Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwa nini Cristiano Ronaldo amestaafu soka la kimataifa?
- Author, Guillem Balague
- Nafasi, Mchambuzi BBC Michezo
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Mpinzani wake wa muda mrefu, Lionel Messi, aliondoka Argentina chini ya mwezi mmoja uliopita huku taifa hilo likimshangilia. Lakini gwiji wa Ureno, Cristiano Ronaldo, ameondoka kwa namna tofauti kabisa. Na huenda mwisho wake ungekuwa hivyo hata iweje.
Ronaldo, mwenye umri wa miaka 41, ametangaza kustaafu soka la kimataifa baada ya miaka 23, lakini uamuzi huo unafuatia pia mvutano wake na kocha Jorge Jesus. Mzozo huo ulimalizika kwa adhabu ya kusimamishwa kwa siku 30, ambazo tayari alikuwa amezitumikia, pamoja na faini ya euro 255.
Adhabu hiyo ilitolewa baada ya mshambuliaji huyo wa Ureno kuondoka kambini mwa timu ya taifa bila ruhusa. Jesus alimuacha benchi katika mechi moja na kusema hakuwa na mpango wa kumtumia katika kikosi cha kwanza cha mechi iliyofuata. Ronaldo akaamua kurejea nyumbani.
Mechi yake ya mwisho ilikuwa dhidi ya Wales, Septemba 24. Anamaliza safari yake ya kimataifa akiwa amefunga mabao 146 katika mechi 234.
Ureno ilitoa ujumbe wa kumshukuru kwa mchango wake, ikimtaja kama balozi wa taifa hilo duniani na mtu aliyehamasisha mamilioni ya watu. Hata hivyo, namna alivyomaliza safari yake ya kimataifa imeacha hisia za uchungu.
Je, angejumuishwa katika kikosi kijacho cha timu ya taifa? Inawezekana. Jesus alisema mlango ulikuwa wazi na uamuzi ulikuwa mikononi mwa Ronaldo. Lakini kilicho wazi ni kwamba hakuwa tena mchezaji anayetarajiwa moja kwa moja kuanza kila mechi. Na Ronaldo hajawahi kupokea hali hiyo kwa urahisi.
Je, huu ni mfano mwingine wa Ronaldo kukasirika anapowekwa pembeni? Kwa kiasi fulani, ndiyo. Alifanya kama ambavyo amekuwa akifanya kila kocha anapokuwa na mashaka kuhusu nafasi yake. Lakini mtazamo huo hauoneshi kikamilifu jinsi alivyobadilika na kukomaa katika kipindi chote cha miaka yake akiwa na timu ya taifa.
Mienendo kama hiyo imejitokeza katika uhusiano wake na takribani makocha wote waliowahi kuiongoza Ureno. Kumekuwa na migogoro, lakini pia ushirikiano wa karibu na makocha pamoja na wachezaji wenzake. Yote hayo yanasaidia kuelewa namna safari yake ilivyofikia mwisho.
Ronaldo alipokuwa mchezaji chipukizi na kujiunga kwa mara ya kwanza na timu ya taifa, aliwasili kambini akiwa amevaa kofia ya baseball iliyogeuzwa nyuma, miwani mikubwa ya jua na vipokea sauti vilivyokuwa na sauti kubwa kiasi cha kusikika hata kwa waliokuwa mbali.
Hakuvua hata kofia yake wakati wa kula pamoja na wachezaji wakongwe kama Luis Figo na Rui Costa. Kocha Luiz Felipe Scolari alimuona kuwa mchezaji mwenye kipaji cha kipekee, lakini ambaye hakuwa amekomaa na alikuwa akipenda kujionyesha.
Scolari alimkemea hadharani, kisha akamwambia faraghani kwamba akibadilisha mwenendo wake, siku moja angekuwa nahodha wa Ureno.
Tamaa yake ya kutwaa taji kubwa ilianza kukabiliwa na majaribu mapema, tena nyumbani kwao. Akiwa na umri wa miaka 19, Ronaldo alicheza fainali ya Euro 2004 katika uwanja wa Estadio da Luz mjini Lisbon, mbele ya taifa lililoamini tayari lilikuwa karibu kutwaa ubingwa.
Lakini bao moja la kichwa la Angelos Charisteas lilitosha kuipa Ugiriki, ambayo haikuwa miongoni mwa timu zilizotarajiwa kufanya vizuri, ushindi wa kushtukiza.
Mwamuzi alipopuliza filimbi ya mwisho, Ronaldo alishindwa kuzuia machozi. Picha ya kijana huyo akilia katika uwanja wa nyumbani ilisambaa duniani kote.
Ilikuwa njia chungu ya kujifunza gharama ya kupoteza fainali, na tukio hilo lilichochea zaidi kiu yake ya kutwaa mataji.
Wakati huo, jezi namba saba ilikuwa ikivaliwa na Figo, hivyo Ronaldo alipewa namba 17. Figo alimsaidia kuzoea mazingira ya timu ya taifa, lakini hakumpa nafasi hiyo kwa urahisi. Figo alipoondoka kwenye timu ya taifa mwaka 2006, jezi hiyo na jukumu la kuiongoza timu vikawa vya Ronaldo.
Septemba 2005, kabla ya mechi ya kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Urusi, Scolari na Figo walikwenda chumbani kwake kumweleza kuwa baba yake amefariki dunia.
Scolari alimpa nafasi ya kurejea nyumbani, lakini Ronaldo aliamua kucheza. Aliwaomba wachezaji wenzake waendelee na shughuli zao kama kawaida, huku yeye akitumia muda katika chumba cha kubadilishia nguo akionesha ufundi wa kuchezea mpira.
Hiyo ndiyo ilikuwa njia yake ya kukabiliana na kifo cha baba yake, ambaye alikuwa na tatizo la ulevi. Ronaldo baadaye alimwita Scolari baba. Timu ya taifa ilikuwa imekuwa sehemu iliyomsaidia kustahimili kipindi hicho kigumu.
Uhusiano wake na kocha Carlos Queiroz haukuwa mzuri. Baada ya Ureno kuondolewa na Hispania katika Kombe la Dunia la mwaka 2010, Ronaldo alipoulizwa na waandishi wa habari kueleza sababu za timu kufanya vibaya, aliwaambia wamwulize kocha.
Ushawishi wake kambini ulikuwa umeongezeka kiasi cha kuanza kubadilisha ratiba na mienendo ya timu. Hali hiyo inaeleza kwa nini kocha alihisi mamlaka yake yalikuwa yakidhoofishwa.
Mwanasosholojia Joao Nuno Coelho anatoa mtazamo muhimu kuhusu namna Wareno wanavyomchukulia Ronaldo. Kwa mujibu wa uchambuzi wake, timu ya taifa ilikuwa imekuwa sehemu ya utambulisho wa Wareno na hitaji la nchi hiyo kutambulika kimataifa.
Katika miaka iliyokumbwa na matatizo ya kiuchumi na kupungua kwa kujiamini kama taifa, timu iliyoweza kupata heshima nje ya nchi ilikuwa na umuhimu mkubwa zaidi ya soka pekee.
Ronaldo alikuwa kiini cha matarajio hayo, lakini pia alizua hisia zinazokinzana. Baadhi ya Wareno walitilia shaka ubinafsi wake na kujiona kwake, huku wengine wakihisi hawakuweza kujitambulisha na hulka yake.
Coelho anaeleza kuwa kadiri muda ulivyosonga, ndivyo ilivyokuwa vigumu zaidi kumkosoa Ronaldo. Taifa lilitaka kujivunia mafanikio yake, lakini wakati mwingine pia lilihisi kutokuwa na uhakika kuhusu namna alivyokuwa akijibeba hasa kujipiga kifua..
Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Jorge Andrade, aliniambia kuwa baadhi ya mashabiki walipendelea wachezaji kama Figo, Eusebio, Paulo Futre au Rui Costa. Hata hivyo, Ureno ilijivunia kuwa na Ronaldo. Na baada ya mafanikio yake kutwaa mataji, mashaka dhidi yake yalipungua.
Chini ya kocha Fernando Santos mwaka 2016, Ronaldo alionesha mabadiliko makubwa. Alikubali kucheza kama mshambuliaji wa kati pembeni ya Nani. Hakuwa amewahi kupokea maelekezo ya kocha kwa urahisi kiasi hicho.
Baada ya Ureno kutoka sare katika mechi yake ya ufunguzi dhidi ya Iceland, alimwambia Nani faraghani kuwa alikuwa na imani na Santos. Taratibu, wachezaji wenzake walianza kumtambua kama nahodha halisi wa timu.
Baada ya kukosa penalti dhidi ya Austria, Ronaldo alikaribia kukosa usingizi usiku huo. Santos alipoamka, alimkuta Ronaldo akiwa tayari macho.
Katika kambi ya mazoezi ya Marcoussis, alichukua kipaza sauti cha shabiki mmoja na kuwaambia mashabiki kuwa Ureno ilikuwa bado haijashinda chochote.
Alikuwa akifurahia jukumu lake jipya la uongozi.
Katika fainali iliyochezwa mjini Paris, Ronaldo aliondoka uwanjani akiwa analia baada ya kuumia. Hakuwa amefanya vizuri katika mashindano hayo, huku maumivu ya misuli yakimzuia kuonesha uwezo wake kamili.
Nani alichukua mikoba ya unahodha. Wakati wa mapumziko, Ronaldo alijipa moyo na kuanza kuwatia nguvu wachezaji wenzake. Kabla ya muda wa nyongeza kuanza, akiwa bado anachechemea, alimwambia Eder kuwa angefunga bao.
Na Eder akafunga.
Hata hivyo, hulka yake ya kutaka kushiriki katika kila jambo haikupotea kabisa. Katika muda wa nyongeza, Ronaldo alisimama eneo la benchi la ufundi akitoa maelekezo kwa wachezaji, hadi mwamuzi wa akiba alipomwamuru kurejea sehemu yake.
Makocha wengine niliozungumza nao waliona kitendo hicho kuwa kilizidi mipaka.
Nguvu yake kubwa, yaani kutaka kuwa na ushawishi katika kila matokeo, pia ilifanya iwe vigumu kwake kukubali mipaka ya mamlaka yake.
Alipoanza kucheza timu ya taifa mwaka 2003, Ureno ilikuwa bado inasaka taji lake la kwanza kubwa. Baadhi ya wachezaji huacha alama katika kipindi fulani, lakini wengine hubadilisha kabisa historia ya timu ya taifa. Ronaldo ni miongoni mwa kundi la pili.
Usiku huo wa Julai 2016 uliipa Ureno taji lake la kwanza la Ubingwa wa Ulaya.
Miaka mitatu baadaye, alifunga mabao matatu dhidi ya Uswisi na kuiwezesha Ureno kufuzu kwa fainali ya kwanza ya Ligi ya Mataifa ya Ulaya, ambayo baadaye ilitwaa ubingwa huo.
Mwaka 2025, akiwa katika umri ambao wachezaji wengi huwa tayari wamestaafu, alinyanyua tena kombe la pili la Ligi ya Mataifa ya Ulaya.
Hakuna mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi ya Ronaldo katika timu ya taifa, wala aliyevaa jezi ya Ureno mara nyingi zaidi yake
Chini ya ushawishi wake, Ureno iliacha kuwa timu yenye vipaji pekee na kuwa taifa linalokwenda katika kila mashindano makubwa likiwa na matarajio ya kutwaa ubingwa.
Kizazi kizima cha wachezaji pia kilikulia katika mazingira ya timu ambayo Ronaldo alisaidia kuweka viwango vya mafanikio.
Hoja ya Coelho inaonekana wazi hapa pia. Taifa dogo lilipata namna ya kutambulika duniani, na kwa takribani miongo miwili Ronaldo alikuwa sura yake.
Baada ya mwaka 2016, mjadala kuhusu Ronaldo ulibadilika. Watu wachache walihoji tena kama alikuwa mbinafsi. Badala yake, swali lilikuwa kama Ureno ilikuwa imemtegemea kupita kiasi.
Katika Kombe la Dunia la mwaka 2018, alifunga mabao matatu dhidi ya Hispania, likiwemo bao la adhabu ndogo baada ya kujaribu mara 45 katika mashindano makubwa. Hata hivyo, Ureno iliondolewa na Uruguay.
Baada ya Kombe la Dunia la mwaka 2026 lililokuwa gumu kwa Ureno, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu Ronaldo kuendelea kuanza katika safu ya ushambuliaji. Hata hivyo, takwimu zinaonesha kuwa kipindi hicho ndicho alichokuwa na kiwango chake bora zaidi cha ufungaji.
Chini ya kocha Roberto Martinez, amefunga mabao 28 katika mechi 37, wastani wa mabao 0.756 kwa kila mechi. Hiyo ni rekodi bora kuliko wastani wa mabao 0.624 aliokuwa nao chini ya Santos.
Shirikisho la Soka la Ureno limetangaza kuandaa heshima maalumu kutambua mchango wake. Hatua hiyo ni muhimu, hasa kwa kuwa namna alivyomaliza safari yake ya timu ya taifa haijawapa mashabiki fursa ya kusherehekea mchango wake kwa namna ambayo wangependa kushiriki.
Mashabiki hawakukulia tu pamoja naye katika kipindi chote hicho. Aliwapeleka pia katika mafanikio ya kihistoria ambayo hawakuwa wamewahi kuyafikia hapo awali.
Imetafsiriwa na Mariam Mjahidi na kuhaririwa na Ambia Hirsi