Kifo cha De Miguel Uwanjani: Kipa Owono afungiwa mechi 12
Kipa wa klabu ya FC Andorra, Jesus Owono, amefungiwa kucheza mechi 12 na kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka la Hispania kufuatia tukio la kugongana na mshambuliaji wa Tenerife, Jesus de Miguel, ambaye baadaye alifariki dunia.
Owono, mwenye umri wa miaka 25, alioneshwa kadi nyekundu baada ya kugongana na De Miguel katika dakika za mwisho za mchezo wa ligi daraja la pili nchini Hispania kati ya timu hizo mbili, Novemba 2.
De Miguel, mwenye umri wa miaka 30, alifariki dunia siku iliyofuata.
Katika taarifa yake, kamati ya nidhamu imesema ililazimika kufanya uamuzi kwa kuzingatia maelezo yaliyoandikwa rasmi na mwamuzi wa mchezo.
Ripoti ya mwamuzi ilieleza kuwa Owono alioneshwa kadi nyekundu kwa kumpiga mpinzani wake kifuani kwa kutumia mguu kwa nguvu kupita kiasi wakati mpira ukiwa unaendelea kuchezwa.
Kamati hiyo imeongeza kuwa kutokana na aina ya kitendo kilichofanyika pamoja na mazingira ya tukio hilo, adhabu ya juu kabisa ya kufungiwa mechi 12 imeonekana kuwa inastahili.
Aidha, shirikisho hilo limeamua mchezo huo ambao ulisimamishwa dakika saba ndani ya muda wa nyongeza hautarudiwa.
Wakati tukio hilo linatokea, timu hizo zilikuwa zikitoshana nguvu kwa mabao 2-2.
Shirikisho limesema matokeo hayo yatabaki kuwa rasmi, likieleza kuwa huo ndio uamuzi unaoheshimu zaidi mazingira ya kipekee na ya kusikitisha yaliyotokea.
Owono bado hajafanya uamuzi kuhusu kurejea uwanjani
Kupitia taarifa iliyotolewa Novemba 4 kwa niaba yake na klabu ya FC Andorra, Owono alisema anapitia siku ngumu zaidi maishani mwake na anahisi maumivu makubwa kutokana na kifo cha De Miguel.
Kwa upande wake, kocha wa FC Andorra, Carles Manso, amesema kipa huyo ambaye ni raia wa Equatorial Guinea bado hajafanya uamuzi kuhusu kurejea kucheza soka kufuatia tukio hilo.
Manso amesema kwa sasa Owono yuko pamoja na familia yake na amepewa uhuru wa kufanya uamuzi wowote kuhusu mustakabali wake wa soka.
Kocha huyo amesema klabu itampa kila aina ya msaada na kuwa karibu naye katika kipindi hiki kigumu.
Ameongeza kuwa Owono atapewa nafasi ya kuamua kama anataka kurejea uwanjani, lini anataka kufanya hivyo, au kama hataki kuendelea tena na soka.
Amesisitiza kuwa uamuzi huo utategemea wakati ambao Owono atajihisi yuko tayari kufanya hivyo.
Soma Zaidi Hapa: