Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Nini kinafuata kwa Lissu, CHADEMA na maridhiano baada ya hukumu?
Hukumu ya kifungo cha miaka minne jela kwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Antipas Lissu, imefungua ukurasa mpya katika safari yake ya kisiasa na mustakabali wa chama hicho, huku ikiibua maswali kuhusu hatma ya uongozi wake, Chama chake, upinzani, demokrasia na nafasi yake katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2030.
Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imesema Lissu hana hatia katika shtaka la uhaini, lakini imemkuta na hatia ya kosa dogo la uchochezi.
Hukumu hiyo ambayo ilianza kujadiliwa zaidi mitandaoni siku moja kabla, kikiwemo chama chake kujitokeza, imehitimisha kesi iliyomweka mahabusu kwa siku 577 tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025.
Sasa, pamoja na hukumu hiyo, kuna masuala kadhaa yanayoweza kuamua mwelekeo wa siasa za upinzani nchini Tanzania katika kipindi kijacho. Lakini nini kilicho mbele?
Kukata rufaa?
Moja ya hatua zinazoweza kufuatwa na Lissu ni kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ya Mahakama Kuu. Kupitia rufaa, anaweza kupinga uamuzi wa kumtia hatiani, adhabu aliyopewa au vipengele vyote viwili, kwa kuwasilisha hoja zake katika mahakama ya juu.
Hata hivyo, rufaa yenyewe haimaanishi moja kwa moja kuwa hukumu ya kifungo itasitishwa. Hilo linategemea taratibu za kisheria na uamuzi wa mahakama kuhusu maombi husika.
Wanasheria wanasema matokeo ya rufaa yanaweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa sababu yanaweza kubadili ama kuathiri hatua nyingine za maisha yake ya kisiasa.
Wakati wa kutoa hukumu, Mahakama ilisema Lissu anaweza kukata rufaa.
Hatma ya Lissu kisiasa
Lissu na siasa ni chanda na pete. Leo anakwenda kuanza safari ya kuwa mfungwa. Kwa misimamo yake huenda asiache siasa, pengine ataendeleza siasa hata gerezani lakini mtu mwiungine mtaani anaweza kujiuliza kama hukumu hiyo itamzuia Lissu kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2030.
Kwa mujibu wa Ibara ya 39 ya Katiba ya Tanzania, mgombea urais anatakiwa, miongoni mwa masharti mengine, kuwa raia wa kuzaliwa, awe na umri wa angalau miaka 40 na awe amependekezwa na chama cha siasa.
Lakini pia mtu huyo awe na sifa za kumwezesha kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi;
Ibara hiyo pia inaweka kizuizi kwa mtu aliyepatikana na hatia ya kosa linalohusu kukwepa kulipa kodi ndani ya kipindi cha miaka mitano kabla ya uchaguzi mkuu, lakini ukiisoma na Ibara ya 67 kuhusu sifa za mtu kuwa mbunge inasema "mtu hatakuwa na sifa za kustahili kuchaguliwa au kuteuliwa kuwa Mbunge, iikiwa mtu huyo amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote, vyovyote linavyoitwa, linaloambatana na utovu wa uaminifu; au
Kwa mantiki hii, suala la sifa za kugombea kwake kama alivyofanya uchaguzi wa mwaka 2020, linatathminiwa kwa kuzingatia masharti yote ya Katiba, sheria za uchaguzi na hali ya rufaa yake.
Pamoja na hilo, kifungo cha miaka minne kinaibua changamoto ya kiutendaji. Ikiwa atatumikia kifungo chote, muda wake wa kutoka gerezani unaweza kuwa karibu na kipindi cha maandalizi ya uchaguzi wa 2030. Hivyo, matokeo ya rufaa na masuala ya utekelezaji wa adhabu yatakuwa na nafasi muhimu katika hatma hiyo.
Hatma ya CHADEMA bila mwenyekiti wake
Kwa CHADEMA, changamoto mpya inaanza. Ni namna ya kuendeleza uongozi na shughuli za chama wakati mwenyekiti wake akiwa gerezani. Wamefanya hivyo akiwa mahabusu kwa miezi 19, kwa matarajio labda angeachiwa. Lakini sasa anakwenda kutumikia kifungo cha miaka minne, japo ana nafasi ya kukata rufaa.
Tangu Lissu achaguliwe kuwa mwenyekiti wa taifa, amekuwa mmoja wa viongozi wakuu wanaohusishwa na msimamo wa chama kuhusu mageuzi ya kisiasa na uchaguzi. Alichaguliwa Januari 2025 na April mwaka huo huo akakamatwa kw akosa la uhaini.
Kukosekana kwake nje ya gereza kunazua swali la namna chama kitakavyoratibu maamuzi yake, kuendesha shughuli zake na kudumisha mwelekeo wa kisiasa.
Hata hivyo, CHADEMA ina viongozi wengine ambao kwa kiwango chao wameendelea kukiongoza chama. Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, yupo na amekuwa akizungumza kwa niaba ya chama na kuhimiza wanachama kuendeleza msimamo wao kuhusu mageuzi.
Mwezi Agosti 2026, Heche alisema baada ya kukutana na Lissu gerezani, mwenyekiti huyo alimhimiza kuendeleza mapambano ya mageuzi. Kauli hiyo ilionyesha kuwa, licha ya kuwa mahabusu, Lissu aliendelea kuwa sehemu ya mwelekeo wa kisiasa wa chama.
Pengine mtu atajiuliza kama Heche na viongozi wengine wataendelea kutekeleza majukumu hayo kwa kusimamia maelekezo ya mwenyekiti, au chama kitaingia katika mjadala mpana zaidi kuhusu namna ya kuendesha uongozi wake katika mazingira mapya au kutafuta mwenyekiti mpya?
Akitoka Mahakamani baada ya hukumu ya Lissu, Heche akiambia moja vyombo vya habari vya ndani kwamba chama hicho kitazungumza.
Hatma ya maridhiano Tanzania
Hatma ya maridhiano ya kisiasa nchini Tanzania ni eneo jingine litakaloathiriwa na hukumu ya Lissu. Mchakato huo hauwezi kuiweka CHADEMA pembeni, kwa kuwa chama hicho ni miongoni mwa wadau wakuu wa siasa za upinzani nchini. Hata hivyo, chama hicho kimekuwa nje ya juhudi mbalimbali za maridhiano kwa kipindi kirefu, licha ya mchakato huo kuonekana kurudi tena tangu wakati ule uliposambaratika muda mfupi baada ya kuanzishwa na utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021.
Juhudi za awali za maridhiano zilianza kwa mazungumzo kati ya Serikali na vyama vya upinzani, wakati Freeman Mbowe akiwa mwenyekiti wa CHADEMA. Hata hivyo, mchakato huo haukuendelea kwa namna iliyotarajiwa, na baadaye chama hicho kikajikuta katika mvutano mpya na Serikali, hasa kuhusu madai ya mageuzi ya kisiasa na uchaguzi.
Sasa, wakati juhudi nyingine za kujenga maridhiano zikianza kufanyika, hukumu ya Lissu inaongeza swali kuhusu namna CHADEMA itakavyoshirikishwa. Kuwa gerezani kwa mwenyekiti wake kunaweza kuwa changamoto katika mazungumzo yanayohitaji uwakilishi na maamuzi ya kisiasa kutoka kwa viongozi wakuu wa chama. Hata hivyo, uwepo wa John Heche na viongozi wengine unaweza kuwa sehemu ya namna chama kitakavyoshiriki mchakato huo.
Lakini hivi karibuni Heche alisema "CHADEMA haitashiriki maridhiano mpaka Lissu atoke". Je msimamo huo utalegezwa na CHADEMA itakuwa tayari kurejea katika meza ya mazungumzo licha ya mwenyekiti wake kufungwa, au itaendelea kusisitiza kuwa ushiriki wa Lissu na kutimizwa kwa madai yake ni sehemu ya masharti ya maridhiano? Bado hatma ya hili ni kizungumkuti.