisha anapata haki ya kusikilizwa kwa mujibu wa sheria.

    "Mwungano wa Ulaya unazihimiza mamlaka za Tanzania kutekeleza dhamira yake ya maridhiano, utawala wa sheria, uhuru wa kujieleza na demokrasia ya vyama vingi," msemaji wa umoja huo alisema Jumamosi, Novemba 7.

    Kauli ya Marekani Wakati huohuo, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, William Trachman, alikuwa ameelezea wasiwasi kuhusu mwenendo wa kesi hiyo muda mfupi kabla ya kutolewa kwa hukumu, akionya kuwa matokeo yake yana athari kwa uhuru wa msingi na utawala wa sheria.

    "Kama mwanasheria wa masuala ya katiba nchini Marekani, binafsi nimewahi kushughulikia kesi za kutetea haki ya uhuru wa kujieleza na haki ya kutendewa kwa mujibu wa taratibu za kisheria. Hizi ni kanuni za msingi za uhuru wa binadamu," alisema Trachman.

    Kauli hizo za hivi karibuni zinatolewa wakati ambapo uhusiano wa kidiplomasia kati ya Washington na Dar es Salaam umekuwa na mvutano, kufuatia Marekani kutangaza mwezi Desemba 2025 kuwa inapitia upya kwa kina uhusiano wake wa pande mbili na Tanzania.

    Lissu alipatikana na hatia ya uchochezi Novemba 6, 2026, huku akiachiliwa huru kwa shtaka la uhaini.

    Lissu alikuwa miongoni mwa waliowania tuzo ya Sakharov mwaka huu, inayotolewa na Bunge la Ulaya kwa kutambua juhudi za kutetea uhuru wa mawazo na haki za binadamu.

    Soma Zaidi Hapa:

  2. UAE yawaokoa watu 22 kutoka meli iliyoshika moto Bahari ya Oman

    Jeshi la Walinzi wa Taifa la Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) limesema limewaokoa watu 22 baada ya moto kuzuka kwenye meli ya mizigo katika Bahari ya Oman.

    Kwa mujibu wa Reuters, jeshi hilo lilisema Jumapili kuwa manusura wote ni raia wa nchi za Kiarabu.

    Mamlaka hazijatoa taarifa kuhusu chanzo cha moto huo wala utambulisho wa meli iliyohusika.

    Pia haijafahamika iwapo tukio hilo lina uhusiano wowote na matukio ya kijeshi yaliyoshuhudiwa katika kipindi cha hivi karibuni katika Bahari ya Oman, eneo ambalo ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta na biashara ya kimataifa.

  3. Iran yawanyonga watu watatu waliokamatwa wakati wa maandamano

    Mamlaka ya mahakama nchini Iran imetekeleza hukumu ya kifo dhidi ya watu watatu waliokamatwa kufuatia maandamano yaliyotikisa mji wa Karaj mwezi Januari, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mizan, linalohusishwa na idara ya mahakama nchini humo.

    Walionyongwa ni Hassan Deoband, Hamid Kazemi na Reza Zanganeh.

    Kwa mujibu wa Mizan, watatu hao walipatikana na hatia ya kushirikiana na Israel na Marekani katika shughuli za kiusalama, pamoja na kushiriki kwa silaha kwenye maandamano ya Januari 8 na 9. Pia walituhumiwa kuhusika katika uharibifu na uchomaji wa maeneo ya umma pamoja na miundombinu ya umeme.

    Shirika hilo limesema hukumu za kifo dhidi yao zilitekelezwa Jumapili baada ya kuidhinishwa na Mahakama ya Juu ya Iran. Mali zao pia zimeamriwa kutaifishwa.

    Mizan imeongeza kuwa watu wengine 10 walikamatwa kuhusiana na kesi hiyo, huku washtakiwa wengine wakihukumiwa vifungo vya kati ya miaka mitano na 10 jela.

    Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakikosoa mara kwa mara matumizi ya hukumu ya kifo nchini Iran, hasa katika kesi zinazohusiana na maandamano na masuala ya usalama wa taifa.

    Soma pia:

  4. Eisenkot akabidhiwa jukumu la kuunda serikali mpya ya Israel

    Rais wa Israel Isaac Herzog amesema amempa kiongozi wa upinzani, Gadi Eisenkot, jukumu la kuunda serikali mpya baada ya uchaguzi wa wiki iliyopita kutotoa mshindi wa wazi.

    Matokeo ya uchaguzi yaliiacha kambi ya Eisenkot na ile ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu bila idadi ya kutosha ya viti vya kuunda serikali katika Bunge la Israel, Knesset.

    Eisenkot sasa ana siku 28 kuunda serikali, huku akiruhusiwa kuomba nyongeza ya hadi siku 14 iwapo itahitajika.

    "Sasa ni wakati wa kuunda serikali ya dharura ya kitaifa. Nitafanya kila niwezalo kuhakikisha tunafanikiwa," Eisenkot, mkuu wa zamani wa jeshi la Israel, aliandika kwenye mtandao wa X.

    Mfumo wa kisiasa wa Israel unalazimu vyama kuunda miungano ili kupata wingi wa viti bungeni, kwani hakuna chama ambacho kimewahi kushinda idadi ya kutosha ya viti kuunda serikali peke yake.

    Katika uchaguzi huo, chama cha mrengo wa kulia cha Likud kinachoongozwa na Netanyahu pamoja na washirika wake kilipata viti 53 kati ya 120 vya Knesset. Kambi ya Eisenkot, inayoongozwa na chama chake cha Yashar pamoja na vyama vingine vya upinzani, ilishinda viti 48.

    Vyama viwili vinavyoongozwa na Waarabu, Muungano wa Orodha ya Waarabu na Orodha ya Pamoja, vilijizolea jumla ya viti 19, hatua inayovifanya kuwa na ushawishi mkubwa katika mchakato wa kuunda serikali.

    Hata hivyo, kabla ya uchaguzi, karibu vyama vyote vya Kiyahudi vilisema havitashirikiana na vyama hivyo vya Kiarabu katika kuunda serikali, jambo linaloweza kufanya mazungumzo ya kuunda muungano kuwa magumu.

    Herzog amesema kuwa baada ya kufanya mashauriano na vyama vya siasa kwa kipindi cha wiki moja, ameamua kumpa Gadi Eisenkot fursa ya kwanza ya kujaribu kuunda serikali mpya.

    Katika taarifa, ofisi ya rais ilisema kuwa Herzog amewaarifu Eisenkot na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuhusu uamuzi huo.

    Taarifa hiyo iliongeza kuwa, baada ya mashauriano na wawakilishi wa vyama vilivyopata viti katika Knesset, Eisenkot alipata uungwaji mkono wa wabunge 67 wa kumteua kuwa waziri mkuu, huku Netanyahu akiungwa mkono na wabunge 46.

    Sheria za Israel zinampa rais mamlaka ya kumchagua mwanasiasa anayeamini ana nafasi bora zaidi ya kuunda serikali ya muungano, bila kuzingatia idadi ya viti ambavyo chama chake kimeshinda bungeni.

    Soma zaidi:

  5. Mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia yaua watu 33, Wahouthi wasema

    Vyombo vya habari vinavyohusishwa na Wahouthi nchini Yemen vimeripoti kuwa watu wasiopungua 33, wakiwemo wanawake na watoto, wameuawa katika mashambulizi ya anga yanayodaiwa kufanywa na Saudi Arabia.

    Hakujakuwa na tamko la haraka kutoka kwa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao unaunga mkono serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa.

    Televisheni ya Al Masirah, inayomilikiwa na Wahouthi, imeonyesha picha za moja kwa moja za waokoaji wakitoa miili kutoka kwenye vifusi vya majengo katika mji wa al-Shariyah, mashariki mwa mji mkuu, Sanaa.

    Picha hizo pia zilionyesha miili ya watoto miongoni mwa waliopatikana kwenye vifusi, huku majeruhi kadhaa wakipelekwa hospitalini kwa machela.

    Shirika la habari la Saba, linaloendeshwa na Wahouthi, limesema mashambulizi hayo yalifanyika Jumamosi na kwamba watu 39 walijeruhiwa.

    Saudi Arabia imeongoza muungano unaopambana na Wahouthi kwa zaidi ya muongo mmoja, ikiisaidia serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa.

    Mapigano nchini Yemen yalikuwa yamepungua kwa miaka kadhaa, lakini yameongezeka tena kutokana na athari za mzozo unaohusisha Iran katika eneo hilo.

    Unaweza pia kusoma:

  6. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.